Showing posts with label UHURU NA JAMHURI. Show all posts
Showing posts with label UHURU NA JAMHURI. Show all posts

9 Dec 2016

Leo ni siku ya Uhuru wa nchi yetu, tunatimiza miaka 55 kama taifa huru. Siku kama ya leo, miaka 55 iliyopita, Tanganyika ilikabidhiwa uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Japo kuna wanaohoji iwapo tupo huru kweli, kwa leo tusherehekee tukio hilo la mkoloni kutukabidhi nchi yetu.

Pia siku ya leo ni siku yangu ya kuzaliwa. Ninamshukuru Mungu kwa kila kitu. 


Ninawashukuru pia wazazi wangu ambao japo ni marehemu kwa sasa, kiroho nipo nao siku zote: marehemu baba Mzee Philemon Chahali na marehemu mama Adelina Mapango. Bwana Mungu awajalie pumziko la milele na mwanga wa milele awaangazie mpumzike kwa amni. Amen. Naishukuru familia yangu hasa dadangu Sr Maria-Solana Chahali na wadogo zangu mapacha Peter (Kulwa) na Paul (Doto). Naomba Bwana Mungu atujalie maisha marefu zaidi, afya njema na mafanikio katika shughuli zetu za kila siku.

Katika maadhimisho haya ya siku yangu ya kuzaliwa, ninatoa zawadi ya kopi za bure za kitabu changu hicho pichani chini.



BONYEZA HAPA kuki-download BURE

11 Dec 2015

‘HAPPY birthday Tanzania…happy birthday me.” Naam, leo ni sikukuu ya Uhuru na Jamhuri, siku ya kuzaliwa kwa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), siku ambayo pia ni ya kuzaliwa kwangu.

Nilizaliwa Desemba 9, miaka kadhaa baada ya uhuru wa nchi yetu, na kila ninapoadhimisha siku ya kuzaliwa, ninaadhimisha pia siku ya kuzaliwa kwa nchi yetu.

Kwa kawaida, maadhimisho yangu ya siku ya kuzaliwa huwa sio sherehe bali hutumia siku hiyo kumshukuru Mungu, sambamba na kufanya tafakuri ya nilipotoka, nilipo na niendapo. Sherehe pekee ilikuwa kuimbiwa wimbo wa ‘Happy Birthday’ na marehemu baba, ambaye kwa bahati mbaya hayupo nasi sasa. Kwa hiyo hii itakuwa birthday yangu ya kwanza kukosa ‘sherehe’ hiyo iliyoambatana na sala za kumshukuru Mungu na kuniombea mafanikio.

Lakini wakati wa kusherehekea siku ya kuzaliwa pamoja na ‘birthday-mate’ (mtu mliyezaliwa naye siku moja) Tanzania imekuwa kama tukio la kihistoria na la kujivunia, kwa upande mwingine kila ninapofanya tafakuri kuhusu ‘mwenzangu’ huyo alipotoka, alipo na aendako huishia kupatwa na maumivu.

Si kwamba nimefanikiwa sana kuliko ‘mwenzangu’ huyo bali angalau kwa upande wangu kila nikiangalia nilipotoka, nilipo na niendako, nimekuwa naona mwanga zaidi. Kwa ‘mwenzangu’ Tanzania, wakati huko alikotoka kulileta matumaini, alipo na aendako (kwa miaka ya hivi karibuni) kulinipa shaka.

-Lengo la kupata uhuru halikuwa kumwondoa tu mkoloni bali pia kujenga jamii yenye amani na usawa, pamoja na mambo mengine. Japo katika miaka 54 ya uhuru wetu, Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani kwa maana ya kutokuwepo vita, lakini katika miaka ya hivi karibuni amani kwa maana ya kuwa na uhakika wa mlo wa kesho, au wanafunzi kuwa na hakika ya ajira wanapomaliza masomo au wakulima kuwa na uhakika wa mauzo ya mazao yao, au wagonjwa kuwa na uhakika wa huduma wanayostahili katika vituo vya afya na uhakika katika maeneo mengine, vimekuwa ni mgogoro.

Kadhalika, amani yetu imeonekana kuwanufaisha zaidi ‘mchwa’ wachache walioigeuza Tanzania yetu kuwa shamba la bibi, wenzetu ambao miaka michache iliyopita tuliwaita kupe, wanaovuna wasichopanda, wanaoneemeka kwa jasho la wengine.

