29 Jan 2016

KATIKA tasnia ya ushushushu kuna kitu kinachoitwa Moscow Rules (yaani Kanuni za Moscow). Hizi ni kanuni za zama za Vita Baridi ambazo majasusi waliopangiwa kazi nchini Urusi walipaswa kuzizingatia, kwa sababu nchi hiyo ilikuwa nguli wa kukabiliana na majasusi. Moja ya kanuni hizo inasema; “Once is an accident. Twice is a coincidence. Three times is an enemy action.” Kwa tafsiri isiyo rasmi; kitu kinachojiri mara moja ni ajali; kikijiri mara ya pili ulinganifu wa bahati mbaya, sio makusudi; kikijiri mara ya tatu ni kitendo cha adui.”

Nimeanza makala hii na angalizo hilo kwani ndio wazo lililoniingia kichwani mara baada ya kusoma kauli za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe.

Wiki iliyopita, Membe alinukuliwa na vyombo vya habari akimkosoa Rais Dk. John Magufuli, angalau katika maeneo matatu. Kwanza, Membe alidai kuwa kiuhalisi, Dk. Magufuli hajapunguza idadi ya wizara kama alivyoahidi bali amepunguza idadi ya mifuko, na kutanabaisha kuwa Rais hajabana matumizi yoyote kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, bali alichofanya ni kupunguza idadi ya mawaziri na sio wizara.

Alichofanya ni sawa na kuwa na mayai kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,” alisema waziri huyo wa zamani ambaye pia alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliowania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.

Lakini unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na yaliyobaki kwenye mfuko mmoja. Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua. Hapa sasa utakuwa hujapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai,”aliongeza Membe.

Membe alidai kwamba Magufuli ameendeleza wizara zile zile lakini kaamua kuzikusanya pamoja, na kuona kuwa mfumo huo mpya wa wizara unaweza kuathiri uwasilishaji wa bajeti bungeni kwa vile mawaziri sasa watahitaji muda mwingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Hilo tutaliona kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka huu. Tuone kama bajeti itaongezeka au itapungua? Kwa sababu kama wizara zimepungua kama tunavyoamini, lazima bajeti ipungue, sasa bajeti ikiongezeka au ikibaki vile vile maana yake hakuna kilichofanyika,”alitahadharisha.

Eneo la pili ambalo Membe alimkosoa Magufuli ni udhibiti wa safari za nje, akidai kuwa Tanzania si kisiwa. Membe, aliyekuwa mtetezi mkuu wa safari mfululizo za Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete nje ya nchi, alisema kuwa safari za nje zina manufaa kwa taifa, na kusisitiza kuwa lazima Rais Magufuli asafiri kwenda nje ya nchi.

Tanzania si kisiwa, hata ukiwa tajiri namna gani lazima utoke nje ya nchi yako,” alisema Membe, na kutahadharisha kuwa nchi yetu inaweza kuwa kama Zimbabwe kwani ukijitenga, utatengwa.
Alisema nchi ina mabalozi 36 tu duniani kote kati ya nchi 194 zinazohitaji uwakilishi huo na kibaya zaidi, mabalozi hawaruhusiwi kuingia kwenye baadhi ya vikao, na hata wakiingia wakifika kwenye hatua ya uamuzi watazuiwa kushiriki.

Eneo la tatu ambalo japo hakumtaja Magufuli wala kukosoa moja kwa moja lakini linaloweza kutafsiriwa kama kuikosoa serikali kuhusu wafanyabiashara, ambapo alitahadharisha serikali kutowachezea.

Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Mtama (CCM) alipongeza kasi ya Magufuli katika vita dhidi ya ufisadi na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi lakini akatahadharisha kuhusu haja ya kuwa mwangalifu katika kuwashughulikia wafanyabiashara. Alidai kuwa wafanyabiashara wana masikitiko makubwa dhidi ya serikali, na anaona suala hilo litaibuka kwa kishindo bungeni.

Licha ya maeneo hayo matatu, Membe alizungumzia kauli ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, aliyedai wafanyabiashara waliomuunga mkono wananyanyaswa. Alieleza kuwa si dhambi kwa wafanyabiashara kufadhili vyama vya siasa wakati wa uchaguzi, na kwamba serikali ya chama kilichoshinda uchaguzi inapaswa kuwakusanya wafanyabiashara wote na kufanya nao kazi na sio kuwaburuza.

Kadhalika, mwanasiasa huyo alizungumzia kuhusu “timua timua” ya watumishi wa umma wanaohusishwa na tuhuma za ufisadi.

Ni rahisi kumshughulikia mtu usiyemfahamu lakini siyo rahisi kumshughulikia mtu unayemfahamu,” alidai Membe, na kuongeza kuwa haitokuwa shida kwa Magufuli kuwashughulikia watendaji aliowakuta serikalini ambao kimsingi hakuwateua, na hawafahamu. Alihoji iwapo Rais ataweza kuwatimua aliowateua mwenyewe.

Kauli hizo za Membe zimezua mjadala mkubwa, hususan kwenye mitandao ya kijamii. Japo kabla yake, aliyekuwa Naibu wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga, alimkosoa Magufuli kuhusu ukubwa wa kabineti yake, ukweli kwamba Membe bado ni kiongozi wa juu wa CCM ilhali Mahanga alihamia upinzani, unaashiria mengi.

Lakini binafsi sikushangazwa na kauli hizo za Membe, hasa kwa vile awali, katika kitabu nilichokichapisha hivi karibuni kuhusu safari ya urais wa Magufuli, mafanikio na changamoto katika urais wake, nilibainisha kuwa moja ya changamoto zinazoweza kumkabili Rais huyo wa Awamu ya Tano ni maadui wa ndani ya chama chake.

Kimsingi, hoja zote za Membe hazina mashiko. Kuhusu anachoita ukubwa wa baraza la mawaziri, la muhimu kwa Watanzania si ukubwa au udogo bali uchapakazi. Ni bora kuwa na mawaziri, manaibu na makatibu wakuu hata 1,000 wachapakazi, kuliko kuwa na serikali ndogo inayokumbatia mafisadi.
Pia Membe alipaswa kufahamu kuwa utendaji kazi wa viongozi wa serikali unategemea sana utendaji kazi na msimamo wa bosi wao, yaani Rais aliyewateua. Ni dhahiri kuwa Membe anatambua kuwa Magufuli si mtu wa porojo, mtoa ahadi anazoshindwa kuzitekeleza mwenyewe (rejea kauli ya “ninawajua wala rushwa kwa majina” ya Kikwete), na kimsingi Watanzania na dunia nzima wanafahamu kuwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu ya Magufuli ni tofauti na zama za nchi kujiendesha yenyewe (on autopilot).

Kuhusu safari za nje, Membe amepotoka mno, pengine kwa sababu kwa wadhifa wake wakati huo, alikuwa mmoja wa wasafiri nje ya nchi mara kwa mara. Kwanza, Rais Magufuli hajawahi kutamka kuwa hatosafiri. Kwa hiyo, kauli ya Membe kuwa lazima atasafiri ni fyongo.

Pili, zuio la safari za nje sio ‘blanket ban’ bali ni kwa safari zisizo na tija. Lakini kwa nini tushangazwe na kauli hiyo ya Membe ilhali tunafahamu misafara ya serikali iliyopita ilivyosheheni wajumbe kwa kutumia fedha za umma? Ni mtu mwenye matatizo tu anayeweza kutetea safari zenye manufaa zinazoligharimu taifa matrilioni ya shilingi huku faida tarajiwa zikiwa pungufu ya gharama husika.

Mwanadiplomasia msomi kama Membe alipaswa kuangalia hapo jirani tu kwa Rais Paul Kagame, kulinganisha idadi ya safari zake nje na zile za Kikwete kisha kuangalia hali ya uchumi kati ya nchi hizo mbili.

Vilevile ni rahisi kwa Membe kuzungumzia mafanikio ya safari hizo kwa vile ni Watanzania wachache wanaofahamu vituko vilivyoambatana na safari hizo. Ni mara ngapi safari hizo za ‘manufaa’ zilijumuisha shopping, kuhudhuria birthday parties, na matukio mengine yasiyo na tija kwa serikali?

Kuhusu wafanyabiashara, ni upuuzi wa hali ya juu kuhisi tu kuwa kuna uonevu dhidi ya mfanyabiashara yeyote. Kama kuwabana wafanyabiashara wakwepa kodi ni uonevu basi Magufuli aongeze dozi, maana hizi sio zama za Tanzania kuwa shamba la bibi.

Membe anadai wafanyabiashara wana masikitiko na suala hilo linaweza kuibuka bungeni. Anamaanisha Bunge limejaa wafanyabiashara au? Na kama masikitiko yao ni kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuwabana ili wasikwepe kodi na kwamba masikitiko hayo yanaweza kusababisha kupoteza wawekezaji, basi na waondoke hata kesho. Hatuhitaji wakwepa kodi nchini. Kimsingi, wanaolalamika wala hawastahili kuitwa wafanyabiashara bali wahujumu wa uchumi wetu.

Na hoja yake kuhusu ‘timua timua’ haishangazi kwani moja ya udhaifu wa serikali ambayo Membe alikuwa waziri ilikuwa ni kuwaonea aibu wanaoboronga, na matokeo yake hali hiyo ilivutia waborongaji wapya kwani walishabaini kuwa hakuna wa kuwachukulia hatua. Hivi Membe anaweza kutuambia lolote kuhusu ahadi ya Riais Kikwete aliyoitoa Februari 2006 kwamba anawafahamu wala rushwa kwa majina na anawapa muda wajirekebishe? Sawa, Magufuli alipoingia Ikulu alikuta orodha hiyo ya wala rushwa aliowajua Kikwete na kuamua kuifanyia kazi?

