Showing posts with label NYUMBANI. Show all posts
Showing posts with label NYUMBANI. Show all posts

7 Oct 2007

MTANZANIA UGHAIBUNI-2

Asalam aleykum,

Niseme bayana kwamba napenda sana kuangalia runinga kila nafasi inaporuhusu. Na kwa mazoea hayo, napenda kutamka bayana kwamba mara nyingi huwa nafahamu mengi ya yanayojiri katika sayari yetu hii. Lakini pia ni vema nikisema kwamba “mahaba” yangu kwa runinga huwa mara kadhaa yananiacha na maswali mengi kuliko ajibu, na kuna nyakati huwa nabaki na majonzi napoona namna wanadamu wenzetu wanavyosumbuka na kuteseka katika sehemu flani za dunia yetu. Ni mengi, lakini linalovuma sana kwa sasa hivi katika “channels” mbalimbali za ni namna utawala wa kidikteta huko Burma unavyoendesha kampeni zao za kimyama dhidi ya watu wasio na hatia ambao wamechoshwa na miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi. Inatia uchungu kuona picha za miili ya watawa wa Kibudha (Buddhist monks) iliyotelekezwa mitaani au inayoelea kwenye maji yote yakiwa ni matokeo ya mtangange kati ya vyombo vya dola vya nchi hiyo dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakidai demokrasia na kupinga udikteta. Inaumiza zaidi kuona kauli “za kisanii” za Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya au Marekani zinazodai kuwa “duni inaona unyama huo na haitavumilia” ilhali hakuna mikakati yoyote thabiti ya kuwapa matumaini watu wanaoteseka huko Burma kwamba siku moja wataamka wakiwa na amani ya kudumu. Ni hadithi zisizotofautiana sana na zile walizosikia wenzetu wa Rwanda wakati wa mauaji ya halaiki,au zile zinazoleta matumaini “hewa” kila kukicha huko Darfur au Somalia.Hili dude linalooitwa “Jumuiya ya Kimataifa” limezidi kuthibitisha kuwa ni la kufikirika zaidi kuliko lenye ufanisi kwani laiti lingetafsiri kauli zake katika vitendo basi kwa hakika dunia ingekuwa ni mahala salama sana.

Hivi runinga zingeendelea kutuonyesha picha hizi za kusikitisha sembuse nchi kama Marekani ingeamua kwa dhati kukomesha mateso yanayoendelea sehemu mbalimbali duniani?Hivi mamilioni ya waliokata tamaa na maisha ingeendelea iwapo tamaa ya mafuta katika seheu kama Iraki ingekuwa ajenda ndogo kuliko kapata haki halisi za binadamu katika sehemu zilizogubikwa na mateso duniani?Kwa hakika dunia ingeweza kabisa kuwa sehemu mwafaka ya kuishi kwa kila binadamu iwapo wale wenye uwezo wa kukomesha mateso hayo wangedhamiria kwa dhati kuhakikisha kwamba hakuna nafasi kwa madikteta kunyanyasa wale wasio na hatia.Nakubali kwaba ugaidi ni tishio kubwa kwa amani ya dunia yetu lakini kuna matishio mengine ambayo yanawaathiri wanadamu kila kukicha kuliko huo ugaidi,matishio hayo yakiwa ni pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu na rushwa zinazodumaza maendeleo ya nchi nyingi za dunia ya tatu licha ya misaada lukuki inayomwagwa kuzikwamua nchi hizo.

Mimi naamini kuwa nchi tajiri na zenye nguvu za kuamua namna gani sie maskini tuishi zina uwezo wa kukomesha uonevu huu.Hivi mabenki makubwa katika nchi hizo yangeamua kwa dhati kuwabana wale ambao wanawekeza mabilioni ya dola kwenye akaunti katika mabenki hayo (ilhali maelfu kwa maelfu ya wanaowaongoza ni maskini wakutupwa ) kwa kuwauliza tu swali jepesi la “mmepata wapi fedha hizi” isingesaidia kuwafanya wabadhirifu,wala rushwa na wezi wa raslimali kujiuliza mara mbilimbili kabla ya kuiba?Mjuzi mmoja wa wizi wa raslimali za baadhi ya nchi za dunia ya tatu alinieleza kwamba kwa kuhofia kutaifishwa raslimali zao,wezi wengi katika nchi hizo hupendelea kuweka fedha zao katika mabenki ya nje kwa vile huko ndiko salama zaidi.Mjuzi huyo alidai pia kwamba nchi na mashirika wahisani hawajali sana kuhusu vilio vya wanaoibiwa au kuwa na uchungu na misaada wanayotoa kwa vile wanafahamu fika kuwa fedha hizo haramu zitarudi mikononi mwao (wahisani) kupitia akaunti za siri za wezi hao.

