Showing posts with label UZALENDO. Show all posts
Showing posts with label UZALENDO. Show all posts

24 Oct 2008


Pamoja na umasikini,madudu ya kisiasa,ufisadi na mengineyo yanayochukiza kuhusu nchi yetu ya Tanzania,mimi (na pengine wewe mwenzangu) bado tunaipenda nchi yetu.Nina sababu lukuki za kuipenda (au hata kuichukia) Tanzania,lakini ya msingi zaidi ni ukweli kwamba mimi ni Mtanzania,Tanzania ni nchi yangu na kwa vyovyote itakavyokuwa huko mbeleni bado nitabaki kuwa Mtanzania.

Hata hivyo,haitoshi kuwa Mtanzania tu.Haitoshi kuipenda Tanzania pasipo kutafsiri mapenzi hayo kwa vitendo.Kwanini?Kwa sababu pasipo kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa bora,inakuwa mahala salama pa kuishi,na inadumu kama nchi,Utanzania na mapenzi yetu kwa nchi yetu yanaweza yasiwe na faida au kuna mahala tunaweza kufika tunapenda kitu kisichokuwepo.Au kibaya zaidi,tunaweza kufika mahala ambapo ukisema "naipenda Tanzania" unaonekana taahira kama hutoishia kupigwa mawe.

Weka pembeni umasikini,weka pembeni maradhi,ufisadi,na matatizo mengine ya kijamii,kiuchumi au kisiasa.Tatizo kubwa na la hatari zaidi kwa Tanzania ni UZALENDO.Ni tatizo kwa sababu uzalendo unapotea kwa kasi.Ni tatizo kwa sababu nchi iko ilipo sasa kutokana na wachache wasio na uzalendo kwa nchi yetu.Ni tatizo pia kwa vile imefika mahala ambapo baadhi ya wenzetu wameanza kutafsiri uzalendo ni sawa na uhaini.Hawa ni wale ambao kwa vile wana uhakika wa kuamka wakiwa salama,kupata matibabu ya daraja la kwanza,kupata mishahara na posho nono sambamba na usafiri wa bure,pamoja privileges nyingine.Wenzetu hawa wanasahau kwamba wana babu,bibi,baba,mama,kaka,dada,wadogo,ndugu,jamaa na marafiki mtaani ambao wanateseka kutokana na matendo ya wasio wazalendo (mafisadi,nk).

Kwa kulinda maslahi yao binafsi na ya wale waliowaweka kwenye ulaji,wenzetu hawa hawataki kusikia neno lolote linalowahusu watu wa kawaida.Kuzungumzia lolote kuhusu kundi hili la walio wengi inatafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu,kwenda kinyume na taratibu na pengine uhaini.Wanachosahau ni kwamba Tanzania ikichafuka,hizo raha zinazowalewesha nazo zitapotea.Badala ya kuwanyanyasa wale wanaohangaika kuifanya nchi yetu iwe katika hali nzuri,wanapaswa kuwaenzi na kuwasapoti.

Tanzania ni yetu sote,sio ya kikundi kidogo cha watu wanaotaka kusikia yale wanayopenda wao tu japo nao wanaona kabisa madudu yanayofannywa na majambazi,mafisadi,wazembe,mafuska wa itikadi,nk.Hizi tabia za kupiga makofi ya shangwe hata chifu anaposahau kufunga zipu yake zitatupeleka pabaya.Amani ina tabia tatu kuu: inachukua muda kuipata/kuijenga,inachukua muda mfupi sana kuiharibu/kuipoteza,na inachukua muda mrefu zaidi kuirejesha pindi ikitoweka (na pengine ikishapotea hairejei tena).Tuna kila aina ya mifano inayotuzunguka:Somalia,DRC (Zaire),Sudan,nk.

Tusipofanya sasa tunachopaswa kufanya kuilinda Tanzania kwa nguvu zote na kuwasapoti wazalendo wote wanaotusaidia kufanya hivyo tutaishia kujilaumu huko mbeleni.Na hakuna sehemu mbaya ya tatizo kama inapofikia hatua ya kusema "laiti tunge..."

