Showing posts with label MAREKANI. Show all posts
Showing posts with label MAREKANI. Show all posts

1 Apr 2016

Moja ya masuala yanayotawala anga za habari na mijadala mbalimbali mtandaoni ni uamuzi wa bodi ya taasisi ya Changamoto ya Milenia (Millennium Challenge Corporation) ya Marekani kusitisha misaada kwa Tanzania. Sababu kuu mbili zilizotolewa na bodi hiyo kuhusu uamuzi huo ni marudio ya uchaguzi huko Zanzibar Machi 20, mwaka huu, ambao licha ya kususiwa na chama kikuu cha upinzani cha CUF, ulilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na nchi wahisani, ikiwa ni pamoja na Marekani.

Sababu ya pili, kwa mujibu wa bodi hiyo, ni uamuzi wa serikali ya Tanzania kupitisha Sheria Uhalifu wa Mtandaoni (Cybercrime Act) ya mwaka 2015 licha ya upinzani mkali dhidi ya muswada wa sheria hiyo, iliyotafsiriwa kuwa imemlenga kukandamiza uhuru wa habari na haki za binadamu.

Kabla ya kuingia katika uchambuzi huu kiundani, nieleze mtazamo wangu kuhusu sababu hizo mbili zilizotolewa na bodi ya MCC. Kwanza, kwa mtazamo wangu, suala la marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ni mzaha wa kidemokrasia, na ni jeraha la kisiasa ambalo historia inaweza kutuhukumu huko mbeleni. Haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za Zanzibar kufahamu kuwa kuna ‘sheria isiyo rasmi’ kuwa ‘kamwe CUF hawapaswi kutawala Zanzibar.’ Bila kuuma maneno, hiyo ndo sababu pekee ya kufutwa kwa uchaguzi wa awali (ambao inadaiwa mgombea wa CUF, Seif Shariff Hamad, alishinda), na kuamiriwa uchaguzi huo urudiwe huku CCM ikiwekeza nguvu zake zote kuhakikisha inashinda. Hata kama CUF wasingesusia uchaguzi huo, bado CCM wangeshinda kwa sababu ‘ni lazima iwe hivyo,’ kwa ‘kanuni’ zao.

Je MCC ipo sahihi kutumia kigezo cha Zanzibar kusitisha misaada yao? Kwa upande mmoja, wapo sahihi. Kwanini? Kwa sababu, hata katika mahusiano yetu ya kawaida tu kibinadamu, anayekupa msaada anapata ruhusa pia ya ‘kukutawala’ kwa kukupa masharti ambayo ukiyakiuka, yanaweza kuathiri mahusiano katika ya mtoa msaada na mpokea msaada. Miongoni mwa masharti ya MCC ni pamoja na masuala ya demokrasia, na haihitaji kukuna kichwa sana kubaini kuwa marejeo ya uchaguzi wa Zanzibar, ambayo binafsi ninayaona kuwa ni mzaha wa kidemokrasia, yamewapa MCC ‘kisingizio chepesi’ hata kama hawangekuwa na sababu nyingine.

Mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa huko Zanzibar ni zaidi ya jipu. Ni kansa ambayo imeshachafua sura ya Tanzania huko nyuma ambapo kwa mara ya kwanza tulizalisha wakimbizi baada ya vurugu za uchaguzi mkuu mwaka wa 2000. Ni kansa ambayo sasa imewapa MCC kisingizio cha kutunyima misaada yao. Kwa bahati mbaya, au makusudi, hakuna utashi wa kisiasa wa kusaka ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo. Kila kiongozi wa CCM, kwa upande wa Bara, anaogopa suala hilo kwa kuhofia ‘kuvunjikiwa na Muungano mikononi mwake.’

Wanasiasa wa Zanzibar sio tu wanaufahamu udhaifu huo bali pia wanautumia vema. Wanaendesha siasa zao cha chuki na uhasama watakavyo wakifahamu fika kuwa hakuna mwana-CCM wa Bara mwenye jeuri ya kuwaingilia.

Sina hakika Zanzibar itaathirika vipi kwa maamuzi ya MCC kukata misaada, lakini kinachowapa kiburi viongozi wa huko ni kwamba ‘Tanganyika’ haina jeuri ya kuisusa Zanzibar, au kuinyooshea kidole katika mwendelezo wa siasa za chuki na ubaguzi.

Lakini kwa upande wa pili, hao MCC ni wanafiki tu. Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa wa siasa za kimataifa kutambua unafiki wa Marekani linapokuja suala la demokrasia. Nchi hiyo ni mshirika mkubwa wa tawala za kidikteta kama vile huko Misri, Saudi Arabia na kwingineko. Sawa, labda Zanzibar wamefanya mzaha wa kidemokrasia lakini vipi kuhusu demokrasia isiyopo kabisa huko Saudi? Well, jibu rahisi ni kwamba Zanzibar na Tanzania sio muhimu ‘kihivyo’ kwa Marekani ilhali taifa hilo linazitegemea mno tawala za kibabe za nchi kama Misri au Saudi, hususan katika masuala ya ushushushu/mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa.

Kuhusu suala la Sheria ya Uhalifu wa Mtandao, hapa kumesheheni unafiki, na upo wa aina mbili: wa Wamarekani na wa sie Watanzania wenyewe. Mie ni mfuatiliaji wa karibu wa masuala ya usalama mtandaoni, ambao kwa namna moja au nyingine unahusiana na hiyo ishu ya Cybercrime Act. Kwa kifupi tu, Marekani ina sheria kandamizi mno dhidi ya uhuru wa raia mtandaoni. Naamini ushaskia kuhusu jamaa anayeitwa Edward Snowden (kama hujamsikia, Wasiliana na Google…haha). Huyu bwana alikuwa mtumishi katika shirika la ushushushu la Marekani linalohusika na kunasa mawasiliano mbalimbali (NSA – National Security Agency), na baadaye nafsi yake ilimsuta, akaamua ‘kuingia mitini’ na kumwaga siri lukuki kuhusu jinsi NSA inavyohujumu haki za raia kimawasiliano. Hawa jamaa wamekuwa wakinasa mawasiliano ya takriban kila mtu, wakishirikiana kwa karibu na mashushushu wenzao wa hapa Uingereza, GCHQ, taasisi ya kishushushu inayohusika na kunasa mawasiliano.

Lakini hata tukiweka kando suala la NSA kunasa mawasiliano mbalimbali (waliwahi kuzua kasheshe kubwa baada ya mashushushu wa Ujerumani kubaini kuwa NSA walikuwa wakinasa kwa siri mawasiliano ya Kansela Angela Markel hadi waliposhtukiwa), mashambulizi ya kigaidi nchini humo mwaka 2001 yalipelekea kuundwa kwa sheria kali kabisa dhidi ya uhuru wa habari na haki za kibinadamu kwa kisingizio cha usalama wa taifa. Kwahiyo, kwa kifupi, ni uhuni tu wa Marekani kudai Sheria ya Makosa ya Mtandaoni inakiuka uhuru wa Watanzania. Sheria zao za wazi na za kificho ni mbaya mara milioni zaidi yetu.

Hata hivyo, katika suala hili la Cybercrime Act, tuna wanafiki kadhaa huko nyumbani. Kwa kumbukumbu tu, mie nilikuwa mtetezi mkubwa wa muswada uliozaa sheria hiyo, yaani Cybercrime Bill, na niliunga mkono kwa nguvu zote jitihada za aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kuhusu muswada huo.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaoinyooshea kidole Marekani na wafadhili wengine kuhusu suala la Tanzania kukatiwa misaada walikuwa mstari wa mbele kuziomba nchi wahisani ziingilie kati kuibana serikali ili muswada huo usipitishwe kuwa sheria. Sasa kama uamuzi huo wa Marekani umechangiwa na ‘kelele’ zao hizo, kwanini leo wanalalamika?

Mie niliunga mkono muswada na sheria hiyo kwa sababu ikitumiwa vema ni nzuri. Hebu nenda Instagram kaangalie uanaharamu unaoendelea huko, kuanzia picha za uchi, ushoga na kila aina ya laana. Huo sio uhuru wa habari, ni uwendawazimu ambao kwa hakika ulihitaji sheria kali kuudhibiti.

Na watu waliopita huku na kule kudai sheria hiyo ni kandamizi na ililenga kuwabana wananchi wasiwasiliane, hawatuambii kama baada ya sheria hiyo kupitishwa wameshindwa kuwasiliana na watu wengine. Kwa kifupi, kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika kambi ya waliopinga muswada na sheria hiyo. Walitumia uelewa mdogo wa wananchi wengi kuhusu masuala ya mtandao, na kuwajenga hofu feki.

Ninakerwa kuona kundi la wanafiki hawa likiilaumu MCC au Marekani au nchi nyingine wahisani kuhusu suala la kutukatia misaada, kwa sababu wao walikuwa mstari wa mbele kuhamasisha nchi wahisani zichukue hatua, na ‘hatua maarufu’ ya wahisani huwa ni kukata misaada. Badala ya kulalamika, wanafiki hawa wanapaswa kufanya sherehe maana wishes zao zimetimia.

Sasa niangalie upande wa athari za uamuzi huo wa MCC kukata misaada. Taarifa nyingine zinaeleza kuwa kuna wahisani wengine nao wamekata misaada japo kuna mkanganyiko kama hatua hiyo ni mwendelezo wa hatua za huko nyuma au ni mpya.

Tuwe wakweli, kwa watu masikini kama sisi, hatua yoyote ile ya kutupunguzia msaada wa aina yoyote ile itatuathiri. Hilo halihitaji uelewa wa jinsi gani misaada inavyofanya kazi au jinsi gani nchi yetu ilivyo mtegemezi mzoefu wa misaada. Tatizo kubwa hapa kuhusu “kukatiwa misaada kutatuathiri au hakutatuathiri” ni tofauti zetu za kiitikadi. Kwa kiasi kikubwa, suala hilo linaangaliwa katika lensi ya u-CCM na u-UKAWA/Upinzani. Kwa wana-CCM, ni mwendo wa ‘kiburi’ kwenda mbele, kwamba “waende tu na misaada yao,” au “hela yenyewe ilikuwa ya mradi wa kifisadi wa Symbion,” mara “ah misaada gani hiyo yenye masharti kibao.” Wanamhadaa nani? Kama misaada hiyo haikuwa na muhimu, kwanini basi tuliiomba in the first place? Hizi hadithi za sungura kusema “sizitaki ndizi hizi” baada ya kushindwa kuzikia mgombani.

Kwa upande wa wana-UKAWA/Wapinzani, bila kujali kuwa wao kama Watanzania ni wahanga watarajiwa wa uamuzi huo wa nchi yetu kukatiwa misaada, wanakenua meno yote 32 kwa furaha, huku wakiwazodoa wenzao wa CCM kwa vijembe kama “ndio matunda ya ubabe wenu huko Zanzibar, tuone sasa…” au “mtaisoma namba” au “mtakula jeuri yenu…”

Ulemavu huu wa kifikra unaosababishwa na kuliangalia suala la kiuchumi kwa mtizamo fyongo wa itikadi za kisiasa. Naam, suala la Zanzibar ni la kisiasa, lakini athari za uamuzi wa Marekani/MCC/wahisani ni la kiuchumi.

Mie sio mchumi ila ninachoelewa fika kuwa uchumi wetu umekuwa tegemezi tangu tupate uhuru. Kabla ya kuipa kisogo siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, tulikuwa tukapata misaada kutoka kwa marafiki zetu wa mrengo wa Ukomunisti. Baada ya kuuzika Ujamaa, tumekuwa kama puto linaloyumbishwa na upepo, tupo radhi kumpigia magoti yeyote anayeweza kutusaidia. Kimsingi, tuna ombwe la kiitikadi: majukwaani, CCM wanasema sie ni Wajamaa, vitendo vyetu havipo kwenye Ujamaa wala Ubepari, tupu tupo tu. Huo ndo ukweli mchungu kuhusu ubabaishaji wetu.

Kwahiyo, tuache kudanganyana kuwa kukatiwa misaada hakutotuathiri. Huko ni kujipa jeuri tu. Tunachoweza kukubaliana ni kwamba suala hilo limeshatokea, tumeshakatiwa misaada, na si ajabu wahisani wengine wakaamua kufata mkumbo na kufanya hivyo pia.

Jukumu letu kubwa kwa sasa sio kuendelea kunyoosheana vidole bali tuwe kitu kimoja kama taifa bila kujali nani hasa aliyetusababishia tatizo hili. Ni tatizo la Watanzania wote bila kujali itikadi zao. Uamuzi wa wahisani kukata misaada utawaathiri wana-CCM wanaodai hautowaathiri kama ambavyo utawaathiri wna-CUF au Chadema wanaokenua meno yote 32 kufurahia hatua hiyo. Na utatuathiri (angalau kisaikolojia) hata akina sie ambao itikadi yetu pekee ni Tanzania yetu. Huo ni ukweli usiopingika: we are all in this together.