Nimeeleza awali kuwa nimelizungumzia suala hilo kwa kirefu kitabuni. Sitaki kabisa kuamini kuwa kauli za Membe ni zake peke yake. Hisia zinanituma kuamini kuwa huu ni moshi tu unaoashiria moto unaowaka ndani kwa ndani ya CCM kati ya makundi makuu mawili: la Hapa Kazi Tu la Magufuli linalotaka kuiondoa Tanzania katika lindi la ufisadi unaoifanya nchi yetu kuzidi kuwa masikini, na kundi la wanufaika wa ufisadi linalomwona Magufuli kama mtu anayewaziba pumzi. Naam, ufisadi ni ‘lifeline’ ya watu walioigeuza nchi yetu Shamba la Bibi, wakivuna wasichopanda.

Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa makada wa CCM, ambao wengi wao wanaimba Hapa Kazi Tu, lakini wakisikia madhambi yaliyofanywa na mwana-CCM fulani wanakimbilia kuwanyooshea vidole wapinzani. Wapinzani wakuu wa Magufuli hawapo Chadema au nje ya nchi bali wapo ndani ya chama hicho tawala. Na njia pekee ya kupambana nao ni kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kutanguliza umoja na mshikamano wa chama. Kuna usemi mchawi akimaliza kuroga mtaa hugeukia familia yake. Majipu yaliyomo ndani ya CCM yasipotumbuliwa mapema yatamkwaza Magufuli na nchi yetu kwa ujumla.


21 Jan 2016


 
MOJA ya mada zinazotawala vyombo vya habari huko nyumbani ni zoezi linaloendelea la bomoabomoa. Zoezi hilo limepokelewa kwa hisia tofauti huku baadhi ya wananchi wakiliunga mkono (hususan wasioguswa nalo) huku wengine wakiilaumu (hususan waathirika wa zoezi hilo)

Kwa upande mmoja serikali na mamlaka husika zipo sahihi kutekeleza zoezi hilo kwa vile suala hilo licha ya kuwa la muda mrefu lakini pia limekuwa na gharama kubwa, kwa serikali na mamlaka husika, kwa maana ya kuwakwamua wakazi wa mabondeni kila yanapojiri mafuriko, na kwa wakazi hao kukumbwa na hasira kubwa kila msimu wa masika.

Kwa maana hiyo, ilikuwa lazima kwa serikali kufika mahala kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo. Na kwa kiasi kikubwa, hakukuwa na njia ya mkato au ufumbuzi rahisi. Na vyovyote ambavyo ingeamuliwa, ilikuwa lazima wakazi hao wa mabondeni waondoke, aidha kwa hiari yao wenyewe au kwa serikali na mamlaka husika kuwaondosha.

Tayari baadhi ya watu wameanza kuhusisha zoezi la bomoa bomoa na upungufu wa Rais Dk. John Magufuli. Sidhani kama wanamtendea haki. Sawa, tunatambua kuwa kubomolewa makazi na kukosa makazi mbadala si kitu kizuri. Lakini hata hivyo, si Dk. Magufuli au serikali yake iliyowashauri wakazi wa mabondeni kuendelea kuishi katika mazingira hatarishi.

Na kama nilivyoeleza awali, mara nyingi wakazi hao wanapokumbwa na mafuriko, serikali hulazimika kuingia gharama ili kunusuru maisha yao. Kwa hiyo, katika mazingira ya kawaida tu, kwa minajili ya kuepusha gharama hizo, ilikuwa lazima kwa serikali kuchukua hatua stahili.

Lakini pia serikali ina jukumu la kuhakikisha usalama wa raia wake. Kuendelea kuwaachia wakazi wa mabondeni kuishi katika mazingira hatarishi kungekuwa ni sawa na serikali hiyo kuzembea kutekeleza jukumu hilo la msingi, yaani jukumu la kuhakikisha usalama wa raia.
Hata hivyo, pamoja na dhamira nzuri ya serikali katika utekelezaji wa zoezi hilo, pengine ni muhimu kuupa nafasi ubinadamu. Kimsingi, makosa yaliyosababisha uwepo wa makazi hatarishi mabondeni ni ya pande zote mbili: serikali na mamlaka husika, kwa upande mmoja, na wakazi hao, kwa upande mwingine.

Si kwamba siku moja tuliamka na kukuta nyumba zimejengwa mabondeni au kwenye hifadhi za barabara. Misingi ya nyumba ilichimbwa, matofali na vifaa vingine vya ujenzi vililetwa, na ujenzi ukafanyika, na hatimaye wakazi hao kuhamia maeneo hayo, na muda wote huo, serikali na mamlaka husika walikuwepo na hawakuchukua hatua stahili. Japo sio kisingizio mwafaka kwa wakazi hao, lakini kwa serikali na mamlaka husika kutozuia ujenzi huo wakati huo inaweza kuwa ilichangia sio tu kuwafanya waliokwishajenga hapo kudhani wana ruhusa isiyo rasmi bali pia kuliwavuta wengine wasio na mahala pa kujenga.

Sasa, kama wasemavyo waswahili yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo, la muhimu kwa sasa ni kupata ufumbuzi utakaozinufisha pande zote mbili.

Kwa vile ujumbe umekwishafika, kwa maana ya wakazi waliosalia mabondeni wamekwishaona yaliyowakuta wenzao, basi sidhani kama kuna ubaya wa kutoa muda wa kutosha na wa kiuhalisia wa kuwaagiza wakazi hao kuhama kwa hiari yao. Kumpa mtu wiki moja ahame sehemu aliyoishi kwa miaka kadhaa sio kuzingatia uhalisia.

Kama iliwezekana kuwapa wakwepa kodi matajiri siku kadhaa walipe madeni, licha ya ukweli kuwa kukwepa kodi ni kosa la jinai, na matokeo yake (tunaambiwa) wengi walitekeleza agizo hilo, basi kwa nini tusijaribu njia hiyo hiyo kwa wakazi wa mabondeni?

Kwa upande mwingine, japo ujenzi wa mabondeni sio tu ni kinyume cha sheria lakini pia unahatarisha maisha ya wakazi husika, madhara yake kwa jamii sio makubwa kama matatizo mengine ya dharura yanayohitaji kushughulikiwa haraka, hususan biashara ya dawa ya kulevya.

Ndio, makazi mabondeni yanahatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo, lakini angalau hayahatarishi uhai wa wasiokaa mabondeni. Vipi kuhusu dawa za kulevya? Yanapoteza uhai wa vijana wetu kila kukicha huku yakichangia uhalifu kwa kiwango kikubwa. Naam, mtumia dawa za kulevya akikosa fedha ya kununulia dawa hizo, njia ya mkato ni kufanya uhalifu.

Kwa maana hiyo biashara ya dawa ya kulevya ina madhara makubwa kwa jamii kuliko makazi ya mabondeni. Lakini kinachoanza kuvunja moyo ni ukimya wa serikali katika kushughulikia suala hilo ambalo lilipewa kipaumbele cha hali ya juu na Rais Dk. Magufuli alipotangaza dira ya serikali yake wakati anazindua Bunge jipya.

Sambamba na suala la dawa za kulevya ni suala la ufisadi. Ndio, ziara za kushtukiza zimezaa matunda lakini kumekuwa na ukimya kidogo hapa katikati, na sio wa ziara hizo tu bali pia hata utekelezaji wa uanzishwaji wa mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi.

Siku chache zilizopita nilikutana na habari kuhusu Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwa amebaini kuna rushwa katika Mahakama. Hilo sio suala geni, na binafsi nilishangaa kusikia Waziri Mwakyembe amebaini sasa ilhali ripoti mfululizo za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikiitaja Mahakama kama miongoni mwa taasisi zinazoongoza kwa rushwa. Je, Waziri Mwakyembe hakuwa akizisoma au kuzisikia habari hizo?

Lakini kilichonikera zaidi ni ukweli kwamba wakati wa mjadala wa ufisadi wa Tegeta-Escrow, zilipatikana taarifa zilizoonyesha majina ya baadhi ya majaji waliopokea mgao uliotokana na ufisadi huo. Hadi leo, majaji hao hawajachukuliwa hatua. Kadhalika, ziliwahi kupatikana taarifa zilizowataja majaji waliotuhumiwa kuwasaidia watuhumiwa wa kesi za dawa za kulevya. Hata hao wanasubiri kuundwa kwa mahakama za ufisadi?

Na tuwe wakweli, hivi kuunda mahakama za ufisadi kunahitaji muda gani hasa ilhali tayari tuna mfumo wa mahakama unaoshughulikia kesi za jinai?

Rais Dk. Magufuli alituasa tumsaidie katika vita dhidi ya maovu mbalimbali yanayoikabili nchi yetu. Kumsaidia si kwa kupiga vigelegele pekee zinapofanyika ziara za kushtukiza au fulani anapofukuzwa kazi bali pia kukosoa pale inapobidi. Matarajio ya wananchi bado yapo juu, na hii ni muhimu sana kwa mafanikio ya mapambano dhidi ya uozo mwingi unaohitaji kushughulikiwa. Kasi hafifu ya kushughulikia matatizo ya ufisadi na uhalifu – kama biashara ya dawa za kulevya – sio tu yaweza kupunguza ari ya wananchi lakini pia yaweza kutoa mwanya kwa wahusika kubuni mbinu mpya, sambamba na kuvutia wahalifu wapya (hususan wale wanaobaini kuwa Shamba la Bibi limefungwa).