28 Sept 2008

Picha kwa hisani ya  Chesi Mpilipili
Shirika la Umeme Tanzania,TANESCO,limetangaza ratiba mpya ya mgao wa umeme ambao tofauti na yale masaa matano ya awali   sasa tatizo hilo litadumu kwa masaa kumi kwa siku.Ni muhimu kuwa tatizo hili linakuja wakati tatizo jingine la nishati ya mafuta likiwa halijatulia sawasawa.Angalau katika suala la kupanda kwa bei za mafuta liko nje ya uwezo wetu kwa vile linakuwa determined na soko la dunia.Lakini inakuwa vigumu kuingia akilini pale ambapo takriban kila mwaka lazima TANESCO watangaze mgao wa umeme.Na ninaposema kila mwaka najaribu ku-neglect power cuts za mara kwa mara zisizo na ratiba ambazo zimekuwa kama suala la kawaida huko nyumbani.

Kwa mtazamo wangu,tatizo kubwa zaidi linaloikabili TANESCO sio uhaba wa fedha bali namna linavyoendeshwa kisiasa.Pengine unaweza kudhani ufumbuzi wa tatizo hilo ni kulibinafsisha shirika hilo la umma.Lakini pengine kabla hujafikiri hivyo ni vema ukaangalia baadhi ya mashirika ya umma ambayo kubinafsishwa kwake hakujaweza kuyafanya yamudu uendeshwaji wa mafanikio.Mfano mzuri ni Sherika la Reli (TRC) ambapo huduma zake zimeendelea kuwa mbovu licha ya kupatiwa mwekezaji ambaye pengine mafanikio yake makubwa yamekuwa katika kuishawishi serikali impatie fedha za kumkwamua kila linapotokea tishio la mgomo wa wafanyakazi.Sikatai kwamba kuna some few success stories katika ubinafsishaji wa mashirika yetu ya umma,mfano mzuri ukiwa TBL,lakini mafanikio hayo yanaendelea kubaki kuwa mithili ya matone kwenye bahari.

Uendeshwaji wa TANESCO kisiasa ndio uliopelekea shirika hilo kusaini mkataba wa ajabu na kampuni ya IPTL.Mkataba huo umeendelea kuiumiza TANESCO kwa muda mrefu sana na hakuna dalili za kuisha kwa tatizo hilo.Ahadi za kupitia mikataba mibovu zimeendelea kubaki ahadi huko akina IPTL wakiendelea kuikalia kooni,hali inayopelekea maumivu zaidi kwa wananchi wa kawaida.

Kuna hujuma za kiwango kidogo dhidi ya TANESCo zinazofanywa na wezi wa mafuta ya transfoma,mita za luku na hata nyaya za umeme.Hujuma hizi zinazodaiwa kuwashirikisha baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa shirika hilo haziwezi kulinganishwa hata kidogo na hujuma kubwa kama hiyo ya IPTL.Hivi inaingia akilini kweli kwa shirika kulilipa shirika jingine hata lisipotoa huduma inayokusudiwa kwenye mkataba?

Kuna Watanzania wenzetu wanaofanya kila liwezekanalo kuona TANESCO haiishi kulingana na matarajio yake na ya wateja wake.Hawa ni pamoja na wale waliotuingiza mkenge kwenye utapeli wa Richmond.Hawa wanaombea ukame ujitokeze tena ili waje na scams nyingine za kuongeza mabilioni ya shilingi kwenye akaunti zao.Ni katika mazingira ya namna hii ndipo tunapojikuta tukipatwa na hisia kwamba hata kuharibika kwa mitambo ya umeme ya Songas (ambapo imepelekea kuwepo kwa mgao huu wa sasa) kunaweza kuwa hujuma ya hao wenzetu ambao kuumia kwa wengi ndio mafanikio yao.

