Showing posts with label UBABAISHAJI WA KIKWETE. Show all posts
Showing posts with label UBABAISHAJI WA KIKWETE. Show all posts

22 Apr 2013


KWA mara ya kwanza, Rais Jakaya Kikwete amewabeza watu wote, wanaodai kuwa ameshindwa kuongoza nchi. 
 
Akizungumza na Watanzania waishio nchini Uholanzi na taarifa yake kurushwa na kituo cha runinga cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete alisema kamwe hajashindwa kuongoza na kusisitiza kama angeshindwa angechukua uamuzi sahihi.
 

“Sijashindwa kuongoza nchi kama watu wengine wanavyosambaza taarifa za kizushi na fitina, nachojua mimi nchi iko katika mikono salama na ninaimudu.

“Msikae na kusikiliza maneno ya wapuuzi wachache ambao wamekuwa wakieneza maneno yao ya umbea katika mitandao na mikutano ya kisiasa. 
“Ukiacha matukio machache ya uvunjifu wa amani ambayo Serikali yangu imekuwa ikiyashughulikia, tumefanikiwa kudhibiti hali hiyo na Watanzania wanaendelea na shughuli zao kama kawaida,” alisema Rais Kikwete.

Alisema japo kuongoza watu ni kazi ngumu na nzito, lakini yeye binafsi ameweza kuongoza kutokana na kulelewa na kukulia katika maadili mema ya uongozi.

Alisema kutokana na misingi hiyo, haoni haja ya kupigizana kelele na watu ambao hawamtakii mema katika uongozi wake.

Aliwataka Watanzania waishio nchini Uholanzi, kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri kwa kutangaza vivutio vya utalii na rasilimali zinazopatikana Tanzania ili kuwavutia.

Kuhusiana na migogoro ya kidini ambayo imekuwa ikitokea nchini, Rais Kikwete aliwataka Watanzania kuhakikisha wanaenzi na kulinda tunu ya umoja na amani, iliyoasisiwa na viongozi wake, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na mwasisi wa Zanzibar, Hayati Sheikh Amani Karume.

“Watanzania tumeachiwa tunu ya amani na umoja kutoka kwa waasisi wa taifa letu, tunapaswa kuienzi, kuilinda na kuidumisha kwa maslahi ya nchi yetu na vizazi vijavyo,” alisema Kikwete.

Kwa muda mrefu, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakimshutumu Rais Kikwete kuwa nchi imemshinda kutokana na kukumbwa na misukosuko mingi.

Miongoni mwa misukosuko hiyo, ni pamoja na mgomo wa madaktari, mgomo wa walimu, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), mauaji ya watu, kutekwa na kujeruhiwa vibaya.

Tuhuma nyingine, ni tatizo la kuenea kwa udini ambalo limesababisha vifo kadhaa Tanzania Bara na Zanzibar. 
 
Lakini katika matukio hayo yote Rais Kikwete amekuwa akiyakemea na kuwataka Watanzania waishi kama ndugu.

CHANZO: Mtanzania

ANAKIMBIA KIVULI CHAKE?

20 Apr 2012

Waziri Mkuu Pinda akifanya usanii wa kulia bungeni katika sakata la maalbino.Je hatorejea tena mbinu hii?

Tusiume maneno.Tanzania hivi sasa inayomba kwa vile Rais tuliye nae,Jakaya Kikwete,ni mithili ya mtu asiyejua kwanini Watanzania walimpa dhamana ya kuongoza nchi yetu-moja ya nchi masikini kabisa duniani licha ya utajiri luluki ilionao.

Kikwete alifanya uzembe kwa kuteua rundo la mawaziri (ambapo ukubwa tu wa Kabineti yake ni mzigo mzito kwa nchi yetu masikini) lakini kana kwamba hiyo haitoshi,akajaza wababaishaji kibao ambao aidha ni maswahiba wake au kwa busara zinazomtosha yeye pekee aliwaona wababaishaji hao kama sehemu muhimu ya timu yake ya kuwaletea Watanzania MAISHA BORA.

