Moja ya masuala yanayotawala anga za habari na
mijadala mbalimbali mtandaoni ni uamuzi wa bodi ya taasisi ya Changamoto ya Milenia
(Millennium Challenge Corporation) ya Marekani kusitisha misaada kwa Tanzania.
Sababu kuu mbili zilizotolewa na bodi hiyo kuhusu uamuzi huo ni marudio ya
uchaguzi huko Zanzibar Machi 20, mwaka huu, ambao licha ya kususiwa na chama
kikuu cha upinzani cha CUF, ulilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na nchi wahisani,
ikiwa ni pamoja na Marekani.
Sababu ya pili, kwa mujibu wa bodi hiyo, ni uamuzi wa
serikali ya Tanzania kupitisha Sheria Uhalifu wa Mtandaoni (Cybercrime Act) ya
mwaka 2015 licha ya upinzani mkali dhidi ya muswada wa sheria hiyo,
iliyotafsiriwa kuwa imemlenga kukandamiza uhuru wa habari na haki za binadamu.
Kabla ya kuingia katika uchambuzi huu kiundani,
nieleze mtazamo wangu kuhusu sababu hizo mbili zilizotolewa na bodi ya MCC.
Kwanza, kwa mtazamo wangu, suala la marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ni mzaha wa
kidemokrasia, na ni jeraha la kisiasa ambalo historia inaweza kutuhukumu huko
mbeleni. Haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za Zanzibar kufahamu kuwa kuna ‘sheria
isiyo rasmi’ kuwa ‘kamwe CUF hawapaswi kutawala Zanzibar.’ Bila kuuma maneno,
hiyo ndo sababu pekee ya kufutwa kwa uchaguzi wa awali (ambao inadaiwa mgombea
wa CUF, Seif Shariff Hamad, alishinda), na kuamiriwa uchaguzi huo urudiwe huku
CCM ikiwekeza nguvu zake zote kuhakikisha inashinda. Hata kama CUF wasingesusia
uchaguzi huo, bado CCM wangeshinda kwa sababu ‘ni lazima iwe hivyo,’ kwa ‘kanuni’
zao.
Je MCC ipo sahihi kutumia kigezo cha Zanzibar
kusitisha misaada yao? Kwa upande mmoja, wapo sahihi. Kwanini? Kwa sababu, hata
katika mahusiano yetu ya kawaida tu kibinadamu, anayekupa msaada anapata ruhusa
pia ya ‘kukutawala’ kwa kukupa masharti ambayo ukiyakiuka, yanaweza kuathiri
mahusiano katika ya mtoa msaada na mpokea msaada. Miongoni mwa masharti ya MCC
ni pamoja na masuala ya demokrasia, na haihitaji kukuna kichwa sana kubaini
kuwa marejeo ya uchaguzi wa Zanzibar, ambayo binafsi ninayaona kuwa ni mzaha wa
kidemokrasia, yamewapa MCC ‘kisingizio chepesi’ hata kama hawangekuwa na sababu
nyingine.
Mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa huko Zanzibar ni
zaidi ya jipu. Ni kansa ambayo imeshachafua sura ya Tanzania huko nyuma ambapo
kwa mara ya kwanza tulizalisha wakimbizi baada ya vurugu za uchaguzi mkuu mwaka
wa 2000. Ni kansa ambayo sasa imewapa MCC kisingizio cha kutunyima misaada yao.
Kwa bahati mbaya, au makusudi, hakuna utashi wa kisiasa wa kusaka ufumbuzi wa
kudumu wa mgogoro huo. Kila kiongozi wa CCM, kwa upande wa Bara, anaogopa suala
hilo kwa kuhofia ‘kuvunjikiwa na Muungano mikononi mwake.’
Wanasiasa wa Zanzibar sio tu wanaufahamu udhaifu huo
bali pia wanautumia vema. Wanaendesha siasa zao cha chuki na uhasama watakavyo
wakifahamu fika kuwa hakuna mwana-CCM wa Bara mwenye jeuri ya kuwaingilia.
Sina hakika Zanzibar itaathirika vipi kwa maamuzi ya
MCC kukata misaada, lakini kinachowapa kiburi viongozi wa huko ni kwamba ‘Tanganyika’
haina jeuri ya kuisusa Zanzibar, au kuinyooshea kidole katika mwendelezo wa
siasa za chuki na ubaguzi.
Lakini kwa upande wa pili, hao MCC ni wanafiki tu.
Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa wa siasa za kimataifa kutambua unafiki wa
Marekani linapokuja suala la demokrasia. Nchi hiyo ni mshirika mkubwa wa tawala
za kidikteta kama vile huko Misri, Saudi Arabia na kwingineko. Sawa, labda
Zanzibar wamefanya mzaha wa kidemokrasia lakini vipi kuhusu demokrasia isiyopo
kabisa huko Saudi? Well, jibu rahisi ni kwamba Zanzibar na Tanzania sio muhimu ‘kihivyo’
kwa Marekani ilhali taifa hilo linazitegemea mno tawala za kibabe za nchi kama
Misri au Saudi, hususan katika masuala ya ushushushu/mapambano dhidi ya ugaidi
wa kimataifa.
Kuhusu suala la Sheria ya Uhalifu wa Mtandao, hapa
kumesheheni unafiki, na upo wa aina mbili: wa Wamarekani na wa sie Watanzania
wenyewe. Mie ni mfuatiliaji wa karibu wa masuala ya usalama mtandaoni, ambao
kwa namna moja au nyingine unahusiana na hiyo ishu ya Cybercrime Act. Kwa
kifupi tu, Marekani ina sheria kandamizi mno dhidi ya uhuru wa raia mtandaoni.
Naamini ushaskia kuhusu jamaa anayeitwa Edward Snowden (kama hujamsikia, Wasiliana
na Google…haha). Huyu bwana alikuwa mtumishi katika shirika la ushushushu la
Marekani linalohusika na kunasa mawasiliano mbalimbali (NSA – National Security
Agency), na baadaye nafsi yake ilimsuta, akaamua ‘kuingia mitini’ na kumwaga
siri lukuki kuhusu jinsi NSA inavyohujumu haki za raia kimawasiliano. Hawa
jamaa wamekuwa wakinasa mawasiliano ya takriban kila mtu, wakishirikiana kwa
karibu na mashushushu wenzao wa hapa Uingereza, GCHQ, taasisi ya kishushushu
inayohusika na kunasa mawasiliano.
Lakini hata tukiweka kando suala la NSA kunasa
mawasiliano mbalimbali (waliwahi kuzua kasheshe kubwa baada ya mashushushu wa
Ujerumani kubaini kuwa NSA walikuwa wakinasa kwa siri mawasiliano ya Kansela
Angela Markel hadi waliposhtukiwa), mashambulizi ya kigaidi nchini humo mwaka
2001 yalipelekea kuundwa kwa sheria kali kabisa dhidi ya uhuru wa habari na
haki za kibinadamu kwa kisingizio cha usalama wa taifa. Kwahiyo, kwa kifupi, ni
uhuni tu wa Marekani kudai Sheria ya Makosa ya Mtandaoni inakiuka uhuru wa
Watanzania. Sheria zao za wazi na za kificho ni mbaya mara milioni zaidi yetu.
Hata hivyo, katika suala hili la Cybercrime Act, tuna
wanafiki kadhaa huko nyumbani. Kwa kumbukumbu tu, mie nilikuwa mtetezi mkubwa
wa muswada uliozaa sheria hiyo, yaani Cybercrime Bill, na niliunga mkono kwa
nguvu zote jitihada za aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, kuhusu muswada huo.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanaoinyooshea kidole
Marekani na wafadhili wengine kuhusu suala la Tanzania kukatiwa misaada
walikuwa mstari wa mbele kuziomba nchi wahisani ziingilie kati kuibana serikali
ili muswada huo usipitishwe kuwa sheria. Sasa kama uamuzi huo wa Marekani
umechangiwa na ‘kelele’ zao hizo, kwanini leo wanalalamika?
Mie niliunga mkono muswada na sheria hiyo kwa sababu
ikitumiwa vema ni nzuri. Hebu nenda Instagram kaangalie uanaharamu unaoendelea
huko, kuanzia picha za uchi, ushoga na kila aina ya laana. Huo sio uhuru wa
habari, ni uwendawazimu ambao kwa hakika ulihitaji sheria kali kuudhibiti.
Na watu waliopita huku na kule kudai sheria hiyo ni
kandamizi na ililenga kuwabana wananchi wasiwasiliane, hawatuambii kama baada
ya sheria hiyo kupitishwa wameshindwa kuwasiliana na watu wengine. Kwa kifupi,
kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika kambi ya waliopinga muswada na sheria
hiyo. Walitumia uelewa mdogo wa wananchi wengi kuhusu masuala ya mtandao, na
kuwajenga hofu feki.
Ninakerwa kuona kundi la wanafiki hawa likiilaumu MCC
au Marekani au nchi nyingine wahisani kuhusu suala la kutukatia misaada, kwa
sababu wao walikuwa mstari wa mbele kuhamasisha nchi wahisani zichukue hatua,
na ‘hatua maarufu’ ya wahisani huwa ni kukata misaada. Badala ya kulalamika,
wanafiki hawa wanapaswa kufanya sherehe maana wishes zao zimetimia.
