Huku mgomo wa madaktari ukiendelea kushika kasi,kuna dalili kwamba walimu nao wanaelekea kuchukua hatua hiyo kutokana na taarifa za magazeti ambapo wamekumbushia kilio chao cha muda mrefu kuhusu maslahi yao.
Kwa mujibu wa gazeti la Tanzania Daima,toleo la leo Jumatano,walimu wametoa wito kwa serikali kutekeleza matakwa yao ya maboresho ya maslahi huku wakitaja viwango wanavyostahili kulipwa.
Habari kamili ni hii hapa chini
Walimu wawasha moto mpya• WATAKA MISHAHARA YA 900,000/-na Datus Boniface
WIMBI la wafanyakazi wa umma kudai nyongeza ya mishahara, posho na marupurupu limechukua sura mpya baada ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kupendekeza viwango vipya vya mishahara wanavyopaswa kulipwa walimu.
CWT kimesema mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu kinataka kuwe na ongezeko la asilimia 100 kwa walimu wote kulingana na viwango vya madaraja yao, ambapo wa Cheti (Daraja A), anatakiwa kulipwa sh laki tano, stashahada alipwe sh laki saba na nusu na yule wa shahada alipwe zaidi ya sh laki tisa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kwa niaba ya Rais wa CWT, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Ezekiah Oluoch, alisema ongezeko hilo linatokana na kupanda kwa gharama za maisha.
“Tumefanya tathmini na kujiridhisha kuwa mapendekezo yetu yanawezekana, serikali inaweza kutulipa fedha hizo kwa sababu ina rasilimali za kutosha,” alisema.
Oluoch alisema mapendekezo hayo yametokana na kikao cha Baraza la Taifa la chama hicho lenye wajumbe 163 wanaowakilisha walimu katika mikoa 21, kilichoketi Januari 31 hadi Februari mosi mjini Morogoro.
Alibainisha kuwa baraza la taifa limeagiza kuwa majadiliano kuhusu nyongeza ya mishahara yaanze mara moja na yawe yamekamilika mwishoni mwa Machi mwaka huu.
Alisema wanataka majadiliano hayo yafanywe mapema ili serikali iyaingize makubaliano kwenye bajeti yake ya mwaka huu.
Oluoch alisema CWT inaamini kuwa majadiliano ni njia pekee ya kupata mwafaka wa ongezeko hilo la mishahara.
Malipo ya poshoCWT inahitaji kulipwa kwa posho za kufundishia na za mazingira magumu kwa walimu hao, kwa kuwa muda wa kazi zao ni tofauti na watumishi wengine wa umma.
Kinataka walimu wote wapewe posho ya asilimia 55 kwa walimu wa masomo ya Sayansi na asilimia 50 wa Sanaa, na posho hizo zianze kulipwa kuanzia Julai.
CWT kimesema kuwa nyongeza ya posho hizo si ngeni kwani Rais Jakaya Kikwete aliwapa ahadi hiyo Siku ya Walimu Duniani Oktoba 5, mwaka 2010.
Olouch alisema posho ya mazingira magumu, inatakiwa kulipwa kwa asilimia 70 kwa mwalimu anayefanya kazi maeneo ya vijijini, kama utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani Oktoba 2010.
Madeni yasiyohusiana na mishaharaCWT kimeitaka serikali kuwalipa walimu fedha zao za madeni yasiyohusiana na mishahara kabla ya Februari 15 na iwapo itashindwa kufanya hivyo, chama hicho kitachukua hatua dhidi ya waajiri waliokaidi makubaliano yaliyofikiwa.
Oluoch aliongeza kuwa awali walikubaliana na serikali kuhusu utaratibu wa kulipa madeni hayo ambayo walihakiki kwa pamoja, wakishirikiana na viongozi wa serikali wa ngazi za wilaya, ambapo sh bilioni 22.5 zilitumwa kwenye halmashauri za wilaya na sh bilioni 3.5 zilitumwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Alibainisha kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alitoa waraka ambao umetafsiriwa vibaya na baadhi ya watendaji wa serikali.
Aliongeza kwamba, baadhi ya watendaji wametafsiri kinyume kuwa ni kuhakiki upya madai ya walimu badala ya kujiridhisha kama anayelipwa ndiye aliyehakikiwa.
Alisema utata huo umechangia halmashauri 50 kutowalipa fedha walimu licha ya kuzipata fedha hizo.
Kulipwa madeni ya mishaharaCWT kinataka kufanyike marekebisho yote ya mishahara na malipo ya mapunjo yafanyike ndani ya mwezi huu bila kukosa.
Oluoch alisema CWT ilifanya kikao na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Simfue Ombeni, Januari 13 mwaka huu na serikali ilitoa taarifa ya kulipwa kwa walimu 18,000 kiasi cha sh bilioni 18.
Aliongeza kuwa CWT kupitia Baraza lake limesikitishwa na kauli ya serikali ya kukosa fomu hizo huku serikali ikificha ukweli, kwani tatizo linafahamika na kwamba walimu wengi hawajarekebishiwa mishahara yao baada ya kupanda madaraja.
Chama hicho kimetaka kufutwa kwa waraka wa serikali wa kupunguza zoezi la upandishwaji wa madaraja kwa asilimia 50 kutokana na maelezo kuwa serikali haina pesa.
Kwa upande mmoja,iwapo serikali itasalimu amri na kutekeleza matakwa ya madaktari,kuna uwezekano mkubwa wa watumishi wa umma katika sekta nyingine nao kudai watendewe haki kama madaktari (iwapo madai ya matabibu hao yatatimizwa na serikali).
Kwa upande mwingine,hata kama madai ya madaktari yataendelea kupuuzwa,umoja na mshikamano wa wataalamu hao wa afya za binadamu unaweza kuwafanya watumishi wengine wa umma kujiuliza mara mbili kwanini nao wasifuate mkumbo.
Hakuna anayetaka kuona migomo ikitawala nchi yetu lakini kwa makusudi kabisa serikali imeonyesha wazi kuwa inathamini zaidi matakwa yasiyo ya lazima ya wabunge kuliko watumishi wengine wa umma ambao licha ya kuwa na mishahara midogo wanakabiliwa na matatizo chungu mbovu,kubwa likiwa uhaba wa vitendea kazi na makazi duni.Ikumbukwe kuwa wabunge wanaolipwa mamilioni kwa kupiga porojo bungeni wanapatiwa kila huduma na mazingira yao ya kazi ni mithili katika nchi zilizoendelea.
Sijui hatma ya harakati hizi za watumishi wa umma kudai haki zao itakuwaje lakini ni muhimu kuikumbusha serikali kwamba kuna tawala kadhaa zilizoanguka kutokana na ngumu ya migomo ya wafanyakazi.