Kabla ya kuangalia chanzo kikubwa cha utendaji wa kiwango cha chini kabisa kwa TANESCO (mbali na uendeshwaji wa kisiasa) ni vema pia kuangalia sera nzima ya nishati nchini.Katika dunia hii ambayo nchi kama zetu za dunia ya tatu (na hivi karibuni hata kwa nchi zilizoendelea) hazina uwezo madhubuti wa kukabiliana na matukio yasiyotarajiwa (eg kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na the current world economy crisis) ni muhimu kujitengenezea mazingira ya kuzuia madhara ya huko mbeleni.Tukiendelea kutegemea mvua zijaze mabwawa ili mitambo ya TANESCO huko Kidatu na kwingineko ifanye kazi sawasawa,tutazidi kuumia.Pasipo kuwa na chombo madhubuti zaidi ya EWURA na TPDC,ni dhahiri wafanyabiashara wa mafuta wataendelea kuuza nishati hiyo kwa bei wapendazo wao.

Lakini ili yote yawezekane ni lazima kila Mtanzania aweke mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi.Maamuzi mengi mabovu ni matokeo ya kukithiri kwa upungufu wa uzalendo na uchungu kwa taifa letu.Wataalam tunao lakini mara nyingi ushauri wao unapuuzwa kwa vile unaonekana kuathiri maslahi binafsi ya mafisadi.Kibaya zaidi,ushauri mzuri kwa maslahi ya taifa unaweza pia kutafsiriwa kuwa ni uchochezi.Siasa inaelekea kutawala kwenye kila nyanja na professionalism inanyang'anywa nafasi yake na hamasa za kisiasa.Nothing good ever comes out of putting emotions (in this case political sentiments) in front of common sense (hapa ni maslahi ya taifa)


18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Mambo?

Siku chache zilizopita nilibahatika kuwa na maongezi na babu mmoja wa Kiskotishi ambaye kwa maelezo yake mwenyewe yeye ni “mkazi wa dunia nzima” (global citizen).Babu huyo anadai kuwa dunia ingekuwa mahala bora sana kama kusingekuwa na mipaka na sheria kali za uhamiaji.Na katika kutimiza azma yake ya kuwa mkazi wa dunia nzima anadai ametembelea takribani nchi 10 katika kila bara.Sijui kama alikuwa anasema ukweli au “ananifunga kamba” tu.Katika maongezi yetu hayo aligusia jambo flani ambalo liliniingia sana na ambalo ndio mada yangu ya wiki hii:UZALENDO.

Kwa mujibu wa babu huyo,enzi zao wakiwa vijana suala la uzalendo lilikuwa likitiliwa mkazo sana.Alidai kuwa japo kwa sasa hali ni tofauti kidogo lakini bado nchi nyingi za magharibi zinatilia mkazo sana suala hilo.Alieleza kwamba akiwa kijana babu yake alikuwa akimwambia kuwa mazingira mazuri watakayoyaweka wakati huo yatakuja kuvinufaisha zaidi vizazi vijavyo.Baba yake pia alikuwa akimweleza hivyo hivyo.Na yeye alipokuwa mtu mzima alikuwa akiwaeleza wanae hivyohivyo.Na sasa anasema amekuwa akitoa changamoto ya aina hiyohiyo kwa wajukuu wake.Furaha aliyonayo ni kwamba utabiri wa babu na baba yake umetimia.Maendeleo yaliyopo hivi sasa yamechangiwa na msingi mzuri uliojengwa karne kadhaa zilizopita.Na kilichowasukuma hao waliotengeneza misingi hiyo si kingine zaidi ya uchungu wao kwa taifa lao na vizazi vijavyo.

