Showing posts with label MILIPUKO DAR. Show all posts
Showing posts with label MILIPUKO DAR. Show all posts

28 Feb 2011

Baadhi ya Watanzania wanaoishi hapa Uingereza waliendesha harambee ya kuchangia wahanga wa milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Picha za harambee hiyo katika mji wa Reading.

                                       Left to Right: JJ, Chisumo, Ms Jestina, Gardol na Frank

                                                      Frank na Ms Jestina
  Ms Jestina

                                                            
                                                       Mdau akichangia
Mkurugenzi wa Locus Impex Shipping,B. Chisumo akifungua harambee

                                  Mtoto Shanelle akimpa mchango Ms Jestina


                                                    Toa ndugu ikiendelea

Shughuli ikiendelea
Wadau

20 Feb 2011








Picha hizi za kutisha zinajieleza zenyewe.Hakuna maelezo yanayotosheleza kueleza kwa ufasaha kuhusu janga hili.Lakini kwa vile kamwe hatutoelezwa chanzo cha milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto,kama ambavyo hatukuelezwa chanzo cha milipuko iliyotokea mwaka juzi huko Mbagala,ni muhimu kwa kila Mtanzania kudai haki yake ya kikatiba ya usalama wa maisha yake.


Ni wazi kuwa wahusika wanapata jeuri ya kutangaza hadharani kuwa hawatajiuzulu kwa vile wanafahamu bayana kuwa aliyewateua kushika madaraka hayo ni mzembe,dhaifu na asiyejua kinachoendelea.Kwa lugha nyingine,YUPO YUPO TU.

Nilighadhibika sana niliposoma kauli ya Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa JWTZ Brigedia Jenerali Paul Meela kuwa hakuna atakayejiuzulu kwa sababu uongozi jeshini sio nafasi za kisiasa.Haya ni matusi kwa Watanzania.Kwani Amatus Liyumba alipohukumiwa kwenda jela kwa ubadhirifu wa fedha za umma hapo Benki Kuu alikuwa mwanasiasa?

Kwa akili finyu ya Brigedia Meela,ni wanasiasa pekee wanaopaswa kuwajibika wanapoboronga.Lakini kwa vile kamanda huyo alikuwa anamwakilisha Mkuu wa Mwajeshi Jenerali Davis Mwamunyange,yayumkinika kuamini kuwa kauli hiyo pia ni msimamo wa mkuu huyo wa majeshi.

Tuliowahi kupitia mambo ya kijeshi tunafahamu kasumba ya jeuri na u-mungu mtu ilivyokomaa vichwani mwa viongozi jeshini.Hii inaimarishwa zaidi na utaratibu wa kawaida jeshini kwamba amri ina mwelekeo mmoja tu: kutoka juu kwenda chini,na haihojiwi.

Kwahiyo,wakati Kamanda Meela anaongea na waandishi wa habari,akilini mwake alikuwa kama anaongea na makuruta ambao ni dhambi kuu kwao kuhoji lolote lile.Na kwa vile Meela alikuwa anawakilisha mabosi wake,mtu pekee ambaye angeweza kumwadabisha ni Amiri Jeshi Mkuu,Rais Jakaya Kikwete.

Lakini takriban miezi mitano tangu baadhi ya Watanzania wenzetu watusaliti kwa kumrejesha Kikwete madarakani (tukiweka kando uchakachuaji wa Tume ya Uchaguzi),naamini kila Mtanzania anafahamu fika kuwa ombwe la uongozi wa taifa lililojiokeza wakati wa awamu ya kwanza ya utawala wa Kikwete,sio tu limezidi kukua bali pia limeifanya Tanzania kuishi kwa kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu.Ni kama hatuna Rais wala serikali.

Na taasisi muhimu kwa ustawi wa taifa kama Idara ya Usalama wa Taifa ziko katika usingizi mzito unaosababishwa zaidi na marupurupu makubwa licha ya utendaji kazi duni na wa chini ya kiwango.Sijui kama watu hawa wanasumbuliwa na mwenendo wa nchi yetu,kwani ingekuwa hivyo tusingeshuhudia mazingaombwe ya kuruhusu mtu kama Edward Lowassa kuwa Mwenyekiti wa kamati nyeti ya bunge ya Ulinzi na Usalama,leave alone ishu kama za Dowans,EPA,nk.

