Pengine umeshawahi kusikia jina la Profesa Allan Lichtman wa Marekani ambaye ana rekodi ya miaka 30 ya kutabiri kwa usahihi kabisa matokeo ya urais katika nchi hiyo.
Pengine utabiri uliompatia umaarufu zaidi ni wa mwaka 2016 ambapo takriban kila kura ya maoni ilionyesha kuwa mgombea wa chama cha Democrats, Hillary Clinton, angemshinda mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump.
Profesa huyo anatumia vipengele 13 vinavyopatikana kwenye kitabu chake kiitwacho "The Keys To The White House" (funguo za kuingilia Ikulu ya Marekani).
Katika vipengele hivyo 13 ni kauli zenye mrengo wa ushindi kwa mgombea aliyepo madarakani. Kwa muktadha wa Tanzania, vipengele hivi hapa chini vinamhusu Rais John Magufuli wa chama tawala CCM anayechuana vikali na mpinzani wake mkuu, Tundu Lissu wa Chadema.
Endapo majibu ya SI KWELI (FALSE) ni matano au pungufu kwa vipengele hivyo, basi mgombea aliyepo madarakani anatabiriwa kushinda. Lakini endapo majibu ya SI KWELI (FALSE) yatakuwa sita au zaidi, basi mgombea huyo ataanguka kwenye uchaguzi husika.
Naomba nitahadharishe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa kanuni hii kutumika kutabiri matokeo ya urais nchini Tanzania. Hata hivyo nimejiridhisha kuwa japo Profesa Lichtman alilenga chaguzi za rais wa Marekani, zaweza pia kutumika kwa muktadha wa Tanzania.
Jana
Januari 9, 2018, wiki moja na siku mbili baada ya kuanza kwa mwaka huu mpya, duru
za siasa za Tanzania zilitikiswa na habari kuhusu kiongozi maarufu wa Chadema,
Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kukutana na Rais John Magufuli kwa “mazungumzo”,
Ikulu jijini Dar es Salaam.
Baada
ya “mazungumzo” hayo Lowassa alimmwagia pongezi Magufuli kwa kile alichokiita “kazi
nzuri anayoifanya” na kutaja mafanikio katika sera ya elimu bila malipo, ujenzi
wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s
Gorge), na ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli ya “standard gauge”.
“Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana
na Mheshimiwa Rais, tumezungumza nae na nimempongeza kwa kazi nzuri
anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo,” alinukuliwa
Lowassa aliyejiunga na Chadema miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2015 baada ya ndoto zake kuwania urais kwa tiketi ya CCM “kuota mbawa.”
Mwanasiasa
huyo ambaye baada ya kujiunga na Chadema alipitishwa kuwa mgombea urais kwa
tiketi ya muungano wa vyama vinne vya upinzani – Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na
NLD – uliofahamika kama UKAWA, aliendelea kusema kuwa “Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza
ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na
kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler’s Gorge
ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha
kusema kwamba tunajenga ajira. Jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi
kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya
kutosha, kwa kweli nakushukuru Mheshimiwa Rais, you made my day.”
Rais
Magufuli kwa upande wake alimpongeza Lowassa kwa kile alichokiita “kutambua
kazi kubwa inayofanywa na Serikali” na kumtaja Lowassa kama mmoja wa viongozi
ambaye kwa wakati wake alitoa mchango wake katika nchi.
Magufuli
alimmwagia sifa Lowassa akidai kuwa “ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha Urais, hakuwahi
kumtukana.”
“Mheshimiwa Lowassa ameniomba mara nyingi
nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya
kwake na mimi nimemwambia ya kwangu. Kwa ujumla Mheshimiwa Lowassa ni
mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani
walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Mhe. Lowassa ambaye kama
alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi,” alisema Rais Magufuli
“Ametaja miradi mbalimbali tunayotekeleza,
ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge utakaogharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 7,
amezungumzia juu ya elimu bure, amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati
nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza
juu ya umeme tulivyosambaza katika vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za
hospitali na mengine” aliongeza Rais Magufuli.
Kwanza,
ni muhimu kutambua kuwa kama Mtanzania yeyote yule, Lowassa alikuwa na kila
haki ya kukutana na Rais wake. Kadhalika, kama mmoja wa viongozi wakuu wa
upinzani, isingepaswa kuwa jambo la kushangaza kwa viongozi hao wawili
kukutana.
Hata
hivyo, Lowassa sio tu amekutana na Magufuli, bali pia ammemwamgia sifa. Je ni
dhambi kwa kiongozi wa chama cha upinzani kumwagia sifa Rais aliyepo
madarakani? Jibu lingepaswa kuwa “si dhambi,” laiti uhusiano kati ya Rais
Magufuli, serikali yake na taasisi zake (kama vile jeshi la polisi, Tume ya Taifa
ya Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa), watendaji wa serikali (hasa
mawaziri na manaibu wao, na wakuu wa mikoa na wilaya), pamoja na chama cha Magufuli
yaani CCM, na chama anachotoka Lowassa, yaani Chadema, na Upinzani kwa ujumla,
ungekuwa mzuri.
Lakini
ukweli ni kwamba japo tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992,
uhusiano kati ya CCM, serikali zake na taasisi zake, na vyama vya upinzani
umekuwa “wa kusuasua,” hali katika miaka miwili tu ya utawala wa Magufuli
imekuwa mbaya zaidi hususan kutokana na ukweli kwamba hakuna jitihada za
kuficha chuki iliyopo dhidi ya Upinzani.
Kama
kiongozi wa ngazi za juu kabisa wa Chadema, na pengine mwanasiasa anayeheshimiwa
zaidi ya kiongozi mwingine yoyote ndani ya chama hicho, ni wazi Lowassa
anafahamu vema msimamo na mtazamo wa chama chake kuhusu Magufuli na utendaji
kazi wake, na serikali yake, na chama chake.
Pengine
kwa kuweka picha sawia, inaelezwa kwamba hadi wakati huu, zaidi ya wana-Chadema
400 ikiwa ni pamoja na viongozi na wanachama, aidha wapo jela au wana kesi
zinazoendelea mahakamani ambazo takriban zote ni matokeo ya chuki za kisiasa
zinazofanywa na Magufuli, serikali yake na chama chake.
Kadhalika,
katika utawala wa Magufuli, vyama vya upinzani ikiwemo Chadema ambayo Lowassa
ni kiongozi wake wa kitaifa vimepigwa marufuku kufanya shughuli zao za kisiasa
ikiwa ni pamoja na mikutano na maandamano. Hayo yanatokea wakati CCM ikiwa huru
kufanya mikutano na maandamano itakavyo, mara nyingi ikitumia raslimali za
umma.