Nimalizie makala hii kwa kukumbushia haja ya kuitumia vizuri fursa hii kuikwamua Tanzania yetu kutoka kwenye lindi la umasikini, unaochangiwa na ufisadi na uhalifu mwingine, sambamba na kuweka vipaumbele vyetu sawia kwa kushughulikia matatizo ya haraka badala ya yale yanayoweza kushughulikiwa taratibu. Ndio, Waingereza wanasema “two wrongs don’t make a right,” yaani kufanya kosa la pili hakulifanyi kosa la kwanza kuwa jambo sahihi, na kwa maana hiyo sina maana kuwa kutochukuliwa hatua dhidi ya ‘wauza unga’ kunahalalisha kutofanya bomoa bomoa. Hata hivyo, haja ya kuwashughulikia wahalifu ni ya dharura mno kuliko ya wakazi wa mabondeni.13 Jan 2016


WIKI iliyopita, watumiaji kadhaa wa mtandao wa kijamii wa Twitter nchini Kenya waliishambulia vikali Serikali ya Tanzania, na Rais Dk. John Magufuli, kutokana na kuanza kwa operesheni ya kudhibiti wahamiaji haramu inayoendelea huko nyumbani (Tanzania).
Aliyeanzisha chokochoko hiyo ni bloga mmoja maarufu nchini humo ambaye awali alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuchukua hatua dhidi ya alichokiita ubaguzi dhidi ya raia wa Kenya wanaoishi nchini Tanzania.’

Bloga huyo si mgeni kwa uchochezi. Ninaita uchochezi kwa sababu madai hayo ya ubaguzi hayakuwa na ukweli wowote. Lakini kwa tunaomfahamu, hatukushangazwa sana na madai hayo, kwa sababu hata huko nchini Kenya, bloga huyo ameshakumbana na misukosuko kadhaa kutokana na kauli zake tata.

Tweets zake kuhusu suala hilo zilisababisha Wakenya kadhaa mtandaoni kuzungumzia uonevu huo huku wakitumia hashtag #OperesheniTimua. Sina hakika kama hilo ndilo jina halisi la operesheni hiyo.

Binafsi niliona shutuma hizo dhidi ya Serikali ya Magufuli kama kichekesho fulani, hasa ikizingatiwa kuwa ni hivi majuzi tu, Wakenya lukuki walikuwa wakimsifu Rais wetu huyo kwa hatua zake mbalimbali za kudhibiti mapato na matumizi, sambamba na kupambana na rushwa, huku wakiilaumu Serikali ya Rais Uhuru.

Majirani zetu hao walikuwa mstari wa mbele katika kuipaisha ‘hashtag’ #WhatWouldMagufuliDo ambayo kimsingi ilikuwa ikionyesha jinsi watu mbalimbali duniani walivyoridhishwa na hatua hizo za Magufuli.

Sasa, tukiafikiana tu kuwa Magufuli amedhamiria kwa dhati kupambana na kila uozo uliopo, basi ni wazi kuwa ilikuwa suala la muda tu kabla serikali yake haijaanza kuvalia njuga suala la uhamiaji haramu. Na ninaamini kuwa majirani zetu wa Kenya hawakutarajia serikali yetu kuwafumbia macho wahamiaji haramu kutoka nchi yoyote ile hata kama ni jirani yetu Kilichonikera zaidi ni kuona tweet ya Naibu Rais wa Kenya William Rutto akifuata mkumbo wa kukemea #OperesheniTimua pasi kujiridhisha vya kutosha kuhusu tuhuma zilizotolewa na bloga husika.
Nilipotafakari kwa undani kuhusu suala hilo nikapatwa na hisia kuwa Tanzania legelege yenye sheria zisizofanya kazi ilikuwa ni habari njema kwa wasioitakia mema nchi yetu. Sio siri kwamba, uzembe mkubwa katika Idara ya Uhamiaji umechangia sana kushamiri kwa tatizo la wahamiaji haramu. Na sio siri pia kuwa majirani zetu, ikiwa ni pamoja na Kenya, walinufaika sana kutokana na uzembe huo.

Lakini zama hizo za raia wa kigeni kununua haki ya makazi nchini mwetu zaelekea kufikia ukingoni, na hiyo si habari njema kwa wanufaika. Lakini hata kama hatua hiyo inawakera basi angalau wangekuwa na ustaarabu katika kulizungumzia suala hilo kuliko kuzusha tuhuma za uongo. Japo ni kweli kwamba kuna raia wengi wa Kenya nchini Tanzania, operesheni hiyo ya kupambana na wahamiaji haramu haiwalengi raia wa kigeni – iwe ni kutoka Kenya au kwingineko – ambao wapo nchini Tanzania kihalali. Iwapo waathirika wengi wa operesheni hiyo ni Wakenya basi labda iwe kutokana na wengi wao kutokuwa nchini mwetu kihalali (nasisitiza labda kwa vile sina takwimu sahihi).

Baadhi ya majirani zetu hao waliochangia mjadala mkali kuhusu mada hiyo walifika mbali na kudai kuwa Tanzania itadhoofika kwa kuwafukuza Wakenya kwa vile inawategemea mno. Binafsi nadhani kauli za aina hii zina madhara zaidi kwa Wakenya wanaoishi kihalali nchini mwetu kuliko madhara kwa serikali na nchi yetu.

Wanaopandikiza chuki hiyo hawapo Tanzania, na endapo kauli zao zitaibua chuki dhidi ya raia wa nchi hiyo, hao wapiga kelele hawatoathirika moja kwa moja bali ndugu zao waliopo nchini mwetu. Lakini si jambo la kushangaza kuona mazuri ya Magufuli yakianza kukera baadhi ya watu. Walishazowea kuiona nchi yetu kama kituko. Na walinufaika na ulegelege uliokuwepo, ikiwa ni pamoja na upungufu katika udhibiti dhidi ya wahamiaji haramu.

Na katika hilo la kukerwa na utendaji unaotia moyo wa Magufuli si majirani zetu hao tu, majuzi nilisikia mahojiano ya kiongozi wa Chadema, Tundu Lissu, akitoa mtizamo wake kuhusu mwenendo wa Magufuli na serikali yake. Lugha yake haikuwa tofauti na inayosikika kwa wengi wa wafuasi wa vyama vya upinzani. Kwao, kufanikiwa kwa Magufuli ni kama kudidimia kwa vyama vyao.

Na hilo sio gumu kulielewa, kwa sababu kwa kiasi kikubwa kushamiri kwa upinzani nchini Tanzania ni matokeo ya udhaifu wa CCM, uliowapa wapinzani nafasi ya kusema chochote, kuliko uimara wa wapinzani binafsi. Kwa maana hiyo, hatua za Magufuli na serikali yake kupambana na mengi yaliyokuwa kero kwa Watanzania kunawanyima wapinzani fursa ya kuongea.

Lawama na shutuma za wapinzani zimevuka mipaka hadi kutugusa baadhi yetu ambao baada ya muda mrefu wa kukosoa mwenendo wa mambo katika nchi yetu, sasa tumepata ahueni kutokana na kazi nzuri ya Magufuli, na tunapata kila sababu ya kupongeza na kuinadi nchi yetu.

Binafsi, nimekuwa miongoni mwa waathirika wa shutuma hizo baada ya kuchapishwa kitabu kinachozungumzia safari ya urais wa Dk. Magufuli, mafanikio na changamoto kwa urais wake. Kuna wanaodai ni mapema mno kuzungumzia mafanikio ya kiongozi huyo, lakini bila kubainisha wakati gani ni mwafaka kuzungumzia mafanikio yake.

Kuna waliokwenda mbali zaidi na kudai kitabu hicho ni jitihada zangu binafsi kutafuta ukuu wa wilaya. Kwa uelewa wangu, shutuma hizo ni matokeo ya hadaa kubwa iliyofanyika kwa wafuasi wengi wa vyama vya upinzani kuwa vyovyote ambavyo ingekuwa, mgombea wao wa kiti cha urais, Edward Lowassa, lazima angeshinda kiti hicho.

Kuishi kinyume cha matarajio hewa si kitu rahisi, na huenda itachukua muda mrefu kwa wapinzani wa Magufuli kubaini kuwa kila zuri analofanya ni kwa maslahi ya Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kiitikadi. Tanzania ya neema si tu kwa waliompigia kura Magufuli bali kila Mtanzania, hata aliyemnyima kura.

Wakati tunaweza kuwaelewa majirani zetu wanaokerwa kuona Tanzania imeamka, haingii akilini kuona baadhi ya Watanzania wenzetu wakijifanya vipofu wasioona mabadiliko makubwa na ya kasi yanayoletwa na Magufuli na serikali yake. Walihadaiwa kuhusu mabadiliko, sasa wanaletewa mabadiliko halisi wanaanza kulalamikia.

Katika mahojiano yake niliyoyataja awali, Lissu anamlinganisha Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine, lakini si kwa uchapakazi wake na chuki yake kubwa dhidi ya wahujumu uchumi bali kile ambacho mwanasheria huyo anadai ni kutoheshimu sheria.

Pia alimfananisha Magufuli na Naibu Waziri Mkuu wa zamani, na sasa Mwenyekiti wa taifa wa TLP, Agustino Mrema, kuwa ni kiongozi anayefanya kazi ili aandikwe na vyombo vya habari. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Hivi kweli mazuri haya mengi yaliyojiri tangu Magufuli aingie madarakani ni kwa minajili ya kupata vichwa vya habari?

Nimalizie makala hii kwa kukumbusha kuwa kinyume na mabadiliko yaliyoahidiwa na Lowassa ambayo yalitarajiwa kutokea kama miujiza pasipo mipango madhubuti, tunachoshuhudia kwa Magufuli ni mabadiliko ya dhati yaliyobainishwa katika mikutano yake mbalimbali ya kampeni za uchaguzi, na kufafanuliwa kwa kirefu katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge jipya.


 Ushauri wangu kwa Watanzania wenzangu ni kupuuzia wote wanaokerwa na mwenendo wa kutia matumaini wa Magufuli na serikali yake. Wanasema ukirusha jiwe kizani kisha ukasikia kelele, basi ujue limempiga mtu. Hizi kelele, kebehi au shutuma dhidi yake ni matokeo ya jitihada zake za kizalendo za kuathiri waliokuwa wakinufaika na mwenendo fyongo wa nchi yetu katika maeneo mbalimbali. 

