WIKI iliyopita yaweza kubaki kwa muda mrefu kwenye kumbukumbu za
Watanzania wanaoishi hapa Uingereza. Kwa upande mmoja, wiki hiyo ilimalizika
kwa mkutano kati ya baadhi yao na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, na kwa
upande mwingine wiki hiyo ilitawaliwa na mizengwe ya ‘kuzuia’ fursa kwa wengi
kukutana na Waziri Mkuu.
Awali, zilipatikana tetesi kwamba Rais John Magufuli angefanya ziara ya kikazi hapa Uingereza, lakini baadaye ikafahamika kuwa Waziri Mkuu Majaliwa ndiye angemwakilisha.
Hatimaye Waziri Mkuu aliwasili hapa kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo, na pia kuwa kiongozi wa kwanza wa kitaifa kuzuru nchini hapa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.
Wengi wa Watanzania wanaoishi nchini hapa walionyesha kiu kubwa ya kukutana na kiongozi huyo mpya, hususan kusikiliza visheni ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa Tanzania na Watanzania, ikiwa ni pamoja na tunaoishi nje ya nchi yetu.
Hata hivyo, kiu hiyo ilikumbana na kikwazo kutoka Ubalozi wa Tanzania hapa Uingereza, haukujali kutoa taarifa yoyote kwa Watanzania wanaoishi hapa kuhusu ujio wa kiongozi huyo wa kitaifa wala kueleza iwapo angekutana nao kwa maongezi.
Baadaye zikasikika tetesi kuwa Ubalozi huo (aidha kama ofisi au baadhi ya maofisa wake) ulitoa mwaliko kwa takriban watu arobaini hivi kuhudhuria ‘kikao’ na Waziri Mkuu. Tetesi hizo hazikueleza jinsi gani ‘wawakilishi’ hao walivyopatikana, lakini kilichoonekana bayana ni suala hilo kuzingirwa na usiri mkubwa.
Binafsi, nilianzisha jitihada za kuutaka Ubalozi uangalie umuhimu wa kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anayeishi hapa anapatiwa fursa ya kuhudhuria mkutano huo. Awali niliweka ujumbe kwenye kundi la ‘Whatsapp’ la Watanzania wanaoishi hapa, japo mapokeo hayakuwa ya kuridhisha.
Baadaye nilichukua jukumu la kuandika makala katika blogu yangu baada ya kuzungumza na Watanzania kadhaa wanaoishi hapa, na ambao walionyesha bayana kutoridhishwa na jinsi Ubalozi wetu ulivyoonekana ‘kuhujumu’ uwezekano wa Watanzania wengi zaidi wanaoishi hapa kukutana na kiongozi wao.
Kwa bahati nzuri, ‘kelele’ za makala hiyo na ‘kilio’ kilichofikishwa kwenye kituo kimoja cha radio huko nyumbani na baadhi ya Watanzania wanaoishi hapa, zilizaa matunda. Hatimaye, Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa tamko kuwa Waziri Mkuu angekutana na Watanzania wanaoishi hapa.
Ofisi ya Waziri Mkuu pia ilijaribu kujitetea kuwa haikuhusika na maandalizi ya mkutano kati ya Waziri Mkuu na Watanzania wanaoishi hapa, japo haikuwahi kulaumiwa na mtu yeyote kwa sababu utaratibu uliozoeleka ni kwa Ubalozi (sio Wizara au ofisi za huko nyumbani) kufanya maandalizi ya mikutano ya viongozi wa kitaifa na Watanzania wanaoishi hapa.
Kwa upande mwingine taarifa hiyo ilikuwa kama inakanusha 'madai ya watu' kuwa kuna watu maalumu waliochaguliwa kuhudhuria mkutano huo (badala ya kuwa mkutano wa wazi kwa kila Mtanzania anayeishi hapa. Hata hivyo, kulikuwa na uthibitisho kwamba awali mpango wa ubalozi ulikuwa ni kwa kundi la watu kadhaa tu kukutana ‘kwa faragha’ na Waziri Mkuu.