Mara kadhaa, maadhimisho ya sikukuu ya uhuru wetu yameambatana na swali gumu, je kweli tupo huru? hasa ikizingatiwa kuwa kwa kiasi kikubwa nchi yetu imeendelea kuwa tegemezi kwa wafadhili, miongoni mwao wakiwa watu walewale tuliowafukuza mwaka 1961.

Kuna wenzetu wengi tu wanaodhani kuwa uhuru wetu ulifanikiwa kumtimua mtu mweupe lakini miaka kadhaa baadaye huku tukiwa huru tumeshuhudia ukoloni mpya unaofanywa na mtu mweusi. Na japo wakoloni hawawezi kuwa na kisingizio cha kututawala, lakini walipoinyonya nchi yetu walikuwa na malengo ya kunufaisha nchi zao na sio watu binafsi. Kadhalika, hawakuwa na uchungu na nchi yetu kwa vile sio yao.

Kinyume chake, wakoloni weusi sio tu ni wenzetu bali wengi wao aidha walisomeshwa bure au kwa fedha za Watanzania wenzao, lakini badala ya kurejesha fadhila kwa kulitumikia taifa kwa uadilifu, wameishia kuwa wanyonyaji wasio na huruma. Tofauti na wakoloni weupe, wenzetu hawa hawana kisingizio japo kimoja kwani wanainyonya nchi yao wenyewe.

Moja ya vikwazo vya kutuwezesha kufaidi matunda ya uhuru ni ukosefu wa uzalendo. Licha ya jitihada kubwa za Mwalimu Nyerere kuhamasisha mapenzi na uchungu kwa nchi yetu – uzalendo- tawala zilizofuatia baada ya yeye kung’atuka zikawekeza katika kuboresha maslahi binafsi badala ya maslahi ya taifa. Japo mabadiliko yaliyoikumba dunia wakati Mwalimu anataka madaraka yalisababisha haja ya mageuzi katika itikadi ya ujamaa, lakini kilichofanyika si mageuzi tu bali kuua kabisa mfumo wa ujamaa.

Kuna wanaodai kuwa isingewezekana kufanya mageuzi ya kisiasa na uchumi huku tukikumbatia mfumo wa ujamaa. Hilo sio sahihi, kwani tunashuhudia taifa kubwa kama China ambalo limefikia hatua ya juu kabisa ya ujamaa yaani ukomunisti, likimudu kuendelea kuwa taifa la kijamaa huku likijihusisha pia na sera za uchumi wa kibepari kama vile uwekezaji.

Nikirejea kwenye siku ya kuzaliwa Tanzania Bara, na yangu, Ninaomba kukiri kuwa baada ya muda mrefu, mwaka huu sikukuu yetu ya kuzaliwa mie na ‘mwenzangu’ inaleta furaha na matumaini.

Na yote hayo ni matokeo ya ninachokitafsiri kama kusikilizwa kwa dua/sala zetu kwa Mwenyezi Mungu kuturejeshea Nyerere na (Waziri Mkuu wa zamani marehemu Edward) Sokoine wengine. Tumejaaliwa kumpata Rais mpya, Dk. John Magufuli, ambaye mwezi mmoja tu tangu aingie madarakani ameweza kwa kiasi kikubwa kurejesha matumaini yaliyopotea.

Na pengine kuashiria kuwa Nyerere amerudi kupitia Dkt Magufuli, mwaka huu tunaadhimisha siku ya uhuru na Jamhuri kwa shughuli za usafi wa mazingira, na hii inakumbusha dhana ya Mwalimu ya Uhuru na Kazi. Na kwa hakika hatuwezi kuwa huru kwa kuwafanyia kazi wenzetu wanaotuibia kila kukicha.

Majuzi akiwahutubia wafanyabiashara wakubwa huko nyumbani (Tanzania), Rais Dk. Magufuli alieleza bayana jinsi tunavyoweza kutoka kundi la nchi masikini na ombaomba na kuwa miongoni mwa nchi wafadhili iwapo tutatumia raslimali zetu vizuri, sambamba na kupambana na ufisadi. Uhuru wa bendera pekee, wa kumwondoa mkoloni mweupe huku tukisumbuliwa na mkoloni mweusi ni tatizo kwani suala si rangi ya mkoloni bali ukoloni wenyewe. Tukimudu kuboresha uchumi wetu na kuweza kujitegemea, tutakuwa na uhuru kamili.

