16 Apr 2018






Africa Confidential Toleo la 28 Machi 2018


27 Machi 2018

Hatua za kidikteta za Magufuli zinakumbana na upinzani unaoongezeka lakini ndio Ameshika uelekeo huo na anatishia wanaomkosoa

Katikati ya muhula wake wa kwanza, Rais John Magufuli anakabiliwa na shinikizo. Huku akikabiliwa na tishio kubwa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vikundi vya kiraia, viongozi wa kanisa, na sasa vijana kwenye mitandao ya kijamii, anaonekana kufurahia mapambano hayo. Dola pia inatishiwa na makundi yenye silaha yaliyokuwa viongozi wa serikali na chama mkoani Pwani (MKIRU). Majibu ya serikali kukabiliana na changamoto hizo yametawaliwa na ukatili ambao haujawahi kuonekana kamwe, na kupelekea kulaaniwa kutoka kila upande.

Kuongezeka kwa vurugu za kisiasa, hasa wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni, kulipelekea lawama dhidi ya utawala wa mabavu wa Magufuli. Ubalozi wa Marekani ulitaka kufanyike uchunguzi kuhusu utekaji na mauaji ya kiongozi wa upinzani jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni. Umoja wa Ulaya baadaye ulionyesha wasiwasi wake kuhusu "mwenendo wa hivi karibuni unaotishia kanuni za demokrasia" baada ya polisi kutumia risasi katika maandamano ya Chadema katika mkesha wa siku ya kupiga kura Februari 17, hali iliyopelekea majeruhi watatu na kuuawa kwa mpita njia.

Wiki mbili baada ya matamko hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ilijibu kwa taarifa yenye kurasa tatu na nusu ikiyahusisha matukio ya huko MKIRU na "vikundi vya ndani na nje ya nchi vinavyochukizwa na jitihada za Magufuli kuondoa ufisadi, biashara ya mihadarati, ujangili, ukwepaji kodi na kujenga uwajibikaji."

Vikundi hivyo vyenye silaha, ambapo baadhi vinadaiwa kuwa na mahusiano na Al-Shabaab ya Somalia, vimewauwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na baadhi ya watendaji wa serikali. Tatizo hilo lilianza tangu mwaka 2014 lakini likafikia kilele mwaka 2017 baada ya operesheni ya kikatili ya vyombo vya dola kushambulia. Serikali inajaribu kuushawishi umma kwamba maandamano ya amani dhidi ya haki za kiraia na mauaji hayo ya MKIRU ni pande mbili za kitu kimoja. Ni watu wachache tu wanaoshawishika kuamini.
Katika ujumbe wao kwa msimu wa Kwaresma, maaskofu wa Katoliki walionya kwamba kuendelea kwa ukandamizaji wa kisiasa kutapelekea migawanyiko itakayohatarisha misingi ya kitaifa ya umoja na mshikamano. Walieleza kwamba kuzuwia shughuli za kisiasa sio halali na kunakiuka katiba. Kituo ch Demokrasia (TCD), ambacho huvileta pamoja vyama vya siasa kilitoa tamko la pamoja na viongozi wa Kikristo na Kiislamu kudai mapitio ya Katiba. Hii ilifuatiwa na kauli ya kuunga mkono ya vikundi zaidi ya 100 vya kiraia.

Jumapili ya Majivu Machi 25 ilishuhudia maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT) wakitoa tamko kali wakiilaani utekaji watu, utesaji watu, upoteaji watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya wanasiasa, mauaji yanayotokana na itikadi za kisiasa, vitisho, kesi za kubambikizwa, na unyanyaswaji wa raia unaofanywa na vyombo vya dola. Pia walitaka katiba mpya iwepo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. "Taifa huongozwa na katiba ambayo ndio msingi wa sheria zote", walisema. "Haiongozwi na ilani za vyama."

Pia kuna changamoto za kisheria. Mahakama Kuu inatarajiwa kusikia kesi mbili za kikatiba zilizoletwa na watetezi wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na Chama cha Wanasheria TLS, Umoja wa Watetezi wa Haki za Binadamu (the Tanzania Human Rights Defenders Coalition), na Taasisi ya sheria na haki za binadamu (the Legal and Human Rights Centre). Kesi zote zinaongozwa na Fatma Karume wa kampuni ya uwakili ya IMMA, ambayo ofisi zake zilichomwa moto Agosti mwaka jana. Akiwa anatoka kwenye familia yenye nguvu ya Karume, amekuwa mwiba kwa utawala uliopo madarakani. TLS inaongizwa na mmoja wa wateja wake, kiongozi wa Chadema Tundu Lissu, ambaye bado yupo Ubelgiji anakopata matibabu ya majeraha ya risasi kufuatia jaribio la kumuuwa.

Kumekuwa na ukosoaji ndani ya CCM pia. Nape Nnauye, mbunge aliyetimuliwa uwaziri mwaka jana, ametoa wito wa kuifanyia marekebisho Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) akieleza "kwa macho makavu" kuwa kama ambavyo taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa manufaa ya dola, pia imekuwa ikiitumikia CCM, inaendeshwa kisiasa.

