Showing posts with label KISWAHILI. Show all posts
Showing posts with label KISWAHILI. Show all posts

9 Jan 2017


Moja ya vipimo kuwa unaitumia vema mitandao ya kijamii ni idadi na aina ya marafiki unaotengeza kupitia mitandao hiyo. Binafsi, nimetengeneza marafiki wengi mno, wanaotoka kada mbalimbali za maisha: wanasiasa, wanataaluma, wasanii, wajasiamali, wakulima, wanafunzi/wanavyuo, na takriban kila kada ya watu.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana sio tu ninaiheshimu sana mitandao ya kijamii lakini pia huwa makini kulinda 'hadhi' yangu mtandaoni. Kadri unavyotengeneza marafiki wengi ndivyo unavyokuwa katika nafasi kupata madhara makubwa zaidi iwapo mtu atakuchafua. 

Mmmoja ya watu nilofahamiana kupitia mitandao ya jamii ni Mhadhiri wa chuo kikuu cha London (University of London), katika Shule ya Stadi za Asia na Afrika (School or Oriental and African Studies - SOAS).

Nilifahamiana na Dkt Hannah mwishoni mwa mwaka jana huko kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Na kilichotufanya tufahamiane ni kuvutiwa na mapenzi yake kwa Kiswahili. Kila siku, Dokta Hannah hutwiti 'neno la siku' (word of the day) la Kiswahili, kisha kulielezea kwa Kiingereza.

Awali nilidhani ana asili ya Tanzania au nchi inayoongea Kiswahili, kwa sababu Kiswahili chake ni fasaha kabisa. Ikabidi nimdadisi. Kwa mshangao mkubwa, kumbe mhadhiri huyu ni Mwingereza wa asili, na wala Kiswahili sio lugha yake ya asili. Alijifunza tu wakati anafanya tafiti zake huko Tanzania na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki. 

Licha ya kuwa mhadhiri, Dkt Hannah ni 'postdoctoral research fellow' (huu utakuwa mtihani wangu na wake kutafuta neno stahili la Kiswahili). Kwa kifupi, mtu anayefanya 'postdoctoral fellowship' ni mhitimu wa shahada ya uzamifu anayeendelea na tafiti za kitaaluma. 

Eneo lake kuu la utafiti ni jinsi lugha zinavyokutana na zinavyobadilika, mkazo wake ukiwa kwenye lugha za Kibantu katika eneo la Afrika Mashariki.

Kwa sasa anafanya utafiti kuhusu mabadiliko ya kisarufi katika lugha za makabila ya Tanzania na Kenya, yaani Kirangi, ki-Mbugwe, ki-Gusii, Kikurya, ki-Ngoreme, ki-Suba Simbiti.

Habari njema zaidi ni kwamba Dkt Hannah amekubali kushiriki jitihada za kuenzi, kudumisha, kuboresha na kukitangaza Kiswahili kupitia kampeni maarufu ya #ElimikaWikiendi. Taarifa zaidi kuhusu ushiriki wake zitatolewa wakati mwafaka. 

Tovuti binafsi ya Dkt Hannah ipo HAPA na unaweza kum-follow Twitter anatumia @itsthegibson

Orodha ya machapisho yake ya kitaaluma:
 

Book Chapters

Gibson, Hannah and Koumbarou, Andriana and Marten, Lutz and van der Wal, Jenneke (2017) 'Locating the Bantu conjoint/disjoint alternation in a typology of focus marking.' In: van der Wal, Jenneke and Hyman, Larry M., (eds.), The conjoint/disjoint alternation in Bantu. Mouton de Gruyter . (Trends in Linguistics. Studies and Monographs) (Forthcoming)
Gibson, Hannah and Marten, Lutz (2016) 'Variation and grammaticalisation in Bantu complex verbal constructions: The dynamics of information growth in Swahili, Rangi and siSwati.' In: Nash, Léa and Samvelian, Pollet, (eds.), Approaches to Complex Predicates.Leiden: Brill, pp. 70-109. (Syntax and Semantics)

