8 Oct 2008
Mitihani zaidi kidato cha nne yavuja Necta iko njia panda
BARAZA la Mitihani Tanzania (Necta) bado liko njia panda kuhusu hatua za kuchukua baada ya mtihani mwingine wa kuhitimu kidato cha nne mwaka huu kuthibitika kuwa umevuja.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa siku kadhaa sasa unaonyesha kwamba, wanafunzi wa kidato cha nne tayari walishakuwa na mitihani hiyo, hivyo wamekuwa wakijibu maswali katika maeneo mbalimbali ya nchi kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani.

Juzi Baraza lilitangaza kuufuta mtihani wa somo la Hisabati ambao ulikuwa uanze kufanywa kwa kile kilichoelezwa kuwa umevuja na kwamba, vyombo vya usalama vinafanya uchunguzi zaidi kwa mitihani mingine ya Kiswahili, Kiingereza, Fizikia na Uraia inayodaiwa kuvuja.

Lakini jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa jeshi lake linawashikilia wanafunzi wawili kutoka kituo cha Perfect Vision, mmoja kwa tuhuma za kukutwa na majibu ya mtihani wa somo la Civics (Uraia) na mwingine kwa kumfanyia mwenzake.

Kamanda Kova alisema watuhumiwa hao, walikamatwa juzi saa 11:00 jioni wakiwa katika kituo hicho kilichopo maeneo ya Ubungo karibu na nyumba za Shirika la Nyumba nchini.

Kwa mujibu wa Kamanda Kova, mwanafunzi wa kwanza kukamatwa ni mtahiniwa wa kujitegemea Rhoda Juma Mombora (37) ambaye alikamatwa na majibu ya mtihani wa somo hilo uliofanywa juzi mchana. Mtuhumiwa wa pili, Clara Haule (20) mkazi wa Makumbusho alikamatwa akimfanyia mtihani Anjela Maganga mwenye namba P1475/0023.

Kova alisema watuhumiwa hao, wanashikiliwa na polisi na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. Idadi ya watuhumiwa inafikiriwa kuongezeka.

Japokuwa ni watahiniwa hao tu walionaswa, wanafunzi mbalimbali waliozungumza na Mwananchi katika maeneo mbalimbali nchini na jijini Dar es Salaam walidai kuwa wana mitihani yote na kwamba hata waliyofanya juzi walikuwa nayo. Walisema baada ya kuingia katika chumba cha mtihani walibaini kuwa ndiyo yenyewe.

"Mitihani yote tunayo hata ule wa jana (juzi) wa somo la Uraia (Civics), tulikuwa nao na baada ya kuingia katika chumba cha mtihani tulibaini kuwa ndiyo wenyewe, swali mpaka swali," alidai mwanafunzi mmoja wa jijini Dar es Salaam (jina tunalo).

Mwanafunzi huyo alidai kuwa walipata mitihani hiyo kutoka kwa watu walio karibu na Baraza baada ya kuchanga fedha na kuwapatia watu hao.

Mazingira ya kuvuja kwa mitihani hiyo yanaonyesha kuwa iliibwa kutokana na mpango wa ndani uliosukwa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kwa lengo la kujipatia kipato.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo baada ya kupata mitihani wanafunzi hao wamekuwa wakitumia simu za mikononi kupeana maswali au majibu kabla ya kuingia katika chumba cha mitihani.

Katika hatua nyingine Umoja wa Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya juu nchini (Tahliso) umetaka mtihani wote wa kidato cha nne ufutwe na kisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe na watendaji wakuu wa Baraza kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo ambayo mara ya mwisho ilitokea mwaka 1998.

Katibu Mkuu wa Tahliso, Mtatiro Julius alisema jana jijini kuwa, kashfa ya kuvuja kwa mitihani hiyo inawahusu viongozi hao moja kwa moja na hivyo hawapaswi kukwepa kuwajibika.