Hivi Rais mwenye busara angeweza kumkabidhi Mustafa Mkulo Uwaziri wa Fedha ilhali historia yake huko nyuma inafahamika vyema?Well,Kikwete hakumpa Mkulo nafasi hiyo kimakosa bali kwa sababu maalum.Teuzi za Mawaziri wa Fedha Barani Afrika huzingatia sana ushkaji kati ya Rais na mteuliwa.Kimsingi,wengi wa mawaziri wa fedha wa Afrika ni kama wahasibu binafsi wa Rais.

Si kwamba Kikwete hajui ufisadi wa Mkulo na mawaziri wengine.HAPANA.Anafahamu fika ila hawezi kuchukua hatua kwa vile Mkulo hafanyi hivyo pasipo uelewa wa bosi wake.Hapa ninamaanisha kuwa kwa kiasi kikubwa,kinacholalamikiwa kuhusu Mkulo kina baraka za Kikwete.

Sijui Tanzania itakuwa katika hali gani wakati huyu mtu anamaliza muda wake hapo 2015!Cha kusikitisha zaidi,wakati nchi inazidi kuangamia yeye yuko bize kushindana na Christopher Columbus kwenye 'safari za uvumbuzi.'

Majuzi kapewa ripoti ya ukaguzi wa fedha za serikali na CAG Ludovick Utouh.Kana kwamba kilichomo kwenye ripoti hiyo ni salamu za hepi bethdei,siku chache baadaye Kikwete huyooo safarini Brazil.Hana habari kuwa nchi inaangamia.Yey na safari,safari na yeye.Basi bora amwondoe Waziri wa Mambo ya Nje,Bernard Membe,kisha yeye Kikwete ajiongezee wadhifa wa uwaziri huo ili akisafiri hata kila wiki tujue moja.

Back to the point ya kumwajibisha Pinda na/au mawaziri,well,kama wabunge watafanikiwa kutekeleza hilo itakuwa vema.Waiwasi wangu mkubwa ni unafiki wa wengi wa wabunge wa CCM.Japo Tanzania yetu inaanza kuonyesha dalili za watu kuchoka kuiona nchi ikigeuzwa shamba la bibi,napatwa na wasiwasi kama wabunge wa CCM watakauwa tayari kumtosa Pinda au kushinikiza mawaziri mafisadi wajiuzulu.Pinda ni msanii anayeweza kuwahadaa wabunge wa chama chake kwa kulia tena hadharani....nao wakalainika.

Lakini,hata kama Pinda na mawaziri mafisadi waking'olewa,bado tutaendelea kuwa na tatizo hapo juu kabisa-yaani Kikwete na urais wake wa sandakalawe (wa kubahatisha).Ameshauthibitishia umma wa Watanzania kuwa sio tu yeye ni dhaifu wa uongozi bali pia hana nia ya kurekebisha chochote dhidi ya kansa inayoitafuna nchi yetu.

Anyway,kama kura ya kutokuwa na imani na Pinda itafanikiwa nadhani hatua itakayofuata ni kura ya kutokuwa na imani na Kikwete mwenyewe.Actually,ni kwa sababu tu ya hizi taratibu za kirasimu za kupiga kura.Sidhani kama kuna Mtanzania yeyote mwenye akili timamu ana imani na Kikwete-hasa baada ya kushindwa kutekeleza hata ahadi alizojiwekea mwenyewe pasipo shinikizo lolote lile.Kitu pekee ambacho amefanikiwa kukitekeleza kwa ufanisi mkubwa ni mashidano yake dhidi ya Vasco da Gama na Christopher Columbus.

MUNGU INUSURU TANZANIA (kwa namna yoyote ile...hata kama ni kwa majonzi) 

20 Sept 2011


Kikwete mtegoni tena
• Asaini tangazo la serikali lililochakachuliwa

na Waandishi wetu

RAIS Jakaya Kikwete amedanganywa tena na baadhi ya watendaji wake, akasaini tangazo lililochakachuliwa.

Septemba 5 mwaka huu, Kikwete alisaini tangazo la kusudio la uanzishaji wa wilaya mpya ya Butiama, lakini katika namna ya kushangaza, sasa inaonekana eneo la wilaya mpya ni Nyamisisi.

Hali hiyo inayotia fedheha kwa Rais wa nchi, imebainika juzi wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipofika Butiama kuzuru kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Pinda alilazimika kuwatuliza wakazi wa eneo hili waliotaka kujua sababu za msingi za Rais kubadili msimamo wake na kuhamishia makao mapya yaliyotakiwa kuwa Butiama na kuyapeleka Nyamisisi.