Journal Articles

Gibson, Hannah (2016) 'A unified dynamic account of auxiliary placement in Rangi.' Lingua, 184. pp. 79-103.
Seraku, Tohru and Gibson, Hannah (2016) 'A Dynamic Syntax modelling of Japanese and Rangi clefts: Parsing incrementality and the growth of interpretation.' Language Sciences , 56 (2016). pp. 45-67.
Gibson, Hannah and Wilhelmsen, Vera (2015) 'Cycles of negation in Rangi and Mbugwe.' Africana Linguistica, 21. pp. 233-257.
Marten, Lutz and Gibson, Hannah (2015) 'Structure building and thematic constraints in Bantu inversion constructions.' Journal of Linguistics, 52 (3). pp. 565-607.
Gibson, Hannah (2015) 'The dynamics of structure building in Rangi: At the Syntax-Semantics interface.' Cambridge Occasional Papers in Linguistics, 8. pp. 41-55.
Gibson, Hannah (2013) 'Auxiliary placement in Rangi: A case of contact-induced change?' SOAS Working Papers in Linguistics, 16. pp. 153-166.

Book Reviews



22 Jan 2008

Usiku huu (kwa saa za hapa Uingereza) msanii wa Bongofleva,T.I.D,alifanya mahojiano mafupi na kituo cha runinga cha BEN cha jijini London,kuhusu ziara ya msanii huyo nchini hapa.Inapendeza kuona msanii kutoka nyumbani akihojiwa,lakini nahisi kulikuwa na tatizo kidogo katika mfumo wa mahojiano hayo ambapo kwa mtizamo wangu,nadhani mtangazaji alitaka interview iwe ya Kiswahili lakini T.I.D alijibu maswali mengi kwa "Lugha ya Mama" (kimombo),japo sina budi kumsifu kwamba aliimudu kwa kiasi chake.Pia sidhani kama mtangazaji huyo atajiskia vibaya iwapo atatokea mtu wa kuhoji kama alijiandaa vya kutosha kufanya mahojiano hayo au ilikuwa ni ghafla.Anyway,kuna clips mbili hapa nilizozirekodi kwa kutumia simu ya zamani kidogo,Sony Ericsson W810i lakini nadhani itakuwa imejitahidi kwenye ubora wa video.Enjoy


17 Apr 2006

KULIKONI UGHAIBUNI

Habarini za huko nyumbani.Naamini mambo yanakwenda vema.Hapa napo ni shwari tu japokuwa viama vyetu vya kawaida bado vinaendelea.Pengine utashtuka kusikia neno “viama” (umoja-kiama,wingi-viama).Ngoja niende moja kwa moja kwenye pointi.

Fikra nilizokuwa nazo wakati niko huko nyumbani,na ambazo nilikuwa nashea na jamaa zangu kibao,ni kwamba maisha ya Ughaibuni ni kama ya peponi:ardhi ya maziwa na asali,kama vitabu vya dini vinavyosema.Tabu ya kwanza niliyokutana nayo ni lugha.Si kwamba mie ni maimuna ambae lugha ya “kwa mama” haipandi.La hasha,lugha hiyo inapanda ki-sawasawa.Tatizo ni kwamba wakati nakuja hapa nilishazowea kuongea Kiswahili changu chenye lafidhi ya ki-Ndamba (ndio,mimi ni Mndamba kutoka Ifakara.Awije mlongo…).Uzuri wa Daresalama nilipokuwa naishi ni kwamba wewe ongea Kiswahili cha aina yoyote,lakini una hakika watu watakuelewa na mtasikilizana bila matatizo.Hapa “kwa mama” unaweza kwenda sehemu na ukawa unaongea kiingereza chenye lafidhi ya ulikotoka na watu wakaishia kukukodolea macho tu.Hawakuelewi unaongea nini.Unakwenda sehemu,unahitaji huduma fulani.Unamuuliza mhudumu hapo,anaonekana kutoelewa unachoongea.Anabaki kukuomba “sorry can you say that again?” (samahani,unaweza kurudia ulichokisema?).Basi hapo inabidi useme neno mojamoja tena taratibu ili muelewane.