Sambamba
na jitihada za Magufuli kubana fursa ya siasa (political space), utawala wa
kiongozi huyo umekuwa mstari wa mbele kuvibana vyombo vya habari na kudhibiti
uhuru na haki ya wananchi kutoa mawazo yao kama Katiba inavyowaruhusu.
Lakini
jingine ambalo Chadema ni mhanga mkubwa, kada maarufu wa chama hicho Ben
Saanane “alipotea” Novemba mwaka jana na hadi leo hajapatikana.
Na
ni wakati ninaandika makala hii nimebaini kuwa Lowassa hajawahi kuongelea suala
la kada huyo (naomba nikosolewe kama nimekosea).
Kubwa
zaidi linaloweza kuhalalisha hasira za Chadema kwa utawala wa Magufuli ni tukio
la hivi karibuni ambapo Mbunge wake maarufu, ambaye pia alikuwa mpinzani
maarufu dhidi ya Magufuli, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kunusurika
kuuawa baada ya shambulio la risasi kadhaa huko Dodoma. Kwa sasa Lissu yupo
nchini Ubelgiji kwa matibabu, lakini japo Lowassa alimtembelea alipokuwa
hospitalini Nairobi, Magufuli hakuwahi kutia mguu kumjulia hali mwanasiasa huyo
ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa upinzani bungeni na Rais wa Tanganyika Law
Society (TLS).
Kwahiyo
japo pongezi za Lowassa kwa Magufuli zinaweza kuwa na uzito, mapungufu ya
utawala wa rais huyo wa awamu ya tano, hususan kuhusiana na chuki na uonevu
dhidi ya vyama vya upinzani, hususan Chadema, yalipaswa “kumzuwia” kada huyo wa
zamani wa CCM kumwaga pongezi hizo.
Kibaya
zaidi, imebainika kuwa Lowassa alishawahi kumwomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mrisho Gambo amsaidie kukutana na Magufuli. Hata hivyo, Gambo alipotamka hilo
hadharani, Lowassa “aliruka kimanga.”
#OMG! So this was actually true. Uzuri wa hii drama ya leo kuhusu Lowassa inathibitisha kuwa sie tuliojivua ushabiki wa Chadema (baada ya ujio wake huko) tulikuwa sahihi. I hope waliotutukana watapata ujasiri wa kutuomba msamaha pic.twitter.com/pctNKaXnaU
Hata
hivyo, jana Magufuli alitamka bayana kuwa Lowassa aliomba mara kadhaa kukutana
naye. Kwahiyo, alichosema Gambo kilikuwa kweli, na Lowassa hakuwa mkweli
alipokana kuwa hajaomba kukutana na Magufuli.
Tukio
hilo la Lowassa kukutana na Magufuli na kumwagia pongezi limepokelewa kwa hisia
tofauti. Wakati kuna kundi dogo la wana-Chadema waliopongeza hatua hiyo, kwa
mfano “kada” mmoja wa chama hicho Yericko Nyerere, wengi ikiwa ni pamoja na
baadhi ya viongozi wamepingana waziwazi na Lowassa.
Wakati
Yericko aliandika haya
Mbunge
maarufu wa Chadema, Godbless Lema alikuwa wa kwanza kueleza bayana kutoafikiana
na pongezi za Lowassa kwa Magufuli.
Mh Lowassa,umeikosea Tanzania kwa kauli baada ya kutoka Ikulu,mema yapi umeyaona katika Serikali hii?Wkt Mbunge Lissu bado anauguza majeraha ya risasi,maiti zinaokotwa,Uchumi unaanguka,Benki zinafungwa ,demokrasia imekufa Bungeni /Nje ya Bunge na Sioi mkwe wako bado yuko Magereza
Baadaye, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema,
Freeman Mbowe, naye alieleza kuwa kauli za Lowassa ni zake binafsi na sio
msimamo wa chama hicho.
"Alichokisema Lowassa leo alipotembelea Ikulu ya Tanzania ni msimamo wake binafsi na wala sio msimamo wa CHADEMA" ~ Freeman Mbowe leo, ameyasema hayo akihojiwa na DW- Idhaa ya Kiswahili jioni hii. pic.twitter.com/WUjOo9qocL
Kadhalika, Mbowe alionekana kumkumbusha Lowassa kuhusu matukio mbalimbali yasiyopendeza katika utawala wa Magufuli
"Kumekuwepo na matukio ya watu kuuawa na kupotea, demokrasia na haki za binadamu zinaminywa, uchumi unazidi kudidimia. Katika mazingira hayo, tunashindwa kuelewa unapata wapi ujasiri wa kuisifu serikali ya Rais Magufuli."- M/Kiti CHADEMA, Freeman Mbowe (Mb) pic.twitter.com/AVXmnNMqg0
Lakini
pengine aliyeeleza kwa kirefu kuhusu suala hilo ni Lissu, ambaye akiwa
hospitalini huko Ubelgiji, alitoa waraka huu hapa chini.
Waheshimiwa
habari za Tanzania na poleni kwa yote.
Naomba
na mimi niseme kwa uchache kuhusu suala hili. Samahani kama 'uchache' wangu
utakuwa mrefu kidogo.
Baada
ya Mwenyekiti kuzungumzia jambo hili, inaelekea kuwa wazi kwamba Mheshimiwa
Lowassa hakumshirikisha Mwenyekiti kabla ya kukubali au kuamua kwenda Ikulu
kukutana na Rais Magufuli.
Na
juzi tu wakubwa wetu hawa wawili walikuwa pamoja hospitalini kumsalimia Mzee
Ngombale Mwiru.
Je,
inawezekana Mheshimiwa Lowassa hakuwa anajua tayari kwamba ana appointment
Ikulu?
Kama
alikuwa anajua, kutokumshirikisha Mwenyekiti wake kuna tafsiri gani hasa?
Katika
mazingira ya sasa ya Tanzania ya Magufuli, uamuzi wowote wa kufanya nae
mazungumzo, hata kwa nia njema yoyote ile, bila kushauriana au kuwashirikisha
viongozi wa juu wa chama, ni uamuzi usio sahihi na mgumu kukubalika.
Vile
vile, kauli za aina ambayo tumeisikia leo kutoka kwa Mheshimiwa
Lowassa, zina athari kubwa kisiasa.
Sio
tu zinachanganya wanachama na wafuasi wetu, lakini pia zinawapa mtaji wa
kisiasa maadui zetu.
Kuanzia
sasa tutegemee sana kuwasikia maCCM yakishangilia 'busara' za Mheshimiwa
Lowassa.