Kadhalika, kama Mwalimu alivyotufundisha, uhuru bila nidhamu ni uwendawazimu. Hatuwezi kuwa na uhuru kamili kama hatuna nidhamu ya matumizi na tuliowapa dhamana ya kutuongoza hawana nidhamu kwa maadili ya taifa.

Ni matumaini yetu wengi kuwa maadhimisho haya ya siku ya uhuru na Jamhuri kwa njia ya uhuru na kazi, sambamba na kasi kubwa ya Dk. Magufuli kutumbua majipu ni ishara njema kuwa Tanzania tuliyoitarajia Desemba 9, 1961 na kufaidika nayo zama za Mwalimu, ipo mbioni kurejea.

Nimalizie makala hii kwa kusema tena ‘Happy birthday Tanzania, happy birthday to me.’

Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu mbariki Rais wetu Dk. John Magufuli.

Mungu tubariki Watanzania. 

18 Dec 2014

Desemba 9, ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa. Niliadhimisha sikukuu hiyo kwa sala, kumshukuru Mungu kwa kunijaalia kuongeza mwaka mwingine katika umri wangu sambamba na kuomba baraka zaidi.
Kadhalika, kama zilivyokuwa sikukuu zangu za kuzaliwa huko nyuma, niliadhimisha siku hiyo kwa kufanya tafakuri ya nilipotoka, nilipo na niendako.
Siku ya kuzaliwa ina pande mbili, moja ya furaha kwa maana ya kutimiza mwaka mwingine katika maisha, na ya pili ni kutambua kwamba umri unakwenda mbele, na hivyo kupitia malengo mbalimbali kuona kama yametimia, na kwa kiwango gani, na wapi panahitaji jitihada zaidi, sambamba na kuweka malengo mapya inapobidi.
Kadhalika, wakati kwa vijana wenye umri mdogo, sikukuu ya siku ya kuzaliwa ni furaha tupu, ambapo kwa mfano, sheria mbalimbali zinatoa ruhusa fulani kwa kutimiza umri fulani, kwa wenye umri mkubwa, sikukuu hiyo huambatana na ukweli mchungu kuwa ‘dakika zinayoyoma.’
Kwa kijana wa miaka 17, kutimiza miaka 18 kunamaanisha fursa ya kupiga kura, kwa mfano. Kwa hapa Uingereza, kutimiza miaka 18 kunamaanisha ruhusa kisheria kutumia kilevi.
Lengo la makala hii si kuzungumzia sikukuu yangu ya kuzaliwa. Ukweli kwamba sikukuu yangu ya kuzaliwa inalingana na sikukuu ya kusherehekea uhuru wa Tanganyika huzua tafakuri nyingine mpya kuhusu nchi yetu.
Wakati sikukuu ya kuzaliwa kwangu ni suala langu binafsi, sikukuu ya uhuru wa Tanganyika ni suala linalomgusa kila mmoja wetu.
Japo hujiskia fahari kuchangia sikukuu ya kuzaliwa na Tanganyika, ukweli mchungu ni kwamba ninalazimika pia kujiuliza nchi yangu imetoka wapi, ipo wapi, na inaelekea wapi, na mara nyingi tafakuri hiyo huvuruga kabisa sikukuu yangu ya kuzaliwa.
Kama nilivyotimiza miaka kadhaa tangu nizaliwe, jana Tanganyika yetu imetimiza miaka 53 tangu ipate Uhuru. Wakati binafsi ninaweza kuhitimisha kuwa angalau nimepiga hatua fulani kimaisha, huku malengo kadhaa niliyojiwekea huko nyuma yakitimia au yakielekea kutimia, kwa mwenzangu Tanganyika hali si nzuri.
Tumefika mahala, baadhi ya Watanganyika wamefikia hatua ya kutamani mkoloni asingeondoka.