Sasa niangalie upande wa athari za uamuzi huo wa MCC
kukata misaada. Taarifa nyingine zinaeleza kuwa kuna wahisani wengine nao
wamekata misaada japo kuna mkanganyiko kama hatua hiyo ni mwendelezo wa hatua
za huko nyuma au ni mpya.
Tuwe wakweli, kwa watu masikini kama sisi, hatua
yoyote ile ya kutupunguzia msaada wa aina yoyote ile itatuathiri. Hilo
halihitaji uelewa wa jinsi gani misaada inavyofanya kazi au jinsi gani nchi
yetu ilivyo mtegemezi mzoefu wa misaada. Tatizo kubwa hapa kuhusu “kukatiwa
misaada kutatuathiri au hakutatuathiri” ni tofauti zetu za kiitikadi. Kwa kiasi
kikubwa, suala hilo linaangaliwa katika lensi ya u-CCM na u-UKAWA/Upinzani. Kwa
wana-CCM, ni mwendo wa ‘kiburi’ kwenda mbele, kwamba “waende tu na misaada yao,”
au “hela yenyewe ilikuwa ya mradi wa kifisadi wa Symbion,” mara “ah misaada
gani hiyo yenye masharti kibao.” Wanamhadaa nani? Kama misaada hiyo haikuwa na
muhimu, kwanini basi tuliiomba in the first place? Hizi hadithi za sungura
kusema “sizitaki ndizi hizi” baada ya kushindwa kuzikia mgombani.
Kwa upande wa wana-UKAWA/Wapinzani, bila kujali kuwa
wao kama Watanzania ni wahanga watarajiwa wa uamuzi huo wa nchi yetu kukatiwa
misaada, wanakenua meno yote 32 kwa furaha, huku wakiwazodoa wenzao wa CCM kwa
vijembe kama “ndio matunda ya ubabe wenu huko Zanzibar, tuone sasa…” au “mtaisoma
namba” au “mtakula jeuri yenu…”
Ulemavu huu wa kifikra unaosababishwa na kuliangalia
suala la kiuchumi kwa mtizamo fyongo wa itikadi za kisiasa. Naam, suala la
Zanzibar ni la kisiasa, lakini athari za uamuzi wa Marekani/MCC/wahisani ni la
kiuchumi.
Mie sio mchumi ila ninachoelewa fika kuwa uchumi wetu
umekuwa tegemezi tangu tupate uhuru. Kabla ya kuipa kisogo siasa ya Ujamaa na
Kujitegemea, tulikuwa tukapata misaada kutoka kwa marafiki zetu wa mrengo wa
Ukomunisti. Baada ya kuuzika Ujamaa, tumekuwa kama puto linaloyumbishwa na
upepo, tupo radhi kumpigia magoti yeyote anayeweza kutusaidia. Kimsingi, tuna
ombwe la kiitikadi: majukwaani, CCM wanasema sie ni Wajamaa, vitendo vyetu
havipo kwenye Ujamaa wala Ubepari, tupu tupo tu. Huo ndo ukweli mchungu kuhusu
ubabaishaji wetu.
Kwahiyo, tuache kudanganyana kuwa kukatiwa misaada
hakutotuathiri. Huko ni kujipa jeuri tu. Tunachoweza kukubaliana ni kwamba
suala hilo limeshatokea, tumeshakatiwa misaada, na si ajabu wahisani wengine
wakaamua kufata mkumbo na kufanya hivyo pia.
Jukumu letu kubwa kwa sasa sio kuendelea kunyoosheana
vidole bali tuwe kitu kimoja kama taifa bila kujali nani hasa aliyetusababishia
tatizo hili. Ni tatizo la Watanzania wote bila kujali itikadi zao. Uamuzi wa
wahisani kukata misaada utawaathiri wana-CCM wanaodai hautowaathiri kama
ambavyo utawaathiri wna-CUF au Chadema wanaokenua meno yote 32 kufurahia hatua
hiyo. Na utatuathiri (angalau kisaikolojia) hata akina sie ambao itikadi yetu
pekee ni Tanzania yetu. Huo ni ukweli usiopingika: we are all in this together.
Kuna mambo mawili ya kupigiwa mstari. Kwanza, kwa
miaka mingi tumekuwa tukiishi kifahari mno kuliko uwezo wetu. Na kimsingi,
uwezo wetu duni haukupaswa kuwepo kwani sie sio masikini hata kidogo. Tuna kila
aina ya utajiri lakini kuna majambazi walioigeuza Tanzania yetu kuwa kitu cha
kubakwa kila kukicha. Kila mwenye uelewa anafahamu kilichojiri katika takriban miaka
30 iliyopita. Tanzania yetu ilikuwa shamba la bibi, watu wanafisadi wapendavyo
kiasi kwamba kuwa na uchungu na nchi ilionekana kama wendawazimu.