Siku moja niliwahi kuulizwa na rafiki yangu mmoja Mkenya kwamba kwanini Tanzania ina amani zaidi kulinganisha na jirani zake.Nikamweleza kwamba pamoja na sababu nyingine ikiwa ni pamoja na hekima na busara za Baba wa Taifa za kuwaunganisha Watanzania na mchango wa lugha ya Kiswahili,sababu muhimu ni kwamba Watanzania licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120 ni kama watu wa ukoo mmoja.Sensa zetu huwa hazichanganui mwingiliano wa makabila huko nyumbani,lakini ni dhahiri kuwa zoezi hilo likijaribiwa litakuwa gumu sana kwa vile kuna mwingiliano mkubwa mno.Nikiangalia kwenye ukoo wetu nakuta kuna ninaowaita ndugu zangu ambao kimsingi asili yao ni makabila tofauti na asili ya ukoo wetu.Na hata hiyo asili yenyewe ya ukoo wetu inaweza kuwa ni ya jumlajumla tu (general) kwani historia inaonyesha kuwa mengi ya makabila ya kibantu yaliyopo huko nyumbani yapo yalipo sasa baada ya mtawanyiko wa Wanguni walioingia nchini kutokea sehemu nyingine.Mama yangu ni M-bena lakini makazi ya Wabena hawa ni Malinyi wilayani Ulanga.Na kuna Wabena wengine huko Iringa ambao kuna madai ya kihistoria kuwa hawa ni watu wa asili moja na hao Wabena wa Malinyi.Ngoja “nisichanganye madawa” (nisikoroge mambo) hapa.Hoja nayotaka kuitengeneza hapa ni kwamba mtu anaweza kufanya ubadhirifu akidhani anainufaisha familia yake pekee kumbe wakati huohuo anawaathiri ndugu zake wengine ambao kwa sababu za kihistoria wako katika makabila mengine.Laiti sote tungeangaliana kama Watanzania wenye asili zinazoshabihiana basi yayumkinika kusema kwamba baadhi ya wala rushwa na wabadhirifu wangeweza kuwa na huruma kwa ndugu zao.Lakini hata tusipoiangalia hoja hii ya umoja katika tofauti zetu (yaani kuwa katika makabila tofauti japo asili zetu zinashabihiana) kuna ukweli usiopingika kwamba kukwaza maendeleo katika kipindi hiki ni sawa na kuvichimbia makaburi vijukuu vitakavyokuwa vinahitaji baadhi ya huduma ambazo baadhi ya wabadhirifu wanazibinafsisha kuwa zao binafsi badala ya kujenga misingi ya vizazi vijavyo.Kuna wakati huwa nashindwa kupata majibu naposikia mtu amekwiba fedha za ujenzi wa mradi flani wa maendeleo japo ana watoto kadhaa katika familia yake na wengine kadhaa zaidi nje ya ndoa.Laiti mtu huyu angekuwa na akili basi ni dhahiri angetambua kuwa watoto wake lukuki aliokuwa nao sasa watamletea wajukuu baadae ambao nao wataleta watoto na wajukuu zaidi,na kwa maana hiyo kitendo chochote cha kukwaza maendeleo hivi sasa kitaathiri vizazi vyake vijavyo.Napenda kuamini kabisa kuwa yeyote yule mwenye upendo wa dhati na vizazi vyake vijavyo,achilia mbali vile vya wenzie,atafanya kila liwezekanalo kuitumikia nchi yetu kwa namna ambayo vizazi hivyo vijavyo havitapatwa na hasira za kubomoa makaburi yetu miaka 20 au 50 ijayo kwa hasira za kutengenezewa msingi mbaya wa maisha.Na kwa wale wanaoamini kuwa kuna moto wa kiyama baada ya kifo basi naamini watafanya kila wawezalo kukata tamaa zao za kidunia kwani bila kufanya hivyo watageuzwa kuwa kuni kwenye moto wa ahera.

Nimalizie kwa kuzungumzia kituko kimoja nilichokisoma katika gazeti flani la wiki iliyopita.Kituko hicho kinahusu kesi ya Profesa Mahalu,ambapo kwa mujibu wa gazeti hilo,wanasheria wa serikali wamekiri kuwa kesi hiyo “haina mwenyewe”.Nachojiuliza ni hiki,kama kesi haina mwenyewe sasa wao wanakwenda mahakamani hapo kumwakilisha nani!Hivi zile kesi za Jamhuri dhidi ya flani zimekufa siku hizi?Ningeelewa walichosema wanasheria hao wa serikali kama wangekuwa wametoka taasisi zinazotoa msaada wa kisheria,ambazo kimsingi zinaweza kudakia kesi yoyote ile kwa minajili ya kutaka haki itendeke.Mie sio mwanasheria,lakini pamoja na umbumbumbu wangu katika taaluma hiyo nadhani hawa waungwana wangeweza kabisa kuitaja Jamhuri kuwa ndio yenye kesi dhidi ya mwanadiplomasia huyo,hasa kwa vile wao ni waajiriwa wa Jamhuri na sio magazeti yaliyoibua madai hayo.Na iwapo walikuwa wakiamini kwamba chanzo za kesi hiyo ni hayo magazeti basi pengine ingeleta maana zaidi iwapo wangeyashawishi magazeti hayo kufungua kesi halafu wao wayasaidie katika kesi hiyo.Lakini pia kama wanadhani hakuna mlalamikaji katika kesi hiyo basi ni bora waachane nayo tu kwa vile kwa namna “wanavyowajibika” ni dhahiri kuwa huko mbele tutasikia vituko vikubwa zaidi ya hiki nachokielezea hapa.Kama dada yangu Freda anavyopenda kusema,hii ni kaaazi kweli kweli.

Alamiski






20 Jul 2007

Asalam aleykum,

Juzi nilipata barua-pepe kutoka kwa rafiki yangu mmoja aliyeko huko nyumbani.Huyu jamaa alikuwa akinilaumu “kirafiki” kwamba inaelekea nimeanza kuishiwa pointi za kuandika ndio maana takriban nusu ya makala yangu iliyopita ilikuwa ina habari “nyepesi nyepesi.”Sikukasirika kwani siku zote nathamini sana ushauri wenye lengo la kujenga au kuleta maendeleo.Nilimjibu kwamba nina pointi lukuki za kuandika,lakini kuna wakati inabidi “tupunguze kasi ya maisha” kwa kuangalia habari za vituko mbalimbali hususan vinavyojiri huku Ughaibuni.Pia nilimhakikishia kuwa “nyepesi nyepesi” hizo sio “fiksi” bali ni habari zinazohusu matukio ya kweli,ila tu yanachekesha kwa namna moja au nyingine.Kicheko ni afya.