Masuala
ya ukiukwaji haki za binadamu, uvunjwaji wa Katiba na mengine mengi sasa
yatajibiwa kwa namna moja: Lowassa amemkubali Magufuli nyie wengine mnapiga
kelele za nini.
Huu
ni mtaji wa bure kwa Magufuli. Ukweli, ambao umesemwa sana humu, ni kwamba
amefeli karibu katika kila jambo.
Hata
hiyo reli anayosifiwa nayo na Lowassa bado ni ndoto tu: nani ajuaye itajengwa
kwa hela za nani???
Za
Wachina kama tulivyoambiwa mwanzoni; au za Waturuki kama tulivyoambiwa baadae;
au za Afrika Kusini kama alivyosema mwenyewe anaenda kumwomba Zuma???
Kama
chama hatujawahi kukataa mazungumzo na Rais au kiongozi mwingine yeyote wa
serikali.
Na
hatukatai kuzungumza na Magufuli kuhusu matatizo mengi na makubwa yanayoikabili
nchi yetu.
Lakini
ni muhimu na lazima viongozi wakuu wa chama washirikishane na washauriane kabla
ya mazungumzo hayo.
Na
baada ya mazungumzo, ni lazima viongozi wakubaliane juu ya kauli za kutoa
hadharani kwa umma ili wote tuwe kwenye ukurasa mmoja.
Katika
mazingira ya sasa, ambako viongozi na wanachama wetu wanashambuliwa hadharani
kwa mapanga na hata kwa risasi, kumsifia Rais ni kumuunga mkono yeye na matendo
yake.
Katika
mazingira ya kesi nyingi za kutunga dhidi yetu, 'kazi nzuri' inayofanywa na
Magufuli ina maana gani hasa, kama sio kuhalalisha ukandamizaji tunaofanyiwa.
Katika
mazingira ambapo hata jumuiya ya kimataifa imeanza kuhoji mwenendo wa Rais
Magufuli, kutoa kauli kwamba 'anafanya kazi nzuri' ni 'kumtupia taulo' la
propaganda litakalomfichia madhambi mengi aliyowafanyia Watanzania katika miaka
hii miwili.
Kwa
vyovyote vile, kitendo cha Mheshimiwa Lowassa sio cha kunyamaziwa au
kuhalalishwa kwa hoja nyepesi nyepesi.
TUNDU
LISSU(MB).
Top of Form
Kadhalika,
kada maarufu wa kike wa chama hicho, Hilda Newton nae alieleza masikitiko yake
kutokana na kauli za Lowassa.
Bila kumung'unya maneno leo Mh @edwardlowassatz kanikwaza mpaka nahisi kupasuka
Yani kabisa umefunga safar unaenda kuongea na adui tena mwenye roho ya Ukatili alaf unamsifia??
Nmeumia sana mpaka machozi yamenitoka, Lowassa katukosea sana yani nchi ipo kwenye mkwamo wa kisiasa yeye anaenda kumsifia adui!!..@tundulissutz kashambuliwa kwa risasi, Serikali ipo kimya hakuna cha uchunguzi wala nin yeye kapata wapi ujasir wa kumsifia adui ??
Kama
alivyotahadharisha Lissu, ni wazi kwamba CCM watakuwa wamepewa “silaha” mpya
katika “kumpamba” Magufuli na “kuwapenda” wapinzani, kwamba “hata Lowassa wenu
anamkubali Magufuli.” Na ni rahisi kwa CCM kuonekana wana mantiki katika hoja
hiyo, kwa kudai “kama mtu muhimu kabisa kwenye chama chenu (yaani Lowassa)
ambaye ndiye aliyekuwa mpinzani mkuu wa Magufuli kwenye uchaguzi mkuu uliopita,
anamkubali mkuu huyo wa nchi, ninyi ni akina nani kumpinga?”
And guess what, Lowassa amewapatia CCM narrative muhimu sana: "hata @edwardlowassatz wenu anamkubali @MagufuliJP" and unless you missed your meds, you can't disagree with them.
Wakati
ni wazi kwamba uamuzi wa Lowassa kukutana na Magufuli, na kumwagia pongezi,
umezua “sintofahamu” huko Chadema, kuna masuala kadhaa ya muhimu yanayopaswa
kuangaliwa kwa makini kwa ajili ya mustakabali wa chama hicho.
Kwanza,
ni muhimu kwa viongozi na wanachama wa Chadema kutambua nafasi ya Lowassa katika
chama hicho. Wakati baadhi ya wachambuzi wa siasa – mie nikiwa mmoja wao –
wanaamini kuwa ujio wa Lowassa katika chama hicho ulikuwa na hasara zaidi
kuliko faida, jitihada zilizofanywa na chama hicho kumpigania mwanasiasa huyo
zimemjengea hadhi ambayo haipo kwa mwanasiasa mwingine yoyote ndani na nje ya
chama hicho.
Ikumbukwe
kuwa hadi wakati jina lake lilipokatwa na vikao vya CCM katika mchakato wa
kusaka mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho tawala, Lowassa alikuwa ndiye
mwanasiasa maarufu kuliko wote Tanzania. Yayumkinika kusema alikuwa mtu wa pili
kwa umaarufu baada ya marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Licha ya
kulazimika kujiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya Richmond,
Lowassa aliendelea kuwa mwanasiasa maarufu na mwenye nguvu kuliko yeyote yule
ndani ya CCM, hata zaidi ya Rais na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho wakati
huo, Jakaya Kikwete.
Na
japo kukatwa kwa jina la Lowassa huko CCM kulimpunguzia kidogo umaarufu wake
kwa siasa za Tanzania – ilikuwa kama miujiza kuona CCM ilikuwa na ujasiri wa
kukata jina la mwanasiasa huyo- alihamia Chadema akiwa na sapoti ya kutosha
kiasi japo si kubwa kama ilivyotarajiwa.
Japo
kuna “tuliopishana nae mlangoni” – kwa maana yeye alipoingia, sie tukatoka –
ujio wake ulipelekea kuwa mwanasiasa maarufu zaidi ya wote wa Upinzani. Na ndio
maana haikuwa vigumu kwake kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA.
Nimeeleza
kuwa baadhi yetu “tulipishana nae mlangoni” kwa sababu mie binafsi nilikuwa
naiunga mkono Chadema, si kama mwanachama bali ukweli kwamba kwa muda mrefu
nimekuwa nikijihusisha na harakati za mapambano dhidi ya ufisadi, na chama hicho
kilijitokeza kuwa championi wa mapambano hayo. Kwahiyo, “naturally” nilijikuita
nikikiunga mkono.