Na kwa kuonyesha watu wa Usalama wamegubikwa na usingizi,wameshindwa hata kumshauri bosi wao Kikwete kuwa safari yake kwenda Mauritania kusaka ufumbuzi wa mgogoro huko Ivory Coast,sio mwafaka wakati huu wa majonzi makubwa kwa Watanzania.Kikwete na washauri wake wanajifanya hawajui kuwa janga la Gongo la Mboto linawagusa zaidi Watanzania kuliko matatizo ya wa-Ivory Coast.Ni rahisi kwa baadhi ya watu kuhisi kuwa Kikwete anakwepa majukumu na kuamua kwenda kuzurura huko ng'ambo.

Tukirejea kauli za wanajeshi wetu,Brigedia Jenerali Meela anasema taarifa za milipuko iliyopita ni kwa matumizi ya jeshi.Kwani JWTZ limegeuka jeshi la mtu binafsi?Sote tunafahamu kuwa hilo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania.Sasa iweje madudu wanayofanya na yanayopelekea kuwaathiri wananchi wasio na hatia yaishie kuchungiuzwa na wao wenyewe kisha findings nazo zibaki kuwa siri yao?

Jibu la maswali haya na mengineyo mengi ni rahisi:Rais tuliyenae ni dhaifu na asiye na uwezo wa kuwawajibisha hata wale aliowateua yeye mwenyewe.Sasa kwa wanaotegemea Kikwete anaweza kudili na maharamia kama wa Dowans (ambao hakuwateua,na sanasana wanamdai fadhila) watakuwa wana jibu la msingi kuhusu kusuasua kwake kuwashughulikia mafisadi.

Picha kwa hisani ya Rev Masanilo wa Jamii Forums


Tunaendelea kuwaletea updates za tukio la milipuko ya mabomu jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali,hadi sasa inakadiriwa zaidi ya watu 20 wamepoteza maisha katika tukio hilo.

Tovuti ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) Idhaa ya Kiswahili inaripoti:
Hali ya taharuki imetanda mji wa Dar Es Salaam, nchini Tanzania, huku wakaazi wakiamka kuomboleza vifo vya zaidi ya watu kumi na zaidi ya wengine 60 kujeruhiwa kufuatia milipuko iliyotokea kwenye ghala la kuhifadhi silaha za kijeshi, lililo karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege.

Wakaazi wa eneo la Gongo la Mboto lililo karibu na ghala hilo wamekesha nje baada ya makaazi yao kubomoka kutokana na mtikisiko wa milipuko hiyo iliyodumu kwa saa kadhaa. Milipuko hiyo ilisikika kwa umbali wa zaidi ya kilomita ishirini kutoka kituo hicho cha kijeshi.

Inaarifiwa kuwa milipuko hiyo ilianza mwendo wa saa mbili usiku.

Msemaji mmoja wa jeshi amesema kuwa kuna watu wengi ambao wamepoteza maisha yao lakini idadi kamili haijajulikana.

Kamanda wa polisi jijini Dar-es-Salaam, Suleiman Kova, ametoa wito kwa raia wa mji kuwa huo watulivu huku maafisa wa ulinzi wakiendelea na mikakati ya kurejesha hali ya uthabiti.

Kova amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mlipuko huo ni ajali na wala sio shambulio la kigaidi.

Ni hii mara ya pili kwa milipuko kama hiyo kutoka jijini Dar es Saalam katika kipindi cha miaka miwili iliyopita mwaka wa 2009 zaidi ya watu ishirini waliuawa na wengine 300 kujerihiwa

Kadhalika,Rais Jakaya Kikwete amewaasa wananchi kuepuka maelezo ya "redio mbao" na badala yake wasubiri taarifa rasmi kutoka serikalini na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Hata hivyo inawezekana Kikwete hajajiuliza kwanini wananchi wanategemea taarifa za "radio mbao" kwani ni dhahiri kuwa penye ombwe la taarifa rasmi,wananchi wanalazimika kugeukia vyanzo vya habari visivyo rasmi.