6 Jan 2016

KWA miaka kadhaa, makala zangu za wiki ya mwanzo wa mwaka huzungumzia matukio mbalimbali yanayotarajiwa kutawala habari katika mwaka husika. Makala hii ni mwendelezo wa utamaduni huo. Inajaribu kufanya ubashiri wa baadhi ya matukio yanayotarajiwa kujiri katika mwaka huu, ndani na nje ya nchi yetu.

Nianze na ubashiri wa matukio ya kimataifa. Mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu nchini Marekani. Kwa kuzingatia mwelekeo wa kampeni zinazoendelea nchini humo, ninabashiri kuwa Hillary Clinton atafanikiwa kushinda kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Democrats, ilhali kuna uwezekano mkubwa wa Donald Trump kuibuka mgombea kwa tiketi ya Chama cha Republicans.

Hata hivyo, uwezekano huo unategemea mambo matatu muhimu. Kwanza, kwa wote wawili, nafasi zao kushinda au kushindwa zitategemea mwenendo wa uchumi wa taifa hilo kubwa duniani. Iwapo uchumi wa Marekani utaimarika zaidi, basi Hillary na chama chake watakuwa na fursa nzuri zaidi hasa kwa kutegemea uungwaji mkono wa Rais wa sasa wa nchi hiyo, Barack Obama, kujivunia rekodi ya uchumi chini ya chama chao. Uchumi ukiyumba, Trump, ambaye ni mfanyabiashara tajiri anaweza kuonekana kama chaguo sahihi kuwa rais ajaye wa nchi hiyo.

Jambo la pili, ambalo pia linawahusu wote wawili, ni hali ya usalama nchini humo. Iwapo hali itaendelea kuwa salama kama ilivyokuwa katika miaka minane ya Rais Obama, mgombea wa Democrats, ambaye ninabashiri atakuwa Hillary, atakuwa na nafasi nyingine nzuri ya kujivunia umahiri wa Rais kutoka Democrats kama Obama kulihakikishia usalama taifa hilo linalowindwa kwa udi na uvumba na vikundi mbalimbali vya ugaidi wa kimataifa. Iwapo kwa bahati mbaya kutatokea tukio lolote kubwa la ugaidi, basi hali hiyo yaweza kumnufaisha mgombea wa Republicans, ambaye ninabashiri atakuwa Trump, kwa kigezo chepesi tu kuwa Democrats wameshindwa kuiweka Marekani kuwa salama.

Jambo la tatu ni mwenendo binafsi wa wanasiasa hao wawili. Kwa upande wa Hillary, uwezekano wa yeye kuibuka mgombea wa Democrats utategemea uchunguzi unaoendelea kuhusu matumizi ya barua-pepe binafsi akiwa Waziri wa Mambo ya Nje. Japo Wamarekani wengi hawaonekani kuguswa na yaliyokwishafahamika kuwemo katika maelfu ya barua-pepe hizo, iwapo uchunguzi utabaini makosa makubwa zaidi, basi nafasi ya mwanamama huyo anayewania kuwa rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo itakuwa finyu, na huenda akalazimika kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.

Kikwazo kingine kwa Hillary ni tuhuma zilizoibuka hivi karibuni zinazoashiria uhusika wake katika tenda inayoihusisha Kampuni ya Symbion ambayo inahusu mradi wa uzalishaji umeme nchini Tanzania. Japo alichofanya mwanasiasa huyo sio kitu cha ajabu katika siasa za Marekani na hata katika nchi nyingine, ikigundulika kuwa taratibu zilikiukwa ili kupendelea marafiki zake, anaweza kuathirika vibaya na pengine kulazimika kujiondoa katika harakati zake za urais.

Wasiwasi mkubwa kuhusu Trump ni ile tabia yake ya kuwa kama bomu lililotegeshwa kwa muda (time bomb). Pamoja na kuendelea kung’ara katika kura za maoni miongoni mwa ‘wagombea’ wa Republicans, mwanasiasa huyo hana upungufu wa vioja, na fursa yake ya ushindi itategemea sana jinsi atakavyodhibiti mdomo wake kati ya sasa na wakati wa mchakato rasmi wa chama chake kuteua mgombea. Na hata akiruka kikwazo hicho, bado kuna wasiwasi iwapo Wamarekani watakuwa tayari kumchagua mwanasiasa asiyetabirika. Na endapo watamchagua, basi taifa hilo linaweza kutengwa na nchi nyingi duniani.

Iwapo Hillary hataibuka mshindi kwa tiketi ya Democrats, ninabashiri kuwa nafasi hiyo itakwenda kwa Bernie Sanders, ambaye hata hivyo ana nafasi finyu kumshinda mgombea yeyote atakayepitishwa na Republicans. Na iwapo Trump hatopitishwa, ninabashiri mbadala wake kuwa aidha Ted Cruz au Marco Rubio.

Katika anga hizo za kimataifa, ninabashiri kuwa hali nchini Burundi itakuwa mbaya zaidi ya ilivyokuwa mwaka jana. Kadhalika, ninabashiri hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuzorota, hasa baada ya jitihada za Rais Joseph Kabila kutaka kuendelea kubaki madarakani.

Kadhalika, ninabashiri kuwa kundi la kigaidi la Boko Haram litaendelea kuisumbua Nigeria, huku kundi jingine la kigaidi la Al-Shabaab likiendelea kuzisumbua Somalia na Kenya. Pia kuna uwezekano wa kuwepo matatizo ya kisiasa huko Afrika Kusini na Zimbabwe yanayoweza kusababisha kung’oka madarakani kwa viongozi wa nchi hizo.

Habari za ugaidi wa kimataifa zinatarajiwa kuendelea kutawala anga za kimataifa huku makundi mawili hatari ya ISIS na Al-Qaeda yakiendelea kuwa tishio duniani, hususan nchi za Magharibi.

Kadhalika, ninabashiri kuwa eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati kuingia katika mgogoro mkubwa utakaoligawa eneo hilo kati ya Waislam wa madhehebu ya Sunni wakiongozwa na Saudi Arabia, na wale wa Shia wakiongozwa na Iran.

Kwa huko nyumbani, ninabashiri kuwa Rais Dk John Magufuli ataendelea na utumbuaji majipu, japo habari ninayobaishiri kuwa itatawala zaidi ni kuibuka kwa skandali mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na ambazo umma haukuwahi kuzifahamu. Kimsingi, harakati za Dk. Magufuli kutumbua majipu zina kila ishara ya kukutana na madudu yaliyosheheni wakati wa utawala wa mtangulizi wake.

Kadhalika, ninabashiri uwezekano wa baadhi ya mawaziri au manaibu wao kufukuzwa kwa kushindwa kuendana na falsafa ya Hapa Kazi Tu. Kwa vile si vema kumwombea mtu mabaya, ninahifadhi majina ya mawaziri ninaodhani wanaweza kuwa waathirika wa awali.

Vile vile, ninabashiri uwezekano wa kuwepo jitihada za chini chini ndani ya CCM kukwamisha dhamira ya Dk. Magufuli kukabiliana na ufisadi, rushwa, ujangili, biashara ya dawa za kulevya, na maovu mengine. Hata hivyo, jitihada hizo hazitafanikiwa.

Kwa upande mwingine, ninabashiri kuwa Dk. Magufuli ataendelea kunga’ra ndani na nje ya nchi, na dunia itaelekeza macho yake nchini Tanzania kutokana na mafanikio makubwa ya kiuongozi na jitihada za kufufua na kuboresha uchumi.

Kingine ninachoweza kubashiri ni ujio wa sura mpya nyingi katika uongozi ngazi za mikoa na wilaya, huku ikitarajiwa kuwa kama ilivyokuwa kwa Baraza la Mawaziri na Makatibu wakuu, wasomi mbalimbali wakiteuliwa kushika nyadhifa za u-RC na u-DC.

Kwa upande wa vyama vya upinzani, ninabashiri uwezekano wa jitihada za kumng’oa Mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, japo haitakuwa jambo la kushangaza iwapo atanusurika. Kwa kiasi kikubwa, uhai wa kisiasa wa Mbowe utategemea uhusiano wake na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Edward Lowassa.

Eneo ambalo ninashindwa kubashiri kwa uhakika ni hali ya kisiasa huko Zanzibar. Hata hivyo, ninaweza kubashiri bila uhakika kuwa CCM itafanikiwa kulazimisha marudio ya uchaguzi, na kuna uwezekano CUF wakasusia. Uwezekano mwingine ni kurejewa kwa kilichofanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, yaani kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa. Ubashiri sio sayansi timilifu (exact science) kwa hiyo nitahadharishe kuwa baadhi ya niliyobashiri yanaweza kuwa kinyume.

Ubashiri huu umetokana na kufuatilia kwa karibu siasa za kimataifa na za huko nyumbani.


Nimalizie makala hii kwa kuwatakia tena heri na baraka za mwaka mpya 2016. Kwa huko nyumbani (Tanzania), kuna kila sababu ya mwaka huu kuwa mzuri kutokana na dalili za awali za utawala wa Dk. Magufuli kuiondoa Tanzania yetu katika lindi la ufisadi na rushwa, vitu vilivyochangia mno kudumisha umasikini wa nchi yetu. Lakini ili afanikiwe, ni wajibu wa kila Mtanzania kutimiza ‘Hapa ni Kazi Tu’ kwa vitendo.Mwaka 1981, nikiwa darasa la tatu, marehemu baba aliamua kustaafu kazi, japo alikuwa amebakiwa na miaka kama 10 hivi ya utumishi katika Shirika la Posta. Wakati huo tulikuwa tunaishi Kigoma. Marehemu baba alikuwa na ndoto za kuwa mkulima mkubwa baada ya kustaafu maana tulikuwa na hekari kama 50 hivi za mashamba ya mpunga huko Ifakara. Kwahiyo, aliamini kuwa savings zake na mafao ya kustaafu vingekuwa mtaji wa kutosha kumwezesha atimize ndoto yake hiyo.