Pinda alikiri bayana kuwa Rais alisaini tangazo hilo akijua kuwa kilichoandikwa ni makao makuu kuwa Butiama bila kujua eneo lililoandikwa ni Nyamisisi.

“Hata kama kuna mtu alitaka makao makuu yawe Nyamisisi, kwa kweli haikupaswa hiyo Nyamisisi kuchomekwa hivyo. Hata mngeniuliza mimi makao makuu yawe wapi, ningesema lazima yawe Butiama tu,” alisema Pinda na kushangiliwa.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tangazo hilo lilikuwa na makosa kutokana na kutaja eneo la makao makuu tofauti na lile lililopendekezwa.

Pinda alisema mpango wa serikali ulikuwa ni makao makuu ya wilaya hiyo yawe katika kijiji cha Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Akijibu malalamiko ya wakazi wa Butiama, walioingia katika eneo la nyumba hiyo, wakimtaka atamke kuwa makao makuu yatakuwa Butiama, Pinda alisema:

“Hili la Butiama kwa kweli linaleta manenomaneno. Sisi serikalini tulidhani ukiwa na wilaya ya Butiama na makao makuu ni lazima yawe Butiama, ili tumuenzi Baba wa Taifa.

Hata hivyo, alisema pamoja na tangazo hilo kuchomekwa neno Nyamisisi, bado mtu aliyefanya hivyo hajafanikiwa, kwani tangazo hilo sio uamuzi wa mwisho wa kuhusu suala hilo.

Aliwataka wananchi wa Butiama kulichukulia tangazo hilo kuwa ni pendekezo tu ambalo wanapaswa kulitolea maoni yao kuhusu kulikubali au kulikataa na kwamba maamuzi ya mwisho kuhusu wapi yawe makao makuu ya wilaya hiyo yatatokana na maoni ya wananchi wenyewe.

Alisisitiza kuwa Butiama ikiwa wilaya sio tu huduma za msingi zitaboreshwa na kuwapa watu sababu ya kwenda wilayani hapo, bali pia itawapa sababu ya kwenda kuzuru nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa.

Pinda pia alimpa fursa mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, kutoa kauli yake kuhusu suala hilo, ambaye alisema yeye asingependa kuliingilia suala hilo.

“Hili suala halina tatizo, ninyi na wananchi wote mtakavyoamua ndivyo iwe hivyohivyo,” alisema Mama Maria.

Maswa watishia kuandamana

Katika hatua nyingine, hatua ya Rais Kikwete kuunda mikoa mipya, imezua balaa baada ya mamia ya wananchi wa wilaya ya Maswa, mkoa wa Shinyanga kuandaa maandamano iwapo serikali itaamua kuyaweka makao makuu ya mkoa mpya wa Simiyu katika wilaya ya Bariadi.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Nguzo Nane na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa wilaya hiyo, wananchi hao wamedai kuwa hawako tayari kutendewa hivyo na wataandamana hata ikilazimu kupigwa risasi.

Katika mkutano huo ulioitishwa kwa ajili ya kutoa maoni ya mapendekezo juu ya nia ya serikali ya kupeleka makao makuu ya mkoa mpya wa Simiyu mjini Bariadi, wananchi hao wamesema uamuzi huo ni dharau kwao na unataka kufanywa kwa ajili ya manufaa ya viongozi wachache.

“Sisi wana Maswa tutaandamana bila kujali itikadi za vyama kama hatutasikilizwa na tuko tayari kupigwa risasi. Hatuwezi kunyang’anywa haki yetu kwa ajili ya ubinafsi wa viongozi wachache,” alisema mkazi mmoja wa Maswa, Thomas Nkola, na kushangiliwa na umati wa wananchi.

Walisema kuwa viongozi wa mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Bariadi wamekuwa na desturi ya ubinafsi katika masuala yenye maslahi ya umma kitendo kilichodhihirika katika ujenzi wa barabara ya lami ya Mwigumbi –Maswa-Lamadi.

“Viongozi wetu wa mkoa wa Shinyanga na wa Bariadi wametuona sisi wa Maswa watulivu sana hivyo wanatumia mwanya huo kutuchezea.