Kuna mambo mawili ya kupigiwa mstari. Kwanza, kwa miaka mingi tumekuwa tukiishi kifahari mno kuliko uwezo wetu. Na kimsingi, uwezo wetu duni haukupaswa kuwepo kwani sie sio masikini hata kidogo. Tuna kila aina ya utajiri lakini kuna majambazi walioigeuza Tanzania yetu kuwa kitu cha kubakwa kila kukicha. Kila mwenye uelewa anafahamu kilichojiri katika takriban miaka 30 iliyopita. Tanzania yetu ilikuwa shamba la bibi, watu wanafisadi wapendavyo kiasi kwamba kuwa na uchungu na nchi ilionekana kama wendawazimu.

Kwa bahati nzuri, Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha baadhi yetu na sasa tumempata Rais, Dkt John Magufuli, ambaye anaonekana amedhamiria kurekebisha mwenendo wa mambo. Kikwazo chetu kikubwa kilikuwa ufisadi, lakini sasa Magufuli ameamua kuvalia njuga kupambana na ufisadi kwa nguvu zote. Mwanzo ni mgumu lakini angalau dalili za mafanikio zimeanza kujionyesha. Tumuunge mkono, tuchukie ufisadi, tuongeze uzalendo, tuikwamue Tanzania yetu, tujikwamue nasi wenyewe, tuache kutafuta njia za mkato za mafanikio, tufanye kazi, tache majungu na kusaka sifa za kijinga mitandaoni, tuwajibike.

Twahitaji kujifunga mikanda. Haiwezekani wafadhili wetu waishi kimasikini ilhali sie wafadhiliwa twaishi kama matajiri. Viongozi wetu waache kuchuana na wauza unga kushindana jinsi ya kuishi kitajiri, wawabane wauza unga hao, majangili na maharamia wengine ili tuiokoe Tanzania yetu.

Je twaweza kujitegemea? Absolutely, lakini tusidanganyane kuwa twaweza kufanya hivyo ghafla ghafla. Tukumbuke, mtoto hazaliwi akatembea. Tumekuwa wategemezi mno wa misaada kiasi kwamba tumesahau kuwa twapaswa kujitegemea. Twahitaji kuchukua na kukubali maamuzi magumu ya kutuwezesha kujitegemea. Ni kama kumlazimisha mtoto anayetambua aanze kutembea kwa nguvu. Sio rahisi, lakini tukimkazania anaweza kusimama mwenyewe na baadaye akaweza hata kukimbia. Hilo linahitaji kujitoka mhanga kwa ajili ya nchi yetu, sambamba na kuweka mbele uzalendo badala ya maslahi binafsi.

Jambo jingine, kwa hisia zangu, japo suala la Zanzibar na Cybercrime Act zinatajwa kama sababu za uamuzi wa kutunyima misaada, ninashawishika kuamini kuwa baadhi ya nchi wahisani hawapendezi na kasi ya Rais Magufuli kuziba mianya ambayo kimsingi licha ya kuwanufaisha mafisadi wa ndani, ilikuwa pia inanufaisha taasisi za kifisadi za kimataifa. Wengi wa majambazi waliokuwa wakitupora fedha zetu mchana kweupe walikuwa hawahifadhi fedha zao katika benki zetu bali zilizopo kwa hao wahisani wetu. Waweza kudhani huu ni utani mbaya, lakini jiulize, je kama unamfadhili mtu pesa za kumsaidia yeye na familia yake, lakini anatumia fedha hizo kununulia bling bling, kuongeza nyumba ndogo, kufanya matumizi ya anasa, nk kwanini usichukue hatua?

Mfano huo unamaanisha hivi: kwanini wahisani wetu walionekana kutokerwa na jinsi pesa walizokuwa wanatupatia zikifisadiwa kila kukicha lakini wakaendelea kutumwagia misaada? Na kwanini sasa, tumempata Magufuli ambaye amepania kwa dhati kupambana na ufisadi, wahisani wanaanza kuleta ‘longolongo’?

Kuna tunaodhani kuwa hao wahisani wanataka tuendelee kuwa wategemezi wao milele. Kwa upande mmoja utegemezi wetu unawapa uhuru wa kukwapua kila raslimali tuliyonayo, na kwa upande mwingine, wananeemesha taasisi zao za fedha kwa vile mafisadi wetu wa ndani wanahifadhi fedha zao kwenye taasisi hizo.

Mwisho, tuache porojo, tuache unafiki, tuwe kitu kimoja, athari za kukatiwa misaada zipo, tukishikamana tutaweza kukabiliana nazo japo mwanzoni itakuwa ngumu. Yawezekana uamuzi huo wa Wamarekani ukawa ‘blessing in disguise’ kwa maana ya kutupa ‘wake-up call’ tuanze kujitegemea kwa lazima badala ya kutembeza bakuli letu huko na kule, kisha kile kidogo kinachopatikana kikaishia kwenye ujenzi wa mahekalu ya mafisadi, ongezeko la magari yao ya kifahari, na kutanua ukubwa wa nyumba ndogo zao.

MUNGU IBARIKI TANZANIA 

20 Feb 2008

Makala yangu katika toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema inazungumzia UHURU.Inaanza kwa kuhabarisha kuhusu tangazo la Uhuru wa Kosovo,kisha inachambua "urafiki mpya" wa Marekani na China kwa Bara la Afrika na kuhitimisha kwamba urafiki huo ni mithili ya Mkutano wa Berlin 1884-5 ulioligawa bara la Afrika miongoni mwa wakoloni.Makala hii inakumbushia pia kwamba kuna uwezekano ziara ya Bush barani Afrika ikabaki kumbukumbu muhimu kwake kutokana na namna alivyonyenyekewa katika kipindi ambacho ni mmoja ya marais wanaochukiwa sana katika sehemu mbalimbali duniani,na very unpopular nyumbani kwake US of A.Kadhalika makala inawashikia bango Mwanyika na Hosea kwamba wajiuzulu haraka sana,sambamba na wale wote waliotajwa kwenye ripoti ya Tume ya Mwakyembe.Pamoja na makala nyingine zilizokwenda shule ya hali ya juu,bingirika na makala hiyo kwa KUBONYEZA HAPA.

17 Feb 2008

Muda mchache uliopita,Kosovo imejitangazia uhuru wake ikiahidi kuwa nchi ya kidemokrasia,katika hatua inayoungwa mkono na Marekani na nchi nyingine za Magharibi lakini ikipingwa vikali na Russia na Serbia.

Spika wa Bunge Jakup Krasniqi,Waziri Mkuu Hashim Thaci na Rais Fatmir Sejdiu,ndio waliosaini tangazo hilo la uhuru ambalo limepokelewa kwa nderemo na vifijo katika nchi hiyo,hususan katika mji mkuu Pristina ambapo maandalizi ya shughuli hiyo yalianza kwa siku kadhaa.

Wakati hayo yakitokea,Rais wa Serbia Boris Tadic amelaani hatua hiyo ya Kosovo kujitangazia uhuru na kubainisha kuwa nchi yake haitambui uhuru huo wa Kosovo.Akijibu mashambulizi,Waziri Mkuu Thaci alisema kwamba kamwe Kosovo haiwezi kuwa tena chini ya himaya ya Serbia.Thaci,mpiganaji wa zamani wa Jeshi la Ukombozi la Kosovo ambalo kati ya mwaka 1998 hadi 1999 lilipambana na majeshi ya Serbia katika vita ya kudai uhuru iliyogharimu zaidi ya maisha 10,000.

Kwa undani zaidi kuhusu kuvunjika kwa nchi iliyokuwa ikijulikana kama Yugoslavia (unamkumbuka Tito!?) hadi kufikia Kosovo,bonyeza KIUNGANISHI hiki

9 Jan 2008


Baada ya Barack Obama kuibuka kidedea huko Iowa,kuna wengi walioanza kuamini kwamba sura mpya imefunguliwa katika siasa za Marekani.Mimi sikuwa mmoja wao,na ushahidi unapatikana kwenye makala zangu zilizopita kuhusu ushindi huo wa Obama.Katika toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema nimejaribu kuangalia namna imani na matumaini ya Obama yalivyomfikisha hapa alipo sasa.Napenda kusisitiza kwamba makala hiyo iliandaliwa kabla ya matokeo ya primaries huko New Hampshire ambapo Hillary Clinton ameibuka mshindi na kuwafanya baadhi ya wachambuzi wa siasa na waendesha kura za maoni "kulamba matapishi yao".

Nikipata muda mwafaka nitachambua kwa kirefu nini nachodhani kimechangia kugeuza upepo uliokuwa ukivuma kuelekea kwa Obama huko New Hampshire.Lakini kwa kifupi,nadhani waendesha kura za maoni waliokuwa wakimpa Obama nafasi kubwa ya ushindi huku wakitabiri kuwa Hillary ataanguka walisahau namna Bradley effect inavyoweza kuwazuga watu pindi panapokuwa mgombea Mweupe na Mweusi.Kwa kifupi kabisa,Bradley effect ni tabia katika chaguzi za Marekani  ambapo  wapiga kura watarajiwa ambao hawajafikia uamuzi watampa nani kura zao (undecided voters) hutoa mtizamo tofauti na namna watakavyopiga kura.Kimsingi,tabia hii huchochewa na ubaguzi wa rangi ambapo undecided voters Weupe huweza kudai kuwa hawajaamua wampe nani kura au kudai kuwa watampa kura mgombea Mweusi lakini huishia kumpa kura mgombea Mweupe.

Kama nilivyosema awali,makala yangu kwenye Raia Mwema inahusu namna imani inavyoweza kuyapa nguvu matumaini ili kufikia malengo flani.Nafasi ya Obama imetumiwa kama kielelezo tu cha namna imani mbalimbali huko nyumbani (kwa mfano,kwamba maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana) zinavyoshindwa kuleta matumaini yanayokusudiwa kutokana na ufisadi,uzembe na ubabaishaji.Pamoja na makala nyingine zilizokwenda shule katika gazeti la Raia Mwema,bingirika na makala yangu hapa.

Baada ya kusoma makala hii sio vibaya ukiburudika na warembo hawa wa Blu3 na kitu chao Hitaji


7 Jan 2008


Kuna mengi yanasemwa kuhusu mwelekeo mzuri wa Barack Obama katika harakati zake za kuingia Ikulu ya Marekani baadaye mwaka huu.Lakini,je mafanikio ya Obama yanamaanisha kukubalika kwa asilimia 100 kwa mtu mweusi katika jamii ya Waamerika au ni matokeo ya kukwepa kile "weusi wenzie" kama Jesse Jackson na Al Sharpton wamekuwa wakikipigia kelele?
Nimekutana na makala hii katika toleo la leo la gazeti la Guardian la hapa Uingereza na nimeona ni vema nikakupa nafasi msomaji mpendwa wa blogu hii nafasi ya kuisoma na kutoa hukumu yako wewe mwenyewe.

Binafsi napenda kumuona mtu mweusi (au hata half-caste) akiwa White House,na kwa maana hiyo ingependeza endapo Januari mwakani Bush angempokea Obama kama "mkazi mpya" katika jumba hilo maarufu hapo 1600 Pennsylvania Avenue NW.Lakini sioni dalili ya hilo kutokea.Na kumbe siko peke yangu mwenye mtazamo wa namna hiyo.Naendelea kuamini kuwa White America bado haiko tayari kumuona mtu mweusi akiwa Rais wa Taifa hilo.Na pengine ndio sababu muhimu ya Republicans "kusherehekea" mafanikio ya Obama (wahenga wanatuonya kwamba ukiona adui yako anasherehekea ushindi wako basi ujue ushindi huo utamnufaisha).Wana sababu kuu mbili,moja,wanafahamu ugumu wa kumzuia Hillary Clinton kuingia Ikulu,na pili,wanafahamu wepesi wa kumwangusha Obama pindi akipitishwa kuwa mgombea wa Democrats.Niite prophet of doom lakini amin nakuambia,pindi Obama akishinda kuwa mgombea,basi shehena zote za White America za kumbomoa mwanasiasa zitaelekezwa kwake.Na atakuwa target rahisi kwao:watapigia mstari jina lake la kati la Hussein na kulikuza utadhani linamaanisha ugaidi (baadhi yao walishajifanya kuteleza ulimi na kumwita Barack Osama),watakumbushia confession yake kwamba zamani hizo alishawahi kubwia unga na kuvuta bangi.Anyway,ndani ya The Huffington Post kuna makala inayoelekea kurandana na mtizamo wangu kuhusu Obama.