Uthibitisho huo ulisikika baada ya mmoja wa maofisa wa ubalozi wetu hapa kujirekodi na kuweka ujumbe wa sauti (voice note) kwenye kundi la Whatsapp (la Watanzania wanaoishi hapa) ambapo pamoja na mambo mengine alikebehi jitihada za kutaka Watanzania wengi zaidi wanaoishi hapa wapate fursa ya kukutana na Waziri Mkuu. Alidai kuwa “hata Rais anapoongea na wazee jijini Dar haimaanishi basi wazee wote wa Dar wataalikwa kwenye mkutano huo.” Alidai kuwa hakuna ubaya kuteua watu wachache tu kuzungumza na Waziri Mkuu, na kuongeza kuwa ‘Watanzania wamezoea kuja wengi japo walioalikwa wachache tu.’
Kwa upande mmoja ninaipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ‘kusoma alama za nyakati’ na kuruhusu mkutano kati ya Waziri Mkuu na Watanzania wanaoishi hapa kuwa wa wazi. Kwa upande mwingine ninaikosoa kwa sababu tamko lake kuwa mkutano huo utakuwa wa wazi sio tu lilitolewa Ijumaa - siku moja kabla ya mkutano – lakini pia haikubainisha muda wala sehemu kutapofanyika mkutano huo. Pengine ni mazoea tu ya huko nyumbani, lakini maisha ya hapa kwa kiasi kikubwa yanaambatana na ‘ratiba kali,’ na taarifa ya muda mfupi na isiyojitosheleza kimaelezo (kama hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu) inaweza kuwa iliwanyima fursa watu wengi zaidi kuhudhuria mkutano huo.
Kwa upande wa Ubalozi wetu hapa, hadi wakati ninaandika makala hii haujafanya jitihada za kuwaomba radhi Watanzania wanaoishi hapa kwa ‘mpango wake fyongo’ ambao laiti ungefanikiwa, basi mkutano huo wa Waziri Mkuu ungekuwa ni kati yake na ‘wateule wachache’ tu. Kadhalika, ofisa ubalozi aliyejirekodi na kukebehi harakati zetu kudai fursa kwa wote kuhudhuria mkutano huo angeomba radhi kwa kauli zake zisizoendana na wadhifa wake wala ustaarabu wetu Kitanzania.
Pengine utata huo ungeweza kuepukika laiti pande mbili zinazohusika na ziara za viongozi wa kitaifa zingewajibika ipasavyo. Kwanza, ubalozi wetu hapa ungeweza kutengeneza mazingira mazuri ya mawasiliano na Watanzania wanaoishi hapa kwa kutumia mitandao ya kijamii au njia nyingine mwafaka. Hisia ni kwamba ‘ukimya’ uliojitokeza kuhusu ziara hiyo ulikuwa wa makusudi (yaani mkutano huo ulipaswa kuwa ‘shughuli ya wateule wachache’).
Pili, idara yetu ya masuala ya usalama imekuwa na utaratibu wa kutanguliza maafisa wake eneo ambalo kiongozi wa kitaifa atatembelea, kitu kinachofahamika kiintelijensia kama ‘advance party.’ Na moja ya majukumu ya waliomo kwenye ‘msafara’ huo ni kubaini yanayoweza kujitokeza wakati wa ziara husika. Kwa hiyo, laiti wangetupia macho ‘sehemu’ za maongezi ya Watanzania wanaoishi hapa (kwa mfano kundi lao la ‘Whatsapp’) basi wangeweza kubaini mapema kuwa kuna kiu ya mkutano na Waziri Mkuu sambamba na shutuma kuwa ubalozi unakandamiza kiu hiyo.
Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa ofisi zetu za ubalozi popote zilipo ziwe kiunganishi kati ya Watanzania wanaoishi nchi hizo na nchi yetu, sio kwa masuala yanayohusu hati za kusafiria tu na masuala ya kidiplomasia bali kudumisha Utanzania wetu kwa upendo, umoja na mshikamano. Balozi zetu kadhaa zimekuwa zikilaumiwa kwa ‘kutokuwa na msaada,’ sambamba na kauli za jeuri/kiburi kwa baadhi ya maofisa wetu wa ubalozi, hali inayodhaniwa inatokana na baadhi yao kukaa huku nje muda mrefu mno kiasi cha ‘kuwadharau Watanzania wenzao.’
Mwisho, iwe ni kwa busara zake binafsi au ofisi yake, shukrani za pekee kwa Waziri Mkuu Majaliwa kuweza kuongea na Watanzania wanaoishi hapa Uingereza. Takriban kila aliyehudhuria mkutano huo ameridhishwa na hotuba ya Waziri Mkuu ambayo imetoa matumaini makubwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuiboresha Tanzania yetu katika kila eneo.