“Mfano ujenzi wa barabara ya lami ya Mwigumbi-Maswa-Lamadi ilitakiwa ianzie Mwigumbi kuja Maswa lakini kutokana na ubinafsi wao imeanzia Bariadi kwenda Lamadi,” alisema mwananchi mwingine, Samwel Kidima.

Walisema licha ya mapenzi mema aliyonayo Rais Jakaya Kikwete ya kuanzisha mkoa huo, ni vizuri mchakato wa kupata makao makuu yake ukaanza upya kwani wa awali haukupitia katika vikao halali kama vile baraza la madiwani na kamati za ushauri za wilaya (DCC) hali ambayo imezua mgogoro mkubwa na kufanya kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya wananchi wa wilaya hizo.

“Rais Kikwete alipoamua kuanzisha mikoa na wilaya mpya alikuwa na nia nzuri sana lakini jambo la kushangaza mchakato wa kutoa mapendekezo ya makao makuu ya mkoa wa Simiyu hayakufuata utaratibu kwani ilitakiwa uanzie katika vikao vya baraza la madiwani na kamati za ushauri za wilaya ndiyo maana jambo hili limezua mgogoro mkubwa na sasa mahusiano kati ya wananchi wa wilaya ya Maswa na Bariadi si mazuri hivyo mchakato uanze upya,” alisema Edward Bunyongoli.

Walisema iwapo serikali itabaki na msimamo wake huo basi wao wataendelea kubaki katika mkoa wa Shinyanga lakini hawako tayari kukubaliana na uamuzi huo uliofanywa kwa ajili ya maslahi ya watu wachache wabinafsi.

“Kama serikali itabaki na msimamo kuwa Bariadi ndiyo makao makuu ya mkoa wa Simiyu sisi tutabaki katika mkoa wa Shinyanga kwani hatuko tayari kukubali uamuzi huo uliotawaliwa na vitendo vya kifisadi,” alisema Kulwa Nangale.

Hii si mara ya kwanza kudanganywa kwa Rais kwani ameshadanganywa zaidi ya mara 12 miongoni mwa mambo aliyodanganywa ni pamoja na ile ya kuzindua mradi wa Bwawa la Manchira lililoko wilayani Serengeti wakati tayari wananchi wamekwishafungua kesi Mahakama Kuu ya Mwanza wakidai fidia.

Kesi hiyo iliyofunguliwa ni matokeo ya viongozi wa serikali wilayani humo kuhusika kuwalipa fidia watu wasiohusika na kuwaacha walengwa waliofanyiwa tathmini.

Pia aliwahi kudanganywa kwamba daraja la Mkenda lililoko Ruvuma ambalo ni njia muhimu kuelekea Msumbiji, lilikuwa limekamilika.

Katika tukio jingine, Rais aliwahi kupewa taarifa zisizo sahihi kuhusu tuhuma za rushwa zilizokuwa zikimkababili Anatory Choya kisha akamteua kuwa mkuu wa wilaya, lakini siku siku chache baadaye akafunguliwa mashtaka na TAKUKURU.

Mwaka juzi, akiwa ziarani Mbeya msafara wa Rais ulishambuliwa kwa mawe na watu, lakini wasaidizi wake wakaja kutoa taarifa kwamba watu hao walikuwa ni wahuni na walikuwa wakimsubiri Rais kwa muda mrefu bila mafinikio.

Hata hivyo, baadaye uchunguzi huru ulibainisha kwamba tukio hilo lilikuwa na mafungamano ya kisiasa na makovu ya mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM kwa mwaka 2005.

Mlolongo huo mrefu wa upotoshaji taarifa kwa Rais uliibuka tena katika utoaji wa magari ya misaada ambapo badala ya kupewa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Longido alipewa wa Ngorongoro.

Tukio hilo lilimfanya mkuu huyo wa nchi kukasirika na kumzodoa mkurugenzi huyo, lakini baadaye ikabainika mkurugenzi huyo alikwenda kutokana na makosa ya maafisa wa Ikulu.

Katika mlolongo huo, tukio kubwa kabisa ni Rais kutia saini kwa mbwembwe Sheria ya Gharama za Fedha za Uchaguzi ambayo ilichomekwa vipengele nje ya Bunge kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Tukio hilo ambalo ni la uvunjifu wa Katiba, liliibuliwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, ambaye awali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fedrerick Werema, alikanusha.

