Wakati wenzetu mnasherehekea timu "zenu" kama Manchester United kuchukua ubingwa,akina sie bado tupo na Simba na Yanga zetu licha ya ubabaishaji wao wa hali ya juu.Kanuni nyepesi ya kumudu kuzipenda klabu hizi kongwe za Tanzania ni kuweka hisia mbele ya busara/akili (putting emotions in front of common sense).
Kwa bahati ya mtende,wana Msimbazi tumepata fursa ambayo laiti tukiitumia vema basi tutapiga hatua kubwa ya kushiriki Ligi ya Mabingwa.Kwa sasa sitaki hata kufikiria itakuwaje kwenye Ligi hiyo,iwapo tutafanikiwa,maana timu zilizopo huko ni hatari.Anyway,kwa muda huu ngoja tushangilie habari hizi njema (hata kama ni ushindi wa mezani)
Simba yawang’oa Mazembe Afrika
• Sasa kuwavaa Wamorocco jijini Khartoum
na Mwandishi wetu, CAIRO, Misri
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba ya jijini Dar es Salaam, imeshinda rufaa yake iliyokata dhidi ya mabingwa mara mbili mfululizo wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2009 na 2010, TP Mazembe ya DR Congo.
Sasa TP Mazembe imeondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa kosa la kumchezesha mchezaji batili.
Huo ni uamuzi wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka (CAF), baada ya kupitia rufaa iliyokuwa imewasilishwa na Simba, kupinga TP Mazembe kumchezesha Janvier Besala Bokungu.
Bokungu (22), beki aliyezaliwa Kinshasa, akiwa mchezaji wa TP Mazembe mwaka 2007, alihamia Esperance ya Tunisia kabla ya kurejea mwaka huu.
Kwa mujibu wa CAF, Kamati ya Mashindano iliamua kushughulikia suala la nyota huyo baada ya Simba kuwasilisha pingamizi kwamba amechezeshwa isivyo halali.
Kamati hiyo imebaini kuwa kwa TP Mazembe kumchezesha Bokungu, ilifanya kosa kwa mujibu wa kifungu namba VIII kinachohusiana na ulaghai. Aidha, kifungu kingine kilichoipa Simba ushindi ni ibara ya 24 na 26 inayohusu uhalali wa mchezaji na ibara ya 29 ya kanuni za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwamba TP Mazembe ilimchezesha Bokungu ambaye bado ni nyota wa Esperance, kwani mkataba wake na wakali hao wa Tunisia, utafikia ukomo Juni mwaka huu, ingawa TP Mazembe wanasisitiza ni mchezaji wao halali.
“Janvier alifuata taratibu zote kuvunja mkataba wake na si Esperance wala Mazembe yenye tatizo na mchezaji huyu, kwa sababu amejiunga nasi kwa maridhiano,” alisema Meneja Mkuu wa Mazembe, Frederic Kitengie.
Simba chini ya Mwenyekiti wake Ismail Aden Rage, ilimkatia rufaa Bokungu, licha ya kung’olewa katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 6-3.
Katika mechi ya kwanza ambayo ilichezwa mjini Lubumbashi, Simba ilifungwa mabao 2-1 kabla ya kupigwa 4-1 kwenye marudiano Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kutokana na maamuzi hayo, sasa Simba itakipiga na mabingwa wa Morocco, Wydad Casablanca jijini Khartoum, Sudan, ambako itapigwa mechi moja tu ili kumpata atakayeingia katika kapu la timu nane bora, ambazo zitacheza ligi ndogo.
Tayari zilizotinga nane bora ni Ahly ya Misri, Raja Casablanca ya Morocco, Enyimba ya Nigeria, Esperance ya Tunisia, MC Alger ya Algeria, Al Hilal ya Sudan na Coton Sport ya Cameroon.
Wakati Simba wakifurahia kushinda rufaa, wakali hao wa Morocco, nao wanafurahia kurejea kwenye michuano hiyo kwani tayari walishang’olewa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 2-1.
Wakati hali ikiwa hivyo, leo Wekundu wa Msimbazi Simba, wanatarajiwa kufanya mkutano mkuu wa mwaka kwenye bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mwaka mmoja tangu uongozi wa Mwenyekiti Ismail Aden Rage kuingia madarakani.
Kwa mujibu wa Rage, mkutano huo utakuwa na ajenda za mawasilisho ya mapato na matumizi ya fedha za mwaka, sambamba na kuwasilishwa kwa bajeti ya mwaka ya Kamati ya Utendaji na mengineyo.
Alisema ni mara ya kwanza Simba kuwasilisha taarifa za mahesabu ya mwaka mapema, jambo ambalo walijiandaa kabla ya uchaguzi mkuu, ikiwa ni mojawapo ya mapendekezo yaliyomo ndani ya katiba.
Uongozi wa Rage uliingia madarakani Mei 9 mwaka jana, baada ya uongozi wa mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Hassan Dalali, kumaliza miaka mitatu ya uongozi wake.