24 Oct 2008


Pamoja na umasikini,madudu ya kisiasa,ufisadi na mengineyo yanayochukiza kuhusu nchi yetu ya Tanzania,mimi (na pengine wewe mwenzangu) bado tunaipenda nchi yetu.Nina sababu lukuki za kuipenda (au hata kuichukia) Tanzania,lakini ya msingi zaidi ni ukweli kwamba mimi ni Mtanzania,Tanzania ni nchi yangu na kwa vyovyote itakavyokuwa huko mbeleni bado nitabaki kuwa Mtanzania.

Hata hivyo,haitoshi kuwa Mtanzania tu.Haitoshi kuipenda Tanzania pasipo kutafsiri mapenzi hayo kwa vitendo.Kwanini?Kwa sababu pasipo kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa bora,inakuwa mahala salama pa kuishi,na inadumu kama nchi,Utanzania na mapenzi yetu kwa nchi yetu yanaweza yasiwe na faida au kuna mahala tunaweza kufika tunapenda kitu kisichokuwepo.Au kibaya zaidi,tunaweza kufika mahala ambapo ukisema "naipenda Tanzania" unaonekana taahira kama hutoishia kupigwa mawe.

Weka pembeni umasikini,weka pembeni maradhi,ufisadi,na matatizo mengine ya kijamii,kiuchumi au kisiasa.Tatizo kubwa na la hatari zaidi kwa Tanzania ni UZALENDO.Ni tatizo kwa sababu uzalendo unapotea kwa kasi.Ni tatizo kwa sababu nchi iko ilipo sasa kutokana na wachache wasio na uzalendo kwa nchi yetu.Ni tatizo pia kwa vile imefika mahala ambapo baadhi ya wenzetu wameanza kutafsiri uzalendo ni sawa na uhaini.Hawa ni wale ambao kwa vile wana uhakika wa kuamka wakiwa salama,kupata matibabu ya daraja la kwanza,kupata mishahara na posho nono sambamba na usafiri wa bure,pamoja privileges nyingine.Wenzetu hawa wanasahau kwamba wana babu,bibi,baba,mama,kaka,dada,wadogo,ndugu,jamaa na marafiki mtaani ambao wanateseka kutokana na matendo ya wasio wazalendo (mafisadi,nk).

Kwa kulinda maslahi yao binafsi na ya wale waliowaweka kwenye ulaji,wenzetu hawa hawataki kusikia neno lolote linalowahusu watu wa kawaida.Kuzungumzia lolote kuhusu kundi hili la walio wengi inatafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu,kwenda kinyume na taratibu na pengine uhaini.Wanachosahau ni kwamba Tanzania ikichafuka,hizo raha zinazowalewesha nazo zitapotea.Badala ya kuwanyanyasa wale wanaohangaika kuifanya nchi yetu iwe katika hali nzuri,wanapaswa kuwaenzi na kuwasapoti.

Tanzania ni yetu sote,sio ya kikundi kidogo cha watu wanaotaka kusikia yale wanayopenda wao tu japo nao wanaona kabisa madudu yanayofannywa na majambazi,mafisadi,wazembe,mafuska wa itikadi,nk.Hizi tabia za kupiga makofi ya shangwe hata chifu anaposahau kufunga zipu yake zitatupeleka pabaya.Amani ina tabia tatu kuu: inachukua muda kuipata/kuijenga,inachukua muda mfupi sana kuiharibu/kuipoteza,na inachukua muda mrefu zaidi kuirejesha pindi ikitoweka (na pengine ikishapotea hairejei tena).Tuna kila aina ya mifano inayotuzunguka:Somalia,DRC (Zaire),Sudan,nk.

Tusipofanya sasa tunachopaswa kufanya kuilinda Tanzania kwa nguvu zote na kuwasapoti wazalendo wote wanaotusaidia kufanya hivyo tutaishia kujilaumu huko mbeleni.Na hakuna sehemu mbaya ya tatizo kama inapofikia hatua ya kusema "laiti tunge..."

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.