Hata hivyo, baadaye sheria hiyo ilirudishwa bungeni na kukarabatiwa kwa mgongo wa mabadiliko ya sheria mbalimbali.

Mei mwaka jana, Rais alipewa taarifa za upotoshaji kuhusu mazungumzo ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na serikali, kwa kuelezwa shirikisho hilo halikuhudhuria mkutano wa saa 4:00 asubuhi kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, TUCTA wakatoa ushahidi wa barua za mwaliko wa mkutano huo wa Aprili 22 mwaka jana, ambazo zilikuwa mbili, moja ikionyesha walitakiwa kufika katika mazungumzo Hazina saa 4:00 asubuhi na nyingine saa 8:00 mchana.

Katika kuonyesha upotoshaji kwa Rais, wasaidizi hao walimpa barua iliyokuwa ikionyesha walipaswa kukutana saa 4:00 asubuhi huku ile ya saa 8:00 wakawa wameificha.

Rais akizungumza na wazee wa mkoa wa Dares Salaam aliwashambulia viongozi wa TUCTA hasa Naibu Katibu Mkuu, Nicolas Mgaya, akimwita mnafiki, mzandiki, na mchochezi.

22 Jul 2011


Moja ya matatizo mengi yanayomkabili mtu tuliyemchagua kuwa Rais wetu,Jakaya Kikwete,ni kutokuwa serious.Yeye ni mwepesi wa kuchekacheka hata kwenye mambo yanayohitaji kuwa serious.Anyway,kwanini nimesema hatuna rais?Sio siri,nimepatwa na kichwa kuuma baada ya kusoma mahojiano yafuatayo kati ya Kikwete na mwandishi wa BBC.Angalia majibu yake,angalia vicheko vyake...na kwa hakika unaweza kuafikiana nami kuwa huyu mtu sio tu mbabaishaji bali yawezekana hajui kwanini ni Rais wetu.Anyway,soma mwenyewe

BBC: Suala la Umeme Mheshimiwa Rais Kikwete ungependa kulizungumzia nini?

Rais Kikwete: Tatizo la umeme kimsingi ni suala la ukame tu. Kwa sababu mabwawa yetu ya kuzalisha umeme yanayotoa umeme karibu MW600 sasa hivi yanatoa umeme kidogo sana. Maji pungufu ndio maana kuna tatizo hilo.

BBC:Mheshimiwa, hili suala si la leo wala si la jana limekuwepo kwa muda mrefu, kwanini serikali haina njia mbadala ya kuweza kutatua suala hili? Tanzania ina raslimali nyingi mheshimiwa Kikwete!

Rais Kikwete: Kwanza serikali haina uwezo wa kufanya mvua inyeshe, unajua unajua hivyo, Kwa sababu (kicheko) ingekuwa na uwezo wa kufanya mvua inyeshe mabwawa yale yangejaa. Ni kweli kuwa Tanzania inazo raslimali za kutosha na katika kipindi hiki - toka wakati ule - sisi tulipoingia tumekuta suala la Ukame na mwaka 2007 tukapata matatizo ya kwanza.

Baada ya pale tukafanya uamuzi kwamba sasa tuanze kuwekeza katika vyanzo vingine; tuongeze uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo vingine. Tuongeze uzalishaji wa umeme kutoka vya vya kutumia gesi asilia twende kwenye makaa ya mawe. Kutoka vyanzo vya gesi asilia tayari tuna mtambo pale Ubungo, na toka mwaka 2009 mpaka sasa tumeshaongeza MW145, itakapofika Disemba tutakuwa tumeongeza MW160 nyingine. Tutakuwa tumeongeza MW300 siyo kidogo.

BBC: Mhe. Kikwete Mmoja katika wabunge Bw. John Mnyika ambaye ni Mbunge wa upinzani ambaye ni Waziri Kivuli wa Nishati amekuwa akilalamika na kwamba amewahi kusema kwamba hili tatizo ni tatizo linalowahusu Watanzania wote na amesema mje pamoja na kuona vipi mtakavyotatua tatizo hili. Na sasa hivi Bungeni wamesimamisha mswada, wa kutoa bajeti ya nishati ya Tanzania. Wewe unachukulia vipi matamshi kama haya kutoka kwa Wabunge?

