18 Apr 2015

KWA siku kadhaa sasa kumekuwa na mjadala mkali, hususani katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu sheria mpya ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni (Cyber Crime Act 2015).


Kabla ya kuuzungumzia mjadala huo, ningependa kumpongeza Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kwa kufanya tukio la kihistoria la kuuweka hadharani muswada husika katika mtandao wa kijamii wa Twitter ili ujadiliwe.
Ninatambua kuna uwezekano wa baadhi ya watu kudai haistahili pongezi kwa sababu, kwanza hilo ni jukumu la kila mtendaji wa serikali, na pili, kuleta muswada huo siku chache kabla haujawasilishwa kwa hati ya dharura Bungeni kusingewapa wadau nafasi ya kutosha kuujadili.



Katika hilo la kwanza, ni muhimu tutambue kuwa Tanzania yetu ya sasa imefikia mahala ambapo kiongozi akitimiza wajibu wake anastahili kupongezwa kwani hata asipotimiza wajibu anaolipwa mshahara kuutekeleza hatoathirika. Ni wazi basi, hata kama January angeamua kutouweka muswada huo hadharani, isingemwathiri lolote.



Kuhusu muswada huo kuwasilishwa kwa hati ya dharura, ninaafikiana na wanaolalamikia hatua hiyo kwa sababu licha ya dhamira nzuri na umuhimu wa kuwa na sheria ya kudhibiti uhalifu wa mtandaoni, bado kulikuwa na haja ya wananchi kupewa elimu ya kutosha kuhusu masuala kadhaa, hasa ikizingatiwa kuwa Watanzania wengi bado ni ‘wageni’ katika masuala ya mtandao (wa intaneti.)



Na pengine kabla ya kuingia kwa undani katika kuzungumzia mjadala huo na muswada huo ambao ulipitishwa na bunge na hadi wakati ninaandika makala hii ulikuwa ukisubiri kuidhinishwa na Rais Jakaya Kikwete ili uwe sheria kamili, ni muhimu kuweka wazi msimamo wangu kwamba ninaunga mkono muswada na sheria husika.



Ninaunga mkono kwa sababu kuu tatu: kitaaluma/kitaalamu, kijamii na binafsi. Kwa upande wa kitaaluma/kitaalamu, huko nyuma niliwahi kufanya kazi katika sekta ya usalama, na kwa muda mrefu nimekuwa nikijihusisha na stadi zinazohusu sekta hiyo.



Kwa hiyo, utaalamu na uelewa nilionao, unanisukuma kuunga mkono haja ya, na umuhimu wa kuwa na sheria ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni.



Kwa kifupi tu, pamoja na faida zake nyingi, mtandao unaweza na umeshaweza kutumika vibaya na kusababisha madhara makubwa.



Pamoja na kurahisisha mawasiliano na kufanikiwa kuiunganisha dunia na kuwa kama kijiji (ninaandika makala hii nikiwa hapa Uskochi, na nikimaliza na kubonyeza ‘send’ inamfikia mhariri wa gazeti hili muda huohuo, tofauti na njia za zamani ambapo ingelazimu kutuma makala hii kwa barua, na kuchukua siku kadhaa njiani), mtandao umekuwa kichaka cha maovu hasa kutokana na teknolojia husika kuwezesha mawasiliano pasipo watu kukutana ana kwa ana.



Kwa mfano, wakati kabla ya ujio wa teknolojia ya mtandao, ilikuwa vigumu kwa ‘mwizi’ kuiba fedha za mwenye akaunti benki bila kufika katika benki husika (au kuziiba wakati mwenye akaunti anaenda kuweka fedha hizo au kuzichukua benki), kwa sasa teknolojia ya mtandao inamwezesha mwizi aliyepo hata mbali na benki au mwenye akaunti kuziiba fedha hizo. Japo pengine hili halijashamiri sana huko nyumbani, ukweli ni kwamba wizi wa aina hiyo umetawala sehemu mbalimbali duniani.



Lakini kiusalama, mtandao umetokea kuwa moja ya nyenzo muhimu za magaidi, ambavyo vikundi maarufu vya kigaidi duniani kama Al-Qaeda, ISIS, Boko Haram na Al-Shabaab, vimekuwa vikiutumia vyema mtandao katika harakati zao dhalimu za ugaidi.