“Nyepesi” za wiki hii ni pamoja na taarifa kwamba “wanene” 7 ndani ya baraza jipya la mawaziri la Gordon Brown (mrithi wa Tony Blair) wamekiri katika nyakati tofauti kuwa walishawahi kutumia “widi” (kwa wale ambao lugha ya mtaani ni mgogoro, “widi” ni bangi au marijuana).Siku kadhaa zilizopita,kiongozi wa chama cha wahafidhina (Conservative Party) David Cameron naye alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kupatikana nyeti kuwa alikuwa akivuta bangi katika siku za ujana wake.Cameron amekataa kuendelea na mjadala wa suala hilo akisema kuwa kila binadamu anaweza kufanya makosa hususan akiwa kijana.Alitaka wanaomshupalia wamhukumu kwa utendaji wake wa kazi wa sasa na sio mambo aliyofanya nyma.Kali zaidi ya zote ni pale Katibu wa Ofisi ya Mambo ya Ndani (Home Office-yaani ni sawa na Wizara ya Mambo ya Ndani huko nyumbani),Jacqui Smith,na waziri mmoja katika ofisi hiyo (hapa katibu wa wizara ni mkubwa kicheo kuliko waziri),Tony McNulty,walipotangaza hadharani kuwa nao walishawahi kuvuta bangi huko nyuma.Na “ushuhuda” huo umekuja wakati mwanamama huyo (Smith) akitangaza mpango wa serikali kuangalia upya uamuzi wa awali wa serikali ya Blair wa kushusha daraja (declassifying) la bangi.Habari kwamba viongozi hao wawili (ambao pamoja na majukumu mengine wana dhamana ya kudhibiti mihadarati) waliowahi kuwa wavuta bangi zimezua mjadala kama kweli wanapaswa kuendelea na nyadhifa zao.Pengine kinachowasaidia ni ukweli kwamba kuna wanasiasa wengine (wakiwamo mawaziri vivuli wa upinzani) ambao nao wameweka bayana kuwa walishawahi kuvuta bangi walipokuwa vijana.Uwazi na ukweli au vituko vya siasa?


Kuna habari nyingine ya majonzi lakini kwa namna flani inaweza inachekesha.Mwanamke aliyekuwa na uzito mkubwa kuliko wote hapa Uingereza,Nazima Hussein,amefariki na kuwaacha wanandugu wakiwa na wakati mgumu baada ya kubambikwa ushuru wa pauni 4,000 (zaidi ya shilingi milioni 8) kutoka kwa manispaa huko Southall,London.Ushuru huo ulitokana na gharama za kuuhudumia mwili wa marehemu ambao ulihitaji watumishi wa kikosi cha zima moto (firemen) 13 kuutoa mwili huo (uliokuwa na unene wa futi 3) kutoka katika flati aliyokuwa akaishi.Na walipoufikisha mochwari huko Uxbridge ilizuka kasheshe nyingine kwani hakuna toroli la kubebea maiti lililomtosha marehemu na pia mafriji yote ya kuhifadhia maiti hayakuweza kumudu ukubwa wa mwili wa marehemu huyo.Marehemu Nazima alifariki akiwa na uzito wa kilo 349 .Habari njema ni kwamba baada ya watu wa Manispaa “kusomeshwa” walikubali kupunguza gharama hadi pauni 3,000 (zaidi ya shilingi milioni 6).Ukiskia msiba mzito ndio huo.

Turejee nyumbani.Siku chache taifa limepewa changamoto ya kutosha kutoka kwa JK kuhusu suala la “kupima ngoma” (ukimwi).Na kwa mujibu wa taarifa za magazeti mbalimbali ya huko nyumbani watu kadhaa wameitikia wito wa Rais kwa kwenda kwenye vituo vya afya kupima ukimwi.Kwa mtizamo wangu,hamasa aliyotoa JK inaweza kuwa na matokeo makubwa sana kwani kwa upande mmoja inaweza kuwasaidia wale waliokuwa hawajui kama wameathirika kuanza kuchukua tahadhari ambazo zitawasaidia kuishi maisha marefu zaidi.Pia kwa wale ambao vipimo vitaonyesha hawajaathirika wanaweza kuachana kabisa na matendo ya ngono zisizo salama,na hata kumrejea Mola wao.Kadhalika,kwa wale watakaokutwa wana virusi vya ukimwi na wakati huohuo wana familia zinazowategemea wanaweza kupata nafasi mwafaka ya kuandaa “future” za familia zao.Jingine ni kwamba kampeni hiyo inaweza kuwafumbua macho wale vichwa sugu na viwembe wanaopenda kujidanganya kuwa ukimwi ni ajali kazini,na eti ajali haina kinga.