Mbunge mwingine wa CCM, Hussein Bashe, ambaye awali hakufahamika kuwa na mtazamo huru, na aliongoza kampeni ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwania urais, naye ametokea kuwa mtetezi wa uhuru wa kujieleza na mawazo mbadala.

Haya na matamko mengine yanaashiria demokrasia ya Tanzania ipo katika kipindi kigumu. Akiongea kwenye shughuli ya TCD ambayo ilipelekea wito wa katiba mpya, Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kilutheri alitanabaisha kuwa kamwe hajawahi kuona polisi wakitumia risasi dhidi ya waandamanaji. "Nini kimebadilika?" aliulizwa.

Moja ya majibu kwa swali lake hilo ni "hakuna kikubwa (kilichobadilika)." Kunapokuwa na upinzani mkali kwenye chaguzi zilizopita, dola na chama tawala vimekuwa vikikimbilia kwenye ukatili. Kufanya vema kwa Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kulipelekea angalau miaka miwili ya ukatili. Ilianza Januari 2011 ambapo polisi walitumia risasi dhidi ya maandamano ya wafuasi wa Chadema Arusha.
Februari 2012, wanaharakati 16 wa haki za binadamu walikamatwa kwa kuunga mkono mgomo wa madaktari. Agosti mwaka huohuo, polisi walimuua kwa risasi muuza magazeti huko Morogoro wakati wa maandamano ya Chadema. Mwezi uliofuata, mwandishi wa habari Daudi Mwangosi aliuawa na polisi kufuatia kupigwa na bomu la kutoa machozi huku akiwa amekandamizwa chini na polisi. Katika mwezi huohuo, kiongozi wa maandamano ya madaktari, Steven Ulimboka alitekwa, akateswa na kuachwa ajifie mwenyewe kwenye msitu nje ya jiji la Dar es Salaam, tukio linalodhaniwa kufanywa na maafisa wa TISS. Baadaye mwaka huo huo, na pia Mei 2013, njia za kikatili zilitumika kukabiliana na maandamano yaliyoambana na wimbi kubwa la machafuko katika historia ya Tanzania.

CCM inakabiliwa na changamoto kubwa kudumisha utawala wake. Kwa kutoongelea suala la ufisadi mkubwa (katika kampeni zake za uchaguzi mkuu wa) mwaka 2015, ilitoa fursa kwa Chadema kupata mafanikio (ya kuridhisha) katika uchaguzi huo. Wimbo la ukandamizaji linaloendelea hivi sasa, linailenga Chadema, na pia linachangiwa na hofu kuhusu vikundi vyenye msimamo mkali vyenye silaha (kama ilivyokuwa huko MKIRU).

Sintofahaumu hiyo inaweza kueleza ukatili mkubwa uliotumika kukabiliana na kilichokuwa kikijiri katika mkoa wa Pwani. Miili kadhaa iliyofungwa kwenye 'viroba' iliyokutwa inaelea maeneo ya (Msasani) Peninsula jijini Dar es Salaam inaashiria jinsi hali ilivyokuwa.

Wizara ya Mambo ya Nje ilitoa tamko masaa tu baada ya tovuti ya African Arguments ya Royal African Society kuchapisha habari iliyoeleza kuhusu matumizi ya silaha za moto dhidi ya waandamanaji huko wilayani Rufiji katika ofisi za halmashauri ya mji.

Kwa kuunganisha vitendo vya vikundi hivyo vilivyokuwa vinavyotumia silaha (huko MKIRU) na upinzani dhidi ya mageuzi yanayofanywa na Magufuli, inatoa kisingizio kwa dola kutumia nguvu dhidi ya makundi yote mawili (vikundi vya MKIRU na upinzani dhidi ya Magufuli).

Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo aliwataka Watanzania kuwa wazalendo dhidi ya tishio kwa amani, umoja, uhuru na mshikamano. Kichekesho ni kwamba aliyasema hayo katika maadhimisho ya viongozi waliopambana na utawala wa mkoloni mwaka 1907 katika Vita ya Maji Maji. Jinsi dola inavyopambana na vurugu na upinzani inarejesha kumbukumbu za jinsi serikali ya mkoloni ilivyopambana na upinzani dhidi yake.

Mafanikio yoyote ya kuelezea kuhusu tishio linaloukabili demokrasia nchini Tanzania yatategemea zaidi makundi mbalimbali ndani ya CCM na tabaka tawala. Wanaoonekana kama wapinzani ndani ya CCM kama Nape na Bashe watabaki ndani ya chama hicho kwa gharama yoyote, wakicheza mchezo mrefu wa subira hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ambapo inatarajiwa Magufuli atamaliza muda wake.

Viongozi wa dini – Magufuli anajitambulisha kama Mkatoliki mcha Mungu – wanaweza kufanikiwa kumshawishi kupunguza matumizi ya vyombo vya dola dhidi ya upinzani. Lakini wanaharakati na wanasiasa wa upinzani wanafahamu fika kuwa kudhibitiwa kwa asilimia 100.