Rais Kikwete: Mimi nasema hivi yeye si Mbunge atoe maarifa yake tu; anayo maarifa gani na anapendekeza kitu gani. Kwa sababu toka Uhuru mabwawa tuliyotengeneza ni Kidatu MW200, Mtera MW80, Kihansi MW 165 mimi nilipokuwa Waziri wa Nishati, pale Pangani tumeongeza.

Sasa ufikirie kwamba toka Uhuru tumeweza kuzalisha umeme wa MW600, lakini toka 2009 mpaka Disemba mwaka huu tutakuwa tumeongeza MW300! Ni jitihada kubwa. Mimi nasema kwamba usipozitambua hizo ni kwamba wewe mwenyewe siyo mkweli.

Sasa ni hivi, unajua hii mitambo ya umeme si mitambo unaenda kununua kama unavyonunua jaketi lako hili. Ni kwamba ukitaka mitambo ya umeme, lazima uweke order wakutengenezee. Huu mtambo unaofika mwaka huu Disemba order tuliweka mwezi wa Juni mwaka jana. Inachukua muda huo kutengeneza. Sasa ingekuwa mnaenda kutafuta mitumba, mitumba ya mitambo tu ya kununua iko mingi kweli. Tukasema hatuwezi kufanya hivyo.

Mimi nasema hivi, kitu kikubwa ni kuwa na subira. Tumefanya jitihada kubwa. Ni lazima watu watambue kuwa tumefanya jitihada kubwa katika miaka hii toka 2009 mpaka sasa hivi 2011 Disemba tutakuwa tumeongeza MW300 kulinganisha na MW600 ambazo tumeziongeza katika miaka yote hii. Nasema ni lazima watu watambue hivi. Sasa kama kuna mtu ana maarifa ya haraka zaidi nasema mtu atoe maarifa hayo na sisi kama yapo tutayafanyia kazi.

BBC: Kuna njia kama umeme wa jua, umeme wa kutokea ardhini wa mvuke, kwanini serikali haitafuti njia mbadala kuzalisha umeme kwa njia hizo?

Rais Kikwete: Nasema hivi, hata umeme wa jua lazima ujenge, umeme wa mvuke lazima ujenge, si kitu cha mwezi mmoja. Nasema huo ndio ukweli wenyewe na wakati mwingine na nyinyi mjifunze hayo mambo ya kitaalamu kulikoni kuuliza tu hivi hivi. Unajua ungekuwa na wewe unauliza kwa hoja - “unajua kwamba hiki kitu hiki ingekuwa umeme wa jua miezi miwili tu upo” - tungeweza kufanya hivyo.

Sisi sasa hivi kwa mfano tunajiandaa kuzalisha umeme wa kutumia Upepo, pale Singida. Tuna mwaka wa tatu sasa tuna mipango na Wakorea wa Kusini, umeme haujakuwepo. Kwa hiyo nasema hayo ni maelezo rahisi. Wanasema “mbona jua lipo?” katengeneze umeme wa jua kama jua lipo! (kicheko).

BBC: Watanzania wamekuwa wakisema (mwisho kabisa) kwamba Tanesco ingebinafsishwa ili waweze kupata makampuni kufanya kazi hiyo ya umeme?

Rais Kikwete: Aah! Kwani ukitaifisha kesho ndio utapata mitambo kesho? Nasema hivi ni vizuri kuelewa tu - kwanza tatizo la msingi - ni maji kukauka kwenye mabwawa. Maji yasingekauka kwenye mabwawa tatizo hili halipo. Maji yamekauka kwenye mabwawa kwa sababu ya ukame. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kuzuia ukame usiwepo. Sasa hiki ndicho kiini cha tatizo. Sasa nasema sisi jitihada ambayo tumeifanya ni kupunguza sasa kutegemea umeme unaotakana na nguvu ya maji.

Toka mwaka 2009 tumewekeza adi Disemba 2011 tutakuwa tumeongeza MW 310, yenyewe hiyo ni hitihada kubwa, ni vizuri ukaitambua jitihada hiyo. Kulikoni kusema kitu tu nasema hata kama huna majawabu rahisi utuambie tu.