Hata hivyo, wanasema 'kuwa na ndoto ya kitu flani ni kitu kimoja, kuitimiza ndoto hiyo ni kitu kingine kabisa.' Mwaka mmoja baada ya kustaafu na familia yetu kurudi kijijini Ifakara, hali ya uchumi ilikuwa mbaya. Tatizo kubwa lililomkabili marehemu baba ni ukubwa wa ukoo huko kijijini ambao ulimtegemea yeye kwa msaada. Na wazazi wangu, yaani marehemu baba na marehemu mama, walikuwa watu wenye huruma mno. Kwahiyo waliona kuwa hawawezi kuacha kuwasaidia ndugu na ukoo kwa ujumla kwa vile tu wana mipango ya kilimo kikubwa. Pengine si wazo la busara lakini upendo ni kitu chenye nguvu mno na kikizidi chaweza kuvuruga kila mpango.

Maisha yangu kama mwanafunzi hapo Ifakara nilipohamia darasa la tatu hadi nilipomaliza darasa la saba, yalikuwa magumu mno. Kuna nyakati tulipitisha usiku kwa kunywa uji wa chukuchuku (usio na sukari wala chumvi), kuna nyakati tulilalia ndizi bukoba za kuchemsha na kikombe cha maji tu, mlo wa mchana ulikuwa wa kubahatisha, na mara kadhaa mchana ulipita kwa kunywa maji tu. Pia kuna usiku kadhaa tuliokwenda kulala bila kutia kitu tumboni.

Nilisoma kwa shida maana hatukuwa na umeme, japo umeme ulifika Ifakara mapema kabla ya sehemu nyingi za Tanzania kwa vile mradi wa umeme wa Kidatu ulikuwa jirani na mji huo. Familia iliyokuwa inahangaika na mlo wa siku moja isingeweza kumudu gharama za umeme ambazo wakati huo zilikuwa shilingi elfu kadhaa tu. Lakini licha ya kujisomea kwa kutumia koroboi na mara moja moja taa ya chemli pale tulipoweza kumudu kununua mafuta ya taa, Mungu alinijaalia nikafaulu kidato cha nne na kupata division one. Laiti ningefeli, ndio ungekuwa mwisho wa safari yangu kielimu maana familia isingemudu kunisomesha shule ya private.

Nikachaguliwa kujiunga na high school Tabora. Namshukuru Mungu kwani shule hiyo ilikuwa ya mchepuo wa kijeshi, maana niliondoka nyumbani nikiwa na nguo chache tu lakini pale shuleni tulitumia muda mwingi tukiwa kwenye yunifomu zetu za magwanda. Na hapo shuleni nilikwenda mikono mitupu, lakini bahati nzuri marafiki walinisaidia hela za matumizi. Na sikujali sana kwa sababu milishazowea shida.

Bahati ilinijia shuleni hapo nilipofanikiwa kuchaguliwa kuwa kiranja mkuu. Kwa vile ilikuwa shule ya kijeshi, 'cheo' changu kilifahamika kama Kamanda Mkuu wa Wanafunzi, kwa kimombo Students' Chief Commander, au kwa kifupi 'Chief.' Mpaka leo baadhi ya niliosoma nao huko Tabora wameendelea kuniita 'chifu.' Kupata ukiranja mkuu Tabora Boys' ilikuwa sio kazi rahisi hata kidogo. Mfumo wa uchaguzi ulihusisha uraia na ujeshi. Sikuomba kugombea bali nilipendekezwa tu. Na kimsingi haukuwa uchaguzi as such kwa sababu final say ilikuwa ni ya utawala wa shule na maafande. Nikabahatika kupata 'wadhifa' huo nikiweka historia ya kuwa 'chifu' mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya shule hiyo (kwa muda huo).

Uchifu ulinisaidia sana kukabiliana na ugumu wa maisha shuleni hapo kwani licha ya privileges kadhaa zilizoambatana na 'wadhifa' huo, pia nilikuwa nikipewa zawadi mbalimbali na wanafunzi wenzangu. Ndo raha za uongozi hizo.

Nilihitimu masomo yangu vizuri na kupata Division Two ya pointi 10. Ninaamini laiti nisingekuwa nakabiliwa na ugumu wa maisha, ningeweza kupata Division One nyingine.

Kutoka hapo nikaenda JKT Maramba, Tanga, na hiyo ilimaanisha maisha mengine ya kijeshi kwa mwaka mzima (ukichanganya na miaka miwili ya ujeshi Tabora Boys'). Lakini bahati ikaendelea kuwa nami kwani baada ya miezi michache tu nikateuliwa kuwa miongoni mwa vijana waliotakiwa kujiunga na Jeshi la Wananchi JWTZ kuwa marubani na mainjinia wa jeshi. Kwahiyo takriban robo tatu ya maisha yangu ya JKT yalikuwa kwenye kambi ya mafunzo ya RTS Kunduchi. Huko ilukwa ni kula na kulala tu tukisubiri utaratibu wa mchujo wa urubani na uinjinia wa jeshi. Mwishowe, sikuchaguliwa na nikarudi JKT Ruvu (kambi ya watoto wa vigogo) kumalizia muda wangu. Hapo napo maisha yalikuwa mtihani kwa sababu licha ya kambi kujaa watoto wa vigogo lakini pia ilikuwa karibu na Dar. Nashukuru Mungu nilipata marafiki kutoka familia zenye kujiweza ambao walinistiri.

Nilipomaliza nikaenda Tanga, na baada ya muda mfupi nikaajiriwa kuwa mwalimu katika sekondari ya Eckenford. Sikupata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu mwaka huo kwa vile kwa wakati huo, kujiunga na UDSM ulihitaji Division One ya Form Six, na mie nilikuwa na Division Two ya point 10 (yani kasoro point moja tu kuwa Division One).

Nikafundisha hapo kwa miaka miwili, kisha nikateuliwa kujiunga na Idara ya Usalama wa Taifa. Jinsi nilivyoteuliwa ni kama muujiza, lakini ninahisi walikuwa wakinifuatilia tangu nilipokuwa Tabora Boys' kwa sababu kuna wakati niliwahi kutembelewa na Afisa Usalama wa Taifa wa Mkoa huo.

Baada ya mwaka mmoja wa mafunzo ya kazi hiyo, nikaingia mtaani, lakini kwa vile nilikuwa na kiu ya elimu, baada ya miezi 9  'mtaani' nikachaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hata hivyo, wakati nikiwa chuoni niliendelea na kazi pia. Nilipomaliza nikarudi ofisini na takriban mwaka mmoja baadaye nikapata promosheni iliyodumu hadi nilipoteuliwa kuja kusoma huku Uingereza.

Japo baadaye yalijitokeza matatizo yaliyopelekea mie kuachana na kazi hiyo, utumishi wangu wa miaka 13 mfululizo haukuwa na doa, na ninajivunia rekodi yangu. Kilichoniponza ni kukataa umimi. Tulikuwa tukilipwa vizuri kabisa, kiasi kwamba nilionekana mjinga kuanza kukosoa maovu mbalimbali yaliyopaswa kukaliwa kimya. Siku zote nilikuwa nikiwaambia maafisa wenzangu, "tusiwe wabinafsi wa kufikiria hii mishahara mikubwa na posho tunazopewa ilhali huko mtaani ndugu, jamaa na marafiki zetu wanataabika. Basi angalau tutimize wajibu wetu na si kuendeshwa na maslahi binafsi." Pengine 'kimbelembele' ndo kiliniponza. Pengine ni ujinga tu, kama baadhi ya watu walivyohitimisha. Lakini deep in my heart, naamini nilifanya kitu sahihi, yaani kusimamia nilichoamini.

Fast forward miaka kadhaa mbele, leo japo sijafanikiwa kuhitimisha safari yangu ya elimu, kwa maana ya Shahada ya Uzamifu ambayo imenichukua kitambo sasa (nililazimika kusitisha masomo kutokana na matatizo niliyokumbana nayo kati yangu na mwajiri/mdhamini wa masomo yangu yaani taasisi niliyokuwa nafanya kazi.) Panapo majaliwa, mwaka huu, jina langu litaanza na "Dokta..."

Leo hii namshukuru Mungu, nimefanikiwa kuendelea kuwatumika Watanzania wenzangu kwa kutumia maandiko yangu, kitu nilichoanza rasmi mwaka 1998. Lakini pia namshukuru sana Mungu wangu na wazazi wangu kwa kuniwezesha kupata shahada tatu, na hii ya nne ndio naihangaikia. Nimepita katika vipindi vigumu mno, kulala na njaa, kusoma kwa koroboi, na kushindwa kuishi kama vijana wenzangu kwa vile nilitoka familia masikini.

Bahati nzuri, nikiwa hapa Uingereza, nilivutowa pia na wazo la kufanya kazi za kujitolea (volunteering). Na baadaye niliajiriwa kwenye taasisi zinazoshughulikia masuala ya wakimbizi. Fursa hizi zimeniwezesha kukutana na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, kutoka Somalia hadi Iraki, Venezuela hadi China, Zimbabwe hadi Kuwait, Eritrea hadi Sri Lanka. Nimejifunza mila na utamaduni wa mataifa mbalimbali. Lakini pengine kubwa zaidi, nimeweza kuwasaidia mamia na pengine maelfu ya watu waliokuja hapa kusaka ukimbizi. Laiti dua na sala zingekuwa zampatia mtu utajiri hapo kwa hapo, basi leo hii ningekuwa bilionea maana nimepata nyingi mno kwa kuwasaidia watu hao ambao wengi walikuja hapa kuokoa maisha yao.