Lakini tatizo la pili ni lile la kujisahau na kujikuta unaingiza maneno ya Kiswahili kwenye lugha yao,hasa pale mtu anapoonekana aidha hataki kukuelewa au ni mgumu wa kuelewa.Hebu fikiri,unakwenda dukani,unamwambia muuza duka “nipatie maji ya kunywa ya Kilimanjaro”,yeye anakuuliza “unasemaje anko?”,unarudia tena,na yeye anarudia kukuuliza unasemaje!Ikifika mara ya tatu kuna hatari ukataka kujaribu kumwelewesha muuzaji huyo kwa lugha ya kwenu.

Kama mawasiliano ni tatizo sugu basi kufanya shopping ni tatizo zaidi.Hili ni tatizo ambalo binafsi nakutana nalo takribani kila napoingia kwenye duka au supamaketi.Sijui tatizo ni hisia kwamba Mtanzania kama mimi sina uwezo wa kununua kitu dukani au vipi!Ile kuingia tu kwenye duka au supamaketi utakuta mlinzi anaanza kukuandama nyuma yako.Hofu ni kwamba labda utakwapua kitu na kuondoka nacho bila kulipa.Kichekesho ni kwamba wakati walinzi wa duka wanahangaika na wewe mtu mweusi,mateja ya kizungu yanatumia mwanya huo kukwapua vitu na kuchomoka navyo bila kulipa.Ndio,Ulaya kuna mateja kibao kama ilivyo huko kwetu.Ipo siku nitakupatia stori hiyo ya mateja wa Ulaya kwa kirefu.Mara nyingi utakuta hao wadokozi wanavizia mtu mweusi aingie dukani nao wakafanye vitu vyao kwa vile wanajua akili za walinzi zitakuwa kwako.

Kwenye mabasi nako wakati mwingine ni adha tupu.Utamkuta mtoto wa kizungu anakushangaa utadhani ameona muujiza flani.Kibaya zaidi ni pale mtoto huyo anapodiriki kumuuliza mama yake kama wewe ni mtu au sana mu.Si mchezo manake.Unaweza kutaka kurusha ngumi lakini ukikumbuka kilichokupeka Ughaibuni huko inabidi umezee tu.Watoto wengine waliolelewa ovyo huweza kudiriki kukugusa ngozi kisha kuangalia mikono yao kama imebakia na rangi nyeusi kwani kwao mtu lazima awe mweupe!

Haya wengi wenu mnaweza kuwa hamyajui si kwa sababu hayaripotiwi na BBC au Skynews bali ni kwa vile wengi wetu tulioko huku tukirudi nyumbani tunapenda kutoa stori nzuuri kuonyesha kuwa huku ni kuku kwa mirija tu,ardhi ya maziwa na asali,na kuficha viama tunavyokumbana navyo kila siku.

Hiyo ndio Ughaibuni,ndugu zanguni.Hata hivyo,naomba nisisitize kwamba viama hivyo havipo kila mji.Ile miji yenye wageni wengi au tuseme watu weusi wengi,kuna unafuu kidogo,japokuwa huko nako kuna viama kama vya umbeya,kusutana na hata kuagiziana mafundi (waganga wa kienyeji) kufanyiziana.Ukibisha kwamba watu wanaagiza wataalam kutoka huko nyumbani kuja kurekebisha mambo yao au kufanyiza kwa njia za asili basi nenda pale Buguruni kwa mwinjilisti flani ambae huja huku mara kwa mara kuhubiri neno la Bwana na kutoa pepo.Huyo ameshasikia maungamo na ushuhuda kadhaa wa hao waagizaji mafundi kutoka huko nyumbani.

Hadi wiki ijayo,Alamasiki

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.