Kwa bahati nzuri, Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha
baadhi yetu na sasa tumempata Rais, Dkt John Magufuli, ambaye anaonekana
amedhamiria kurekebisha mwenendo wa mambo. Kikwazo chetu kikubwa kilikuwa
ufisadi, lakini sasa Magufuli ameamua kuvalia njuga kupambana na ufisadi kwa
nguvu zote. Mwanzo ni mgumu lakini angalau dalili za mafanikio zimeanza
kujionyesha. Tumuunge mkono, tuchukie ufisadi, tuongeze uzalendo, tuikwamue
Tanzania yetu, tujikwamue nasi wenyewe, tuache kutafuta njia za mkato za
mafanikio, tufanye kazi, tache majungu na kusaka sifa za kijinga mitandaoni,
tuwajibike.
Twahitaji kujifunga mikanda. Haiwezekani wafadhili
wetu waishi kimasikini ilhali sie wafadhiliwa twaishi kama matajiri. Viongozi
wetu waache kuchuana na wauza unga kushindana jinsi ya kuishi kitajiri,
wawabane wauza unga hao, majangili na maharamia wengine ili tuiokoe Tanzania
yetu.
Je twaweza kujitegemea? Absolutely, lakini
tusidanganyane kuwa twaweza kufanya hivyo ghafla ghafla. Tukumbuke, mtoto
hazaliwi akatembea. Tumekuwa wategemezi mno wa misaada kiasi kwamba tumesahau
kuwa twapaswa kujitegemea. Twahitaji kuchukua na kukubali maamuzi magumu ya
kutuwezesha kujitegemea. Ni kama kumlazimisha mtoto anayetambua aanze kutembea
kwa nguvu. Sio rahisi, lakini tukimkazania anaweza kusimama mwenyewe na baadaye
akaweza hata kukimbia. Hilo linahitaji kujitoka mhanga kwa ajili ya nchi yetu,
sambamba na kuweka mbele uzalendo badala ya maslahi binafsi.
Jambo jingine, kwa hisia zangu, japo suala la Zanzibar
na Cybercrime Act zinatajwa kama sababu za uamuzi wa kutunyima misaada,
ninashawishika kuamini kuwa baadhi ya nchi wahisani hawapendezi na kasi ya Rais
Magufuli kuziba mianya ambayo kimsingi licha ya kuwanufaisha mafisadi wa ndani,
ilikuwa pia inanufaisha taasisi za kifisadi za kimataifa. Wengi wa majambazi
waliokuwa wakitupora fedha zetu mchana kweupe walikuwa hawahifadhi fedha zao
katika benki zetu bali zilizopo kwa hao wahisani wetu. Waweza kudhani huu ni
utani mbaya, lakini jiulize, je kama unamfadhili mtu pesa za kumsaidia yeye na
familia yake, lakini anatumia fedha hizo kununulia bling bling, kuongeza nyumba
ndogo, kufanya matumizi ya anasa, nk kwanini usichukue hatua?
Mfano huo unamaanisha hivi: kwanini wahisani wetu walionekana
kutokerwa na jinsi pesa walizokuwa wanatupatia zikifisadiwa kila kukicha lakini
wakaendelea kutumwagia misaada? Na kwanini sasa, tumempata Magufuli ambaye
amepania kwa dhati kupambana na ufisadi, wahisani wanaanza kuleta ‘longolongo’?
Kuna tunaodhani kuwa hao wahisani wanataka tuendelee
kuwa wategemezi wao milele. Kwa upande mmoja utegemezi wetu unawapa uhuru wa
kukwapua kila raslimali tuliyonayo, na kwa upande mwingine, wananeemesha
taasisi zao za fedha kwa vile mafisadi wetu wa ndani wanahifadhi fedha zao
kwenye taasisi hizo.
Mwisho, tuache porojo, tuache unafiki, tuwe kitu
kimoja, athari za kukatiwa misaada zipo, tukishikamana tutaweza kukabiliana
nazo japo mwanzoni itakuwa ngumu. Yawezekana uamuzi huo wa Wamarekani ukawa ‘blessing
in disguise’ kwa maana ya kutupa ‘wake-up call’ tuanze kujitegemea kwa lazima
badala ya kutembeza bakuli letu huko na kule, kisha kile kidogo kinachopatikana
kikaishia kwenye ujenzi wa mahekalu ya mafisadi, ongezeko la magari yao ya
kifahari, na kutanua ukubwa wa nyumba ndogo zao.
MUNGU IBARIKI TANZANIA