"Waziri anapaswa kuwajibika mwenyewe kwa kulinda heshima yake, lakini zaidi kwa manufaa ya umma kwani ameshindwa kuwasimamia vema watendaji wa chini yake," alisema Mtatiro na kuongeza:

"Kitendo cha mitihani kuvuja na serikali kuufuta mmoja na kuacha mingine iendelee kitazalisha wasomi wasiokuwa na uwezo,".

Kwa mujibu wa Mtatiro, inasikitisha kuona serikali inakiri kuvuja kwa mtihani wa Hisabati kwani kauli hii inaleta uwezekano wa mitihani yote kuwa imevuja kwa kuwa mitihani hiyo iliandaliwa pamoja na kusambazwa pamoja.

"Hali ya kuvuja kwa mitihani nchini imekuwa ya kawaida sana ingawa miaka mingine serikali inakanusha tuhuma hizo. Katika hili la mwaka huu, ni lazima Rais Jakaya Kikwete atumie nafasi yake kuwawajibisha watendaji wake," alisema.

Mtatiro alibainisha kuwa tatizo la kuvuja kwa mitihani nchini linatokana pamoja na mambo mengine tamaa ya fedha na walimu kutolipwa mishahara mizuri.

Aliitaja sababu nyingine ya kuvuja kwa mitihani kuwa ni ubinafsi na uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji wakuu katika kusimamia mitihani na upole wa Rais Kikwete katika kuwachukulia hatua watendaji wake wanaoboronga kazini.

"Upole wa Rais Kikwete ndiyo unaosababisha watendaji wa chini wajione kuwa wako huru na hakuna wa kuwawajibisha," alisema.

Juzi Baraza lilifuta mtihani wa Hisabati baada ya kubainika umevuja. Hata hivyo Baraza halikuwa tayari kutaja sehemu wala watu waliokamatwa na mtihani ambao sasa utatungwa mwingine na kufanywa Oktoba 27, mwaka huu.

Mwaka 1998, Baraza hilo lilifuta mitihani yote baada ya kubaini kuwa mingi ilivuja na hivyo kulazimika kusogeza mbele tarehe ya kuanza kwa mitihani na hali inaonekana inaweza kujirudia mwaka huu kutokana na mitihani hiyo kuzagaa kama njugu.

Awali Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk Joyce Ndalichako alisema baraza hilo limeanza kufanya uchunguzi wa uvujaji wa mitihani mingine nchi nzima baada ya kupata taarifa juu ya kuwepo kwa mitihani zaidi kwenye mikono ya watahiniwa ikiwemo Kingereza, Kiswahili, Fizikia na Uraia.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi kuhusu kuvuja kwa mitihani, Dk Ndalichako alisema vyombo vya usalama vimekamata mitihani ya Kiswahili, Kiingereza, Uraia, Fizikia pamoja na Historia na kwamba, uchunguzi zaidi unafanyika, lakini hakutaja sehemu ambazo mitihani hiyo ilikamatwa kwa kile alichoeleza kuhofia kuharibu uchunguzi unaoendelea.

Kashfa ya kuvuja kwa mitihani ni mwendelezo wa kashfa mbalimbali zinazoendelea kulikumba Baraza hilo baada ya hivi karibuni kuripotiwa kuibwa vyeti 4,000 vikiwa na namba bila ya majina.

SOURCE: Mwananchi

MBONA HII INATOKEA KILA MWAKA LABDA TATIZO KWA MITIHANI YA MWAKA HUU NI HIYO MEDIA ATTENTION.KUNA WATU WENYE JUKUMU LA KUHAKIKISHA MITIHANI HAIVUJI,NA WANALIPWA KWA KAZI HIYO LAKINI MWAKA HADI MWAKA MAMBO YANAENDELEA KUWA YALEYALE.NA SIJUI KWANINI HADI MUDA HUU UONGOZI WA NECTA HAUJAWAJIBIKA.ANYWAY,WANAJUA KWA UTAMADUNI WETU KUBORONGA SIO SABABU TOSHA YA KUJIUZULU MAJUKUMU WALIYOKABIDHIWA.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.