Hata
hivyo, ujio wa Lowassa katika chama hicho ulinikimbiza. Sababu kuu ni binafsi
zaidi, na nisingependa kuongelea hapa, lakini sababu nyingine ni kile
nilichotafsiri kama usaliti wa Chadema. Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2006, chama
hicho “kilimkalia kooni” Lowassa kumtuhumu kuwa ni fisadi, na ndicho
kilichofanya jitihada kubwa zilizopelekea mwanasiasa huyo kujiuzulu Uwaziri
Mkuu mwaka 2008.
Mmoja wa watu walionipa kiu ya uandishi asema "Lowassa anawaadhibu Mbowe,Lissu,nk kwa kumwita fisadi for 9 yrs." Mtu huyo ni Johnson Mbwambo
Sasa
bila hata kutumia jitihada kidogo tu za busara, chama kilichomwandama Lowassa
kuwa ni fisadi, kwa miaka 9 mfululizo, yaani 2006 hadi 2015, kilionekana kituko
kwa baadhi yetu tuliokuwa tukikiamini, kwa sababu, pamoja na mengine,
isingewezekana kutumia miezi mitatu (Julai 2015 Lowassa alipojiunga na chama
hicho hadi Oktoba wakati wa uchaguzi mkuu) kumsafisha vya kutosha.
Na
gharama ya ujio wa Lowassa ilikuwa kubwa. Moja kubwa zaidi ilikuwa lazima kwa
Chadema “kuitosa” turufu yake muhimu, ajenda ya vita dhidi ya ufisadi.
Ililazimika kufanya hivyo kwa sababu kuzungumzia ufisadi ilhali chama hicho
kimemkumbatia mwanasiasa kiliyemwita “baba wa ufisadi” kwa miaka 9 mfululizo
ingeonekana kioja.
Kadhalika,
kwa kumpokea Lowassa, Chadema ilikuwa haina jinsi ya kukwepa tuhuma kutoka CCM
kuwa chama hicho upinzani ni cha kifisadi kwa sababu ya kumkumbatia mwanasiasa
ambaye kilikuwa kikimuita fisadi. Jitihada za Chadema kujibu mashambulizi kuwa “kama
Lowassa ni fisadi mbona hajachukuliwa hatua,” zilikuwa hazina mashiko.
Lakini
jingine lililoipa jeuri CCM ni ukweli kwamba kwa chama hicho, Lowassa alikuwa
ni “makapi” sambamba na wanasiasa wengine waliomfuata huko Chadema. Hiyo
ilikipa chama hicho tawala “jeuri” ya namna flani. Na waliitumia vema kwenye kampeni,
kwamba “hawa jamaa si lolote si chochote. Yani wameshindwa hata kutafuta
mgombea wao wenyewe mpaka wakasubiri makapi kutoka kwetu ndo wakapata mgombea
urais.” Na pamoja na maneno hayo kuwa machungu, ndo ukweli ulivyokuwa.
Chadema
na UKAWA kwa ujumla walikuwa na takriban mwaka mzima wa kujipanga; kuafikiana
kuhusu mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo, na kumnadi, huku wakitumia “advantage”
ya “vita vya wenyewe kwa wenyewe” kati ya zaidi ya makada 40 waliokuwa
wakichuana kuteuliwa na CCM.
Badala
yake, kumbe tayari kulikuwa na makubaliano ya siri kati ya uongozi wa baadhi ya
viongozi wa juu wa Chadema kwamba wasubiri kutangaza mgombea wao hadi baada ya
mchakato wa CCM kupata mgombea wake, ka maana ya “kumhifadhia nafasi Lowassa
endapo jina lake litakatwa huko CCM.”
Kabla
ya kwenda mbali na makala hii ningependa nishauri Chadema irejee suala hilo la
Lowassa kuandaliwa nafasi ya kuwania urais japo wakati huo alikuwa CCM. Hatua
stahili zinapaswa kuchuliwa dhidi ya wote waliohusika na mpango huo.
Na
ujio wa Lowassa ulipelekea Chadema kumpelekea mmoja wa magwiji wa siasa za
upinzani, Dokta Willbrord Slaa. Umahiri wa Dokta Slaa haukuwa tu katika
kuchukia ufisadi kwa dhati bali umahiri wake mkubwa katika kujenga hoja kisomi.
Kadhalika, alikuwa akiaminiwa na watu mbalimbali muhimu ndani ya serikali,
kiasi kwamba baadhi yao walihatarisha ajira zao kwa kumpatia mwanasiasa huyo
nyaraka muhimu zilizoiwezesha Chadema kuwa na ushahidi mbalimbali katika vita
yake dhidi ya ufisadi.
Na
kuonyesha kuwa alikuwa na msimamo imara, Dokta Slaa aliamua kujiweka kando katika
uongozi kupinga Lowassa kupewa ugombea urais wa UKAWA. Lakini jambo la
kusikitisha mno, kiongozi huyo aliyekifanyia mengi chama hicho alidhalilishwa
na kutukanwa kupita kiasi.
Na
“akina sie” tulishindwa kustahimili ujio wa Lowassa, na kwa vile kwa baadhi
yetu ilikuwa muhimu kumzuwia asiingie Ikulu, na hivyo kulazimika kumpigia
kampeni mpinzani wake yaani Magufuli, tulitukanwa kila aina ya matusi. Sijui
watu hawa waliojitoa ufahamu wataweka wapi sura zao pindi Lowassa “akirejea
nyumbani” CCM.
Wakati
anajiweka kando na uongozi wa Chadema, Dokta Slaa alikitahadharisha chama hicho
kuwa ili kuleta mabadiliko ya kweli (badala ya hayo “ya kisanii” aliyokuwa
akiyanadi Lowassa) chama hicho kinahitaji mkakati makini utakaoongozwa na watu
makini. Na kwa hakika, tangu wakati huo, Chadema imekuwa kama kundi la
wanaharakati wa kudandia hoja kuliko chama cha siasa chenye ajenda ya
kueleweka. Uamuzi wa kuitelekeza ajenda ya vita dhidi ya ufisadi ulipelekea chama
hicho kutokuwa na ajenda moja ya maana, huku CCM “wakipora” kiurahisi ajenda ya
vita dhidi ya ufisadi.
Je
mustakabali wa Chadema ukoje? Japo sio rahisi sana kubashiri kwa uhakika kuhusu
hatma ya chama hicho, binafsi – kwa kutumia uzoefu wangu na uelewa wa kutosha
wa siasa za Tanzania, sambamba na kuwa na fursa ya kufahamu “yanayojiri nyuma
ya pazia” la siasa za nchi yetu – ninadhani kuwa kuna uwezekano mkubwa tu kwa
Lowassa kurudi CCM kama sio kuachana kabisa na siasa.