Huko nyumbani kuna tatizo kuhusiana na suala la uzalendo.Wapo wapuuzi fulani ambao wanaendesha mambo utadhani hakuna kesho au labda Tanzania haitakuwepo miaka 50 ijayo.Na hawa ndio baadhi yao waliripotiwa kutishia maisha ya waandishi wa KULIKONI na THIS DAY kwa sababu magazeti hayo yameapa “kula nao sahani moja” (kuwaweka hadharani).Hawa ni watu ambao hawana uchungu si kwa nchi yao tu bali hata kwa wajukuu zao.Ukweli ni kwamba mtu anayekula fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule hana upeo wa kufikiria kwamba kwa kufanya hivyo huenda wajukuu wa mtoto wake wa mwisho watakaopaswa kwenda shule miaka 20 ijayo wanaweza kukosa nafasi hiyo kwa upuuzi uliofanyika mwaka 2006.Kuna watu wanafanya mchezo na maisha ya Watanzania wenzao kwa kutumia fedha za wenzao bila hata kuwashirikisha hao waliowekeza.Jamani,hata sheria za kawaida mtaani si kwamba bwana au bibi harusi mtarajiwa hawezi kutumia michango ya harusi yake mwenyewe pasipo kuwajulisha wanakamati?Sembuse hao ambao wamekabidhiwa fedha ambazo baadae wanapaswa kuzirejesha kwa wahusika!Nadhani mnaniapata hapo.

Wabadhirifu wa mali za umma na wala rushwa ni sawa na majambazi tu.Ni majambazi ambao silaha yao kubwa ni dhamana walizokabidhiwa kuwatumikia wananchi.Majambazi hawa wanachoiba sio fedha tu bali hata haki za Watanzania wenzao.Na kama walivyo majambazi wengine,hawa wakishahisi kuwa wanafahamika hukimbilia kutumia silaha kuu mbili:rushwa na vitisho.Kama gazeti linachimba maovu yanayofanywa na watu flani wasio na uchungu na nchi yao,basi waandishi wa gazeti hilo watafuatwa ili “wadakishwe kitu kidogo kuua soo.”Na itapoonekana kuwa gazeti hilo na waandishi wake wako ngangari katika kutetea maslahi ya Taifa na hivyo kukataa kuuza taaluma yao kwa kupokea rushwa basi hapo ndipo vitakapoanza vitisho.Sio huko nyumbani pekee ambako waandishi wa habari wanaovalia njuga kufichua maovu katika jamii wanakumbana na vitisho kutoka kwa wahusika.Mwaka 1996,Veronica Guerin, mwandishi wa habari wa kike huko Northern Ireland alipigwa risasi na kuuawa kutokana na makala za uchunguzi kuhusu biashara ya madawa ya kulevya nchini humo.Mwaka juzi,waandishi kadhaa wa magazeti ya Daily Record na Sunday Mail ya hapa Uingereza waliripoti kupokea vitisho kutokana na habari za uchunguzi walizokuwa wakiandika kuhusiana na magenge ya uhalifu.Kadhalika,mwaka jana waandishi wa habari wa magazeti kadhaa nchini Italia waliripoti kupokea vitisho baada ya kuripoti tuhuma za rushwa kuhusiana na klabu ya soka ya Genoa ya nchini humo.

Mifano hiyo michache inaonyesha ni jinsi gani watu waovu wanavyopenda kuendelea na maovu yao bila kubughudhiwa.Lakini haiwezekani watu wenye uchungu na nchi yetu wawaachie kufanya ufisadi wao wapendavyo.Naamini kila mzalendo anaelitakia mema Taifa letu atahakikisha kuwa wanahabari wanaosimama kidete kuwafichua wala rushwa na wabadhirifu hawabughudhiwi hata kidogo.Mjenga nchi ni mwananchi na mvunja nchi ni mwanachi pia.Tukiendelea kuwalea hawa majambazi wa mali na haki zetu basi tujue kuwa sio tu tunajitengezea “future” mbaya bali pia vizazi vijavyo vitatuhukumu kwa kuwaachia watu wachache wasio na uchungu na nchi yetu kutuharibia mambo.Tukiamua kwa nia moja tunaweza kuwadhibiti majambazi hao.

Alamsiki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.