Waziri wa Afya amelielezea Bunge kuwa kuna mpango wa kuwapima ukimwi wale wote wanaofika hospitali kwa matibabu.Wazo hilo ni zuri sana lakini linahitaji tahadhari ya namna flani.Wapo wanaosema kuwa ukimwi ni sawa na maradhi mengine yasiyo na tiba kama kansa au kisukari.Hapana,ukimwi ni tofauti sana hasa kwenye namna jamii yetu inavyowaangalia walioathirika na ukimwi (unyanyapaa).Nadhani wapo watakaokubaliana nami kwamba baadhi ya watumishi wa taasisi za afya wana tabia ya kukiuka maadili ya taaluma yao kwa kutoa siri kuhusu afya za wagonjwa.Naamini baadhi ya wasomaji wameshawahi kunong’onezwa na dokta au nesi flani kuwa “yule nanihii anao (ukimwi).” Sasa kama Wizara ya Afya itatekeleza dhamira yake ya kutaka watu wote wanaofika hospitali wapime ukimwi inapaswa pia kuboresha mambo kadhaa ikiwa pamoja na kuhakikisha kuna washauri nasaha wa kutosha watakaoweza kuwasaidia hao watakaobainika kuwa “wanao.” Naamini pia kuwa kuna sheria inayowabana watumishi wa afya kutoa “siri” ya ugonjwa wa mtu,na katika mpango huu wa Wizara ni muhimu sheria hiyo ikaimarishwa zaidi kwani bila kufanya hivyo si ajabu watu wanaweza kukwepa kwenda hospitali sio kwa kuhofia kupimwa na kukutwa wanao bali kwa kuwaogopa hao wauguzi wasioweza kuhifadhi siri za wagonjwa.Pia Wizara inapaswa kuweka bayana iwapo mpango huo wa kumpima kila mgonjwa utakuwa ni suala la hiari au la lazima.Kwa hapa,wagonjwa wanahamasishwa kupima ukimwi lakini hawalazimishwi.Pasipo kuweka misingi mizuri,nia nzuri ya Wizara ya Afya inaweza kuleta mkorogano usio wa lazima,maana si ajabu tukasikia flani kanyimwa nafasi ya kuonana na daktari kwa vile tu kukataa kupima ukimwi.Ifahamike kuwa suala la kupima au kutopima ni haki ya mtu binafsi.

Pia nimesoma habari iliyonisikitisha husu kilio cha Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwamba imekuwa ikipata ushirikiano hafifu kutoka kwa waajiri katika suala la kuhakiki vyeti vya taaluma za waajiriwa.Unajua utandawazi umeleta mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na fursa ya mtu kujipatia taaluma bila kutia mguu chuoni.Vipo vyuo kadhaa duniani vinavyotoa kozi kwa njia ya mtandao,lakini tatizo ambalo limekuwa likizisumbua hata nchi za Magharibi ni lile la baadhi ya vyuo vya kitapeli ambavyo vinaweza kukupatia cheti cha Udaktari wa Falsafa kwa wiki moja.Ukiona mfumuko wa madokta (sio wale wa hospitali) usikimbilie kufikira kuwa pengine siku hizi PhD zimekuwa rahisi.Ukweli ni kwamba PhD feki zimetapakaa sana kutokana na vyuo feki (japo vingine vimeandikishwa kisheria) ambavyo wanachojali wao ni fedha tu ya huyo anayehitaji PhD ya chapchap.Inatuuma sana sie wengine ambao tunazeekea maktaba kutafuta huo udokta “wa kwelikweli” huku wenzetu “wanasomea baa au kwenye nyumba ndogo zao” na wanaamka asubuhi na “hangover” wakiwa madaktari wa falsafa.Nadhani falsafa pekee waliyonayo “vilaza” hawa ni kuhusu waganga gani wa kienyeji wanasaidia mtu kula rushwa na aendelee kuonekana mwadilifu au namna ya kutogonganisha magari kati ya mama watoto na nyumba ndogo.

Ukweli mchungu ni kwamba TCU ina wakati mgumu kufanikiwa katika azma yake hiyo njema,kwani wengi wetu tunajua kuwa baadhi ya waajiri nao wana elimu za kutilia mashaka.Pia nadhani kuna mapungufu ya kisheria kuhusu matumizi ya vyeti feki,kwani nakumbuka jeshi la polisi halikuchukua hatua yoyote lilipobaini kuwa mbunge mmoja hakuwa mkweli kuhusu elimu yake ya sekondari.Sasa kama ufeki wa vyeti vya sekondari “sio big deal” kwa polisi je hao wenye PhD feki wataweza kuguswa?Enewei,tuna vita kadhaa tunazopenda zianze dakika hii:dhidi ya wala rushwa,majambazi,wabadhirifu,wauza unga,nk.Pengine siku moja itatangazwa vita ya kitaifa dhidi ya vyeti na taaluma feki.Yote yanawezekana.

Alamsiki


22 Aug 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa gazeti hili maridhawa.

Leo nina mada nzito na nakuomba msomaji uifatilie kwa makini kwa manufaa ya Taifa letu.Labda kabla “sijaivaa” mada hiyo nitoe mfano mmoja wa hapa Uingereza.Miongoni mwa matatizo makubwa ya kijamii yanayoikabili nchi hii ni suala la matumizi ya madawa ya kulevya hususan miongoni mwa vijana.Watu wanabwia unga kama hawana akili nzuri.Kipindi hiki cha summer nacho kinasaidia kupata “jeshi jipya la wabwia unga" hasa kwa vile baadhi ya vijana huenda mapumzikoni (summer holiday) nje ya nchi wakiwa mbali na wazazi wao.Ukisimuliwa vituko vinavyotokea pwani za sehemu kama Hispania (kwa mfano Ibiza,Majorca na kwingineko) utabaki mdomo wazi.Hata hivyo,serikali na taasisi nyingine zimekuwa zikifanya jitihada kubwa kupambana na tatizo hilo japokuwa mafanikio si makubwa sana.

Kwa huko nyumbani tatizo naliona kubwa sana zaidi ya kubwia unga ni matumizi ya bangi.Sijui ni kwa vile madhara ya bangi ni ya polepole zaidi ya kubwia unga,au sijui kwa vile bangi imezoeleka sana,ukweli unabaki kuwa hatua madhubuti dhidi ya uvutaji bangi hazijatiliwa mkazo sana na vyombo husika.Kwa bahati mbaya sijaona utafiti wowote rasmi uliofanywa kuonyesha ukubwa wa tatizo hili,lakini naamini pindi utapofanyika matokeo yake yatakuwa ya kutisha.