Kwanini
Lowassa anaweza kurudi CCM? Kuna sababu kuu mbili. Moja ni dalili za wazi kuwa
ndoto zake za urais kupitia chama hicho ni kama zimeyeyuka. Umaarufu wake
umegubikwa na kuibuka na kuimarika kwa umaarufu wa Lissu. Ni dhahiri kwamba
ikipigwa kura ya maoni kuwa nani kati ya Lowassa na Lissu awe mgombea urais kwa
tiketi ya Chadema mwaka 2020, Lissu ataibuka mshindi. Na Lowassa anafahamu kuwa
hakuna njia ya mkato kwa yeye “kulazimisha” awe mgombea katika uchaguzi mkuu
huo ujao, licha ya ukweli kwamba alishatangaza kuwa atagombea.
Sababu
nyingine ni binafsi zaidi. Lowassa ni mmoja wa matajiri wakubwa nchini
Tanzania. Kama utajiri huo ulipatikana kihalali au kifisadi, si lengo la makala
hii kujiingiza katika mjadala huo. Lililo wazi ni ukweli kwamba licha ya kuwa
mwanasiasa, yeye pia ni mfanyabiashara. Na kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika,
serikali ya Magufuli imefanikiwa kutumia nyenzo yake muhimu dhidi ya wapinzani
ambao pia ni wafanyabiashara, KODI.
Inaelezwa
pia kwamba mali mbalimbali za mwanasiasa huyo zipo hatarini kutokana na uwepo
wake huko Upinzani. Inadaiwa kuwa hata jengo la Tanesco Ubungo ambalo serikali
imetangaza kulivunja, linamilikiwa na Lowassa, na tishio la kulivunja lilikuwa
kama kufikisha ujumbe kwake.
Katika
hili, Lowassa hatoonekana mtu wa ajabu akiamua kurudi CCM ili asibughudhiwe
kuhusu biashara na mali zake. Ni nani kati yetu anayeweza kujitoa mhanga kwa
ajili tu ya imani yake ya siasa? Si kama hawapo ila ni adimu mnooo! Na kibaya
zaidi, hata akiamua kung’ang’ania huko Chadema, hatma yake na ya chama hicho haieleweki
kwa sababu hadi muda huu – na hii ni licha ya zuwio la Magufuli dhidi ya vyama
vya upinzani kufanya shughuli zao za siasa – chama hicho kikuu cha upinzani “kipo
kipo” tu. Hakina ajenda moja ya kueleweka zaidi ya kudandia kila tukio
linalojiri.
Iwapo
Lowassa ataamua kubaki Chadema, hiyo itakuwa fursa mwafaka kwa chama hicho
kumpumzisha. Naamini kuwa wana-Chadema wakiweka kando ushabiki wa kisiasa,
wanafahamu fika kuwa mwanasiasa huyo hana nguvu, uwezo wala mvuto wa
kukabiliana na siasa hatari zinazoendelea muda huu huko nyumbani.
"Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, atangaza kurejea CCM. Asema anaridhishwa na uchapakazi wa Rais Magufuli"#FutureTweet#MarkThisTweet [Future Tweet ni tweet ya kufikirika japo yaweza kuwa kweli] pic.twitter.com/DiiKxtbwj3
Kwa upande mwingine, tukio la Lowassa kukutana na Magufuli Ikulu linaweza pia kuhusishwa na tamko la hivi karibuni la Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, ambaye kama Lowassa, alimmwagia sifa Magufuli.
Je kuna disconnect kati ya baadhi ya viongozi wakuu wa upinzani na wengi wa wafuasi wa vyama hivyo? pic.twitter.com/IkA9566Oop
Nimefanya uchambuzi kuhusu kauli za wanasiasa hao wawili hapa, lakini ninachoweza kugusia hapa ni haja ya kutambua kuwa wanasiasa hao bado wanatunzwa na serikali kutokana na nyadhifa walizowahi kushika huko nyuma. Haihitaji uelewa mkubwa kuhusu "siasa za kibabe" kuhisi kwamba huenda "malezi" wanayopewa na serikali yametumika kama "chambo" cha kuwavuta karibu na Magufuli. Kuhusu matatizo yanayoikabili Chadema muda huu,ukweli ni kwamba ni zaidi ya uwepo wa Lowassa ndani ya
chama hicho. Japo huu ni ukweli mchungu usioruhusiwa kabisa kusikika ndani ya
chama hicho, licha ya kazi nzuri ya kuifikisha Chadema ilipo leo, mwenyekiti wa
taifa Mbowe anapaswa kutoa fursa kwa wana-Chadema wengine kusukuma gurudumu la
chama hicho. Na hatua hiyo wala haihusiani na mchango wake mkubwa wa kumleta
Lowassa ndani ya chama hicho na “kumpa” ugombea urais wa UKAWA.
Kirefu
cha Chadema ni Chama cha DEMOKRASIA na Maendeleo. Sasa ni demokrasia gani hiyo
ambayo inaruhusu mwenyekiti mmoja kuwa madarakani milele? What if “uenyekiti wa
milele” ni miongoni mwa vikwazo kwa maendeleo ya chama hicho?
Lakini
hata kama “muda wa Mbowe kutoka madarakani haujafika,” busara tu inapaswa
kumfahamisha kiongozi huyo kuwa ni vema kuzingatia busara za akina Nyerere
waliojing’atua wakiwa bado wanahitajika. Sipendi kubashiri hili, lakini laiti
Mbowe asipohamasisha mageuzi kwenye medani ya uongozi wa chama hicho, haitokuwa
jambo la ajabu akiishia kung’olewa kwa nguvu.
Na
kwa bahati mbaya kwake, hili “songombingo” alilolianzisha Lowassa jana linaweza
kuwa kama mnyororo mrefu ambao mahala flani yupo Mbowe. Ndiye aliyemkaribisha
Lowassa.
Moja
ya mapungufu makubwa mno yanayoitafuna Chadema muda huu ni pamoja na kulipuuza
kundi muhimu linalokisaidia mno chama hicho, lundo la vijana wanaoshinda na
kukesha katika mitandao ya kijamii wakijaribu kukinadi chama hicho angalau kwa
kuikemea serikali ya Magufuli au CCM kwa ujumla.
Laiti
chama hicho kingekuwa na ajenda ya kueleweka, basi jeshi hili la vijana
lingekuwa nyenzo muhimu mno. Ni rahisi kuwalaumu vijana hawa kuwa “kazi yao
kubwa ni kudandia hoja tu,” lakini ukweli ni kwamba chama chao hakiwapatii
ajenda ya/za kueleweka. Kibaya zaidi, hata pale wanapojaribu kutengeneza ajenda
wao wenyewe – kwa mfano jitihada za kumsaka Ben Saanane – hawapati sapoti ya
kutosha kutoka uongozi wa juu wa chama hicho.