Ukimaliza kusoma jipoze na clip hii ya Common featuring Dwelle iendayo kwa jina The People

28 Oct 2007

Asalam aleykum,

Kwanza nianze kwa salamu za rambirambi kwa familia,ndugu,jamaa na marafiki wa marehemu Salome Mbatia,aliyetutoka hivi majuzi kutokana na ajali ya gari.Sote ni wasafiri,mwenzetu ametutangulia tu,Bwana ametoa Bwana ametwaa,jina lake lihimidiwe milele.Baada ya rambirambi hizo naomba kuzungumzia suala moja ambalo kwa naona kwa namna flani linaathiri umoja wetu wa kitaifa.Jambo hilo ni kuendekeza itikadi za chama kwenye matukio ambayo kimsingi ni ya kitaifa zaidi kuliko kichama.Katika picha mbalimbali kuhusu msiba wa marehemu Mbatia nimeona “makada” lukuki wa chama tawala wakiwa katika magwanda yao ya kijani na nyeusi.Nikabaki najiuliza,hivi waungwana hao wangevaa mavazi yao ya kawaida wangeonekana hawana majonzi ya msiba huo?Au walivaa mavazi hayo kwa maagizo ya kiongozi flani?Kama ni maagizo kutoka ngazi za juu,mbona viongozi wakuu wa chama hicho walikuwa kwenye mavazi yao ya kawaida tu (hasa suti nyeusi)?JK,Malecela,Karume,Makamba,nk wote walikuwa wamevalia suti nyeusi na wala sio magwanda ya kijani na nyeusi,pengine kwa sababu msiba huo ulikuwa wa kitaifa,na hata jeneza la marehemu halikuvikwa bendera ya CCM bali ya Taifa.

Nafahamu marehemu Mbatia alikuwa mwanachama,kada na kiongozi wa chama dume,lakini marehemu pia alikuwa naibu waziri wa serikali ambayo japo inaongozwa na CCM lakini inawatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao.Katika utekelezaji wa majukumu yake ya unaibu waziri,marehemu Mbatia alikuwa akigusa maisha ya kila Mtanzania,awe mwanachama wa CUF,TLP,Chadema,au kama sie tusio memba wa chama chochote.Nafahamu waliovaa magwanda ya CCM watasema kuwa walitinga mavazi hayo kutokana na nafasi ya marehemu katika chama,lakini sote tunafahamu kuwa alama za chama (mfano bendera,vipeperushi,mavazi,nk) zina tabia ya kuvuta hisia hasi katika mikusanyiko ya isiyo ya kichama.Nafahamu pia kwamba kila mwombolezaji alikuwa na haki ya kuvaa vyovyote atakavyo lakini pia naamini wengi wetu tunapojiandaa kwenda kwenye misiba huwa tunatafakari nini cha kuvaa,na kuepuka mavazi ambayo yanaweza kuleta hisia tofauti.

Hakuna dhambi kuweka maslahi ya chama mbele ya chama kingine lakini ni dhambi kubwa kuweka maslahi ya chama mbele ya maslahi ya taifa.Chama cha siasa kinaweza kufa lakini taifa lazima liendelee kuwa hai.Mtu anaweza kuamua kuhama chama kimoja na kuingia kingine kadri apendavyo,lakini ni mbinde kwelikweli kuhama utaifa wako na kuchukua mwingine kirahisi namna hiyo.Nafahamu kuna watakaopingana nami,lakini binafsi naamini kwamba kuna wenzetu wamekuwa wakituletea “politiki” hata pale pasipostahili.Yaani matukio kadhaa ya kitaifa yamekuwa yakiporwa na hao wanaotaka kutuonyesha namna gani walivyo wakereketwa kwenye siasa.Na katika hili sio wanachama wa kawaida tu bali hata baadhi ya viongozi wenye nyadhifa serikalini.Kuweka kando mambo ya chama na kuzungumzia masuala ya kitaifa hakumfanyi kiongozi wa serikali kukosa sifa za uongozi.Kuna vikao na mikutano ya chama,na huko ndiko mahala pa kupiga propaganda za vyama.

Kwa kawaida huwa naanza makala zangu na habari za ughaibuni lakini niliona ni vema katika makala hii nikaanza na mada hiyo ya msiba wa marehemu Mbatia,na “kuwananga” wale walioleta mambo ya siasa kwenye msiba huo wa kitaifa.Huku ughaibuni,duru za kisiasa zinaelekea zaidi eneo la Ghuba ambapo kwa upande mmoja hali ya usalama ni ya wasiwasi huko kaskazini mwa Irak kwani majeshi ya Uturuki yameripotiwa kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya Wakurd.Waturuki wanadai kuwa lengo la mashambulizi hayo ni kuwadhibiti wapiganaji wa kikundi cha PKK kinachipigania kuunda kwa taifa huru la Wakurd.Kwa upande mwingine,kuna dalili kwamba Marekani inajiandaa kuivamia Iran.Majuzi,Marekani ilitangaza vikwazo kadhaa dhidi ya Iran,lakini zaidi ya hapo kuna taarifa kwamba jeshi la anga (US air force) limeomba fedha za dharura dola milioni 88 kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye ndege za kivita ziitwazo B2 ili ziweze kuhimili uzito wa mabomu yanayojulikana kama “Big Blu” au “the Mother of All Bombs” (mama wa mabomu yote).Mabomu hayo yana uzito wa takriban tani 13 kila moja,na yana uwezo mkubwa zaidi wa kupenya vizuizi (ardhi,miamba,nk).Inasemekana kuwa majengo ya kituo cha nyuklia cha Iran huko Natanz yapo futi 75 chini ya ardhi,Inaelezwa pia kwamba tayari Marekani imeshatambua “targets” 1000 nchini Iran ambazo zitakuwa za kwanza kushambuliwa pindi mambo yatapokuwa mambo.

Mahesabu ya kisiasa yanaashira pia kwamba wazo la mkutano kati ya Israel na Palestina utakaofanyika hivi karibuni huko Annapolis,Marekani (ambao unatarajiwa “kuzaa” taifa la Palestina) ni miongoni mwa dalili za Marekani kujipanga kuivamia Iran.Yaani mantiki hapo ni kwamba kwa kuunda taifa la Palestina,kelele za mataifa ya Waarabu wa Sunni kama Saudi Arabia na Misri zitakuwa sio kubwa sana pindi Iran itakaposhambuliwa na Marekani.Hata hivyo,wazo la kuishambulia Iran linaangaliwa kwa wasiwasi na baadhi ya wajuzi wa siasa za kimataifa na diplomasia.Kuna wanaodhani kwamba ni vema Marekani ikamaliza kibarua ilichojipachika huko Irak na Afghanistan kabla ya kukimbilia kuivamia Iran.Pia wanaonya kwamba uvamizi dhidi ya Iran unaweza kuzua wimbi kubwa la ugaidi wa kimataifa (pengine kutokana na madai kwamba Iran imekuwa ikivisaidia baadhi ya vikundi vinavyodaiwa kuwa vya kigaidi,mfano Hizbollah),kukongoroa kabisa hali ya usalama nchini Irak na pengine kusababisha bei ya mafuta kupanda zaidi ya dola 100 kwa pipa.

Sababu zinazotolewa na Marekani kuhusu umuhimu wa kuidhibiti Iran ni pamoja na kwamba dunia itakuwa mahala salama zaidi iwapo Iran haitakuwa na uwezo wa kutengeneza au kumiliki silaha za nyuklia (ilishasemwa huko nyuma kuwa dunia itakuwa salama zaidi pindi Saddam Hussein atapong’olewa madarakani).Ukweli ni kwamba Iran yenye uwezo wa kinyuklia ni tishio kwa swahiba mkuu wa Marekani,Israel.Pia kuna wanaotaka Bush aingie kwenye vitabu vya historia kwa “kuiadhibu na kuidhibiti Iran na hivyo kuepusha madhara yanayoweza kutokea pindi nchi hiyo ikiweza kutengeneza na kumiliki silaha za maangamizi”.Waumini wa mawazo haya wanatambua kuwa Bush amebakiwa na muda mchache kabla hajafungasha virago vyake kutoka jengo lilipo namba 1600 Pennsylvania Avenue (makazi ya rais,White House),na wanadhani kwamba asipotumia muda huu kuishikisha adabu Iran,basi inaweza kuwa vigumu mno kufanya hivyo mbeleni hususan iwapo mgombea yoyote wa chama cha Democrats atamrithi Bush.

Nirejee tena huko nyumbani.Hapa nina mawili.Kwanza,katika kikao kilichopita cha Bunge tulisikia namna baadhi ya watendaji katika Wizara ya Maliasili na Utalii wanavyoendeleza ufisadi.Waziri alieleza kuwa ameshakabidhi orodha ya wahusika mahala panapostahili,na akaahidi kuendelea kuwabana mafisadi katika wizara hiyo.Tukio la hivi karibuni ambapo magogo kadhaa yalikamatwa yakiwa tayari kusafirishwa nje,limezuia “mchezo wa kuigiza” ambapo wakati Waziri anasema hivi baadhi ya watendaji wake wanadiriki kumpinga hadharani kwa kusema vinginevyo.Hivi hawa wanaompinga Waziri wanapata jeuri hiyo wapi?Nimeona kwenye gazeti la “Habari Leo” ambapo Waziri Maghembe alieleza kwamba amejipanga vizuri kukabiliana na matatizo yote ndani ya wizara yake,ikiwa ni pamoja na tatizo la ufisadi.Yayumkinika kutabiri kuwa dhamira yake nzuri inaweza isifanikiwe kutokana na kiburi kilichojengwa na baadhi ya anaowaongoza katika wizara hiyo ambapo bila kujali protokali au nidhamu wanadiriki kupinga hadharani na kauli halali ya serikali (kupitia waziri wake).Hivi jeuri,kiburi na kujiamini kwa “wazalendo” hao inatoka wapi?

Mwisho,ni ushindi wa Simba dhidi ya Yanga.Mwenye kununa na anune,lakini ndio hivyo tena,milioni 50 hazikufanikiwa kumaliza uteja wa watani wetu wa mtaa wa Jangwani.Nilishatabiri katika makala za nyuma kuwa atakaefungwa kwenye mapambano wa watani wa jadi ataingia kwenye mgogoro.Mie nadhani kufungwa huko ni sehemu ndogo tu ya tatizo linaloikabili Yanga.Ukiangalia maelezo aliyotoa Mwenyekiti wa klabu hiyo pale mfadhili wao alipojitoa (kwa muda!?) ambapo alieleza kwa undani na kwa kuzingatia vipengele vya sheria kuhusu utata uliopo kwenye suala zima la klabu hiyo kugeuzwa kampuni.He!!muda si mrefu Mwenyekiti huyohuyo alisikika tena akipita huku na kule kuomba radhi.Je ina maana yale maelezo aliyotoa awali hayakuwa sahihi?Mie naamini yalikuwa,bado yako na yataendelea kuwa sahihi kama kweli Yanga (na Simba pia) wanataka wafike sehemu wakajiendesha wenyewe kwa mafanikio na kuachana na utegemezi.Yote yanawekana iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake.

Alamsiki

12 Sept 2007

Asalam aleykum,

Katika makala yangu iliyopita,nilizungumzia kuhusu kile ambacho wachambuzi wa siasa za kimataifa wanakiona kama kurejea kwa kasi kwa mbio za silaha (arms race) zenye uwezo mkubwa na wa kisasa zaidi kuliko hapo awali au sasa.Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeonekana kuguswa na namna Russia inavyoongeza kasi katika teknolojia na uzalishaji wa silaha za kisasa.Muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii,nimeona taarifa moja inayoeleza kuwa Russia imefanikiwa kufanya majaribio ya kile inachokiita “Baba wa Mabomu Yote” (Father of all Bombs).Teknolojia hiyo mpya inaelezwa kuwa na uwezo mara nne zaidi ya ile ya Marekani inayojulikana kama “GBU-43 Massive Ordnance Air Blast” (MOAB) au “Mother of all Bombs” (yaani “Mama wa Mabomu Yote”) ambayo ilifanyiwa majaribio yenye mafanikio mwaka 2003.Tofauti na teknolojia ya awali ya mabomu,hilo la kisasa la Russia ni la “thermobaric,” yaani linatumia oksijeni iliyopo hewani (atmospheric oxygen) kusababisha mlipuko badala ya kutumia kemikali nyingine (oxidizing agent) kuleta matokeo hayo (mlipuko).Silaha za ki-“thermobaric” zina tabia ya kutoa nishati kubwa zaidi kuliko zile zisizotumia teknolojia hiyo,na inaelezwa kwamba bomu hilo jipya la Russia lina uwezo wa kuteketeza kabisa maisha katika eneo mzunguko la maili nne.