Kuna kundi maalumu nitalolizungumiza hapa:wasanii hususan wale wa Bongofleva.Nilipokuwa huko nyumbani nilijaribu kufanya utafiti usio rasmi kujua msanii gani anatumia bangi na nani hatumii.Kwa kuwa utafiti huo haukuwa rasmi naomba nisitoe “takwimu” zangu lakini ukweli ni kwamba bangi imekuwa ina wafuasi wengi sana miongoni mwa wasanii wetu.Unajua tatizo mojawapo la uvutaji bangi ni kwamba huwezi kujificha iwapo ni mtumiaji.Kuna vitu flani-flani huwa havifichiki pindi mtu akishapuliza majani hayo haramu.Ilinishtua nilipogundua kuwa karibuni robo tatu ya wasanii wa kundi flani maarufu huwa hawawezi kutumbuiza jukwaani bila kupata misokoto kadhaa ya bangi.Jamani,hii sio hadithi ya kutunga au Isidingo bali ni hali halisi.Kwa bahati mbaya,watu hawajali sana.Na ndio maana hata kwenye tungo za baadhi ya wasanii maarufu wa Bongoflava unasikia bangi ikitajwa kwa namna ya kusifiwa utadhani imekuwa chai.Sintotaja majina ya watu hapa lakini kwa harakaharaka nimesikia nyimbo tatu,mbili kati ya hizo zikiwa zimeimbwa na msanii mmoja ambapo baadhi ya maneno ni kama “mimi nina kijiti cha…na wewe leta kijiti cha …” (kijiti ni bangi,na ukisikia kijiti cha mwanza basi inamaanisha bangi inayotoka mwanza),nyingine kuna maneno “…nitembezee chata…” (kutembeza chata ni kupasiana bangi) na msanii mwingine hakuona aibu kusema waziwazi “…pobe nakunywa,bangi navuta…”Wahusika wanaweza kujitetea kwamba hizo ni nyimbo tu na wao hawatumii kilevi hicho lakini haihitaji PhD kujua kwamba mtu hawezi kusifia kitu kibaya kama hakitumii au kukipenda.

Miongoni mwa hofu zangu kuhusu matumizi ya bangi kwa baadhi ya wasanii ni kwamba mara nyingi (kwa mujibu wa utafiti wangu usio rasmi) baada ya kuvuta bangi na kutumbuiza,msanii husika hujikuta “akizidishiwa ulevi” kwa ofa za pombe kutoka kwa mashabiki au wapambe.Lakini pia kuna watu wanaoitwa “groupies” ambao mara nyingi ni akinadada ambao wanamwandama msanii na wako tayari kufanya lolote kumridhisha msanii huyo.Sasa mtu akishakuwa na “cocktail” ya bangi na pombe,je akipewa ofa ya tendo la ndoa na “groupie” kondom inakumbukwa kweli?Lakini hilo ni tatizo dogo ukilinganisha na lile la “utaahira”.Najua ni vigumu kumshawishi mvuta bangi aamini kuwa bangi inachangia katika kuleta madhara kwenye ubongo,lakini ukweli ndio huo.

Naomba ieleweke kwamba simaanishi kuwa wasanii wote ni wavuta bangi bali pointi yangu ni kwamba ulevi huo haramu umepata wafuasi wengi kwenye fani kama wanavyosema wenyewe.Nawajua wasanii kadhaa ambao wanajiheshimu ambao wanaelewa kuwa licha ya bangi kuwa ni kitu haramu pia ina madhara kwa afya ya mvutaji.Kwenye utafiti wangu “bubu” niligundua kwamba miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya vijana kujiingiza kwenye utumiaji wa bangi ni hoja ya kipuuzi kwamba “inaleta kujiamini na hisia za ubabe!!!”Nilidokezwa na rafiki yangu mmoja aliewahi kufanya “shooting” ya video ya tangazo flani lililokuwa limemhusisha msanii mmoja wa “mkoani” kwamba nusura amwombe bosi wake atafute mtu mwingine wa kutokea kwenye tangazo hilo kwa vile msanii huyo alibugia misokoto kama minane hivi siku waliyokuwa wanajiaandaa na shooting hiyo.

Sasa nyie vijana,na hasa baadhi ya wasanii,mnaoendekeza uvutaji bangi mkae mkielewa kwamba mnajitafutia matatizo kwenye maisha yenu.Lakini pia wakati umefika sasa kwa uvutaji bangi kuonekana kama tatizo sugu linalohitaji kutupiwa jicho kali.Wale wanaovuta bangi kwa kisingizio cha “imani zao za kidini” (ndio,wapo wanaodai kuwa wao ni marastafari na bangi ni majani matakatifu) watambue kwamba wanavunja sheria na wakati huohuo wanatuletea uwezekano wa kuwa na mataahira siku za mbeleni.Watambue kuwa nchi yetu ni masikini na wakati huu ambao jitihada zinaelekezwa katika kupambana na majanga kama ya ukimwi wao wanatuongezea mzigo mwingine wa kukabiliana na tatizo la uchizi unaosababishwa na weed (bangi).

Alamsiki

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Habari za huko nyumbani

Mojawapo ya tofauti kubwa kati ya jamii ya hawa wenzetu na huko nyumbani ni namna uhuru wa kujieleza (freedom of expression) unavyothaminiwa.Of course,uhuru huo unaambatana na wajibu,kwa sababu kama wanataaluma wa kanuni za maisha wanavyosema,uhuru bila wajibu ni sawa na kukaribisha vurugu.Kadhalika,uhuru huo sio wa asilimia 100 (absolute),kwa vile hakuna kitu kama hicho duniani.Lakini ukilinganisha na huko nyumbani,yayumkinika kusema kwamba hawa wenzetu wana uhuru mkubwa zaidi wa kujieleza.Sambamba na hilo ni uhuru wa taasisi zinazopaswa kuujulisha umma nini kinaendelea katika jamii yao na hata nje ya jamii hiyo.Hapa nalenga zaidi kwenye taasisi za habari:hususan magazeti na vituo vya radio na runinga.