Hadi muda huu,hakuna kiongozi yeyote aliyewajibika au kuwajibishwa.Watanzania wanatarajia kuona Waziri wa Ulinzi Dkt Hussein Mwinyi,Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Davis Mwamunyange na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi hilo,Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo,wakiwajibishwa mara moja.Lakini kwa namna tunavyofahamu udhaifu wa Rais Kikwete katika kuwashughulikia watendaji wake,kuna uwezekano mkubwa wa Dkt Mwinyi,Mwamunyange na Shimbo kuendelea na madaraka yao

Kilicho wazi ni kuwa serikali itapoteza fedha za walipa kodi kuunda tume kama ile ya milipuko ya Mbagala mwaka 2009,na kisha ripoti ya tume hiyo kuishia kuwa karatasi za kufungia vitafunio.

Japo hakuna anayetaka kutumia janga hili la milipuko kama mtaji wa kuwahukumu watawala wetu,lakini kuna umuhimu mkubwa wa kuunganisha matukio yaliyopita na tukio hili na uwajibikaji duni wa serikali iliyopo madarakani.

Ni muhimu pia kutafakari dhamira ya serikali kuilipa kampuni ya kitapeli ya Dowans,sambamba na mpango wa kuwapatia wabunge shilingi bilioni 90 kila mmoja,huku mipango endelevu ya kuepusha na kukabiliana na majanga ikipuuzwa.

Ukweli ulio bayana ni kwamba serikali ya Kikwete na CCM yake haisumbuliwi na hali ya kutokuwa na uhakika na usalama wa wananchi.

Endelea kutembelea tovuti hii kwa habari na uchambuzi zaidi kuhusu tukio hili la kusikitisha.

16 Feb 2011




Habari kutoka Dar es Salaam zinaeleza kuwa milipuko kadhaa imetokea maeneo ya Gongo la Mboto.Hata hivyo habari nyingine zinadai kuwa milipuka hiyo imetokea maeneo ya Kisarawe

Bado hakuna taarifa rasmi kuhusu eneo na chanzo cha milipuko hiyo japokuwa habari zilizopo zinadai milipuko hiyo imetokea kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mtandao wa Jamii Forums umemnukuu Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Brigedia Jenerali Abdulrahman Shimbo akisema "Hali ni mbaya Kikosi namba tano maghala yamelipuka ni hatari, watu wahame, maghala yako karibu karibu sana, tunaomba wananchi wahame sasa hivi, tunajitahidi kuzuia moto unaotokana na hilo unaweza kwenda mbali sana hadi Kilomota kumi, wananchi walioko karibu na maghala ya kikosi Gongo la Mboto wasogee mbali sasa hivi."

Hadi sasa hakuna taarifa kamili kuhusu idadi ya majeruhi japokuwa picha zilizotumwa na baadhi ya watumiaji wa huduma ya mtandaoni ya Twitter zinaonyesha majeruhi wakiwa katika hali mbaya



Tukio hili la kusikitisha linatokea wakati Serikali ikiwa haijaweka hadharani ripoti ya vyanzo vya milipuko iliyotokea kwenye Kambi ya JWTZ Mbagala mwezi Aprili na Mei mwaka juzi.

Wakati huo,aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Dokta Hussein Mwinyi aliahidi kuwa angewajibika iwapo ingebainika amezembea.Lakini simulizi hizo ziliishia hapo baada ya vile Serikali kupitia Wizara inayoongozwa na Mwinyi kuamua kuiweka ripoti hiyo 'kapuni'

Wakati tovuti hii inaendelea kukusanya habari za uhakika kuhusiana na milipuko hiyo ni muhimu kwa Watanzania kudai haki zao za msingi za usalama wa maisha yao na mali zao.Haiyumkiniki kuona 'intelijensia' ya vyombo vya dola ikiwa na 'ufanisi mkubwa' katika kukandamiza haki za kikatiba za wananchi lakini ikishindwa kuepusha majanga kama haya.

Upatikanaji wa taarifa sahihi unakuwa mgumu hasa kutokana na vyombo 'rasmi' vya habari nchini Tanzania kutowajibika ipasavyo kuwajulisha wananchi kinachoendelea.Tovuti zote za magazeti 'makubwa' hazina breaking news hadi wakati naweka habari hii.

(Video kwa hisani ya Dedichjr na Picha kwa hisani ya Jamii Forums)

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.