Katika tukio linaloweza kuonekana la kufikirika tu, magaidi wanaweza kutumia mitandao ya kijamii au hata ‘Whatsapp’ kusambaza ujumbe unaoweza kutishia amani na kusababisha madhara makubwa.



Sheria ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni imekuja wakati mwafaka hasa kwa kuzingatia uwepo wa taarifa zinazoashiria tishio la ugaidi, kufuatilia shambulio la kigaidi lililofanywa hivi karibuni na magaidi wa Al-Shabaab huko Garissa, nchini Kenya na kusababisha vifo takriban 150.



Ninathamini sana haki za raia kuwasiliana pasipo hofu ya serikali au taasisi zake za usalama kuyafuatilia mawasiliano yao, lakini pia ninatambua kuwa ili serikali iweze kutekeleza jukumu lake la kulinda usalama wa raia, inalazimika kufahamu mawasiliano yasiyo na nia nzuri kwa taifa letu.



Katika zama hizi hatari tunazoishi, ni vigumu mno kupata uwiano stahili kati ya uhuru na sheria kwani wahalifu wanaweza kuutumia uhuru huo kwa dhamira mbaya inayoweza kupelekea raia wasiweza kuutumia uhuru wao vyema.



Kijamii, Tanzania yetu imefika mahala pabaya, angalau huko kwenye mitandao ya kijamii. Na kama kuna sehemu inayoweka ushahidi wa wazi kuhusu hicho ninachoongelea, basi ni kwenye mtandao wa kijamii unaohusu picha, Instagram, ambao kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo unavyozidi kuwa uwanja wa matusi na kila lisilopendeza machoni.



Kwa upande wa blogu, licha ya kuwa bado tuna blogu nyingi zinazoitumikia jamii ipasavyo, kumeibuka utitiri wa blogu za ngono na matusi huku nyingine zikijipa uhuru wa kuwachafua watu na kuwasababishia madhara makubwa katika maisha yao. Ilikuwa lazima tufike mahala tuseme ‘sasa yatosha.’ Hakuna uhuru usioambatana na kuzingatia wajibu.



Mwaka jana, binti mmoja wa Kitanzania alikumbana na madhila ya unyanyasaji mkubwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter, na siku chache baadaye alikutwa amekufa. Japo hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kati ya unyanyasaji huo wa mtandaoni na kifo cha binti huyo, yayumkinika kuhisi kuwa matukio hayo mawili yalikuwa na uhusiano japo hata kama ni wa mbali. Na baada ya tukio hilo la kusikitisha, zilisikika kelele mbalimbali za kuitaka serikali ichukue hatua madhubuti kukabiliana na unyanyasaji wa mtandaoni (cyber bullying).



Sababu yangu ya tatu ya kuunga mkono sheria hiyo ya kupambana na uhalifu wa mtandaoni ni ya binafsi. Baada ya kifo cha binti huyo, nilisimama kidete na baadhi ya wanaharakati wa haki za jamii kuhamasisha mapambano dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni, kosa ambalo ni sehemu ya uhalifu wa mtandaoni.



Katika hali ya kushangaza na kusikitisha, liliibuka kundi lililoanzisha mashambulizi makali dhidi yetu tuliokuwa tukikemea vitendo vya unyanyasaji wa mtandaoni. Binafsi, niliandamwa hadi kiasi cha kuitwa muuaji hadharani, jambo ambalo linaniumiza nafsi hadi muda huu. Nilishindwa kabisa kuelewa kwanini dhamira nzuri ya kukemea maovu igeuke kuwa kosa lililowaudhi watu hao.



Naomba ieleweke kuwa sababu hii ya tatu ni ya binafsi na ningesihi isiangaliwe pekee bali pamoja na hizo mbili niliotaja hapo awali, ili isilete hisia kuwa mimi ni mbinafsi ninayeunga mkono sheria hiyo kwa vile ‘itawakomoa’ waliowahi kuninyanyasa mtandaoni huko nyuma.
Wakati jamii inaweza kuuhitaji muda mrefu kujadiliana kuhusu haja ya kuwa na sheria ya kukabiliana na uhalifu mtandaoni, ni muhimu kukumbuka kuwa wahanga wa uhalifu huo hawana muda wa kusubiri. Waingereza wanasema kumcheleweshea mtu haki yake ni sawa na kumnyima haki hiyo (justice delayed is justice denied).



Wahanga wa uhalifu wa mtandaoni wanastahili haki sawa kama hao wenye hofu kuwa sheria hiyo inaweza kutumiwa na serikali kukandamiza uhuru wa mawasiliano.