Nitakuwa mwenye roho mbaya iwapo nitazungumzia mabaya tu yaliyoiandama na yanayoendelea kuiandama nchi. Lakini kwa vile tafakuri katika siku muhimu kama hiyo inalenga zaidi kuangalia maeneo yanayoifanya isiwe timilifu, basi inakuwa vigumu kutoyapa uzito matatizo badala ya mafanikio.
Kadhalika, siku hiyo ni ya kupima mzani wa mafanikio na kufeli, na pindi mzani ukielemea upande wa kufeli, basi lazima taa ya tahadhari iwashwe kwani hali hiyo yaweza kuashiria matatizo zaidi huko mbele.
Kati ya sababu za kudai Uhuru kutoka kwa mkoloni ni kutaka kujitawala wenyewe, sambamba na kuondokana na mfumo wa kibaguzi uliotufanya tuwe mithili ya wageni katika nchi yetu wenyewe.
Miaka kadhaa baada ya Uhuru, jitihada zilizoongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, zilionyesha matunda ya uhuru na si tu tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga jamii yenye usawa lakini pia tulimudu kujitegemea wenyewe.
Matatizo yalianza kujichomoza baada ya Mwalimu kuondoka madarakani na hatimaye kufariki kwake. Kimsingi, nchi yetu ilikuwa kama ipo mikononi mwa Nyerere, na ilikuwa inasubiri aondoke tu ili irejee mahala pabaya pengine zaidi ya ilivyokuwa kabla ya Uhuru.
Ieleweke kwamba wakati mkoloni alikuwa na ‘excuse’ (japo isiyokubalika) ya kuiba raslimali zetu kwa ajili ya matumizi ya viwanda vyao huku Ulaya, wakoloni weusi kwa maana ya Watanganyika wenzetu waliosomeshwa na Watanganyika wenzao waliojinyima ili wapate viongozi, hawana sababu moja hata ya kutusaliti.
Yaani angalau mkoloni angeweza kujitetea kwamba acha niibe kwa sababu hii nchi si yangu. Lakini kwa wakoloni weusi, Watangayika wenzetu wanaoendekeza ufisadi hawawezi kudiriki kujitetea kwa namna yoyote ile, hasa ikizingatiwa kwamba kihistoria, takriban sote ni ndugu kwa kuzingatia asili yetu.
Kwa maana hiyo, kiongozi anayekabidhiwa dhamana kisha akafanya ufisadi, anajiathiri yeye mwenyewe pia kwa sababu mahala fulani, kuna mtu wake wa karibu atakayekuwa mhanga wa ufisadi huo.
Tusiende mbali. Angalia skandali ya ufisadi wa hivi karibuni wa Tegeta Escrow. Baadhi ya wabunge walikuwa wakitokwa na mapovu kutetea kuwa fedha fedha hizo si za umma ilhali nao ni sehemu ya umma wanaoukana. Takriban wote waliojivika kilemba cha itikadi, mdudu anayeiangamiza Tanganyika yetu kwa kasi kubwa.
Si kwamba watu hawa wamekunywa maji ya bendera kiasi cha kutoelewa kitu kingine chochote zaidi ya maslahi ya chama chao bali itikadi yatumika tu kama kilemba cha kufika nia zao mbaya.
Lakini pia suala la Tegeta Escrow limeibua tena tatizo moja linalotukwaza kama Taifa. Hili ni utegemezi wetu kwa wanasiasa na taasisi kama vyama vya siasa na watu, kwa maana ya wanasiasa.
Ukiweka kando kelele ndogo kwenye mitandao ya kijamii kudai wananchi watendewe haki kwa kurejeshewa fedha zilizokwapuliwa katika akaunti ya Tegeta Escrow na wahusika wawajibishwe, kwa kiasi kikubwa suala hilo liliachwa mikononi mwa wanasiasa.
Katika hili, ninaweza kumlaumu Mwalimu Nyerere kidogo. Pengine kwa vile tulikuwa tukihangaika kujenga Taifa lenye kujali usawa wa binadamu, na hivyo kuleta umuhimu wa wateule wachache wa kusimamia mambo, zama hizo zilikuwa za viongozi kama miungu-watu.