Ni
hivi, wengi wa hawa vijana wanahatarisha maisha yao kwa kuwa tu “upande usiotakiwa”
na serikali ya Magufuli. Hawategemei malipo yoyote zaidi ya kuamini kuwa siku
moja wanaweza kukiingiza chama chao madarakani. Hakuna jitihada za makusudi za
uongozi wa juu wa chama hicho kuwa karibu na kundi hili muhimu.
Ukiwa
UVCCM una uhakika wa angalau “kuhongwa na Bashite” au kualikwa kwenye “mnuso”
sehemu flani. Lakini ukiwa kijana wa upinzani, “zawadi” kubwa yaweza kuwa
kusumbuliwa na vyombo vya dola na kuishi maisha ya wasiwasi. Kwahiyo vijana wa
upinzani wana kila sababu ya kuichukia siasa, kwa sababu inahatarisha maisha
yao, lakini mapenzi yao katika imani ya chama inawalazimisha kung’ang’ania
hivyo hivyo.
Niionye
Chadema kuwa katika zama hizi za “ununuzi wa binadamu kama zama za utumwa,”
chama hicho kisishangae pindi wengi wa vijana hawa watakapoamua kubwaga
manyanga na kukubali “kununuliwa.” Kwanini waendelee kuhatarisha maisha yao
ilhali uongozi wa juu wa chama hicho hauna muda nao?
Akina
Hilda Newton, Ben Malisa, Bob Wangwe, Ndehani Mwenda, Noel Shao, Gift Nanyaro
ni miongoni mwa vijana wanaofanya kazi kubwa kwa ajili ya Chadema, bila ya
matarajio ya malipo au fadhila flani, zaidi ya kuhatarisha maisha yao. Kama
ilivyo kawaida ya mwanadamu yeyote yule, inaweza kufika mahala mtu akarudi
nyuma na kujiuliza, “is it worth it?” Na japo sitarajii kuona makada hao vijana
wakiamua kuipa kisogo Chadema, lakini sintoshangaa baadhi yao wakiamua kuipa
kisogo siasa, hasa kama tasnia hiyo itaendelea kuwa “yenye manufaa kwa genge
flani tu.”
Nihitimishe
makala hii kwa kukuhamasisha msomaji kujipatia nakala yako ya kitabu changu kipya
cha kielektroniki kinachochambua kwa kina miaka miwili ya utawala wa Magufuli.
Baadhi
ya niliyaoyazungumzia kwenye makala hii yamezungumwa kwa kirefu katika kitabu
hicho ambacho hakielemei upande wowote. Kitabu hicho kwa sasa kinasubiri
uzinduzi rasmi utakaokiwezesha kununulika kwa “mobile money” kama m-pesa,
tigopesa,nk. Nitawataarifu. Ila kwa wasiohitaji kusubiri, waweza kukinunua HAPA
Jana, Septemba 07, 2017, majira ya mchana, zilipatikana taarifa kwamba Tundu
Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Mbunge wa Singida Mashariki, Mnadhimu wa
Kambi Rasmi ya Upinzani, na Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), amepigwa risasi
kadhaa na kujeruhiwa vibaya.
Tukio hilo la kutisha lilitokea jijini
Dodoma, wakati Mbunge huyo aliposhuka nyumbani kwake eneo la Area D,
inakoelezwa alienda kwa ajili ya kujipatia mlo wa mchana.
Kabla ya kuingia kiundani kwenye makala hii, nitumie fursa hii kutoa salamu
za pole kwa Lissu, na kumwombea apone haraka. Salamu za pole pia kwa viongozi,
wanachama na wafuasi wa Chadema, chama ambacho Lissu amekuwa akikiwakilisha kwa
ufanisi mkubwa.
Pia ni vema nitahadharishe mapema kwamba intelijensia sio sayansi timilifu
kwa asilimia 100, kwa kimombo wanasema “intelligence is not an exact science.”
Okey, sasa tuingie mtamboni. Hadi muda huu kuna dhana za msingi tatu ambazo
zinatokana na‘mchujo’ wa dhana mbalimbali.
Dhana ya kwanza na ambayo pengine ni maarufu zaidi ya zote ni kwamba
jaribio hilo la mauaji ya Lissu lina mkono wa dola. Kwamba sio siri kuwa Lissu
amekuwa ‘akiisumbua mno’ serikali, ambapo wafuasi wake wanamwona kama jasiri
asiye na uoga wa kusema ukweli, ilhali wapinzani wake wakimwona kama mchochezi.
Yayumkinika kuhitimisha kwamba kama kuna mwanasiasa wa upinzani ambaye
amekuwa ‘mwiba mchungu’ kwa serikali ya Rais John Magufuli basi si mwingine
bali Lissu.
Na pengine kinachoongeza uzito kwenye dhana hii ni ukweli kwamba Agosti 18
mwaka huu, Lissu aliwaeleza wananchi kwamba anafuatiliwa.
Namnukuu "Naomba kabla sijaanza
Mazungumzo yangu nimuombe Mkuu wa idara ya Usalama wa Taifa anaitwa Kipilimba
au Inspekta Generali wa Polisi Simon Sirro, wale vijana ambao wamewatuma na kwa
wiki tatu mfululizo wananifuata kila nilipo wanaotembea na gari ya Toyota premio
namba T460CQV, jana niliwakaba Kanisani St. Peter's.”
Kwa upande mwingine serikali ya Magufuli ni kama ilikuwa inatafuta ‘kulaumiwa
bure.’ Kwa sababu, Hadi muda huu hakuna sababu moja ya msingi kwa serikali hiyo
kuyafanya maisha ya wanasiasa wa upinzani yawe magumu kiasi hiki. Magumu kwa
maana ya kuwanyima kila aina ya fursa ya kufanya siasa (political space).
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, zaidi ya viongozi na wafuasi 400 wa Chadema
wameshakamatwa tangu Magufuli aingie madarakani. Mtu atayedai kuwa kiongozi
huyo ‘anawachukia wapinzani’ hatoonekana mtu wa ajabu japo huenda akatupwa jela.