Kwanini nimeandika yote haya? Kwa sababu licha ya kila shida niliyopata katika masiha ya umasikini niliokulia, nilijifunza kuhusu utu. Nimejifunza mengi kuhusu wale waliojinyima kwa ajili yangu, waliogawana nami kidogo walichokuwa nacho, walionishirikisha katika utajiri wa familia zao, walionijali licha ya kutoka familia masikini. Na pia nimejifunza kuwa wema hauozi. Mamia kwa maelfu ya wakimbizi niliowasaidia hapa Uingereza, ninapokutana nao mpaka natamani kujificha kwa jinsi wanavyonimwagia shukrani, sala na dua. Nimejifunza kuhusu utu.

Leo ninamiliki kampuni japo ndo imeanza tu mwezi uliopita. Jana nilikutana na mwalimu wangu (mentor) wa masuala ya biashara, akaniuliza  matarajio yangu kwa mwaka huu 2016. Nijamjibu kwa utani "ninataka hadi kufikia mwisho wa mwaka huu niwe nimetengeneza paundi milioni moja za kwanza kwa kampuni yangu..." kisha nikacheka. Hakupendezwa na kicheko hicho.Akaniambia "japo unaona kama mzaha, lakini una kila nyenzo ya kukuwezesha kutimiza hilo. Cha muhimu, amini katika uwezo wako wa kiakili, upeo wako mkubwa, na historia yako ulivyotoka kwenye umasikini hadi kufikia hapa." Hawa 'wazungu' hawana tabia ya kumpa mtu sifa asizostahili. Kama wewe ni 'bomu' watakwambia, kama wewe ni mzuri watakwambia. Hakuna 'kuzugana.'

Huko nilikotoka na nilikopitia ndo kwanifanya kuwa mtu niliye leo: namchukulia kila mtu kuwa ana thamani yake. Siangalii tofauti ya kielimu kama sababu ya kumdharau mtu ambaye hakubahatika kuelimika sana. Digrii zangu hazina thamani kama sina utu. Kidogo ninachomudu kukipata hapa (ambacho pengine ni kikubwa sana kwa shilingi yetu huko nyumbani) hakinifanyi kujiona tofauti na wanaopata pungufu ya changu.

Namshukuru Mungu kwa baraka zake, nawashaukuru marehemu wazazi wangu kwa kunifundisha kuwa humble (mtu asiyejikweza) na kuwa mtu wa msaada, nawashukuru wote walioniwezesha kupitia safari yangu ndefu iliyojaa milima na mabonde, hasa wale walionifundisha kujali utu badala ya kitu.

Kwa sie Wakristo, tunafundishwa katika Biblia Takatifu kuwa 'wajikwezao watashushwa, na wajishushao watakwezwa.' Naomwomba Mungu aniwezesha kuwa mtu niliye leo hata nikitokea kufanikiwa kimaisha kiasi gani. 

Ndoto yangu ya utotoni ni kuwa daktari wa utabibu ili niweze kuwasaidia watu wengi kadri iwezekanavyo. Bahati mbaya sikufanikiwa. Ndoto yangu ya pili ilikuwa kuwa shushushu (kwa hamasa za Willy Gamba), nilifanikiwa kuitimiza, nikalitumikia taifa langu kwa nguvu zangu zote. Bahati mbaya mambo yakaenda 'kushoto.' Ndoto yangu ya sasa ni kutumia elimu, kipaji, ujuzi na uzoefu wangu kuendelea kuwasaidia watu wengine hususan wale wanaoishi katika hali kama niliyokulia. 

Ninatumaini msomaji mpendwa waweza kujifunza kitu kimoja au viwili katika stori hii.

Happy new year!


2 Jan 2016Heri ya mwaka mpya. Nina furaha kuwafahamisha kuwa kitabu kipya, "Dokta John Pombe Magufuli: Safari ya Urais, Mafaniko na Changamoto katika Urais wake" sasa kinapatikana. Kitabu hiki ni mfululizo wa vitabu kadhaa ninavyotarajia kuvichapisha mwaka huu 2016. 

Wakati kitabu hiki kikiingia sokoni, kitabu kingine kuhusu taaluluma ya Usalama wa Taifa kipo katika hatua za mwisho, na matarajio ni kukiingiza sokoni mwishoni mwa mwezi huu.

Kitabu hiki cha Dokta Magufuli kina sura sita. Katika utangulizi, kitabu kinazungumzia mazingira ya uchaguzi mkuu uliopita, msisitizo ukiwa kwenye hali ya nchi ilivyokuwa kabla ya uchaguzi huo.

Kadhalika, utangulizi huo unaelezea mabadiliko ya ghalfa ya kisiasa, hususan ndani ya CCM, yaliyojitokeza kufuatia jina la mwanasiasa aliyekuwa maarufu kuliko wote wakati huo, Edward Lowassa, kukatwa na chama hicho tawala wakati wa mchakato wa kupata mgombea wake wa kiti cha urais.

Sura ya kwanza inamtambulisha Dokta Magufuli, kwa kuangalia historia fupi ya maisha yake. Sura ya pili inaeleza mchakato aliopitia Dkt Magufuli hadi kuibuka mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM. Sura hii inachambua kwa undani ushindani miongoni mwa makada zaidi ya 40 waliochukua fomu kuwania urais kupitia chama hicho.

Sura ya tatu inaelezea fursa alizokuwa Dokta Magufuli na CCM kwa ujumla katika kipindi cha kampeni na uchaguzi mzima kwa ujumla. Sura hii inachambua uimara wa mwanasiasa huyo sambamba na turufu za kawaida za CCM katika kila uchaguzi. Kwa uapnde mwingine sura hiyo yaangalia pia mapungufu yaliyopelekea urahisi kwa Dokta Magufuli kumshinda mpinzani wake mkuu Lowassa, sambamba na mapungufu ya UKAWA yaliyoiwezesha CCM kushinda.

Sura ya nne inajadili changamoto na vikwazo kwa Dokta Magufuli na CCM kwa ujumla wakati wa kampeni. Kadhalika, sura hii inazungumzia jinsi Lowassa na UKAWA walivyoshindwa kutumia changamoto hizo za wapinzani wao.

Sura ya tano inajadili urais wa Dokta Magufuli tangu aingie Ikulu, wakati sura ya mwisho inajadili changamoto zinazoukabili urais wake na kutoa mapendekezo.

Nimejitahidi kadri nilivyoweza kuandika kitabu hicho kama mtu niliyeufuatilia uchaguzi huo kwa karibu. Natambua kuna wanaoweza kuwa na hofu kuwa 'niliisapoti CCM na Dokta Magufuli wakati wa kampeni, na kutoiunga mkono UKAWA na Lowassa.' Naomba kuwatoa hofu kwani kitabu hiki ni si cha kiitikadi bali kwa ajili ya Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kiitikadi.

UTAKIPATAJE?

Bei ya kitabu sasa ni Shilingi 4,000 tu. Ili kukipata, nunua kwa M-PESA namba 0744-313-200 jina JOHN ZABLON MPEFO au TIGO-PESA namba 0652-112-071 jina CHRISTINE JOHN MANONGI

KARIBUNI SANA

31 Dec 2015

KUTOKANA na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu, wiki mbili zilizopita nilishindwa kuwaletea makala kwenye safu hii. Hata hivyo, kwa bahati nzuri nilichopanga kuandika katika makala hiyo kimechukua sura mpya kati ya wiki iliyopita na muda huu ninapoandika makala hii.
Nilidhamiria kuzungumzia maoni ya wananchi mbalimbali kuhusu uteuzi wa baraza la mawaziri la Rais Dk. John Magufuli. Kimsingi, japo baraza hilo limepokelewa na wengi kama linaloweza kumsaidia Rais kutekeleza kauli-mbiu yake ya ‘Hapa ni Kazi Tu,’ baadhi ya sura zilizomo kwenye baraza hilo zilionekana kama zinazoweza kuwa kikwazo.
Uteuzi ulionekana kuwagusa wengi ulikuwa wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Nikiri kwamba nami nilikuwa miongoni mwa walioshtushwa na uteuzi huo japo tetesi ziliashiria mapema kuhusu uwezekano wa msomi huyo kuwamo katika baraza hilo jipya.
Wakati wengi waliohoji kuhusu Profesa Muhongo kupewa uwaziri walielemea kwenye ukweli kwamba alilazimika kujiuzulu katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow, binafsi nimeendelea kutatizwa na kauli yake ‘ya dharau’ kuwa Watanzania hawana uwezo wa uwekezaji mkubwa, na wanachomudu ni biashara ya juisi tu.