MSIKILIZE HAPA

19 Jul 2011




Kama kuna kosa ambalo Watanzania watalijutia kwa muda mrefu sana ni lile walilofanya mwaka 2005 na kisha kulirudia mwaka jana kumchagua Jakaya Kikwete kuwa Rais wa nne wa Tanzania.Tusiume maneno,mengi ya matatizo yanayoikabili nchi yetu kwa sasa ymesababisha,yanasababishwa au yamechangiwa au yanachangiwa na ubabaishaji wa Kikwete.

Ni nani mwenye akili timamu asiyefahamu kuwa wakati kelele dhidi ya ufisadi zinaelekezwa kwa "mapacha watatu" waliobaki wawili (ie Lowassa na Chenge,na Ristam aliyejiuzulu),Kikwete ni sehemu muhimu kabisa ya tuhuma zinazoelekezwa kwa wanasiasa hao.Hapa simaanishi kuwatetea mafisadi hao bali ninachojaribu kupigia mstari ni ukweli kwamba Kikwete hana tofauti na Lowassa,Chenge au Rostam.Na hilo halihitaji ufafanuzi.Yeye anajua,mapacha watuatu waliobaki wawili wanajua,na kila Mtanzania mwenye akili tiammu anajua.Kwanini hadi leo Kikwete bado ni Rais wetu ni swali gumu kulijibu just like lile la kwanini alichaguliwa mara ya kwanza mwaka 2005 na baadaye 2010 ilhali wanamjua walikuwa wanatambua bayana kuwa hana sifa za kushika wadhifa huo mkubwa kabisa katika nchi yetu.

Anyway,lengo la makala hii sio kujadili ubabaishaji wa Kikwete katika utendaji kazi wake bali lengo ni kukemea kwa nguvu kubwa uhuni uliofanywa na Kikwete wa kufanya harusi ya mdogo wake kwenye Ikulu ndogo ya Bagamoyo.Hivi kwa kuwa Rais,Kikwete anadhani kuwa Watanzania wametoa urais kwa ukoo wake mzima?Kwanini asikodi ukumbi kwa fedha zake kisha akamfanyia sherehe mdogo wake?

Kama huelewi kwanini ninalamika,Ikulu iwe ile ya Magogoni au hizo ndogo za wilayani na mikoani ni mahala patakatifu-kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.Si mahala ambapo kila Tom,Harry and Dick anaweza kufanya atakalo.Lakini licha ya utakatifu huo wa Ikulu,ifahamike kuwa mahala hapo panaendeshwa kwa fedha za walipakodi.Kwa mantiki hiyo,kufanyia sherehe mahala hapo ni sawa na kuwabebesha gharama Watanzania kwa ajili ya harusi ya ndugu wa Kikwete.Sidhani hata waliompigia kura mwaka jana au 2005 walitamani kuona kura waliyompigia Jakaya inageuzwa kuwa mithili ya kuupigia kura ukoo wake mzima.

Huu ni uhuni unaopaswa kukemewa vikali.Rais anaweza kuzurura nje ya nchi atakavyo (inaelekea kama hakuna namna ya kumwelewesha kuwa safari zake za mara kwa mara nje ya nchi ni mzigo mkubwa kwa Watanzania) lakini kamwe tusiruhusu nafasi ya Urais ikageuzwa kuwa kama cheo cha kifamilia.

Madhara ya kumwacha Kikwete aendelee na madudu yake ni kwamba anaweza kumaliza muda wake hapo 2015 na kuiacha Tanzania ikiwa jina tu-haina maadili,haina raslimali,na kibaya zaidi,nafasi ya urais ikaishia kuwa na heshima ndogo kuliko ya mwenyekiti wa serikali ya mtaa.

PICHA: Kwa hisani ya Global Publishers

20 Jun 2011


Sio siri kwamba Rais Jakaya Kikwete anapenda sana kusafiri.Kuna vijimikutano vya kimataifa mbavyo kwa hakika visihitaji Tanzania iwakilishwe na Rais na badala yake akaenda Waziri Mkuu au kwa stahili kabisa Waziri wa wizara husika.Lakini asipokwenda yeye,watajuaje kama Kikwete ndiye Rais wa Tanzania?

Tuweke hilo kando.Tatizo jingine la Kikwete ni kutoa kauli ambazo yayumkinika kuamini kuwa hazijafanyiwa tafakuri ya kutosha.Huku nyuma,alishawahi kusema haelewi kwanini Tanzania ni masikini,na Waziri Mkuu wake,Mizengo Pinda, akaakisi kauli hiyohiyo.Sasa kama Rais hajui chanzo cha umasikini wa nchi anayoongoza,anafanya nini hapo Ikulu?

