Kikundi cha kigaidi cha Taliban huko Aghanistan kilikuwa kipo tayari kumwachia huru Sajenti wa Jeshi la Marekani Bowe Bergdahl ili kumpata mwanamama huyu. Magaidi wa ISIS nao walikuwa wapo tayari kumwachia mwandishi wa habari wa Marekani waliyemuua kwa kumkata kichwa, James Foley iwapo mwanamama huyo angeachiwa huru. Je kwanini takriban kila kikundi kikubwa cha kigaidi kinamhitaji Aafia Siddiqui?
Miaka miwili iliyopita, maafisa waandamizi wa masuala ya usalama wa taifa nchini Marekani walipokea 'ofa' ya kushangaza kutoka Pakistani. Iwapo Marekani wangekubali kumwachia mwanamke mmoja anayetumikia kifungo kirefu huko Texas kwa kosa la jaribio la kuua, basi Sajenti Bowe Bergdahl aliyetekwa na Taliban tangu mwaka 2009 angeachiwa huru.
Kwa mujibu wa taarifa za kiusalama, Rais Barack Obama na maafisa wake walikataa 'ofa' hiyo. Kumwachia mwanamke huyo, Bowe Bergdahl kunekinzana na msimamo wa Marekani wa kutofiki amakubaliano na magaidi. Kadhalika, kumwachia huru mwanamke huyo kungemrejesha uraiani mtu hatari kwa usalama.
Siddique, mwenye umri wa miaka 42, na anayefahamika kwenye anga za kupmbana na ugaidi kama 'Lady al-Qaeda' ameshahusishwa na mmoja wa magaidi wahusika wa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 Khalidi Sheikh Mohammed, na wakati flani alikuwa katika orodha ya magaidi wanaosakwa zaidi (most wanted terrorist list).
Gaidi huyo wa kike alipata elimu yake katika chuo kikuu kinachoheshimika sana duniani cha M.I.T na ana shahada ya uzamifu (PhD). Mwaka 2008, alikamatwa akiwa na kemikali ya Sodium Cyanide, pamoja na nyaraka za jinsi ya kutengeneza silaha za kemikali, mabomu ya kusababisha madhara makubwa (smart bombs) na jinsi ya kuitumia Ebola kama silaha. Maofisa wa Shirika la Upelelezi la FBI walipojaribu kumhoji, mwanamke huyo alichukua silaha na kufyatua risasi.
Japo Marekani haikulipa uzito wazo la kubadilishana mwanamke huyo na 'mateka waliokuwa mikononi mwa magaidi,' Siddique amekuwa turufu muhimu kwa magaidi kila linapokuja suala la 'kubadilishana mateka' mbalimbali wa Marekani na Ulaya walio mikononi mwa magaidi.
Jumanne iliyopita, kikundi cha kigaidi cha ISIS kilidai gaidi huyo wa kike aachiwe huru ili nao wamwachie huru mwanamke mmoja wa Kimarekani aliyetekwa huko Syria alipokuwa akifanya kazi katika shirika la misaada ya kibinadamu. Maafisa wanaamini kuwa ISIS inawashikilia mateka angalau Wamarekani wengine wanne, ikiwa ni pamoja na mwandishi wa habari Steven Sotloff. Magaidi hao wanataka kulipwa Dola za Marekani milioni 6.6 ili wamwachie huru mwanamke huyo mtumishi wa shirika la misaada ya kibinadamu ambaye ndugu zake wameomba jina lake lihifadhiwe.
Wakati Ikulu ya Marekani imekuwa ikikataa katakata wazo la kumwachia huru mwanamke huyo gaidi ili kuwezesha kuachiwa huru kwa mateka wa nchi hiyo waliopo katika mikono ya magaidi, "Twafahamu kuna wanaotengeneza mazingira katika 'Wizara ya Ulinzi' ya kuangalia uwezekano wa kubadilishana mateka kwa kumtumia Siddique."
Mjadala mkubwa uliibuka baada ya kuchinjwa kwa Foley kuhusu aidha kulipa fedha kwa magaidi au kuwaachia wafungwa kama wanavyodai magaidi hao. Marekani, tofauti na nchi nyingi za Ulaya, huwa hailipi fedha kwa ajili ya kuachiwa huru raia wake waliotekwa. Na inaelezwa kuwa hiyo ni miongoni mwa sababu zinazowavunja moyo magaidi kuwateka nyara Wamarekani kwa minajili ya kudai fidia ili mateka hao waachiwe huru, kwa mujibu wa mtaalam mmoja wa ugaidi.
Siddique ni kama 'celebrity' flani nchini Pakistan, ambapo kifungo chake mwaka 2010 kilipelekea maandamano nchini humo (Pakistan). Matokeo ya kifungo cha Siddique yalikuwa hahabari zilizoongoza katika magazeti yote makubwa.
Hukohuko Pakistan, kikundi kijiitacho 'Brigedia ya Aafia Siddique'kimeshafanya mashambulizi kidhaa dhidi ya serikali ya nchi hiyo kama upinzani na malalamiko yao dhidi ya wanachokiona kama kifungo kisicho cha haki kwa mwanamke huyo hatari.
CHANZO: Jarida la Foreign Policy