Kwa bahati mbaya au pengine kwa makusudi, Profesa Muhongo hajawahi kuona haja ya kuifuta kauli hiyo au pengine japo kujaribu kuifafanua. Wanaomfahamu, wanadai ni mchapakazi mzuri. Lakini kwa kuzingatia taratibu za ajira kwa hapa Uingereza, miongoni mwa sifa za uchapakazi ni uhusiano mwema na watu (people skills) na uwezo wa kuwasiliana nao kwa ufanisi (communication skills).
Ili uchapakazi ulete ufanisi, ni lazima mtendaji amudu kuelewana na watu wengine, kwa maana ya uhusiano bora unaojali utu na heshima. Kadhalika, ni muhimu kwa mhusika kuweza kuwasiliana nao kwa ufanisi. Sasa, kiongozi anayedharau uwezo wa wenzake, kama hiyo kauli ya Muhongo kuwa uwezo wa Watanzania katika uwekezaji unaishia kwenye kuuza juisi tu, anajiweka katika wakati mgumu katika utendaji kazi wake.
Hata hivyo, kwa bahati nzuri inaelekea Profesa Muhongo ameanza kubadilika. Majuzi, nilikutana na habari inayomhusu na ambayo ilinipa faraja kubwa. Alinukuliwa na vyombo vya habari vya huko nyumbani akihamasisha Watanzania wazawa kujitokeza na kushiriki kuwekeza katika sekta ya umeme.
Kwa tafsiri ya haraka, ni wazi kauli hiyo inaashiria kuwa Profesa Muhongo sasa ana imani na Watanzania, kwamba wanaweza kuwekeza sio kwenye biashara ya juisi pekee bali hata kwenye sekta ya umeme.
Japo hajaomba radhi wala kutolea ufafanuzi kauli hiyo ya awali, kuna umuhimu wa kuangalia suala hilo katika mtizamo wa ‘yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo.’
Rai hiyo ya Waziri Muhongo kuwataka wazawa wajitokeze kuwekeza katika sekta ya umeme ni ya kizalendo na inaendana na jitihada zinazofanywa na nchi kama Nigeria na Rwanda ambazo zimekuwa zikihamasisha sana wazawa kujitokeza na kushiriki kwenye uwekezaji katika sekta mbalimbali, badala ya kuliacha suala la uwekezaji kuwa la wageni tu.
Lakini wakati Profesa Muhongo ‘akijisafisha,’ kwa bahati mbaya kuna Waziri mwingine mpya ameanza kuonyesha mkanganyiko katika kauli zake, hali inayoleta wasiwasi iwapo anamudu kuendana na kaulimbiu ya ‘Hapa ni Kazi Tu.’
Mwishoni mwa wiki mbil zilizopita. Vyombo vya habari vya huko nyumbani vilimnukuu Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, akiutaka uongozi wa Jeshi la Polisi kumfikishia taarifa kuhusu tatizo sugu la biashara haramu ya dawa za kulevya. Kauli hiyo ya waziri iliamsha furaha na matumaini kwa Watanzania wengi, hususan katika mitandao ya kijamii.
Cha kushangaza, baada ya hapo, Waziri Kitwanga alinukuliwa akitoa kauli za kuvunja moyo ambapo alidai, namnukuu, “Sina listi ya wauza dawa za kulevya, na orodha hainisaidii zaidi ya kuwa na mfumo mzuri wa kuyadhibiti.” Hivi hizo dawa za kulevya zinajiuza zenyewe au kuna watu wanaohusika kuziingiza au kuzisafirisha? Kama kuna wahusika, iweje waziri adai orodha ya wahusika haimsaidii katika jitihada za kudhibiti biashara hiyo haramu inayogharimu maisha ya vijana wengi wanaoyatumia?
Na kauli yake kwamba hana orodha inaashiria upungufu wake. Anataka orodha ijilete yenyewe ofisini kwake? Angejihangaisha kidogo tu kwenda mtandaoni au kupitia mafaili ya Jeshi la Polisi hususan Kitengo cha Dawa za Kulevya au huko Usalama wa Taifa, angeweza kupata kirahisi orodha hiyo. Binafsi, ilinichukua dakika mbili tu kwenye Google kukutana na orodha kadhaa za wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo.
Waziri Kitwanga aliendelea kudai, namnukuu, “Sijui kama Rais alipewa orodha, hajawahi kuniambia ila kama mna ushahidi mnisaidie nilifanyie kazi.” Japo ni mapema mno kumhukumu, lakini kauli hii haiendani kabisa na kaulimbiu ya Dk. Magufuli ya ‘Hapa ni Kazi Tu.’ Kama Waziri Kitwanga hajui iwapo Rais alipewa orodha hiyo, na kama hajamwambia, kwa nini asimuulize bosi wake iwapo yeye Waziri ana dhamira ya kweli kushughulikia suala hilo?
Halafu kwa vile katika nukuu ya kwanza ametanabaisha kuwa orodha hiyo
(ya wahusika katika biashara ya dawa za kulevya) haimsaidii katika jitihada za kuidhibiti biashara hiyo, sasa anataka wananchi wamsaidieje? Na pengine kinachovunja moyo zaidi ni hilo la kudai ushahidi. Si kazi ya wananchi kutafuta ushahidi kwani kuna watendaji wanaolipwa mishahara kwa ajili ya kazi hiyo. Na hata ingekuwa ni jukumu la wananchi, Waziri Kitwanga si raia wa kigeni, ni mwananchi pia, na kwa maana hiyo wito wake kwa wananchi unamhusu yeye pia.

Moja ya vikwazo vyetu katika matatizo mengi yanayoikabili nchi yetu ni ukosefu wa nia ya dhati ya kupambana na matatizo husika. Sambamba na hilo ni kukosekana kwa ubunifu. Laiti Waziri Kitwanga angekuwa mbunifu, asingekurupuka kutoa kauli hizo za juzi kwani kimsingi zinahusu majukumu ambayo Watanzania na Rais Dk. Magufuli wanataraji ayatekeleze kwa ufanisi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge jipya, Rais Magufuli alieleza bayana kuwa vita dhidi ya ufisadi, rushwa na dawa za kulevya ni ngumu na hatari kwani inahusisha wakubwa. Na wiki mbili zilizopita, Waziri Kitwanga alinukuliwa akijigamba kwamba hahofii kufa (akimaanisha kuwa hatishwi na nguvu kubwa ya wahusika katika biashara hiyo ya dawa za kulevya). Lakini kauli zake katika siku zilizofuata zinaweza kujenga picha ya mtendaji mwenye hofu ya kukabiliana na tatizo hilo.
Wengi tunaitakia kila jema Serikali ya Rais Magufuli, na makala hii inatekeleza hilo lakini kwa kukosoa upungufu uliojitokeza. Kama kweli tuna nia ya kumsaidia Rais wetu na serikali yake, basi tusiishie kusifia tu bali pia kukosoa pale inapobidi.
Nimalizie makala hii kwa ushauri kwa Waziri Kitwanga, mamlaka zinazohusika na suala la dawa za kulevya na serikali kwa ujumla: ni vigumu kuwakamata wahusika wakuu wa dawa za kulevya kwa urahisi. Wanatumia mbinu nyingi ikiwa ni pamoja na kuficha au kuharibu ushahidi. Moja ya njia zilizoonyesha mafanikio sehemu mbalimbali duniani ni kuwabana wahusika kwa ukwepaji kodi na kile Waingereza wanaita ‘proceeds of crime,’ yaani mali zilizopatikana kutokana na uhalifu. Njia hiyo sio tu husaidia kuwapunguzia wauza dawa za kulevya uwezo wao kifedha, lakini pia huwezesha kubaini utajiri wao ulivyopatikana (na hivyo kuleta uwezekano wa kubaini uhusika wao katika biashara haramu) na pia kuwalipisha fidia kutokana na maovu yao.
Penye nia pana njia, pasipo na nia pana visingizio25 Dec 2015

11 Dec 2015

Julai 8 mwaka huu itabaki moja ya siku zenye kumbukumbu chungu maishani mwangu. Ni siku ambayo baba yangu mzazi, Mzee Philemon Chahali alifariki dunia baada ya kuugua kama kwa wiki hivi.  Japo miaka 7 kabla ya hapo nilikumbwa na msiba mwingine ambapo mama yangu mepndwa, Adelina Mapango, alifariki baada ya kupoteza fahamu kwa zaidi ya miezi mitano, na japo hakuna msiba wenye nafuu, lakini angalau marehemu mama alifariki nikiwa huo Tanzania nilikoenda kumuuguza.  Lakini katika kifo cha baba, kilitokea nikiwa mbali na nyumbani. Na kwa hakika, nyakati za misiba, tunahitaji mno sapoti ya wenzetu kutuliwaza na kukabiliana na uchungu wa kufiwa.

Kwanini ninarejea habari hiyo ya kuskitisha? Kwa sababu tukio hilo ndilo lilinipa nafasi ya kumfahamu vema zaidi mmoja wa wanasiasa maarufu nchini Tanzania, January Makamba, Mbunge wa CCM Bumbuli na mmoja wa makada zaidi ya 40 waliojitokeza kuwania Urais kupitia CCM, na alifanikiwa kuingia katika 'Tano Bora.'

Mara baada ya kutangaza kuwa nimefiwa, January alinipigia simu kunipa pole, na kuulizia jinsi ya kuwasilisha rambirambi yake, ambayo baadaye aliiwasilisha. Pengine kwa watu wengine wanaweza kuliona hili kama ni jambo dogo tu na la kawaida. Lakini kimsingi, sote twafahamu viongozi wetu walivyo busy na majukumu yao, ambayo kwa kiasi kikubwa huwafanya waonekane kama binadamu wasiofikika (inaccessible). Kwa Afrika, ni vigumu sana kukuta kiongozi awe wa kisiasa au kwenye sekta nyingine akiwa karibu na raia wa kawaida, au kufuatilia yanayowasibu. Na kwa wanaomfahamu, amekuwa akiwasaidia watu wengi waliofiwa na wenye matatizo mbalimbali, at least ninaowafamu mie mtandaoni. Ni wazi mtu akiwa mwema kwa watu mtandaoni lazima pia ni mwema katika maisha yake nje ya mtandao.

Nimeanza makala hii na suala hilo binafsi kwa sababu ndilo lililonipa fursa ya kumfahamu kwa karibu zaidi. Awali nilimfahamu kama mwanasiasa kijana aliye karibu na watu wengi, hususan mitandaoni, lakini sikujua 'human side' (utu) yake. 