Kuna magazeti hapa ambayo ni mithili ya hayo yanayoitwa “ya udaku” huko nyumbani.Magazeti kama The Sun,News of the World,Daily Mirror,nk yamebobea sana katika kuibua skandali mbalimbali hapa Uingereza.Inapotokea kwamba habari flani imepotoshwa basi hao walioguswa na habari hiyo wataamua aidha kukanusha au kukimbilia mahakamani kudai fidia.Wakati mwingine watajwa kwenye habari hizo hulazimika kukiri makosa yao hadharani.Kwa mfano,juzijuzi iliripotiwa kuna Naibu Waziri Mkuu John Prescott alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na katibu muhtasi wake Tracey Temple.Katika sekeseke hilo ambalo bado halijatulia ilimzalimu Bwana Prescott kukiri kuwa yaliyosemwa na magazeti ni kweli.

Nakumbuka mwanataaluma mmoja huko nyumbani aliwahi kuvitaka vyombo vya habari kuwa na ujasiri wa kutaja majina ya watuhumiwa bila kuwa na hofu ya kuburuzwa mahakamani,iwapo vyombo hivyo vina uhakika na walinachoripoti.Hebu chukulia mfano wa habari kama hii: “kiongozi wa chama kimoja cha siasa kinachoanzia na herufi C anadaiwa kuwa na uhusianowa kimapenzi na mtangazaji flani ambaye jina lake linaanzia na herufi D…”Hivi habari kama hiyo si ni sawa na chemsha bongo kwa msomaji?Hali ilikuwa mbaya sana miaka ya nyuma kwa sababu ilikuwa ni vigumu mno kujua ni mtuhumiwa gani hasa anazungumziwa katika stori husika.Hata hivyo,kuna dalili kwamba mambo huenda yakabadilika hasa baada ya ujio wa magazeti jasiri ambayo yako tayari kwa lolote.Ukweli ni kwamba kama ushahidi upo wa kutosha hakuna haja ya kuficha jina la mhusika (labda ithibitike kuwa kumtaja kutaathiri uchunguzi,au kwa sababu za kimaadili).

Siyalaumu magazeti yanayoshindwa kutaja majina ya wahusika katika skendo flani japokuwa nayapa changamoto kufanya hivyo.Siyalaumu kwa sababu sio kosa lao,sio uoga,bali ni mazingira yaliyopo.Siasa za nchi yetu baada ya uhuru hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 zilikuwa zimegubikwa na usiri mkubwa.Kutaja madhambi ya kiongozi ilikuwa dhambi,na hapa tunazungumzia kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa.Usiri sio mbaya kama unatumiwa kwa manufaa ya wengi,lakini kwa bahati mbaya baadhi ya watu walikuwa wanautumia kuficha maovu yao.Waliofilisi mashirika ya umma walinufaika sana na siasa za usiri.Viongozi hawakuwa tayari kusikia kauli nyingine zaidi ya sifa,na kuwakosoa ilikuwa ni kujichimbia kaburi.Kwa hiyo,hali tuliyonayo sasa ni matokeo ya miongo kadhaa ya kuishi katika siasa za kusifia na si kukosoa.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni miongoni mwa maeneo ambayo yameathiriwa sana na kutokuwepo uhuru wa kutoa mawazo sambamba na uoga wa kuadhibiwa unapoongea kinyume na matakwa ya wakubwa.Nilikuwa sijazaliwa wakati mataifa haya yanaungana,na sijafanya utafiti wa kutosha iwapo Muungano huo ulifanywa kwa ridhaa ya wadau (wananchi) au yalikuwa ni maamuzi tu ya viongozi.Miaka nenda miaka rudi watu wamekuwa wakiongea “chini ya uvungu” kwamba Muungano huu una matatizo mengi tu japokuwa yanaweza kutatuliwa pale penye nia.Baadhi ya viongozi wamekuwa wanakwepa kuzungumzia matatizo yaliyopo kwa madai ya “kukwepa jinamizi la Muungano.”

Hivi karibuni kumekuwa na harakati za kisheria na kisiasa kuhusu Muungano.Kundi la Wazanzibari limefungua kesi kuhusu Muungano,Mchungaji Mtikila nae anaonekana kuukalia kooni Muungano,na viongozi wa serikali kutoka Bara walikutana na wale wa viswani kujadiliana kuhusu suala la Muungano.Juu ya hayo serikali ya awamu ya nne ina waziri anaeshughulikia suala la Muungano.Hata hivyo,kauli za Waziri Kiongozi wa Zanzibar Samsi Vuai Nahodha kuwa suala la mafuta ni la kisiwa hicho pekee,sio kitu cha kukiacha kipite hivihivi tu.Scotland,sehemu ya muungano unaounda United Kingdom (Uingereza) ina utajiri mkubwa wa mafuta.Lakini japokuwa kumekuwa na kelele za hapa na pale kuhusu muungano huo,utajiri wa mafuta haujawahi kuipa kiburi Scotland ifikirie kujitoa katika muungano huo au itumie mapato yote ya mafuta peke yake.Sasa kelele zimeanza hata kabla hayo mafuta hayajapatikana huko Zanzibar,je yakipatikana si ndio itakuwa mshikeshike!

Mimi nadhani suala la Muungano linazungumzika.Ikibidi kufanya kura ya maoni kujua matakwa ya sasa ya wananchi kuhusu Muungano,basi na ifanyike bila kuogopa matokeo yake.Siasa za kuogopana na kubembelezana zimepitwa na wakati,na iwapo itathibitika kuwa upande mmoja wa Muungano hauridhiki na muundo au kuwepo kwake,basi jitihada za dhati zifanyike kupata ufumbuzi.Tukiendelea na siasa za usiri na kujidanganya kwamba kila kitu kinakwenda vizuri,si ajabu siku moja Muungano huu ukavunjikia mahakamani.Hiyo itakuwa aibu sana hasa kwa wale wanaodai kukwepa “jinamizi la kuvunjikiwa na Muungano.”Inatokea huko Serbia-Montenegro,inaweza pia kutokea huko nyumbani iwapo wanasiasa wetu hawatafanya jitihada za makusudi.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa makala hii.

