Showing posts with label LUO. Show all posts
Showing posts with label LUO. Show all posts

6 Jan 2008


Nimesoma makala moja ndefu katika toleo la leo la Sunday Times (la hapa Uingereza) kuhusu hali ilivyo kwa majirani zetu wa Kenya.Kwa kweli inatisha na kusikitisha.Mauaji na ubakaji ni miongoni mwa unyama unaozidi kushamiri nchini humo.Lakini inasikitisha zaidi kuona hata watoto wadogo wa miaka 12 wanakumbwa na ukatili huo.

Lakini kilichonikurupusha kuandika makala hii ni habari kwamba vurugu hizo zinahusisha pia makundi mawili hatari:Mungiki (la Wakikuyu) na Taliban (la Waluo).Kwa namna inavyoonekana,makundi haya ni sawa na magenge ya wahalifu ambayo kwao vurugu za aina yoyote ni sawa na msimu wa mavuno.Inaelezwa kwamba Mungiki wamekuwa wakiwatahiri kwa nguvu "mateka" wao wa Kiluo (kwa mila zao,wanaume wa Kiluo huwa hawatahiri) huku Taliban wakijibu mashambulizi kwa kuwafyeka mapanga Wakikuyu.

Inatisha na kusikitisha kusikia kwamba watu kadhaa waliuawa kinyama kwa kuchomwa moto wakiwa ndani ya kanisa walilojihifadhi.Kwa nchi ambayo asilimia kubwa ya wakazi wake ni Wakristo,hiyo ni ishara kwamba chuki kati ya makundi yanayopingana zimevuka nguvu za mshikamano wa jamii kama dini na utaifa,na inaelekea kinachoangaliwa sasa ni ukabila tu.

Haihitaji ujuzi wowote wa mambo ya uchaguzi kubaini kwamba Kibaki amejirejesha kwa nguvu madarakani.Hivi anajisikiaje wakati yeye yupo Ikulu,mamia ya Wakenya wenzake,ikiwa ni pamoja na Wakikuyu wenzie,wanapoteza maisha yao kila siku huku wengine wanaishi kwa hofu na mashaka ya kuuawa,kubakwa,kutahiriwa kwa nguvu na udhalilishaji mwingine usiopaswa kufanyika katika jamii yoyote ile iliyostaarabika.Damu inayomwagika kila kukicha (sambamba na mateso yanayowakuta wananchi wasio na hatia) iko mikononi mwa Kibaki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.