Kinachochochea mbio za silaha ni sawa na kile wanafalsafa wanachokiita “domino effect” yaani badiliko (change) moja linapelekea badiliko jingine jirani,nalo linapekea badiliko jingine,na jingine kwa jingine,na kadhalika.Yaani ni kama kugongwa gari la kwanza kwenye foleni ndefu ambapo la kwanza litaligonga la pili,la pili litaligonga la tatu,na kadhalika,na kadhalika.Kwa Russia kutambulisha mafanikio yake hayo,ni dhahiri kwamba Wamarekani nao watakuna vichwa ili waibuke na teknolojia kali zaidi ya hiyo ya Russia (pengine wataamua kuiita “babu wa mabomu yote” maana tayari tuna “baba” na “mama,” na si ajabu Russia nao watajibu mapigo kwa kuja na “bibi wa mabomu yote”).Wajuzi wa mambo wanadai kuwa miongoni mwa mambo yanayoichochea Russia kuelekeza nguvu zake kwenye uboreshaji wa teknolojia ya silaha ni faida kubwa inayopata nchi hiyo kwenye biashara ya mafuta na gesi,na ukweli kwamba Rais Putin alikuwa shushushu mwandamizi ndani ya shirika la kijasusi la uliokuwa Muungano wa Jamuhuri za Kisovieti (USSR) ambapo shirika hilo lilikuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya teknolojia ya silaha.
Habari nyingine “nyepesi” kutoka Russia zinasema kwamba jiji la Ulyanovsk nchini humo limetoa “off” kwa wafanyakazi wote ili wapate fursa ya kufanya tendo la ndoa katika maadhimisho ya “Siku ya Kutunga Mimba jijini Ulyanovsk” (the Day of Conception in Ulyanovsk).Ruhusa hiyo ya mapumziko imetolewa kama sehemu ya mpango wa manispaa ya jiji hilo ujulikanao kama “Give Birth to a Patriot” (Zaa Mzalendo) ambapo watakaofanikiwa kudunga au kudungwa wanaweza kuibuka na zawadi ya gari,fedha au friji.Jiji hilo ndipo alipozaliwa Vladmir Lennin, na mpango huo wa kuhamasisha uzazi ni sehemu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Lenin mwezi huu.Washindi wanatarajiwa kupatikana kwa kuzingatia heshima ya ndoa yao pamoja na sifa bora kama wazazi,na watapatikana kutokana na maamuzi ya jopo la majaji.Mambo hayo!!

Kabla ya kugeukia masuala ya huko nyumbani,ngoja nizungumzie suala moja ambalo mie binafsi linanigusa.Nilipokuwa Mlimani (UDSM) nilibahatika kuchukua somo liitwalo “Gender and Family Relations” (yaani Jinsia na Mahusiano ya familia).Naomba kukiri kwamba kabla ya hapo,sikuwa na uelewa wa kutosha kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii na picha nzima ya usawa wa kijinsia katika jamii mbalimbali.Sasa majuzi nilisoma gazeti la Guardian la hapa Uingereza na kukutana na habari isemayo kwamba serikali (ya hapa) ina mpango wa kuwachukulia hatua wanaume wanaonunua huduma ya ngono.Kimsingi,huduma nyingi,ikiwemo ngono,huhusisha mtoaji huduma na mpokeaji huduma,lakini katika dunia yetu ambayo tumezowea kuyaona makosa ya wanawake pekee ilhali yetu wanaume yakionekana ni ya “ya kishujaa,” suala la ukahaba limeendelea kwa kiasi kikubwa kuwa kosa la wanawake wanaojihusisha na biashara hiyo kuliko wateja wao ambao ni wanaume (hapa sizungumzii ukahaba kati ya watu wa jinsia moja).Neno “malaya” ni maarufu zaidi kuliko neno “fuska” na baadhi ya wachambuzi wa mahusiano ya jamii wanadai hiyo inasababishwa na tabia ya kuona matendo hasi (negative) ya mwanamke kuwa mabaya zaidi ya yale hasi ya mwanaume.Hata linapokuja suala la nyumba ndogo,tunashuhudia kuwa ni rahisi kwa mwanaume kuwa nazo hata 10 kama ana uwezo wa kuzimudu lakini mwanamke akijaribu hilo basi muda si mrefu anaweza kujikuta anafungashiwa virago vyake.Nchi za Magharibi zimepiga hatua flani katika kuleta usawa wa kijinsia,na miongoni mwa mitihani mikubwa katika eneo hilo ni ugombea (candidacy) wa Hillary Clinton kwenye kinyang’anyiro cha kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat.Na mshawasha zaidi unaeletwa na mgombea mwingine kutoka jamii ambayo hadi sasa bado inaonekana ni ya kuongozwa zaidi badala ya kuongeza,yaani watu weusi (Blacks).Historia inasubiri kuandikwa iwapo Hillary atafanikiwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Marekani,au Barack Obama atafanikiwa kuwa Mweusi wa kwanza kuwa rais.Bibi,mama na dada zetu wanastahili pongezi (au hukumu) sawa na sie akina kaka,baba na babu.

Sasa mambo ya huko nyumbani.Nilipigwa na butwaa niliposoma habari katika gazeti moja la nyumbani kuwa huko Mwanza kampeni za kugombea uongozi wa CCM ziligeuka kuwa uwanja wa vita pale washabiki wa kambi za wagombea flani walipoamua “kufanyiana kweli” na kutupiana mawe.Sijui wangapi walijeruhiwa katika patashika hiyo lakini nachoshindwa kuelewa ni namna kila raslimali,ikiwemo vurugu,inavyotumika kutafuta uongozi wa kisiasa.Hivi kuna nini huko kwenye uongozi hadi watu watake kutoana roho?Yaani ukereketwa umekolea namna hiyo hadi watu wawe tayari kuweka rehani usalama wao kwa ajili ya mgombea flani?Cha kusikitisha ni kwamba si ajabu wapambe hawa hawa ndio watakuwa wa kwanza kulalamika kuwa mgombea wao “hafai” pale atapowatelekeza baada ya kupata anachohitaji (uongozi).Pasipo busara za haraka kutumika tunaweza kujiwekea katika mahali pabaya sana kama tutawaruhusu baadhi ya watu kuhatarisha amani kwa vile tu wanataka kupata uongozi.

Nimesoma pia ushauri wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM,Philip Mangula,ambaye baada ya kubwagwa huko Iringa alitahadharisha kwamba kuna wakati itafika uongozi wa chama hicho utagombewa kwa mfumo wa tenda (bid) na “bidder” mkubwa ndiye atakayeibuka kidedea.Pengine ana hoja ya msingi hapo,lakini inaweza kufunikwa na ukweli kwamba haya anayoyaona sasa yamekuwa yakitokea kwa muda mrefu,na kipindi hicho alikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya sio tu kukosoa bali hata kukomesha matumizi ya “takrima” kwenye kusaka uongozi.Hata wazo lake kwamba ni vema kwa wanachama wa CCM wenye madaraka mengine (kama ubunge au uwaziri) wakatoa mwanya kwa wale wasio na madaraka (japo sio kosa,si ajabu baada ya uchaguzi huu kumkuta mtu akiwa na vyeo zaidi vitano) mawazo hayo yangekuwa na “mwangwi” mkubwa zaidi iwapo yangetolewa katika kipindi ambacho Mangula alikuwa madarakani.Yayumkinika kusema kuwa ni vigumu kurekebisha mapishi pindi ukiwa nje ya jiko,na majaribio ya kufanya hivyo nje ya jiko yanaweza kutafsiriwa tofauti na baadhi ya watu.

Na huko Morogoro,baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa miongoni mwa nafasi katika mkoa huo,Waziri Ngasongwa nae “aliwatolea macho” TAKUKURU kwa kile alichodai walishindwa kuzuwia baadhi ya wagombea kutoa “takrima” kwa wapiga kura.Swali pana zaidi ni je waziri anadhani taasisi hiyo ilishindwa (kwa mujibu wake) kutekeleza majukumu yake kwa vile ni sehemu ya mapungufu yake ya kila siku au ni katika tukio hilo tu?Iwapo jibu ni hilo la pili basi wapo wanaoweza kuhisi kuwa waziri ameweza kuona matatizo hayo kwa vile tu yamemgusa yeye binafsi. “Bottom line” ni kwamba iwapo mlolongo wa vimbwanga vinavyoendelea kwenye uchaguzi wa CCM vitachukuliwa kuwa ni mambo ya kawaida tu basi tunaweza kufika mahala tukajilaumu huku tukisema “laiti tungejua wakati ule…”Bahati mbaya,kwa wakati huo tutakuwa tumechelewa kuweza kufanya mabadiliko yoyote ya msingi.Ushauri huu sio wa kupandikiza chuki bali ni kwa ajili ya hatma ya taifa letu kwa manufaa yetu sasa na kwa vizazi vijavyo.

Neno la mwisho kabisa ni kuungana na wapenzi na mashabiki wa msanii maarufu anti Shenaz ambaye alikutana na mauti kwenye ajali ya basi huko Mbeya.Kwa tunaomfahamu,dada huyo alikuwa akipendezesha kila shughuli aliyokuwepo.Na tofauti na umaarufu wake,alikuwa mcheshi na asiye na chembe ya dharau.Mungu airehemu roho ya marehemu,Amina.

Alamsiki


2 Aug 2007

Asalam aleykum,

Wanasema kuwa siasa inahitaji kuwa na mvuto (appeal).Lakini mvuto wa mwanamama Myra Bushell,mshindi wa uchaguzi mdogo wa kanseli kwa tiketi ya chama cha Liberal Democrats cha hapa Uingereza,ni zaidi ya mvuto wa kawaida unaohitajika kwenye siasa.Myra aligombea na kushinda nafasi ya uwakilishi kwenye kanseli ya Bideford huko Devon,huku akiwa ni mcheza-uchi/nusu uchi kwenye vilabu (stripper) na mwendesha huduma ya ngono-kwa-simu (phone-sex-line) ambayo anachaji pauni 1.50 kwa dakika (takriban shilingi 3500 za huko nyumbani).Yeye anajitetea kuwa hayo ni maisha yake binafsi nje ya siasa,lakini tayari wajumbe watatu wa kanseli hiyo wameshajiuzulu kupinga vitendo vya mwanasiasa huyo ambaye pia ana tovuti yake ya huduma za ngono.Myra anajitetea kwamba wakati anautumikia umma kama mwanasiasa,anapaswa pia kumudu gharama za maisha,na ndio maana amekuwa akijihusisha na shughuli hizo “nyeti.” Habari njema kwake ni kwamba katibu (clerk) wa kanseli hiyo,George McMauchlan,ametamka bayana kuwa Myra hajavunja sheria yoyote ya maadili ya kazi ya ujumbe wa kanseli kwa vile “shughuli zake binafsi nje ya siasa” haziathiri utendaji wake wa kazi.Kaazi kweli kweli!!


Tukiachana na habari hizo za mwanasiasa “stripper”, kwa takriban wiki nzima iliyopita,medani za sera za nje za Marekani ilikuwa imetawaliwa na habari kwamba taifa hilo lilikuwa linajiandaa kutekeleza mpango wa kuziuzia silaha baadhi ya nchi za Kiarabu na Mashariki ya Kati.Wanufaika wakubwa wa mpango huo ni pamoja na Saudi Arabia,Misri,na kama ilivyo ada,Israel.Hata hivyo,mpango huo umezaa mvutano wa namna flani kwenye duru za siasa za ndani za Marekani kwani wapo wanaodhani kwamba hoja ya serikali ya Bush kuwa inaziuzia silaha nchi kama Saudi Arabia na Misri ili,pamoja na mambo mengine,kudhibiti kujitanua kijeshi kwa Iran,inaweza kupingana na ukweli kuwa rafiki wa leo anaweza kuwa adui wa kesho,na silaha unazompatia leo kujilinda zinaweza kutumika kesho kukudhuru.Na mpango huu umekuja wakati wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaoona kuna kuyumba kwenye urafiki wa muda mrefu kati ya Marekani na Saudi Arabia.Hivi karibuni,Saudi iliweka bayana mtizamo wake kuhusu vita ya Irak kwa kusema kuwa uvamizi wa Marekani nchini Irak unachochea machafuko na suluhisho pekee ni kwa majeshi ya kigeni kuondoka nchini Irak.Pia kumekuwepo shutuma za hapa na pale kwamba Saudi Arabia inavisapoti vikundi vya madhehebu ya Sunni nchini Irak ili kuvikabili vikundi vya madhehebu ya Shia ambavyo inadaiwa vinapata sapoti ya Iran.Kitakwimu na kujiografia,Saudi ni taifa la ki-Sunni wakati Iran ni la ki-Shia,na mahusiano kati ya nchi hizo mbili sio mazuri.Saudi kwa upande wake inahofia sana kukua kwa nguvu za kijeshi za Iran,hasa kwa vile hadi sasa,ukitoa Israel,Saudi ni taifa lenye nguvu kubwa katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati.

Wakati mwingine ni vigumu kuzielewa sera za nje za Marekani kwani kwa jinsi flani ilipaswa kujifunza kutokana na maamuzi yake ya zamani ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakiiumiza kichwa katika kipindi hiki tulichonacho,kwa mfano msaada wake wa silaha kwa Irak wakati Saddam alipokuwa rafiki wa nchi hiyo,na misaada yake kwa mujahidina wa Afghanistan wakati wa vita dhidi ya Muungano wa nchi za Kisovieti (USSR).Tawala za nchi nyingi za Kiarabu na Ghuba sio za kidemokrasia (kwa vipimo vya nchi za magharibi),na miongoni mwa sababu zinazodaiwa kuchangia kuibuka kwa siasa za msimamo mkali wa kidini katika nchi hizo kushindwa kwa tawala hizo kuleta mabadiliko ya manufaa ya kisiasa,kiuchumi na kijamii.Lakini katika kukoroga zaidi mambo,baadhi ya tawala hizo zimekuwa zikuvikumbatia na kuvifadhili vikundi vyenye msimamo mkali wa kidini ili tawala hizo ziendelee kuwa madarakani.Kwa uchambuzi mwepesi,yayumkinika kusema kuwa hatma ya tawala hizo kwa muda mrefu sio ya kuaminika sana,na Marekani inaweza kujutia huko mbeleni kwa kuzilinda tawala hizo kwa misaada ya kijeshi.