MHALAKI (SOCIALITE) AONGOZA MAPAMBANO KUPITIA MTANDAO WA KIJAMII WA INSTAGRAM

Mashtaka yanayofunguliwa na taasisi za kiraia na matamko ya viongozi wa dini ni kitu kimoja, lakini wito wa kufanyika maandamano unaotolewa na bloga mwenye makazi yake Los Angeles (Marekani), Mange Kimambi, ni changamoto tofauti kabisa kwa Magufuli. Kimambi amekuwa sura ya hadharani ya wito wa maandamano ya nchi nzima tarehe 26 Aprili dhidi ya Magufuli.

Akifahamika zaidi kwa masuala ya fasheni na habari zinazohusu watu maarufu, akaunti ya Instagram ya Kimambi imekuwa ikihamasisha na kuyapa umaarufu maandamano hayo, yanayotarajiwa kufanyika siku ya Muungano, ambayo ni kumbukumbu ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Kimambi anayedhaniwa kuwa anashirikiana na wanaharakati nchini Tanzania, anachukuliwa kwa uzito mkubwa na mamlaka za nchi hiyo. Akiongea kwenye tukio moja Machi 9 kijijini kwake Chato, Magufuli alisema "tusubiri na tuone wakiandamana, na watanitambua." Siku chache kabla, Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba aliwatuhumu waandaaji wa maandamano hayo kuwa wanapanga kuuwa watu na kisha kuvitupia lawama vyombo vya dola. Maonyo mengine yametolewa na angalau makamanda wa polisi wa mikoa saba. Inafahamika kuwa viongozi wa serikali na chama (tawala) wameelekezwa kuhamasisha upinzani dhidi ya maandamano hayo na tayari watu kadhaa wameshakamatwa.

Kimambi ni mwanaharakati ambaye haingekuwa rahisi zamani kumtarajia. Alipata umaarufu mwaka 2009 kupitia blogu yake ya 'U-Turn' ambayo ilikuwa ikisimulia kuhusu maisha yake kama mhalaki huko Dubai. Baadaye alihamia katika makazi yake ya sasa, Los Angeles, kabla ya kuanza kuiteka Instagram mwaka 2015, ambapo alimpigia Magufuli kampeni yenye ufanisi, licha ya yeye kushindwa kuteuliwa kugombea ubunge jimbo la Kinondoni.

Alimgeuka Magufuli takriban Mei 2016 ambapo alipinga vikali kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge. Anachanganya upinzani wa kisiasa na nguvu yake kama mhalaki anayeweza kumjenga au kumbomoa mtu kwa kutumia mitandao ya kijamii. Awali ilikuwa kuhusu picha zake binafsi na "selfies" lakini baadaye mabadiliko yakajitokeza. Kufikia mwishoni mwa mwaka 2016, akaunti yake ikawa sehemu kuu ya harakati za mtandaoni za upinzani dhidi ya serikali, na sehemu ya kuona nyaraka mbalimbali zilizovuja.

Akaunti yake imechukua nafasi ya Jamii Forums, jukwaa la maoni mtandaoni lililokuwa kitovu cha upinzani mtandaoni, na ambalo waanzilishi wake wanakabiliwa na kesi mahakamani na wamekuwa wakisumbuliwa na mamlaka kwa muda mrefu.

Huku akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 1.4* kwenye Instagram, uwezo wa Kimambi kuwafikia watu unawazidi wanasiasa wote wa Tanzania, japo kuna shaka kuhusu maandamano ya April 26. Kujitokeza kwa watu wengi kwenye maandamano hayo kutategemea uwezo wa waandaaji wake wa maandamano hayo nchini Tanzania, ambao wanaokabiliana na utawala usio na huruma – polisi watamwaga risasi kwa ajili ya kuuwa, kama ambavyo wamefanya huko nyuma.

Haitojalisha hata kama hakuna mtu atayejitokeza kuandamana Aprili 26. Kutoka umbali wa kilomita 26,000, Kimambi tayari ameweza kufanya zaidi ya kutikisa mkia wa chui kwa kutumia simu ya mkononi tu. Na laiti ikitokea asalimisha yeye mwenyewe, mara moja kukamatwa kwake kutakuwa tukio kubwa kabisa litakaloiweka Tanzania kwenye macho na masikio ya dunia nzima.

MAELEZO YANGU: Makala hii ni tafsiri ya neno kwa neno ya makala ya gazeti maarufu la duniani la habari za kuchunguza kuhusu bara la Afrika la AFRICA CONFIDENTIAL Toleo laMachi 28, 2018 lililokuwa na kichwa cha habari "Enemies Without And Within."

Nimejitahidi kadri nilivyoweza kufanya tafsiri ya karibu kabisa kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili. Ni vigumu kufanya tafsiri timilifu kwa asilimia 100 hasa pale mwandishi na mtafsiri ni watu wanaoongea lugha mbili tofauti. Ni rahisi kwa mtu aliyeandika mwenyewe kufanya tafsiri ya alichoandika kuliko kazi hiyo kufanywa na mtu mwingine.
* Idadi ya "followers" kwenye akaunti ya Mange kwa sasa ni watu milioni 1.8.






0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.