Mfumo wa siasa enzi hizo uliwapa madaraka wateule wachache ambao kila walichosema kilikuwa sahihi hata kama si sahihi, na ukaribu wao na watawaliwa ulikuwa mdogo mno.
Miongoni mwa madhara ya mfumo huo ndio hii hali tuliyonayo sasa ambapo wananchi wamekuwa wategemezi wa kupindukia kwa taasisi kama serikali au vyama vya siasa, na watu, hususan, wanasiasa.
Sasa angalau katika zama hizo za Mwalimu, kwa kiasi kikubwa sote tulikuwa na maslahi yanayolingana, yaani ujenzi wa Taifa kwa faida ya wote. Hivi sasa tuna wahuni wengi tu waliojiingiza kwenye siasa kwa maslahi yao binafsi. Na kama nilivyotanabahisha awali, maslahi ya chama yamekuwa kama kitu cha kuficha tu maslahi binafsi.
Ni muhimu kutambua udhaifu wa taasisi zetu na wanasiasa wetu. Lakini hata taasisi hizo zingekuwa timilifu na wanasiasa wetu kuwa imara, ukweli unabaki kuwa wao ni sehemu ya tabaka tawala, na kwa kiasi kikubwa wanatetea maslahi ya tabaka hilo, ilhali wananchi wengi wapo tabaka la chini.
Na kwa vile hatuna tabaka la kati la kueleweka, utegemezi kwa vyama vya siasa/ serikali au wanasiasa utaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi.
Wakati jana Tanganyika yetu imetimiza miaka 53, hivi kuna anayeweza angalau kubashiri hali itakuwaje miaka 20 kutoka sasa?
Kwa kasi hii ya mafisadi kushindana kuifilisi nchi, Tanganyika ya mwaka 2050, kwa mfano, itakuwa na tembo hata mmoja? Je, madini tuliyonayo ambayo yanawanufaisha zaidi wawekezaji na watawala wetu yatadumu kwa muda gani? Na hata hayo mafuta na gesi ambayo tunanyimwa haki ya kuona mikataba yake, yatakuwa neema au laana  kwetu?
Hadi wakati ninaandika makala hii, maazimio ya Bunge kuhusu skandali ya Tegeta Escrow hayajajibiwa. Ukimya wa Rais Jakaya Kikwete unaanza kuwafanya baadhi ya wananchi kuhisi kuwa tumeliwa.
Wananchi wanaishia kuonyesha masikitiko tu pasipo dalili ya kushinikiza wapatiwe haki yao kwa njia za amani.
Tumeona nguvu ya umma inavyoweza kuzaa matunda. Watanzania walihamasishana hadi msanii Diamond akashinda tuzo tatu kwenye Tuzo za Video za Kituo cha Televisheni cha Channel O (CHOAMVA). Tumeshuhudia pia nguvu ya umma ilivyomwezesha mwakilishi wa Tanzania katika Big Brother 2014 kuwa mshindi na kujinyakulia dola za Kimarekani 300,000. Kwanini basi nguvu hiyohiyo isitumike kushinikiza sio tu maazimio ya bunge kuhusu Tegeta Escrow yafanyiwe kazi bali pia kudai mabilioni yetu yaliyoibiwa na kufichwa katika mabenki nchi Uswisi yarejeshwe?
Nihitimishe makala hii kwa kumtakia mwenzangu Tanganyika heri na baraka ya kutimiza miaka 53. Lakini ninaomba pia kutumia fursa hiyo kumkumbusha (kwa maana ya wananchi wenzangu) kuwa tulipotoka kulikuwa na matumaini, tulipo si kuzuri na tuendako hakueleweki.
Ni wajibu wetu kubadili mwelekeo huu. Hili si suala la hiari bali la lazima iwapo twataka kuiona Tanganyika yetu ikiishi maisha marefu ya furaha na amani.