Na taarifa zaidi kutoka Irak zinaeleza kuwa “picha haziivi” kati ya mkuu wa majeshi ya Marekani nchini humo,Jenerali David Petraeus,na Waziri Mkuu wa Irak,Nour al-Maliki.Inasemekana kuwa Maliki alishamuomba Rais Bush amwondoe Jenerali huyo msomi mwenye shahada ya kwanza katika sayansi (Bachelor of Science),shahada ya uzamili katika Utawala wa Umma (M.A in Public Administration) na shahada ya uzamifu kwenye siasa za kimataifa (PhD in International Relations) na alishakuwa (assistant) Professor kwenye US Military Academy. “Bifu” (kupingana) kati ya Maliki na Jen Petraeus kunatokana na baadhi ya maamuzi yanayopingana kati ya watu hao muhimu kwa mafanikio au kutofanikiwa kwenye sera ya Bush kuhusu Irak.Inaelezwa kuwa Maliki haafikiani na mpango majeshi ya Marekani unaoelekea kuasisiwa na Jen Petraeus wa kuvipatia silaha vikundi vya madhehebu ya Sunni ili vipambane na wapiganaji wa Al-Qaeda nchini humo.Maliki ambaye ni muumini wa madhehebu ya Shia anaelekea kuhofia kuwa silaha hizo zinaweza kutumika dhidi ya vikundi vya madhehebu ya Shia,au kwa mtizamo wa muda mrefu,kuchangia vita vya wenyewe kwa wenyewe pindi majeshi ya Marekani yatakapoondoka (kama kuna kuondoka kweli).

Baada ya mjadala wa siasa za kimataifa,hebu tegeukie mambo mengine ya huko nyumbani.Nitahadharishe kuwa naamini baadhi ya ntakayoandika hapa yatawaudhi watu flani lakini kuudhika kwao kutakuwa na maana moja tu kwangu:kwamba ujumbe umefika na wabadilike badala ya kununa.Binafsi,nadiriki kusema kuwa mzazi makini hawezi kumrushusu binti yake kuingia kwenye mambo ya u-Miss.Kwanini?Kwa sababu inaelekea wengi wa mabinti wanaotafuta u-miss huwa aidha wanarubunika kuwa wenye tabia mbovu baada ya kupata majina au pengine fani nzima ya u-miss ni kichocheo cha umalaya (samahani kwa maneno makali).Yaani kila kukicha utaskia sijui Miss nanihii katembea na mume wa mtu,au Wema Sepetu kapigwa picha za utupu,au Faraja Kotta kalibwaga buzi lake lililoiba fedha wapi sijui,na vituo vingine mia kidogo.Kuna kasoro kwenye fani ya u-miss lakini jamii inaelekea imelifumbia macho suala hilo.Lundenga,Chipungahelo na wadau wengine wa fani ya u-miss wana jukumu la kuithibitishia jamii kuwa tatizo haliko kwenye fani hiyo bali ni kwa baadhi tu ya washiriki.Na kama tatizo ni washiriki basi watuambie bayana inakuwaje wanaweza kupenya katika ngazi mbalimbali hadi kifikia levo ta taifa na kuanza kutuonyesha madudu yao.Rafiki yangu mmoja mwandishi wa habari aliwahi kunidokeza kuwa fani hiyo imetawaliwa sana na viongozi,wadhamini na mapromota walafi wa kula uroda ambao wanarahisishiwa kazi na mabinti wenye tamaa ya umaarufu wa chapchap,ambao kwao sio ishu kuvua “makufuli” yao ili wakwae u-miss.Ujumbe wangu kwenu ni simpo:msipokuwa makini mtaondoka kwa kilo mbili,na kwa vile mnathamini sana umaarufu,basi kudhoofika kwa afya zenu kutatawala sana kurasa hizohizo zinazoripoti kila siku namna mnavyoibemenda Amri ya Sita kama hamna akili nzuri.Mkikasirika shauri yenu lakini mmezidi kufanya mambo ya aibu.

Halafu kuna mambo mawili yamenisikitisha sana.La kwanza ni hii tabia ya ubabe inayoelekea kumkolea msanii TID.Binafsi,nazipenda sana kazi za kijana huyu,na mwanzoni nilikuwa namtofautisha na wasanii wengine wa bongo kwa vile amewahi kukaa ugahibuni kwa muda wa kutosha na amekuwa akipata mialiko ya nje mara kwa mara.Lakini pengine kwa kutotambua kuwa taswira (image) ya msanii ni muhimu katika kumuweka au kumporomosha kwenye chati,ameendelea kushika vichwa vya habari kwa matukio yasiyopendeza.Wimbo wake naoupenda sana unaitwa “chagua moja”,nami ujumbe wangu kwake ni mfupi:chagua moja kati ya kujiporomosha wewe mwenyewe kwa matendo yasiyofaa au jirekebishe tabia zako ili uendelee kubaki kuwa “Top In Dar.” Usikasirike,ni somo jepesi tu hilo.

Jingine lililonikera ni gazeti la RISASI ambalo katika toleo lake la Julai18-20 lilikuwa na habari kwamba “Warembo TZ wapiga picha za X tupu…zasambazwa mitaani,baadhi yao ni washiriki wa kusaka mataji ya u-miss.” Kinachosikitisha sio kama iwapo habari hiyo ni ya kweli au ya kubuni bali ni picha zilizotumika kwenye habari hiyo.Rafiki yangu mmoja aliyeko Marekani amenifahamisha kuwa wasichana walioko kwenye picha hizo ni wacheza filamu za ngono (porn stars) wa Marekani na wala sio Watanzania.Kwa kuthibitisha alichokuwa anasema,alinipatia tovuti ambazo zina picha za Wamarekani hao weusi.Kama picha zilizotumiwa na RISASI ni feki basi yayumkinika kusema kuwa hata habari yenyewe ni feki.Hivi ni uzembe wa mhariri kucheki ukweli wa habari husika au ndio kuwafanya Watanzania wajinga kwa kuwapa habari “sensational” ambazo hazina ukweli?Nyie ni watu wazima ambao mmeshatengeneza faida ya kutosha kwa kuandika udaku lukuki wa kweli,sasa tamaa ya nini hadi mfikie hatua ya kunyofoa mapicha kwenye mtandao na kuzusha habari?Shame on you!

Alamsiki

27 Jul 2007

Asalam aleykum,

Katika makala iliyopita niliwapa kituko kimoja kuhusu memba 7 wa kabineti ya Bwana Gordon Brown ambao walikiri hadharani kuwa walishawahi kuvuta bangi wakati wa ujana wao.Maendeleo zaidi (“update”) kuhusu stori hiyo ni kwamba hadi sasa idadi hiyo imefikia mawaziri 10.Lakini wananchi wanaonekana hawajashtushwa sana na “confessions” (vitubio…naamini niko sahihi hapa,au kuna neno jingine linalowakilisha wingi wa kutubu?BAKITA msaada tafadhali) pengine kwa sababu wananchi mawaziri hao watahukumiwa na utendaji wao wa kazi na sio historia zao za kale.Joji Bushi,huyu raisi wa sasa wa Marekani alikuwa “mtu wa matingas” (mlevi) kabla hajamrejea Bwana,lakini ulevi wake wa zamani haukuwa kikwazo kwa yeye kugombea nafasi hiyo ya juu kabisa ulimwenguni.Hata mie nadhani sio vema kumhukumu mtu kwa mambo alofanya zamani,alimradi anayofanya sasa yawe yanaridhisha.Wengi tunafahamu kwamba kuna wale waliosoma seminari na baadae kuingia kuutumikia umma,lakini si ajabu kukuta baadhi yao ni wala rushwa.Kwa maana hiyo,yayumkinika kusema kuwa bora kuwa mtu ambaye kwenye ujana wake alifanya mambo yasiyopendeza lakini sasa anafanya yale yanayotakiw,a kuliko yule ambaye CV yake ya ujana wake ni “supa” lakini kwa sasa anashiriki kuhujumu uchumi wa Taifa letu “changa” (nadhani neno “changa” sasa limeshapitwa na wakati maana taifa letu lina umri wa miaka 45,na naamini huko mtaani ukimwita mtu mwenye umri huo “mchanga” basi patakuwa hapakaliki hapo).

Kwa wale waliokuwa wanafuatilia stori ya Shambo,yule ng’ombe “mtakatifu” kwa Wahindu wa huko Skanda Valle,magharibi ya Wales,habari “latest” ni kwamba “ng’ombe-mungu” huyo amepelekwa mbele ya haki baada ya polisi 30 kuvamia hekalu lake na kumchukua kwa ajili ya kwenda kumchinja.Kwa wale ambao stori hii iliwapitia kando,ni kwamba Shambo alitakiwa kuuwawa baada ya kugundulika kuwa ana kifua kikuu (TB),na hivyo kuhatarisha afya za mifugo mingine katika eneo hilo.Lakini,Shambo si ng’ombe wa kawaida,bali ni “mungu” wa Wahindu,na waumini waliapa kuwa hawako tayari kuona “mungu” wao huyo akiuawa na binadamu.Baada ya mamlaka husika (DEFRA) kuwafahamisha waumini kuwa Shambo anapaswa kuuawa ili kuzuwia kuenea ugonjwa aliokuwa nao.Waumini walipinga uamuzi huo na hatimaye wakakata rufaa Mahakama Kuu ambapo amri ya kumuua “mungu” huyo ilitengeliwa.Lakini mamlaka husika zikaamua kukata rufaa Mahakama ya Rufaa ambapo iliamualiwa kuwa Shambo anastahili kuuawa.Zoezi la kumchukua “ng’ombe-mungu” huyo halikuwa jepesi kwani waumini walijitutumua kadri ya uwezo wao kuhakikisha kuwa Shambo hachukuliwi,na hapo ndipo ikabidi waletwe polisi kumaliza songombingo hiyo iliyochukua zaidi ya masaa 12,huku sakata zima kati ya waumini na DEFRA likiwa limedumu kwa wiki 12.Pengine kufanana kwa namba 12 katika matukio hayo kunaweza kuwa uhusiano na “umungu” wa ng’ombe huyo.

Tukiachana na “safari ya mwisho” ya ngombe-mungu Shambo,tuelekeze macho yetu huko nyumbani.Hebu ngoja kidogo.Kuna nchi inaitwa Guam.Je unaweza ku-guess iko wapi?Enewei,nilikuwa nachemsha kidogo ubongo wako.Nchi hiyo ni “koloni” la Marekani (well,iko chini ya mamlaka ya Marekani) na kwa mujibu wa sensa ya karibuni Guam ina wakazi 173,456.Bila kuingia kwa undani kuhusu jiographia,siasa na porojo nyingie kuhusu ka-nchi hako ambako ni kisiwa,ngoja nikudokezee kuhusu timu yake ya taifa.Hebu angalia matokeo ya mechi zake za hivi karibuni.Ilifungwa 10-0 na China,ikafungwa 15-1 na Hong Kong,na ikalambwa 9-0 na Korea ya Kusini.Kwa sasa inashilia nafasi ya 199 kwenye listi ya FIFA ya ubora wa soka duniani.Nafasi hiyo ndio ya mwisho kabisa,lakini habari njema kwa nchi hiyo ni kwamba haiko pekee kwenye nafasi hiyo kwani Djibouti, East Timor, Belize, the US Virgin Islands, Montserrat, American Samoa, Sao Tome e Príncipe na Aruba pia zinashikilia kwa pamoja nafasi hiyo ya 199.Wahenga walisema kilio cha wengi ni harusi.Kocha wa timu hiyo anawalaumu zaidi wachezaji wake kwa tabia yao ya kuendekeza pati,kujichanganya na magelifrendi wao (au wake zao) na kuthamini zaidi mambo ya binafsi kuliko majukumu yao ya soka.Pia wachezaji wa timu hiyo wanashutumiwa kwa kuzembea mazoezi,na hata wanapofika mazoezini wengi wao huwa wamechoka kutokana na “kujirusha” (sio kujirusha kimazoezi bali “kiaina”).Kiungo wa timu hiyo,Alan Jamison,ameeleza kuwa mara kwa mara akiwa usingizini amekuwa akisumbiliwa na ndoto moja:anaota kuwa amefunga goli (la mpirani…) na uwanja unalipuka kwa mayowe.Kwa bahati mbaya kila asubuhi anapoamka anagundua kuwa timu yake haijapata na haitarajii kupata ushindi hivi karibuni.