Leo nina hasira.Muda mfupi kabla ya kuandika makala hii niliongea na mzazi wangu huko Ifakara.Akanisimulia stori mmoja ambayo kimsingi ndio iliyonifanya niwe na hasira.Hata hivyo,naomba niwatoe hofu kwamba hasira nilizonazo haziwezi kupoteza ladha ya makala hii.

Mzee ana matatizo ya moyo.Sasa kama unavyojua mambo ya miji midogo kama Ifakara.Hospitali zipo lakini wataalamu ni wachache.Lakini kwa kumbukumbu zangu wakati flani aliwahi kunieleza kwamba kuna daktari mmoja mwenye zahanati yake binafsi mjini hapo ambae inaaminika kuwa ni mtaalam wa mambo ya moyo.Katika maongezi yetu kwenye simu aliniambia kuwa moyo bado unamsumbua.Nikamuuliza kwanini asiende kwa huyo mtaalam wa magonjwa ya moyo.Jibu alilonipa ndilo lililonifanya nipandwe na hasira niliyonayo hadi sasa.Anasema kwamba jirani yake aliyekuwa akisumbuliwa na matizo ya moyo alikwenda kumuona huyo daktari hivi karibuni,lakini jibu alilopewa lilimfanya mgonjwa huyo kurudi nyumbani akiwa na ugonjwa mwingine mpya:hofu ya kufa.Kisa?Aliambiwa na mtaalamu huyo wa moyo kwamba hivi “kwanini wewe ambaye umebakiwa na wiki mbili tu za kuishi (kutokana na umri wako mkubwa) unataka kutibiwa moyo badala ya kuuacha usimame wenyewe muda ukifika”!

Laiti maelezo hayo ya mzazi wangu yangekuwa yanatoka kwa mtu wa kawaida tu nisingeamini kwamba nchi yetu ina baadhi ya watu wanaojiita madaktari ambao wanaweza kukiuka maadili ya kazi yao kwa kiwango hicho!Nadhani hata ukienda gereji na gari lililochoka sana,bado mafundi makenika watakupa matumaini ya namna flani badala ya kukibilia kukwambia kwamba ukalitupe gari lako.Na hapo tunazungumzia kitu ambacho unaweza kukinunua kipya.Maisha hayawezi kununuliwa upya.Tukirudi kwenye stori niliyopewa na mzee,basi jirani yake (ambaye si kama amekula chumvi sana) tangu alipoambiwa na daktari kwamba amebakiwa na wiki mbili kufa,amepatwa na hofu ya ajabu.Kwani kuna mtu ambaye haogopi kufa?Na hasa kama umepewa tahadhari kama hiyo na daktari.Mzee wangu baada ya kusikia stori hizo kutoka kwa jirani yake alinieleza bayana kwamba bora aendelee kuugua kuliko kwenda kwa daktari ambae amegeuka kuwa mtabiri wa urefu wa maisha ya wagonjwa.Nilimpoza kwa kumwambia kuwa naamini huyo daktari alieongea upuuzi huo hajui wajibu wake na anakiuka tu maadili ya kazi yake.

Laiti jirani ya mzee wangu angekuwa amekumbana na kioja hicho hapa Ughaibuni huenda angejikuta anapata utajiri wa ghafla endapo angefungua mashtaka dhidi ya daktari aliemtishia uhai wake.Sio siri,hawa wenzetu wanatoa kipaumbele kikubwa sana kwa suala la afya sambamba na kuhakikisha kuwa watumishi katika sekta ya afya wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili.Na sio katika sekta ya afya pekee bali sehemu nyingi zinazotoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi zinabanwa sana kuhakikisha kuwa huduma hizo zinatolewa katika kiwango stahili.Pengine kingine kinachowasaidia viongozi katika taasisi mbalimbali za huduma hapa Ughaibuni ni ile tabia ya kufuatilia nini kinachoongelewa kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi zao.Mganga mkuu akisoma gazeti na kukuta malalamiko kuhusu hospitali yake,hapuuzi bali atakimbilia kumjibu mlalamikaji huyo kuwa atachunguza suala lililolalamikiwa.Na haishii kutoa ahadi tu bali hatua lazima zitachukuliwa.Lakini kinachosikitisha huko nyumbani ni ile kuona gazeti flani limeripoti kuwa hospitali flani “imeua” mgonjwa na wala husikii habari hiyo ikikanushwa au kukubaliwa na uongozi wa hospitali husika.

Sehemu nyingi zinazotoa huduma huko nyumbani zina masanduku ya kutoa maoni.Lakini lile vumbi unaloliona kwenye mengi ya masanduku hayo linatosha kuthibitisha kuwa masanduku hayo ni sawa na urembo tu kwenye makorido ya sehemu husika.Kwa mtizamo wangu,nadhani tatizo la msingi ni ile tabia iliyojengeka kwa baadhi ya watumishi kwenda kazini kuonekana tu wamekwenda kazini na mwisho wa mwezi wapate mishahara yao,na si kwenda kutumikia wale wanaowafanya wapate mshahara.Unadhani mtumishi wa benki anaejua dhahiri kwamba ni fedha za wateja ndio zinaiwezesha benki hiyo kuwepo na kumlipa mshahara,atamdharau mteja anaekuja hapo kupata huduma?Kama mtumishi anajiona hataki “kubughudhiwa” na wanaohitaji huduma kazini kwake,si alale tu nyumbani,au aache kazi?Tuone kama hatakufa kwa njaa.Kumbe basi kinachompa shibe (kazi) ni sharti akiheshimu na kukitumikia kwa moyo wake wote.