Katika hotuba zake mbalimbali, Rais Magufuli ameshindwa kuficha hisia zake
dhidi ya upinzani na wapinzani. Juni 12 mwaka huu, Rais Magufuli alimweleza
Spika Job Ndugai maneno yafuatayo
“Tumia mbinu hiyohiyo ya
kuwafanya wasiropokee Bungeni, waropokee nje na kule tutadili nao vizuri
kwasababu wanapokua kule ndani wana kinga wanaweza wakatukana chochote, sasa
kinga wanayoitumia vibaya bungeni kainyooshe wewe. Wawe wanatoka kule bungeni,
ukishamfukuza hata mwezi mzima… atakuja aropokee huku, na mimi nakueleza waache
waropokee huku nitadili nao, wala siwatishi lakini hatuwezi kuwa kwenye vita
wewe unaanza kugeuka kupiga wale wanaokwenda mbele…. ni nafuu unyamaze ukalale.”
Kwa kuangalia jinsi watendaji wa serikali ngazi za mkoa na wilaya
wanavyochuana na polisi kuwanyanyasa wapinzani, hususan wa Chadema, dhana kuwa
serikali ina mkono katika jaribio la mauaji ya Lissu ni kama ‘ready-made.’
Hata hivyo, pamoja na ‘dalili zote’ kuashiria uwezekano wa mkono wa
serikali katika jaribio la kumuua Lissu, dhana hii inakosa mantiki kiuhalisia.
Ni kwamba hakuna tija kwa serikali kumuua Lissu. Sawa, sio siri kuwa uhusiano
kati ya serikali na Lissu/ wapinzani sio mzuri, lakini haitokuwa na tija yoyote
kwa serikali ya Magufuli kumuua Lissu.
Na hata kama ingekuwa lazima ‘aondoke,’ basi kuna ‘njia mwafaka zaidi’ za
mauaji ya watu maarufu (assassination), huku 'kifo cha ajali' ikiwa maarufu na rahisi zaidi.
Halafu kinachotatiza katika tukio la jana, na kinachopunguza zaidi nguvu ya
dhana kwamba ‘kuna mkono wa serikali,’ ni jinsi waliofanya shambulio hilo
walivyoonekana kama wanahitaji publicity ya kutosha. Kwanini? Jibu lipo kwenye
uchambuzi wa dhana ya tatu.
Dhana ya pili ni dhaifu kuliko nyingine mbili. Hii inahusisha mbio za urais
mwaka 2020. Kwamba kila siku Lissu amekuwa akijitengenezea mazingira ya mgombea
mwafaka wa Chadema/Upinzani katika uchaguzi mkuu ujao, wala halina mjadala. Sio
kwamba Lissu amekuwa hodari katika masuala mbalimbali kwa vile anataka urais
(hajawahi kutamka nia ya kugombea nafasi hiyo) lakini umahiri wake bungeni na
katika masuala ya kisheria na kitaifa kwa ujumla, unamfanya kuwa kipenzi cha
takriban kila mfuasi wa Chadema.
Dhana hii dhaifu inasema kuwa jaribio hilo la mauaji ni kazi ya wapinzani
wa kisiasa wa Lissu, hususan ndani ya chama chake.
Udhaifu wa dhana hii ni kwamba, kama ambavyo kwenye dhana ya kwanza, hakuna
tija katika kumdhuru Lissu hadharani. Kwamba hata kama kungekuwa na lundo la
wapinzani wa kisiasa wa Lissu huko kwenye chama chake, kwanini wafanye ‘operesheni’
hiyo waziwazi badala ya kuandaa mkakati wa siri?
Na kama ilivyokuwa kwenye dhana ya kwanza, hata kama wapinzani wa kisiasa
wa Lissu ndani ya chama chake wangekuwa wahusika, kwanini basi tukio hilo
lifanyike katika mazingira ya ‘kusaka publicity kwa nguvu’?
Hiyo inatuacha na dhana moja, ya tatu, na ya mwisho. Ya mwisho lakini sio
haba katika mantiki. Dhana hii inaeleza kwamba jaribio hilo la mauaji
limefanywa makusudi na kile wajuzi wa mambo wanaita ‘rogue elements.’ Hizi zilitusumbua sana katika utawala wa Awamu
ya Nne wa Rais Jakaya Kikwete. Rogue elements hizi zinajumuisha watumishi
halali wa vyombo vya dola wanaofanya shughuli zisizo halali. Nani anawatuma?
Hiyo ni habari nyingine.
Kuna kitu kinachofahamika kama ‘Deep state.’ Kila nchi ina tafsiri yake
kuhusu ‘deep state’ lakini tafsiri nyepesi kwa mazingira yetu ni ushirika wa
watu wenye nguvu katika serikali na jamii – mfano vigogo (hususan wa zamani) wa
vyombo vya dola, wafanyabiashara wenye uwezo mkubwa na wanasiasa kutoka upande
wowote ule, lakini zaidi chama kilichopo madarakani.
Dhana hii inaliona tukio la kujaribu kumuua Lissu kama njia rahisi ya
kuichafua serikali ya Rais Magufuli, ambayo kwa bahati mbaya/makusudi
ilishajitengenezea mazingira ya kulaumiwa pindi la kutokea likimtokea
mwanasiasa wa upinzani kama Lissu. Rais anaposhindwa kudhibiti ‘chuki zake’
dhidi ya wapinzani, anawapa nafasi nzuri ‘wabaya wake’ kutenda kitu kisha ikawa
rahisi tu lawama kuelekezwa kwake.
Ndio maana dhana ya kwanza – kwamba kuna mkono wa serikali ya Magufuli
kwenye jaribio la kumuua Lissu – inaonekana kama yenye uzito kwa vile "kuna
sababu ready-made.”
Dhana hii inapata uzito kutokana na ukweli kwamba Magufuli amejitengenezea
maadui wengi, wenye nguvu, na baadhi yao wakiwa viumbe hatari. Kuna watu
waliozowea kuishi maisha ya kifalme ambao sasa wanalazimishwa kuishi maisha ya
kawaida. Hawa watu wakipata upenyo wa kumdhuru Magufuli, hawatosita kufanya
hivyo.
Lakini kwa vile ni ‘vigumu mno’ (angalau kwa wakati huu) kufanikisha
jaribio la kumdhuru kiongozi huyo, njia nyepesi inaweza kuwa katika ‘kuua character
yake,’ ambayo bahati nzuri kwa ‘wabaya wake,’ sio nzuri sana.
Kumekuwa na malalamiko kadhaa hasa kutoka upande wa upinzani kumtuhumu
Magufuli kuwa ni dikteta. Na ukifuatilia mwenendo wa siasa zetu kwa muda huu,
sio siri kwamba kuna chembe chembe za udikteta. Kwahiyo, ni rahisi kwa ‘wabaya
wa Magufuli’ kutumia mwanya huo kujenga picha ya “serikali ya dikteta yamuua
mpinzani wake mkubwa.”