Nimeizungumzia timu ya taifa ya Guam ili kutengeneza mazingira mazuri ya kuitupia madongo timu yetu ya iliyokwenda kutuaibisha huko Aljeria.Kulikuwa na umuhimu gani wa kuingia gharama ya kuwapeleka watalii hao kama walikuwa hawajajiaanda kwa mashindano?Enewei,mie najua kwanini walipelekwa hivyohivyo:POSHO.Posho ya safari.Linapokuja suala la posho ya safari usishangae chama cha mchezo wa bao au drafti (kwa mfano) kumpeleka mchezaji kipofu.Wanajua kabisa kuwa kipofu hawezi kucheza drafti au bao lakini hilo haliwasumbui viongozi hao kwani tayari watakuwa wamejipatia visenti vya kupeleka kwenye nyumba ndogo zao (utafiti usio rasmi umeonyesha kuwa asilimia kubwa ya fedha inayopatikana kwa rushwa au ubadhirifu inaishia kwenye nyumba ndogo).Viongozi walichagua wanamichezo wazembe wanastahili lawama nyingi zaidi kuliko wazembe hao waliokwenda kututia aibu huko Aljeria (ukiachia huyo mmoja aliyeambulia medali ya fedha).Nawalaumu zaidi viongozi hao kwa vile hawana cha kujitetea kwa kuchagua wanamichezo wasio na uwezo wa kutuletea ushindi.Angalau timu ya taifa ya Guam inaweza kujitetea kwani kijinchi chenyewe kina watu wachache zaidi ya wilaya ya Kinondoni.Tanzania ina watu zaidi ya milioni 30,na miongoni mwao ni wanamichezo wenye vipaji ambavyo aidha vinapuuzwa,haviendelezwi au vinaminywa na viongozi walafi wa madaraka na fedha lakini hawana hata chembe ya mawazo endelevu ya ushindi kwenye michezo.Kwenye nchi za kidikteta viongozi kama hawa wanaporejea kutoka mashindanoni wanapokelewa na karandinga kuelekea Segerea.

Majuzi tumesikia EWURA ikidai kwamba waziri Meghji kadanganya kuhusu uwezo wa mamlaka hiyo kuwabana wafanyabiashara wa mafuta.Sijui nani anasema ukweli kwani sijaona sheria iliyoanzisha mamlaka hiyo ila ni dhahiri kuwa kuna kitu hakiko sawia.Kuna umuhimu gani wa kuwa na mamlaka isiyo na uwezo wa kisheria katika kutekeleza majukumu yake?Au kwa mfano sahihi,kuna umuhimu gani wa kufuga mbwa mwenye mapengo na ambaye akisikia kelele za “mwizi,mwizi” anakwenda kujificha?Inanikumbusha mchapo mmoja nilowahi kusimuliwa huko Tanga kuwa baba mwenye nyumba mmoja alipoamshwa na mkewe na wanawe kuwa wamesikia watu wanavunja dirisha akaanza kulia na kuwaacha watoto hawajui la kufanya.Tukiachana na mifano hiyo,swali la muhimu ni kuwa hivi huku kurushiana mpira kunamsaidia vipi mwananchi wa kawaida?Nilishapendekeza huko nyuma kwamba njia nyepesi ya kudhibiti bei ya mafuta ni “kuchimba mkwara wa nguvu” kwamba atakayezidisha bei stahili ya mafuta atafutiwa leseni.La muhimu hapa sio kwamba amri hiyo itolewe na Meghji au EWURA,bali itekelezwe.Hakuna mfanyabiashara aliye tayari kufutiwa leseni na kwa hakika watatekeleza amri hiyo.

Mwisho,tumeambiwa na Profesa Maghembe kuwa wizara yake ina baadhi ya watendaji ambao kwa jina jepesi tunaweza kuwaita mafisadi.Hao ni pamoja na wale wanaoshiriki kwenye biashara ilopigwa marufuku ya kusafirisha magogo nje.Waziri anastahili pongezi kwa kuweka bayana uozo huo.Lakini unategemea nini kwenye wizara ambayo Severe alipewa uhamisho na akagoma kuhama na hadi leo bado anapeta?Prof Maghembe anasema amepeleka majina ya wahusika kwenye “ngazi za juu” kwa vile yeye hana uwezo kisheria kuwawajibisha.Pengine tunachopaswa kufahamu ni kuwa lini majina hayo yamewasilishwa huko ngazi za juu,na kwanini mafisadi hao bado wanaendelea kuuza maliasili zetu.Sintoshangaa kusikia mmoja wao akiitisha press conference kama ile ya gavana wetu na “kutupa somo la uzalendo.”Kwa vile mafisadi hawa wanajulikana,kuendelea kuwaacha madarakani ni sawa na kuwapa nafasi ya kufuja kwa kasi zaidi (kwa vile wanaelewa kuwa maamuzi kutoka “ngazi za juu” yanaweza kuwahamisha kutoka kwenye ulaji) na kuharibu ushahidi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.Sheria ichukue mkondo wake ili kuzuia virusi vya ufisadi kusambaa zaidi (wanaoona mafisadi hao wanazidi kupeta wanashawishika kuiga ufisadi wao).

Nimalizie kwa kumpongeza Waziri Mwapachu kwa kuhitimisha bethidei yake kwa kuwatembelea watumishi wa Wizara yake huko Dodoma.Ni mfano wa kuigwa.Pia hoja yake ya kuwa na “data bank” ya simu ni nzuri (japo ufanisi wake ni mgumu) na inaweza kuigwa kwenye maeneo mengine kwa mfano kuanzisha daftari la kudumu la wala rushwa.

Alamsiki


13 Jul 2007

Asalam aleykum,

Baada ya matukio ya hivi karibuni yaliyotuweka matumbo moto kufuatiwa mahayawani flani kuamua kuendesha kampeni yao ya kishetani ya kutaka kulipua mabomu huko London na hapo Glasgow (Waskotishi bado hawaamini kuwa ugaidi umeingia kwenye ardhi yao) sio wazo baya kuanza makala hii kwa habari “nyepesi nyepesi.” Gazeti la Daily Mail la hapa liliripoti hivi karibuni kuhusu matokeo ya utafiti yaliyoonyesha kuwa wanaume wenye aibu wana nafasi kubwa ya kupata magonjwa ya moyo kuliko wale wasio na aibu!Hizi tafiti nyingine…we acha tu.Kwa mujibu wa gazeti hilo,utafiti huo ulifanyika kwa kipindi cha miaka 30 uliwahusisha maelfu ya wanaume ambapo watafiti kutoka chuo kikuu cha Northwestern cha Chicago,Marekani walipokuwa wanafanya ufuatiliaji wa wawaliowahoji kwenye utafiti huo walibaini kuwa asilimia 60 kati yao (waliohojiwa) walikuwa wameshafariki,huku chanzo kikuu cha vifo kikiwa “heart attack” (nadhani kwa Kiswahili sahihi ni msongo wa moyo).Mambo hayo!

Na ukisikia duniani kuna mambo usidhani ni utani.Mzembe mmoja amekamatwa huko New Hampshire (Manchester) baada ya kushindikana kwa jaribio lake la kutaka kufanya uporaji benki huku akiwa amejivika matawi ya miti kama “camouflage” (kificho) yake.Jamaa huyo,James Coldwell,aliingia kwenye tawi la benki ya ushirika ya Citizens,huku akiwa amejivika majani na kuwatisha wahudumu wa benki hiyo kabla ya kufanikiwa kuondoka na kitita cha fedha,lakini alinaswa na polisi muda mfupi baadaye kwani triki yake ya “uninja wa majani” haikumsaidia kwa vile majani hayo hayakufunika sura yake,na wanausalama waliweza kuitambua vizuri kwenye CCTV.

Jumuiya ya Ulaya (EU) nayo ilijikuta kwenye wakati mgumu hivi karibuni baada ya kutoa filamu fupi kwa ajili ya promosheni ya kuhamasisha Jumuiya hiyo ambapo wahusika kwenye filamu hiyo ya sekunde 44 yenye jina “Let’s Come Together” walikuwa wakifanya “ngono nyepesi” (soft porn).Wapinzani wa wazo la Muungano wa nchi za Ulaya waliishambulia EU kwa kupoteza fedha za walipa kodi kwa kutengeneza filamu hiyo waliyoiona kuwa ni mwendelezo wa ubabaishaji wa Jumuiya hiyo.Nilipomtumia rafiki yangu flani habari hiyo kutoka gazetini alitania kwa kusema labda na sie tunahitaji “kampeni chafu” kama hiyo ya EU “kuuza” wazo la Muungano wa Afrika Mashariki ambao unaelekea kuwakera wadau wengi.

Nae mwanamama Amy Beth Ballamura amaepigwa marufuku kutia mguu kwenye pwani yoyote ya Uingereza baada ya kufanya majaribio zaidi ya 50 ya kujiua kwa kurusha baharini.Miongoni mwa sababu zilizopelekea kuchukuliwa kwa hatua ya kumdibiti mwanamama huyo ni pamoja na kuzitia huduma ya uokoji (emergency services) gharama ya zaidi ya pauni milioni 1 (zaidi ya shilingi bilioni mbili za huko nyumbani) kila wanapoitwa kwenda kumuokoa.Lakini pamoja na “tamaa” yake ya kujitoa roho,askari mmoja aliambulia tuzo ya ushujaa mwaka 2003 baada ya kusikia kelele za kuomba msaada kutoka baharini na kuamua kujitosa majini kufuata kelele hizo,ambapo alifanikiwa kumuokoa mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 44.Cha kushangaza ni kwamba kama kweli alikuwa na nia ya kujitoa uhai sasa hizo kelele za kuomba msaada zilikuwa za nini?

Enewei,baada ya "nyepesi nyepesi" hizo (zote ni habari za kweli na wala sio kuwa “nawapiga fiksi” wasomaji wangu wapendwa) sasa tuangalie mambo ya muhimu zaidi huko nyumbani.Kwanza niseme siafikiani na hoja za Waziri wa Sheria Mama Nagu kwamba Bunge halipaswi kufanya kazi ya kupitia mikataba kabla ya kutiwa saini ili libaki na uhalali wake wa kuiwajibisha Serikali kwa mujibu wa dhamana ya mgawanyo wa mamlaka, kuchunguzana na kuwajibishana.Siafikiani naye kwa sababu hoja za baadhi ya wabunge kuwa mikataba hiyo ifikishwe kwao kabla ya kusainiwa zilizingatia ukweli kwamba kuna mapungufu makubwa yanayoendelea katika suala zima la kusaini mikataba mbalimbali.Mantiki nyepesi (simple logic) inaweza kutueleza kwamba maslahi ya nchi ni muhimu zaidi ya huo mgawanyiko wa madaraka.Hivi kwa mfano wazo la mikataba kuletwa bungeni lingekubaliwa,halafu nchi inufaike kwa kuingia mikataba yenye maslahi kwa Taifa,tatizo linakuwa wapi?Hivi kipi bora,kulinda mgawanyiko wa madaraka huku mikataba ya ajabu ajabu ikiendelea kuwepo au “kupindisha sheria” kwa kuileta mikataba hiyo bungeni kabla haijasainiwa halafu nchi ikanufaika nayo?

Pia nimesoma kwenye gazeti moja la huko nyumbani kwamba lile tishio la wafugaji huko wilayani Kilombero limerejea tena.Nitamke bayana kuwa hili linanihusu binafsi kwa vile mie ni “mwana wa pakaya” naetokea mitaa ya huko.Hawa wafugaji ni wakorofi,watovu wa nidhamu na wavunja sheria wakubwa.Maagizo kadhaa yameshatolewa kuwataka waheshimu sheria za nchi lakini wameamua kuweka pamba masikio.Mamlaka husika zinapaswa kuliangalia suala hili kwa makini zaidi kwani wanachofanya wafugaji hao sio tu kinahatarisha amani (mifugo yao inakula mazao ya wakulima,na hilo pekee linatosha kuzusha ugomvi) lakini pia hawawatakii mema wakulima kwani kwa kuswaga mifugo yao kwenye mashamba wanamaanisha kuwa wanataka wakulima hao wakose chakula na hela wanazojipatia kwa kuuza akiba ya mavuno yao.Hili ni bomu la wakati (time bomb) kwani japo hakuna bondia wa Kindamba (kama yupo basi samahani kwani sijamsikia) lakini hiyo haimaanishi kuwa mtu atakaeswaga mifugo yake kwenye mashamba ataachwa afanye anavyotaka.Hapo itakuwa kuchukua sheria mkononi,na japo mie ni mpinzani mkubwa wa kuchukua sheria mkononi,natambua dhahiri kuwa mtu “anapoletewa za kuleta” anaweza kabisa kuiweka sheria kando,hususan pale haki yake inapopuuzwa kwa makusudi.Kwa vile mkoa wa Morogoro umebahatika kuwa na RC ambaye ni “mjeshi” mstaafu basi hapana shaka Brigedia Jenerali Kalembo huyo atatumia “mbinu za medani” kuwadhibiti wafugaji hao wenye uhaba wa nidhamu.