Alamsiki

17 Apr 2006

KULIKONI UGHAIBUNI

Habarini za huko nyumbani.Naamini mambo yanakwenda vema.Hapa napo ni shwari tu japokuwa viama vyetu vya kawaida bado vinaendelea.Pengine utashtuka kusikia neno “viama” (umoja-kiama,wingi-viama).Ngoja niende moja kwa moja kwenye pointi.

Fikra nilizokuwa nazo wakati niko huko nyumbani,na ambazo nilikuwa nashea na jamaa zangu kibao,ni kwamba maisha ya Ughaibuni ni kama ya peponi:ardhi ya maziwa na asali,kama vitabu vya dini vinavyosema.Tabu ya kwanza niliyokutana nayo ni lugha.Si kwamba mie ni maimuna ambae lugha ya “kwa mama” haipandi.La hasha,lugha hiyo inapanda ki-sawasawa.Tatizo ni kwamba wakati nakuja hapa nilishazowea kuongea Kiswahili changu chenye lafidhi ya ki-Ndamba (ndio,mimi ni Mndamba kutoka Ifakara.Awije mlongo…).Uzuri wa Daresalama nilipokuwa naishi ni kwamba wewe ongea Kiswahili cha aina yoyote,lakini una hakika watu watakuelewa na mtasikilizana bila matatizo.Hapa “kwa mama” unaweza kwenda sehemu na ukawa unaongea kiingereza chenye lafidhi ya ulikotoka na watu wakaishia kukukodolea macho tu.Hawakuelewi unaongea nini.Unakwenda sehemu,unahitaji huduma fulani.Unamuuliza mhudumu hapo,anaonekana kutoelewa unachoongea.Anabaki kukuomba “sorry can you say that again?” (samahani,unaweza kurudia ulichokisema?).Basi hapo inabidi useme neno mojamoja tena taratibu ili muelewane.

Lakini tatizo la pili ni lile la kujisahau na kujikuta unaingiza maneno ya Kiswahili kwenye lugha yao,hasa pale mtu anapoonekana aidha hataki kukuelewa au ni mgumu wa kuelewa.Hebu fikiri,unakwenda dukani,unamwambia muuza duka “nipatie maji ya kunywa ya Kilimanjaro”,yeye anakuuliza “unasemaje anko?”,unarudia tena,na yeye anarudia kukuuliza unasemaje!Ikifika mara ya tatu kuna hatari ukataka kujaribu kumwelewesha muuzaji huyo kwa lugha ya kwenu.

Kama mawasiliano ni tatizo sugu basi kufanya shopping ni tatizo zaidi.Hili ni tatizo ambalo binafsi nakutana nalo takribani kila napoingia kwenye duka au supamaketi.Sijui tatizo ni hisia kwamba Mtanzania kama mimi sina uwezo wa kununua kitu dukani au vipi!Ile kuingia tu kwenye duka au supamaketi utakuta mlinzi anaanza kukuandama nyuma yako.Hofu ni kwamba labda utakwapua kitu na kuondoka nacho bila kulipa.Kichekesho ni kwamba wakati walinzi wa duka wanahangaika na wewe mtu mweusi,mateja ya kizungu yanatumia mwanya huo kukwapua vitu na kuchomoka navyo bila kulipa.Ndio,Ulaya kuna mateja kibao kama ilivyo huko kwetu.Ipo siku nitakupatia stori hiyo ya mateja wa Ulaya kwa kirefu.Mara nyingi utakuta hao wadokozi wanavizia mtu mweusi aingie dukani nao wakafanye vitu vyao kwa vile wanajua akili za walinzi zitakuwa kwako.

Kwenye mabasi nako wakati mwingine ni adha tupu.Utamkuta mtoto wa kizungu anakushangaa utadhani ameona muujiza flani.Kibaya zaidi ni pale mtoto huyo anapodiriki kumuuliza mama yake kama wewe ni mtu au sana mu.Si mchezo manake.Unaweza kutaka kurusha ngumi lakini ukikumbuka kilichokupeka Ughaibuni huko inabidi umezee tu.Watoto wengine waliolelewa ovyo huweza kudiriki kukugusa ngozi kisha kuangalia mikono yao kama imebakia na rangi nyeusi kwani kwao mtu lazima awe mweupe!

Haya wengi wenu mnaweza kuwa hamyajui si kwa sababu hayaripotiwi na BBC au Skynews bali ni kwa vile wengi wetu tulioko huku tukirudi nyumbani tunapenda kutoa stori nzuuri kuonyesha kuwa huku ni kuku kwa mirija tu,ardhi ya maziwa na asali,na kuficha viama tunavyokumbana navyo kila siku.

Hiyo ndio Ughaibuni,ndugu zanguni.Hata hivyo,naomba nisisitize kwamba viama hivyo havipo kila mji.Ile miji yenye wageni wengi au tuseme watu weusi wengi,kuna unafuu kidogo,japokuwa huko nako kuna viama kama vya umbeya,kusutana na hata kuagiziana mafundi (waganga wa kienyeji) kufanyiziana.Ukibisha kwamba watu wanaagiza wataalam kutoka huko nyumbani kuja kurekebisha mambo yao au kufanyiza kwa njia za asili basi nenda pale Buguruni kwa mwinjilisti flani ambae huja huku mara kwa mara kuhubiri neno la Bwana na kutoa pepo.Huyo ameshasikia maungamo na ushuhuda kadhaa wa hao waagizaji mafundi kutoka huko nyumbani.

Hadi wiki ijayo,Alamasiki

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.