Na hilo linatuleta kwenye suala la publicity. Kwamba jaribio la mauaji hayo
liwe na mwangwi wa kutosha ndani na nje ya Tanzania. Mwangwi huo ni wa makusudi
ili uakisi taswira inayojengeka kuwa ‘Magufuli ni dikteta. Na madikteta
hunyanyasa wapinzani wao, na ikibidi hata kuwaua.’
Kwahiyo, kama kuna funzo kubwa kwa Magufuli katika tukio hili ni kuepuka
mazingira yaliyopo ya uhasama mkubwa dhidi ya upinzani hususan Chadema.
Kiongozi huyo anatambua fika kwamba kuna watu wapo radhi kufanya lolote lile
kumng’oa, na kwa vile ‘njia za kawaida’ sio rahisi, basi inakuwa ‘anything
goes,’ liwalo na liwe.
Na dhana hii ya tatu inaleta uhusiano kati ya tukio la jana la jaribio la
kumuua Lissu na lile la hivi karibuni la kuchomwa moto kwa ofisi za kampuni ya
uwakili wa IMMA. Kama hili la Lissu, tukio la moto nalo lilifanyika katika
mazingira ya kuvutia publicity, yaani kama kulikuwa na jitihada za makusudi za
kuushawishi umma kwamba “mnaona huyu dikteta Magufuli anakoelekea? Sasa
anachoma hadi ofisi wa ‘wabaya’ wake.”
Nihitimishe uchambuzi huu kwa kueleza bayana masuala mawili matatu. Kwanza,
lengo la uchambuzi huu mfupi sio kuingilia kazi za vyombo vya dola
vinavyoendelea na uchunguzi kuhusu jaribio la kumuua Lissu. Nimefanya uchambuzi
huu kama mtu mwenye uelewa wa masuala ya intelijensia na siasa za Tanzania
yetu, ikiwa ni pamoja na “yanayojiri nyuma ya pazia.”
Pili, lengo la uchambuzi huu sio kumshawishi mtu yeyote abadili mtazamo
wake kuhusu “nani ana/wanahusika.”
Mwisho, kama nilivyotanabaisha awali, tasnia ya intelijensia sio sayansi
kamilifu kwa asilimia 100 (intelligence is not an exact science). Kwa maana
hiyo, japo uchambuzi huu ni karibu kabisa na hali halisi, sio rahisi sana
kufikia hali halisi yenye uhakika wa asilimia 100.
Nimalizie kwa kumtakia afya njema Bwana Lissu huku nikiamini kuwa malaka
husika zitafanya kila jitihada kuwanasa wahusika, sio tu kwa minajili ya
serikali kujinasua bali ili Bwana Lissu atendewe haki.
Iliwahi kuripotiwa kuwa Mkurugenzi wa Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu, aliipinga Tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt Emmanuel Nchimbi kuchunguza mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi.Moja ya sababu alizotoa Lissu ni Tume hiyo kuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mstaafu Stephen Ihema,ambaye alimtuhumu kuwa na rekodi ya utendaji kazi yenye walakini.
Katika pitapita yangu mtandaoni, nimekutana na habari inayomhusu Jaji Mstaafu Ihema, ambapo alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii, na sasa kamati hiyo imevunjwa kutokana na kulalamikiwa mno kwa vitendo vya rushwa miongoni mwa wajumbe.
Binafsi nimeguswa sana na habari hii hasa kwa vile inahusu tuhuma za rushwa kwa kamati iliyokuwa inamjumuisha Jaji Mstaafu Ihema.Sasa tukiamini kuwa Jaji Ihema ameshindwa jukumu la ujumbe tu kwenye tume hiyo ya ushauri,kwanini tumwamini kwenye uenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa kifo cha marehemu Mwangosi?
Wakati ninawapongeza wanahabari waliojitokeza jana kuifahamisha bayana Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwa wanalaani vikali mauaji ya mwanahabari mwenzao yaliyofanywa na jeshi la polisi,ningependa kushauri kuwepo upinzani zaidi dhidi ya Tume hii ambayo kuna kila dalili kwamba itaishia kuwa kiini-macho tu.Awali,hofu yangu kuhusu Tume hiyo ilielemea zaidi Watanzania wameshashuhudia utitiri wa tume ambazo mara nyingi ripoti zake zimeishia kufungiwa maandazi na vitafunwa vingine badala ya kuwekwa hadharani//hatua kuchukuliwa.Wengi wetu tunakumbuka kuhusu tume ya milipuko ya mabomu huko Mbagala na Gongo la Mboto.Hadi leo hakuna kilichoelezwa kuhusu ripoti ya tume hiyo...and life goes on.
Je wewe ni mdau wa habari? Unapenda kuona uchunguzi wa kifo cha marehemu Mwangosi unafanywa independently na watu wasio na harufu ya utendaji kazi wenye walakini?Basi ungana na wanahabari kupiga kelele dhidi ya tume hiyo ya kisanii
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Dk Wilbrod Slaa akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.
Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.
Mbunge wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Singida Magharibi Mheshimiwa Tundu Lissu akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.
Mbunge Wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Ubungo Mheshimiwa John Mnyika akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.
Mbunge wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Mbeya Mjini Mheshimiwa Joseph Mbilinyi aka Mr II(SUGU) akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.
Viongozi wa chadema wakifurahia kadi nyingi za CCM zilizorudishwa leo jioni kwenye mkutano
Deo Munish Katibu mkuu wa BAVICHA akiteta jambo na mmoja aliyehudhuria mkutano wa CHADEMA Wa uzinduzi wa kampeni ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.
Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akiwaaga wananchi waliokuwa wamefurika makao makuu ya chama kinondoni walikofika wakitokea jangwani usiku huu
Mbowe akiwatania wanachama ofini kinondoni baada ya wananchi kuanza kudai chama kimfukuze John Shibuda.Alikuwa akijifanya hasikii wanachosema na hapa anajaribu kuwasikiliza zaidi.hata hivyo Mbowe aliwaondoa wasiwasi na kusisitiza kuwa chama kinao utaratibu wa kushughulika na viongozi wanaokiuka maadili ya chama na kuwaomba wawaamini kama viongozi kuwa wanaouwezo wa kulishughulikia jambo hilo na mengine
Mh.Mbowe na Mnyika wakiwa wamesimama kwenye gari wakati wa matembezi wakitoka kwenye mkutano
Aliyekua Mbunge wa Arusha Mjini(CHADEMA)Mheshimiwa Godbless Lema akiwa juu ya gari huku akishangiliwa na vijana jioni baada ya mkutano
Sehemu ya umati uliowasindikiza viongozi wa chadema toka jangwani hadi kinondoni.wamesambaa yapata saa 2 usiku.