Tukiweka hilo kando, katika siasa za hivi karibuni za Tanzania, January alikuwa mwanasiasa wa kwanza kabisa kutangaza azma yake ya kuwania urais mwaka huu. Alitoa nia yake takriban mwaka mzima kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato huo. Wengi walipokea tamko lake hilo, hasa kwa matarajio kuwa lingewashawishi wanasiasa wengine waliokuwa wanawania nafasi hiyo kujitokeza, na hiyo ingesaidia kuwafahamu vizuri. Kwa hiyo, kwa kifupi, January ndiye aliyepuliza rasmi kipenga cha kuwania urais wa awamu ya tano/

Wakati ukaribu wa mwanasiasa huyo kijana na wananchi, hususan katika mitandao ya kijamii ilikuwa ni turufu yake muhimu, moja ya downsides za kufahamiana na watu wengi ni uwezekano wa baadhi ya 'wakorofi' kujipa uhuru wa kusema chochote kile hata isipostahili. Na katika hili, January alikumbana na mengi: wapo waliomdhihaki wakiona dhamira yake ya urais kama ndoto tu, kashfa zisizostahili, nk. Hata hivyo, mara zote alimudu kuwajibu 'wapinzani' wake kwa lugha ya kistaarabu.

Baadaye alichapisha kitabu chake kilichokuwa na visheni yake ya urais. Again, kitabu hicho kilipokelewa kwa mtizamo chanya na Watanzania wengi japo kulikuwa na kundi dogo 'waliokiponda.' Kimsingi, kitabu hicho kilikuwa na masuala mengi ya msingi kuhusu matatizo ya Tanzania yetu na mikakati ya kuyakabili. Kwahiyo, kinaweza kabisa kuwasaidia watu mbalimbali wanaotaka kuifahamu vema nchi yetu.

Mchakato wa CCM kumpata mgombea wake ulipoanza rasmi, January aliibuka kuwa mwanasiasa pekee tishio kwa Edward Lowassa, kada amabye alitajwa kuutaka urais kwa miaka kadhaa. Tofauti na Lowassa ambaye umaarufu wake ulichangiwa zaidi na uwezo wake wa kifedha, mafanikio ya January katika kampeni yake yalichangiwa zaidi na ukaribu wake kwa watu, hususan vijana.

Na japo hakufanikiwa kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, kuingia kwake kwenye 'Tano Bora' ni mafaniko makubwa kabisa, hasa ikizingatiwa kuwa bado ni kijana anayeweza kuyatumia mafanikio yake ya mwaka huu katika chaguzi zijazo. Yayumkinika kuhitimisha kuwa mwanasiasa pekee ambaye mpaka muda huu anatajwa kuwa rais ajaye wa Tanzania baada ya Magufuli ni January.

Baada ya Magufuli kushinda urais, zikaanza tetesi kuwa 'January anataka Uwaziri Mkuu.' Ni muhimu kukumbuka kuwa katika muda mwingi wa harakati zake za kisiasa, mwanasiasa huyo amekuwa akiandamwa na 'wasemaji wasio rasmi' wanaojifanya kumjua zaidi ya anavyojijua mwenyewe. Hakuna wakati au mahali popote ambapo January alisema ana matarajio ya kuwa Waziri Mkuu. Ni hisia tu za watu - waliomtakia mema kutokana na mchango wake mkubwa katika kampeni za CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, na 'wabaya' wake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakimzushia vitu mbalimbali.

Rais Magufuli alipomtangaza Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu, yakazuka maneno kuwa 'January kakosa Uwaziri Mkuu,' kana kwamba alitangaza kuwa anawania au anatarajia nafasi hiyo. 

Baada ya kitendawili cha uwaziri mkuu kuteguliwa, likabaki fumbo la baraza la mawaziri. Hapo napo yakazuka maneno chungu mbovu. January akapangiwa Wizara kadhaa na 'wanaomjua zaidi ya anavyojijua mwenyewe.' Lakini kuna waliodiriki kuweka 'chuki' zao hadharani na kuombea asiwemo kabisa katika baraza jipya la mawaziri. Ukiwauliza 'kwa lipi alilowakosea,' nina hakika hawana jibu.

Jana baraza likatangazwa. Na January akapanda kutoka Unaibu Waziri katika Awamu iliyopita na kuwa Waziri Kamili. Haya ni mafanikio makubwa kwa mwanasiasa kijana kama yeye. Kama kazini, hiyo ni promosheni, kutoka unaibu waziri hadi uwaziri kamili. Lakini kwa vile 'wabaya' wake walishampangia wizara, January kupewa Uwaziri katika ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira imetafsiriwa nao kama 'amepewa kitu pungufu.' Jamani, mtendeeni haki mwanasiasa huyu. Pungufu kivipi ilhali kiukweli amepandishwa cheo kutoka unaibu waziri hadi kuwa waziri kamili?

Jana nilitwiti matarajio yangu kwa January katika nafasi hiyo mpya, na ninashukuru mapokeo yalikuwa mzuri. Maeneo mawili ya majukumu yake ya kiuwaziri ni muhimu sana, na nina hakika atawashangaza wengi. Kwa upande wa Muungano, sote twaelewa hali ya kisiasa ilivyo huko Zanzibar. Kwahiyo, kwa nafasi yake, January anatarajiwa ku-play role muhimu katika jitihada za kutafuta suluhisho la mgogoro wa kisiasa visiwani humo. Lakini licha ya mgogoro huo, moja ya vitu vinavyotishia ustawi wa Muungano wake ni kero zake za muda mrefu. Kwa vile Janaury ni msomi katika tasnia ya usuluhishi wa migogoro (confilict resolution), na kutokana na profile yake kubwa kimataifa, ninatarajia kuwa ataweza kuyashughulikia masuala yote mawili kwa ufanisi mkubwa.

Na katika suala la mgogoro wa kisiasa huko Zanzibar, hali ya 'ubinadamu' kwa maana ya utu au 'humani side' ya January itakuwa na umuhimu wa kipekee. Migogoro ya aina hiyo inahitaji mtu mwelewa, mtulivu, na mwenye busara, sifa ambazo January anazo. Kuweza kuwashawishi Wazanzibari waweke maslahi ya taifa mbele ya maslahi ya vyama vyao kunahitaji mtu ambaye anapoongea anaonekana kama ndugu au rafiki na si mwanasiasa au kiongozi flani. Kwa kifupi, human side ya mpatanishi ni muhimu mno katika tasnia ya utatuzi wa migogoro.

Lakini kama kuna eneo ambalo ninatarajia makubwa zaidi kutoka kwa mwanasiasa huyo ni MAZINGIRA. Moja ya masuala muhimu kabisa dunain kwa sasa ni masuala ya mazingira. Japo kwa Afrika, masuala hayo hayazungumziwi sana japo bara hilo ndilo lililo hatarini zaidi kimazingira, hususan kutokana na matatizo ya kiuchumi na umasikini, Mijadala mbalimbali muhimu inayoendelea duniani kwa sasa nipamoja na kuhusu masuala ya mazingira. Kubwa zaidi ni suala la global warming ambalo wanasayansi wanatahadharisha kuwa lisiposhughulikiwa kikamilifu linaweza kupelekea kuangamia kwa sayari yetu.

Kwa nchi masikini kama Tanzania, masuala ya mazingira yana umuhimu wa kipekee (japo hayazungumziwi inavyostahili) kwa sababu kama tunakwama katika kukabiliana na matatizo yaliyo katika uwezo wa kibinadamu, hali inakuwaje tunapokabiliwa na matatizo ya kiasili (natural) yaliyo nje ya uwezo wa kibinadamu?

Kwa upeo mkubwa alionao na uhodari wake wa kuwasilisha hoja, sintoshangaa kuona huko mbeleni January akitokea kuwa mmoja wa watu muhimu duniani katika masuala ya mazingira. Na uzuri ni kwamba ameingia katika wizara inayishughulikia masuala hayo wakati ambapo jina la Tanzania limeanza kuvuma kwa uzuri kutokana na sifa za uchapakazi wa Rais Magufuli.

Ninasema pasi hofu kuwa sintoshangaa miaka michache ijayo tukashuhudia kwa mara ya kwanza Tanzania ikitoa mshindi wa Tuzo ya Nobel aidha katika usuluhishi wa mgogoro wa Zanzibar au masuala ya mazingira, au hata yeye kuchaguliwa kuwa Mtu wa Mwaka wa jarida la kimataifa la TIME la Marekani (TIME's Person of the Year). 

Nimalizie kwa kueleza kuwa lengo la makala hii ni kuweka sawa kumbukumbu kuhusu watu muhimu katika tanzania yetu, kama January, kwa mahitaji ya sasa na huko mbeleni. Kma taifa, tunakabiliwa na mapungufu makubwa ya uhifadhi wa kumbukumbu. Na japo mie si mbashiri, natumaini kuna siku makala hii itatumika kama reference baada ya 'January kuishangaza dunia' katika eneo fulani. 

Mwisho, ninawatakia kila la heri mawaziri wote walioteuliwa na Rais Magufuli katika kabineti yake mpya, nikiwa na matumaini makubwa kuwa wataendana na kasi yake ya uchapakazi na hivyo kutupatia Tanzania tunayostahili. 

Nawatakia siku njema.Nunua Vitabu Vyangu

Categories

STOP ALBINO KILLINGS

STOP ALBINO KILLINGS

Blog Archive

© Evarist Philemon Chahali 2006-2014

JUMUIKA NAMI TUMBLR

  Sehemu Ninahifadhi Nyaraka Zangu!

Powered by Blogger.

Bonyeza picha kununua kitabu hiki

Featured post

Mwaka 1981, nikiwa darasa la tatu, marehemu baba aliamua kustaafu kazi, japo alikuwa amebakiwa na miaka kama 10 hivi ya utumishi katika ...

The Evarist Chahali Weekly

Download "Chahali Blog ANDROID App"

Download Chahali Blog BLACKBERRY App

UNGANA NAMI FACEBOOK

Instagram