Safari hii kaibuka na madai kwamba kinachokwaza maendeleo yetu ni ukosefu wa fedha.Fedha zipi hizo?Mbona yeye kiguu na njia huku safari zake zikilibebesha taifa mzigo mkubwa wa gharama?Na fedha zipi anazozungumzia ilhali wabunge wetu wanalipwa mamilioni ya posho kwa "ku-rubber stamp" kila kinachowasilishwa kwao na serikali huku jitihada kubwa zaidi wanayofanya ni kubamiza meza (pongezi) kama sio kuwazomea wabunge wa upinzani?

Hebu soma porojo zake hapa chini

JK: Ukosefu wa fedha unakwamisha maendeleo
Sunday, 19 June 2011 20:57
Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amesema ukuaji wa kasi wa uchumi na maendeleo katika Bara la Afrika unakwamishwa na ukosefu wa fedha za kutosha za kugharimia miradi ya maendeleo. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jana, Rais Kikwete alikuwa akizungumza kwenye siku ya kwanza ya mkutano wa Kimataifa wa mwaka huu wa Taasisi ya Smart Partnership Dialogue ambao pia unajulikana Langkawi International Dialogue 2011, ulioanzishwa rasmi mwaka 1995. 
Rais Kikwete alisema kwamba njia za jadi za kupata fedha za kutosha ili kuharakisha ukuaji kasi wa uchumi, hazina uwezo wa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo. 
Rais Kikwete alisema kutokana hali hiyo ni lazima nchi za Afrika zitafute namna nyingine mpya ya kugharimia maendeleo ya bara hilo na watu wake. 
“Tatizo ni ukosefu wa fedha za kutosha kugharimia miradi inaweza kuzitoa nchi za Afrika na watu wake katika umasikini kwa haraka zaidi,” Rais Kikwete, mjini Kuala Lumpur, Malaysia. 
Shabaha kuu ya Smart Partnership ama Langkawi International Dialogue ni kufanya majadiliano ya kimataifa ya jinsi ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi duniani. Mada kuu katika mkutano wa mwaka huu ni ‘Enhancing Smart Partnership for Socio-Economic Transformation’. 
Akishiriki katika mjadala huo, Rais Kikwete aliwaambia mamia ya washiriki tatizo kubwa linalokwamisha ukuaji kasi wa uchumi na maendeleo katika Afrika ni ukosefu wa fedha za maendeleo kwenye sekta binafsi, sekta ya umma na kwa Serikali. 
Rais alisema chanzo kikuu cha fedha za maendeleo kwa nchi masikini za Afrika ni misaada ya maendeleo (ODA), lakini sasa fedha za ODA zimekuwa zikipungua na wakati mwingine hazipatikani.
“Hata ukitofautiana na kampuni yenye asili ya nchi inayotoa misaada, basi utanyimwa misaada hata kama kampuni yenyewe ndiyo yenye makosa,” alisema Rais Kikwete. 
Rais alisema wakati mwingine inakuwa vigumu kuvutia fedha za maendeleo kutoka nje. 
“Hakuna fedha za kutosha kwenye masoko ya fedha ya ndani na msingi mzima wa kifedha ni dhaifu sana. Msingi wa fedha wa ndani ni dhaifu na hata msingi wa fedha za kigeni wa nchi zetu ni masikini,”alisema Rais Kikwete. 
Rais alisema hali hiyo imezifanya nchi za Afrika kujikuta katika wakati mgumu wa kutimiza wajibu na majukumu yake katika kuwaletea wananchi maendeleo. 
“Hivyo, sisi katika Afrika tunahitaji kutafuta na kuangalia njia nyingine za ubunifu zaidi za jinsi ya kupata fedha za maendeleo,” alisema Rais Kikwete. 
Mapema mkutano huo ulifunguliwa na Waziri Mkuu wa Malaysia, Dato’ Sri Mohammed Najib Tun Abdul Razak ambaye hotuba yake ilizungumza masuala mengi na matatizo mengi yanayoikabili dunia kwa sasa pamoja na umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea.

CHANZO: Mwananchi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.