Kikao cha Bunge kinaelekea ukingoni na miongoni mwa hoja nilizovutiwa nazo ni ile ya Mheshimiwa Shabiby (wa Gairo) kuhusu ujanja unaofanywa na baadhi ya wamiliki wa mabasi makubwa ya abiria.Alieleza kuwa mengi ya mabasi yanayotumika sasa yamefanyiwa “usanii” kwa kuweka mabodi mapya kwenye “chasis” na injini za malori au za kale.Kuna jina moja tu linalowafaa “wasanii” hawa nalo ni “WAUAJI.” Wanathamini sana kukwepa gharama za kununua mabasi mapya lakini hawajali hata chembe madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na vitendo vyao vya “kuunda mabasi feki.” Kwa upande mwingine tuseme bila kuonekana aibu kwamba mabasi ya namna hiyo yanafahamika hata bila kuwa na ujuzi wa umakanika kwani ulifika pale stendi ya mabasi Ubungo unaweza kukutana na basi ambalo linaonekana dhahiri kuwa bodi yake “imepachikwa” sehemu isiyostahili.Trafiki yeyote aliyehitimu mafunzo yake vyema na mwenye uchungu na maisha ya Watanzania wenzie hawezi kuliruhusu basi “lililovimba mbavuni utadhani lina ujauzito” liendelee na safari,na mabasi ya namna hiyo yako mengi tu.Wanaofanya hivyo wanajua bayana kuwa wanavunja sheria na kuhatarisha maisha ya abiria wao lakini hawajali kwa vile hakuna aliyechukuliwa sheria hadi leo.Si ajabu tukisikia kuwa baadhi ya mabasi hayo yanatumia injini za matrekta au hata za mashine za kusaga….(nashindwa kumalizia,nimekabwa na kicheko japo jambo hili sio la kuchekesha hata chembe.)

Mwisho,wakati Gavana wetu keshatamka bayana kuwa hatojiuzulu (utadhani alijichagua mwenyewe kwenye posti hiyo),sie wapenzi wa Simba tunajipoza kwa kusherehekea ubingwa wetu ambao kidogo umetibuliwa na hizi habari za viongozi kugombea mapato ya mechi huko Morogoro.Wito kwa watani wetu wa jadi Yanga ni huu:Micho akirudi (kama kweli atarudi) ashauriwe kukutana na Twalib Hilal apewe darasa kuwa ukocha sio sawa na ukatibu mwenezi wa klabu: ukocha ni vitendo vingi maneno machache lakini Mserbia Micho kila siku “anachonga” kuhusu hili au lile lakini matunda ya kazi yake kwenye dimba ni haba.Enewei,asilaumiwe sana kwani alishawahi kusema kuwa wachezaji wake hawafundishiki,na katika mechi ya juzi anaweza kuongeza sababu kuwa “lile tumbo la kuendesha” limechangia kukosa ushindi.

Alamsiki






KULIKONI UGHAIBUNI-71


Asalam aleykum,

Baada ya matukio ya hivi karibuni yaliyotuweka matumbo moto kufuatiwa mahayawani flani kuamua kuendesha kampeni yao ya kishetani ya kutaka kulipua mabomu huko London na hapo Glasgow (Waskotishi bado hawaamini kuwa ugaidi umeingia kwenye ardhi yao) sio wazo baya kuanza makala hii kwa habari “nyepesi nyepesi.” Gazeti la Daily Mail la hapa liliripoti hivi karibuni kuhusu matokeo ya utafiti yaliyoonyesha kuwa wanaume wenye aibu wana nafasi kubwa ya kupata magonjwa ya moyo kuliko wale wasio na aibu!Hizi tafiti nyingine…we acha tu.Kwa mujibu wa gazeti hilo,utafiti huo ulifanyika kwa kipindi cha miaka 30 uliwahusisha maelfu ya wanaume ambapo watafiti kutoka chuo kikuu cha Northwestern cha Chicago,Marekani walipokuwa wanafanya ufuatiliaji wa wawaliowahoji kwenye utafiti huo walibaini kuwa asilimia 60 kati yao (waliohojiwa) walikuwa wameshafariki,huku chanzo kikuu cha vifo kikiwa “heart attack” (nadhani kwa Kiswahili sahihi ni msongo wa moyo).Mambo hayo!

Na ukisikia duniani kuna mambo usidhani ni utani.Mzembe mmoja amekamatwa huko New Hampshire (Manchester) baada ya kushindikana kwa jaribio lake la kutaka kufanya uporaji benki huku akiwa amejivika matawi ya miti kama “camouflage” (kificho) yake.Jamaa huyo,James Coldwell,aliingia kwenye tawi la benki ya ushirika ya Citizens,huku akiwa amejivika majani na kuwatisha wahudumu wa benki hiyo kabla ya kufanikiwa kuondoka na kitita cha fedha,lakini alinaswa na polisi muda mfupi baadaye kwani triki yake ya “uninja wa majani” haikumsaidia kwa vile majani hayo hayakufunika sura yake,na wanausalama waliweza kuitambua vizuri kwenye CCTV.

Jumuiya ya Ulaya (EU) nayo ilijikuta kwenye wakati mgumu hivi karibuni baada ya kutoa filamu fupi kwa ajili ya promosheni ya kuhamasisha Jumuiya hiyo ambapo wahusika kwenye filamu hiyo ya sekunde 44 yenye jina “Let’s Come Together” walikuwa wakifanya “ngono nyepesi” (soft porn).Wapinzani wa wazo la Muungano wa nchi za Ulaya waliishambulia EU kwa kupoteza fedha za walipa kodi kwa kutengeneza filamu hiyo waliyoiona kuwa ni mwendelezo wa ubabaishaji wa Jumuiya hiyo.Nilipomtumia rafiki yangu flani habari hiyo kutoka gazetini alitania kwa kusema labda na sie tunahitaji “kampeni chafu” kama hiyo ya EU “kuuza” wazo la Muungano wa Afrika Mashariki ambao unaelekea kuwakera wadau wengi.

Nae mwanamama Amy Beth Ballamura amaepigwa marufuku kutia mguu kwenye pwani yoyote ya Uingereza baada ya kufanya majaribio zaidi ya 50 ya kujiua kwa kurusha baharini.Miongoni mwa sababu zilizopelekea kuchukuliwa kwa hatua ya kumdibiti mwanamama huyo ni pamoja na kuzitia huduma ya uokoji (emergency services) gharama ya zaidi ya pauni milioni 1 (zaidi ya shilingi bilioni mbili za huko nyumbani) kila wanapoitwa kwenda kumuokoa.Lakini pamoja na “tamaa” yake ya kujitoa roho,askari mmoja aliambulia tuzo ya ushujaa mwaka 2003 baada ya kusikia kelele za kuomba msaada kutoka baharini na kuamua kujitosa majini kufuata kelele hizo,ambapo alifanikiwa kumuokoa mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 44.Cha kushangaza ni kwamba kama kweli alikuwa na nia ya kujitoa uhai sasa hizo kelele za kuomba msaada zilikuwa za nini?

Enewei,baada ya "nyepesi nyepesi" hizo (zote ni habari za kweli na wala sio kuwa “nawapiga fiksi” wasomaji wangu wapendwa) sasa tuangalie mambo ya muhimu zaidi huko nyumbani.Kwanza niseme siafikiani na hoja za Waziri wa Sheria Mama Nagu kwamba Bunge halipaswi kufanya kazi ya kupitia mikataba kabla ya kutiwa saini ili libaki na uhalali wake wa kuiwajibisha Serikali kwa mujibu wa dhamana ya mgawanyo wa mamlaka, kuchunguzana na kuwajibishana.Siafikiani naye kwa sababu hoja za baadhi ya wabunge kuwa mikataba hiyo ifikishwe kwao kabla ya kusainiwa zilizingatia ukweli kwamba kuna mapungufu makubwa yanayoendelea katika suala zima la kusaini mikataba mbalimbali.Mantiki nyepesi (simple logic) inaweza kutueleza kwamba maslahi ya nchi ni muhimu zaidi ya huo mgawanyiko wa madaraka.Hivi kwa mfano wazo la mikataba kuletwa bungeni lingekubaliwa,halafu nchi inufaike kwa kuingia mikataba yenye maslahi kwa Taifa,tatizo linakuwa wapi?Hivi kipi bora,kulinda mgawanyiko wa madaraka huku mikataba ya ajabu ajabu ikiendelea kuwepo au “kupindisha sheria” kwa kuileta mikataba hiyo bungeni kabla haijasainiwa halafu nchi ikanufaika nayo?

Pia nimesoma kwenye gazeti moja la huko nyumbani kwamba lile tishio la wafugaji huko wilayani Kilombero limerejea tena.Nitamke bayana kuwa hili linanihusu binafsi kwa vile mie ni “mwana wa pakaya” naetokea mitaa ya huko.Hawa wafugaji ni wakorofi,watovu wa nidhamu na wavunja sheria wakubwa.Maagizo kadhaa yameshatolewa kuwataka waheshimu sheria za nchi lakini wameamua kuweka pamba masikio.Mamlaka husika zinapaswa kuliangalia suala hili kwa makini zaidi kwani wanachofanya wafugaji hao sio tu kinahatarisha amani (mifugo yao inakula mazao ya wakulima,na hilo pekee linatosha kuzusha ugomvi) lakini pia hawawatakii mema wakulima kwani kwa kuswaga mifugo yao kwenye mashamba wanamaanisha kuwa wanataka wakulima hao wakose chakula na hela wanazojipatia kwa kuuza akiba ya mavuno yao.Hili ni bomu la wakati (time bomb) kwani japo hakuna bondia wa Kindamba (kama yupo basi samahani kwani sijamsikia) lakini hiyo haimaanishi kuwa mtu atakaeswaga mifugo yake kwenye mashamba ataachwa afanye anavyotaka.Hapo itakuwa kuchukua sheria mkononi,na japo mie ni mpinzani mkubwa wa kuchukua sheria mkononi,natambua dhahiri kuwa mtu “anapoletewa za kuleta” anaweza kabisa kuiweka sheria kando,hususan pale haki yake inapopuuzwa kwa makusudi.Kwa vile mkoa wa Morogoro umebahatika kuwa na RC ambaye ni “mjeshi” mstaafu basi hapana shaka Brigedia Jenerali Kalembo huyo atatumia “mbinu za medani” kuwadhibiti wafugaji hao wenye uhaba wa nidhamu.

Kikao cha Bunge kinaelekea ukingoni na miongoni mwa hoja nilizovutiwa nazo ni ile ya Mheshimiwa Shabiby (wa Gairo) kuhusu ujanja unaofanywa na baadhi ya wamiliki wa mabasi makubwa ya abiria.Alieleza kuwa mengi ya mabasi yanayotumika sasa yamefanyiwa “usanii” kwa kuweka mabodi mapya kwenye “chasis” na injini za malori au za kale.Kuna jina moja tu linalowafaa “wasanii” hawa nalo ni “WAUAJI.” Wanathamini sana kukwepa gharama za kununua mabasi mapya lakini hawajali hata chembe madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na vitendo vyao vya “kuunda mabasi feki.” Kwa upande mwingine tuseme bila kuonekana aibu kwamba mabasi ya namna hiyo yanafahamika hata bila kuwa na ujuzi wa umakanika kwani ulifika pale stendi ya mabasi Ubungo unaweza kukutana na basi ambalo linaonekana dhahiri kuwa bodi yake “imepachikwa” sehemu isiyostahili.Trafiki yeyote aliyehitimu mafunzo yake vyema na mwenye uchungu na maisha ya Watanzania wenzie hawezi kuliruhusu basi “lililovimba mbavuni utadhani lina ujauzito” liendelee na safari,na mabasi ya namna hiyo yako mengi tu.Wanaofanya hivyo wanajua bayana kuwa wanavunja sheria na kuhatarisha maisha ya abiria wao lakini hawajali kwa vile hakuna aliyechukuliwa sheria hadi leo.Si ajabu tukisikia kuwa baadhi ya mabasi hayo yanatumia injini za matrekta au hata za mashine za kusaga….(nashindwa kumalizia,nimekabwa na kicheko japo jambo hili sio la kuchekesha hata chembe.)

Mwisho,wakati Gavana wetu keshatamka bayana kuwa hatojiuzulu (utadhani alijichagua mwenyewe kwenye posti hiyo),sie wapenzi wa Simba tunajipoza kwa kusherehekea ubingwa wetu ambao kidogo umetibuliwa na hizi habari za viongozi kugombea mapato ya mechi huko Morogoro.Wito kwa watani wetu wa jadi Yanga ni huu:Micho akirudi (kama kweli atarudi) ashauriwe kukutana na Twalib Hilal apewe darasa kuwa ukocha sio sawa na ukatibu mwenezi wa klabu: ukocha ni vitendo vingi maneno machache lakini Mserbia Micho kila siku “anachonga” kuhusu hili au lile lakini matunda ya kazi yake kwenye dimba ni haba.Enewei,asilaumiwe sana kwani alishawahi kusema kuwa wachezaji wake hawafundishiki,na katika mechi ya juzi anaweza kuongeza sababu kuwa “lile tumbo la kuendesha” limechangia kukosa ushindi.