9 Dec 2010



JAMAA mmoja ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Joseph, leo asubuhi alikutwa na kamera yetu akiwa ameanguka katika Barabara ya Forest mjini Morogoro, pembezoni mwa uzio wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Morogoro, akidai kwamba alikuwa ametokea katika hospitali hiyo na kwamba hali yake ilikuwa imezidi kuwa mbaya.

Akizungumza na mtandao huu, Joseph alisema: "Nimetoka humu ndani (hospitali) kutibiwa na baada ya kupewa dawa niliruhusiwa kurudi nyumbani, nilipofika hapa nimezidiwa na njaa pamoja na ukali wa dawa hizo na kujikuta nikiishiwa nguvu na kuanguka.

Kama kuna mtu ana shilingi elfu moja anisaidie nikanunue walau uji," alisema Joseph huku akionekana akitetemeka kwa njaa pamoja na ukali wa dawa hizo.



Alipoulizwa anasumbuliwa na ugonjwa gani alidai ni homa ya matumbo (typhoid) iliyoambatana na homa kali.

Mwandishi wetu alimpatia kiasi hicho cha fedha ambapo pia baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo walimuunga mkono mpiga picha wetu kwa kumuongezea kiasi cha fedha na baadaye kumwinua hadi kwenye mgahawa uliopo jirani na Shule ya Sekondari ya Morogoro.

Baada ya kupata hudumu hizo, Joseph alizinduka na kauli yake ya kwanza ilikuwa ni kuushukuru mtandao huu na wananchi wengine kwa kumpatia msaada huo.

Picha na Habari kwa Hisani ya Global Publishers



WAKATI HALI IKIWA HIVYO KWA MLALAHOI HUYU,GAZETI LA Mwananchi LILIRIPOTI HABARI IFUATAYO.ISOME KISHA ULINGANISHE NA HABARI HIYO YA KUSIKITISHA HAPO JUU,KISHA TAFAKARI KUHUSU MIAKA 49 YA UHURU WETU

Mashangingi ya mawaziri yazua utata 
Sunday, 28 November 2010 21:05

Sadick Mtulya

WAKATI mawaziri na manaibu wawaziri wakikabidhiwa magari mapya, baada ya kuapishwa Jumamosi iliyopita, serikali imeibuka na kusema sio mapya ni ya zamani.Kauli hiyo inaibua utata kutokana na kuwa baada ya kuapishwa viwanja vya Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, kila waziri alikabidhiwa dereva mpya na gari jipya aina ya Toyota GX V8, badala ya gari aina ya Toyota VX V8 iliyokuwa ikitumiwa na mawaziri waliopita.

Ununuzi wa Toyota GX V8 mpya, unashiria serikali bado haijawa tayari kuunga mkono msimamo wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye amekuwa akisikika akitaka kusitishwa ununuzi wa magari ya kifahari ili kupunguza matumizi ndani ya serikali.

Toyota GX V8 moja huuzwa kati ya Sh210 milioni hadi Sh240 milioni, hukuToyota VX V8 moja inauzwa sio chini ya Sh180 milioni.Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Miundombinu, Omari Chambo, alisema magari hayo sio mapya na kwamba, yaliyotumiwa na mawaziri waliopita.Rais Jakaya Kikwete ameigawanya iliyokuwa Wizara ya Miundombinu na kuwa wizara mbili; Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi.

“Yale magari sio mapya, yalikuwepo. Kwanza uliyaona au unasema tu, hamjayachunguza vizuri jamani, fanyeni uchunguzi,’’ alisema Chambo na kukata simu.
Mawaziri wote na baadhi ya manaibu walikabidhiwa magari hayo (GX V8), huku manaibu wengine wakikabidhiwa VX V8.Sababu ya baadhi ya manaibu mawaziri kukabidhiwa VX V8 badala ya GX V8, ni kutokana na kutokamilishwa kwa taratibu za kutokamilika.

Mmoja wa manaibu mawaziri (jina tunalo), alikabidhiwa VX V8 iliyokuwa ikitumiwa na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifungo na Uvuvi, John Magufuli, ambaye sasa ni Waziri wa Ujenzi.Gazeti moja la kila siku (si Mwananchi) limeeleza kuwa ununuzi wa magari hayo, umegharimu serikali Sh9.3 bilioni na kwamba, takwimu za iliyokuwa Wizara ya Miundombinu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2005/06 magari makubwa ya kifahari yapatayo 6,000 yalikuwa yamenunuliwa na serikali kwa gharama inayokadiriwa kufikia Sh160 bilioni.

Miongoni mwa magari hayo ni Toyota Land Cruiser (VX/ GX V8, Prado) yapatayo 1,655, Nissan Patrol na Land Cruiser 885, Mitsubishi Pajero 400 na mengineyo.

Tangu kipindi cha serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kumekuwepo na mjadala kuhusu matumizi makubwa ya serikali hasa katika ununuzi wa magari ya kifahari kutokana na kuendeshwa kwa gharama kubwa.Wadau wengi wanataka viongozi watumie magari ya kawaida kama ilivyo kwa nchi ya Kenya na Rwanda


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.