Wakati ninatambua mapungufu makubwa ya vyombo vyetu vya dola katika kusimamia na kutoa haki, na hivyo kuelewa vema hofu ya wanaopinga sheria hiyo, ni muhimu pia kutambua kuwa serikali ikiwa na nia ya kuminya haki haihitaji sana kuwa na sheria rasmi.
Tumeshuhudia gazeti la MwanaHalisi likifungiwa kwa kutumia ‘visingizio’ vingine, na wakati huo hatukuwa na sheria ya makosa ya uhalifu wa mtandaoni.



Ni kweli kwamba serikali na taasisi zake zinaweza kuitumia vibaya sheria hiyo kuminya uhuru wa mawasiliano, lakini pia ni muhimu tutambue kuwa serikali hiyohiyo ina sheria nyingine kadhaa, na pengine ‘kali’ zaidi ya hiyo ya kuzuwia uhalifu wa mtandaoni, na ikitaka kuzitumia kuminya uhuru, inaweza kufanya hivyo muda wowote.



Kuna sheria kama ile ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 na sheria ya kukabiliana na ugaidi ya mwaka 2002, ambazo zinaipa serikali uwanja mpana tu wa kuzitumia vibaya ikitaka kufanya hivyo.



Kimsingi, mjadala unaoendelea kuhusu sheria hiyo unatokana na suala ambalo nimekuwa nikiliongelea mara kadhaa katika makala zangu: upungufu wa imani ya wananchi wengi kwa serikali yetu. Imefika mahala wananchi wengi hawaiamini serikali, na ndio maana baadhi ya wanaopinga sheria hiyo wanadai imeletwa haraka kwa minajili ya kuisaidia CCM katika uchaguzi mkuu ujao.



Hofu kuwa sheria hiyo inaweza kutumika vibaya ina mantiki, lakini tatizo sio sheria hiyo ambayo kwa hakika imechelewa sana, bali mfumo wa kifisadi unaoathiri nyanja mbalimbali za maisha ya Mtanzania. Hakuna polisi anayeweza kumkamata mtu kwa vile tu kafanya umbeya kwenye ‘Whatsapp’ yake iwapo mfumo tulionao unazingatia sheria na haki.



Kwa bahati mbaya hilo linaweza kutokea kwa sababu baadhi ya polisi wetu wanaofahamika kwa tabia yao ya kupenda rushwa. Je tupuuzie madhila yanayowakumba wahanga wa uhalifu wa mtandaoni hadi tutakapokomesha rushwa kwenye taasisi kama jeshi la polisi au ‘tuue ndege wawili kwa jiwe moja,’ kwa maana ya kuendeleza mapambano dhidi ya mfumo wa kifisadi sambamba na kutumia ipasavyo sheria hiyo mpya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni?



Wakati kwa kiasi kikubwa mjadala kuhusu sheria hiyo unafanywa kistaarabu, na tayari kuna petition imewekwa mtandaoni kumsihi Rais Kikwete asiridhie sheria hiyo, kuna kundi dogo la wanufaika wa uhalifu wa mtandaoni linalojaribu kujificha katika hoja kuwa sheria hiyo ni mbaya.



Na pengine la kusikitisha zaidi ni kuona dhamira nzuri ya Naibu Waziri January Makamba kuuweka hadharani muswada husika ikichukuliwa na baadhi ya ‘wanyanyasaji wa mtandaoni’ kumshambulia yeye binafsi kana kwamba sheria hiyo ni yake binafsi. Tatizo hapa ni kuweka mkazo kwa mtu badala ya suala husika.



Nimalizie makala hii kwa kusisitiza kuwa ninaamini sheria hiyo dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ina umuhimu mkubwa kwa usalama wa taifa letu na kwa Watanzania kwa ujumla. Sheria husika haiwalengi raia wema bali wahalifu wa mtandaoni.



Badala ya kuwekeza nguvu nyingi kuhofia madhara yake, ni muhimu kama jamii tujiongoze kistaarabu na kukumbushana wajibu wetu kama raia wema. Tusiwe vigeugeu wa kuilaumu serikali kila tunapokutana na picha za ngono au maiti mtandaoni lakini serikali ikisikia kilio chetu kuhusu haja ya kuchukua hatua kali, na hivyo kuja na sheria kama hiyo ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni, twaishia kuilaumu pia.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.