Alamsiki

22 Aug 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Kabla sijaenda kwenye mada yangu ya leo ngoja nielezee kichekesho kimoja nilichokisoma kwenye mtandao kuhusu maandalizi ya timu ya Moro United katika majukumu ya kitaifa yanayowakabili.Kiongozi mmoja wa timu hiyo alinukuliwa akisema kwamba timu hiyo imeamua kufuta safari ya kwenda nchini Ufaransa kwa vile wamekosa nafasi ya sehemu ya kufikia “kutokana na hoteli nyingi kujaa kipindi hiki cha summer…”Hiki ni kichekesho kwa sababu Ufaransa ni nchi na sio kijiji au mtaa wenye hoteli moja au mbili.Kilichonisikitisha ni ukweli kwamba mwandishi aliyeripoti habari hiyo hakufanya jitihada yoyote ya kumuuliza kiongozi huyo ni hoteli zipi na katika miji gani ya Ufaransa ambazo timu hiyo ilipanga kufikia,na hapo ingekuwa rahisi kwa mwandishi huyo kuhakiki hoja hiyo kwenye tovuti ya hoteli au sehemu zilizotajwa.Tunaambiwa kuwa badala ya Ufaransa sasa timu hiyo itakwenda Italia,kana kwamba huko Italia sasa ni majira ya baridi au hakuna watalii waoweza kujaza hoteli “kama ilivyokuwa huko Ufaransa.”

Enewei,tuachane na ubabaishaji huo.Majuzi nilipata barua pepe kutoka kwa rafiki yangu mmoja anayesoma siasa kama mimi japo yeye eneo lake la utafiti ni Kusini Mashariki mwa bara la Asia na mimi eneo langu ni Afrika.Katika barua hiyo,niliombwa kutoa mawazo yangu kuhusu kile ambacho rafiki yangu alikiita kukua kwa kasi kwa interests za China katika bara la Afrika.Tangu Januari mwaka huu viongozi wa juu wa nchi hiyo wameshatembelea nchi 15 za Afrika.Wakati Waziri Mkuu Wen Jiabao ametembelea Misri,Ghana,Congo,Angola,Afrika Kusini,Uganda na Tanzania,Rais Hu Jintao ametembelea Morocco,Nigeria na Kenya,huku Waziri wa Mambo ya Nje Li Zhaoxing amezuru Libya,Senegal,Cape Verde,Mali,Liberia na Nigeria.Wafuatiliaji wa siasa za kimataifa wa nchi za Magharibi wanaonekana kuwa na kihoro kwa namna mambo yanavyoonekana kwenda vyema kwa China na marafiki zake wa Afrika.Eti wanadai kuwa tofauti na mapatna wakuu wa biashara wa Bara la Afrika,yaani Marekani na Uingereza,China haijali sana kuhusu masuala ya haki za binadamu na ndio maana baadhi ya misaada ya nchi hiyo imekwenda kwa nchi ambazo rekodi zake katika haki za binadamu sio za kuuridisha sana.Kwa mujibu wa tovuti ya Council for Foreign Relations, China iliipatia Sudan ndege za kivita aina ya Shenyang na silaha vyote vikiwa na thamani ya dola zaidi ya milioni 100,na kati ya 1998 na 2000 ilitoa misaada ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 1 kwa Ethiopia na Eritrea wakati nchi hizo zikiwa kwenye vita.Lakini pia wachambuzi hao wanadai kuwa katika kupata mikataba minono China haijali sana wale wanaoomba “teni pasenti” kusaini mikataba yenye utata,na ziadi ni suala la kutumia wataalamu wake badala ya wazawa kwenye nchi inazoshirikiana nazo.

Hata hivyo,pamoja na “longolongo” hizo ukweli unabaki kwamba mchango wa China kwa Afrika ni wa manufaa kwa bara hilo lenye mlolongo wa matatizo.Kwa mfano,mwaka jana uchumi wa Afrika ulikuwa kwa asilimia 5.2 ambayo ni rekodi ya juu kabisa,na miongoni mwa sababu muhimu ni mchango wa China kwenye uchumi wa bara hilo.Pia China ilifuta madeni kwa Afrika yanayofikia takribani dola bilioni 10,mwaka juzi ilichangia askari 1500 kwenye majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa barani Afrika,na ujenzi wa miundombinu unaofanywa na nchi hiyo ni wa gharama nafuu na unazingatia muda.

Jambo jingine la hivi karibuni ambalo limegusa hisia za duru za kisiasa za nchi za Magharibi ni kikao cha 7 cha Umoja wa Afrika (AU) ambapo Rais wa Iran,Mahmoud Ahmadinejad,na mwenzie wa Venezuela,Hugo Chavez,walihudhuria.Viongozi hao wawili wanaonekana kama “miiba mikali” kwa Marekani na washirika wake.Nchi zote hizo mbili zinajivunia “silaha” zake yaani mafuta,na kwa namna flani Marekani na marafiki zake wanaishia kulalamika tu bila kuchukua hatua yoyote dhidi ya nchi hizo pengine kwa kuhofia madhara kwenye suala nyeti la “wese” (mafuta).

Mara nyingi Afrika inavuta zaidi hisia za siasa za kimataifa kwenye majanga-kama vita,ukimwi,nk-pale inapoonekana kuwa bara hilo linaweza kukumbatiwa na wale wanaoonekana (kwa Marekani na wenzie) kuwa ni nguvu tishio.China ina uchumi unaokuwa kwa kasi ya kutisha,yaani ile shaa kama wanavyosema watoto wa mjini,na ukichanganya na watu wake zaidi ya bilioni moja,wachumi wa nchi za Magharibi wanaiangalia nchi hiyo kwa makini sana.

Enzi za Vita Baridi,washiriki wakuu-nchi za Magharibi chini ya Marekani,na za Mashariki zikiongozwa na Urusi-walipigana vikumbo ndani ya Afrika ili kuliweka mikononi bara hilo.Mbinu chafu sana zilitumika katika kutekeleza azma hiyo ikiwa ni pamoja na mauaji ya wanasiasa kama Patrice Lumumba,na sapoti kwa wanaharamu kama Jonas Savimbi na UNITA yake.Yayumkinika kusema kwamba bara la Afrika halikupata nafasi ya kupumua baada ya mapambano dhidi ya ukoloni kwani mara baada ya uhuru likajikuta limewekwa mtu kati kwenye mapambano kati ya ubepari na ukomunisti.

Ni matarajio yetu kwamba iwapo hao wanaowashwa na kukua kwa mahusiano kati ya China na Afrika wataamua kufanya lolote basi haitokuwa kuligeuza bara letu kuwa uwanja wa mapambano ya kiitikadi.Kwa kuwa hali kwa sasa iko shwari,acha tufaidi ukarimu wa wajukuu wa Mwenyekiti Mao na mwenzie Zhou Enlai (fasheni za zamani zinarudi,je suti za chwenlai nazo zitarudi?).

Alamsiki

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Mwaka juzi gazeti maarufu duniani la TIME lilimtangaza George W.Bush kuwa “mtu wa mwaka (2004)” –au “Person of the Year” kwa lugha ya kwa mama.Katika uchambuzi wake kuhusu Bush,gazeti hilo lilimnukuu Rais huyo wa Marekani akisema kwamba “inapotokea kuwa hoja au mawazo yako yanazua mjadala au upinzani basi ni dalili kwamba yana uzito…kwa maana yangekuwa ya kipuuzi wala watu wasingejishughulisha nayo.”Alikuwa anazungumzia upinzani anaokumbana nao katika utendaji wa kazi zake za kila siku.Sio siri kuwa Bush anachukiwa na watu wengi hata ndani ya nchi yake.Lakini japo mie sio shabiki wake,namhusudu kwa jinsi anavyoweza kufanya mawazo yake yakubalike hata kwa wale ambao aidha hawayapendi au hawaafikiani nae.

Mwaka jana wakati nakuja huko nyumba,nilibahatika kukaa kiti kimoja na mama mmoja wa Kimarekani.Ni mtu mwongeaji sana,nami niliitumia nafasi hiyo kumdadisi siasa za Marekani hasa kuhusu mgawanyiko mkubwa wa kiitikadi nchini humo baina ya wale wa mrengo wa kulia(conservatives) na wale wa mrengo wa kushoto (liberals).Mwanamama huyo ambaye alinifahaisha baadaye kuwa ni mwanaharakati wa mazingira,alieleza kuwa kwa kiasi kikubwa mgawanyiko huo unachangiwa na siasa za Bush na maswahiba zake kama Dick Cheney,Donald Rumsfield,Paul Wolfowitz,na wengineo ambao wanajulikana kiitikadi kama “neo-conservatives” (sijui wanaitwaje kwa lugha yetu ya Taifa!).Miongoni mwa imani za hawa jamaa ni kuhakikisha kuwa Marekani inatumia ipasavyo nafasi yake kama Taifa lenye nguvu kabisa duniani.Kwa maana hiyo,ni “haki” yake kutumia “ubabe” wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuvamia zile nchi zinazoonekana kuwa “korofi”.Ipo siku nitawazungumzia kwa kirefu jamaa hawa ambao takriban wote ni wadau wa taasisi moja isiyo ya kiserikali iitwayo “The Project for The New American Century” (Mradi wa Karne Mpya ya Marekani,kwa tafsiri isiyo rasmi).Turudi kwa yule mama.Basi akanambia kuwa japo yeye binafsi ni mpinzani wa Bush na hao neo-conservatives wenzake kuna wakati huwa “anamzimia sana” kutokana na jinsi anavyoweza kufanya maamuzi yake yatekelezwe hata pale kwenye upinzani mkubwa.Waingereza wana msemo “kama humuwezi unayeshindana nae basi bora uungane nae tu,”na ndio maana hata wale wasioafikiana na Bush mwishowe hujikuta hawana jinsi bali kuendana na mawazo au maamuzi yake.

Muda mfupi uliopita nilipata ujumbe kutoka kwa rafiki yangu flani aliyeko huko nyumbani akinijulisha kuwa kuna mwandishi mmoja ameandika makala katika gazeti flani la kila siku (la hapo Bongo) kupingana nami katika hoja ya makala yangu moja ya hivi ambayo nilimfananisha Rais Jakaya Kikwete na kiongozi wa chama cha Conservatives cha hapa Uingereza,David Cameron.Kwa mujibu wa ujumbe niliopata,mwandishi huyo aliyepingana nami anadai sikuwa sahihi kuwalinganisha wanasiasa hao .Kwa bahati mbaya hadi natayarisha makala hii nilikuwa sijapata hoja zote zilizotolewa kukosoa makala yangu.Kwa mantiki hiyo itakuwa vigumu kujibu hoja baada ya hoja bali nachoweza kusema kwanza ni kwamba makala ya mwandishi huyo ni uthibitisho tosha kuwa gazeti hili la KULIKONI ni kipenzi cha wengi,na ndio maana linazaa hoja na makala katika magazeti mengine.Pili,kama gazeti la TIME lilivyomnukuu Bush naamini makala yangu hiyo ilikuwa na uzito ndio maana ikamsukuma mwandishi huyo kuijadili japo hakuafikiana na nilichokiandika,kwa kuwa laiti ingekuwa ya kipuuzi asingepoteza muda wake kupingana nayo.”

Kwa faida ya mwandishi huyo,Kikwete anashabihiana sana na David Cameron katika maeneo flani.Kwa mfano,wote wawili wako katika vyama ambavyo kabla ya wao kushika hatamu za uongozi kwa kiasi flani vilikuwa vinaonekana kama ni vya “wateule wachache” tu.Ushindi wa tsunami kwa Kikwete ni dalili tosha kuwa hata baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani walimpigia kura kuonyesha kuwa kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais kuliiongezea nguvu CCM.Hoja nyingine japo inaweza kuwa si nzito sana ni kwamba wanasiasa hao wana sifa inayofanana ya kuwa handsome,na kwa taarifa yako u-handsome unalipa sana kwenye siasa.Lakini kingine ni lugha zao wanazotumia.Wanaongea lugha za watu wa kawaida wa mtaani,yaani wanajua wananchi wanatarajia nini kwao.Ndio,Cameron anafuata siasa za mrengo wa kulia kuelekea kati (right-centre) na Kikwete kama mwana CCM nadhani atakuwa ni wa siasa za mrengo wa kushoto kuelekea kati (left-centre),na japo Cameron ni Mwingereza na Kikwete ni Mtanzania,la muhimu hapa ni jinsi wananchi wanavyowahusudu kutokana na utendaji wao.Kura za maoni hapa Uingereza zinaonyesha kuwa Cameron amempiku Tony Blair kwa kupendwa na wananchi na naamini kuwa hata kama Watanzania wataamshwa usingizini kupiga kura za maoni,Kikwete ataibuka kidedea kwa sana.Kwenye siasa umaarufu wa mwanasiasa haugemei sana kwenye itikadi zake au chama chake,sehemu aliyozaliwa au umri wake bali kukubalika kwake miongoni mwa wananchi,na hicho ndicho kilichonipelekea kuwafananisha wanasiasa hao.

Mwisho,siamini kuwa mwandishi wa makala hiyo alikuwa anatafuta umaarufu kupitia makala yangu au gazeti hili la KULIKONI,bali alikuwa anatumia haki yake ya kikatiba kutoa mawazo yake.Nampa changamoto aendelee kusoma gazeti hili ilimradi isiwe kwa nia ya kupinga kila kitu hata kama ameishiwa na hoja.Kama alivyoimba Mista Two (Joseph Mbilinyi) kwenye wimbo wake “Sugu” kwamba huwezi kuizuia mvua kunyesha,KULIKONI ni kama jua na mvua,halizuiliki.

Alamsiki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.