28 Apr 2009



YAH,WANASEMA NI SUALA LA MTIZAMO: KUSEMA GLASI IKO HALF EMPTY AU HALF FULL.HABARI MBILI ZIFUATAZO ZINADHIHIRISHA MANTIKI YA MSEMO HUO.

Na Boniface Meena

UMAARUFU wa Rais Jakaya Kikwete unaonyesha kuendelea kuporomoka, kwa mujibu wa ripoti ya matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Mpango wa Utafiti wa Elimu ya Demokrasia nchini (Redet).

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa utendaji kazi wa Rais Kikwete, ambaye aliingia madarakani mwaka 2005 kuongoza serikali ya awamu ya nne, umeshuka kwa asilimia 28 mwaka jana ukilinganisha na matokeo ya utafiti ya mwaka 2006.

Pamoja na kushuka kwa asilimia hiyo, utafiti huo umeonyesha kuwa wananchi waliohojiwa wanaridhika zaidi na utendaji wa Rais Kikwete, kuliko wanavyoridhishwa na utendaji kazi wa baraza lake la mawaziri ambalo utendaji wake umekubaliwa na asilimia 18 tu.

Kwa mujibu wa utafiti huo, watu wanaoridhika sana na utendaji kazi wa Kikwete ni asilimia 39.5 tu kulinganisha na asilimia 69 iliyoonyesha kuridhika naye sana mwaka 2006.

Akitoa taarifa ya utafiti huo jana kwa waandishi wa habari, mtafiti mkuu wa Redet, Dk Benadetha Killian alisema kuwa ukilinganisha takwimu za Oktoba 2006 na Oktoba 2007, asilimia ya wale wahojiwa ambao wanasema wanaridhika sana na utendaji kazi wa Rais Kikwete imepungua kutoka asilimia 69 Oktoba 2006 hadi asilimia 44 mwezi Oktoba 2007 na sasa imefikia asilimia 39.5 hadi Novemba mwaka jana.

Dk. Killian alisema kuwa ukichambua undani wa mwenendo huo utaona kwamba wakati idadi ya wanaosema wanaridhika sana iliteremka kwa tofauti ya asilimia 23, kati ya mwaka 2006 na 2007, kasi ya kutoridhika sana imepungua ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2007/08 wakati idadi ya wahojiwa ambao walisema wanaridhika sana ilipungua kwa tofauti ya asilimia 4.5 tu.

Kwa mujibu wa Dk. Killian, ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya utafiti huo ulifanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na sampuli ilichaguliwa katika ngazi tatu ambazo ni wilaya na vijiji/mitaa na katika kila ngazi sampuli ilipatikana kwa kutumia mtindo wa sampuli nasibu.

"Katika kila wilaya, watafiti walitakiwa kuchagua vijiji viwili (kwa maeneo ya shamba) au mitaa miwili (kwa maeneo ya mjini) kwa kutumia njia ya sampuli nasibu. Katika kila wilaya, jumla ya watu 50 walichaguliwa kwa ajili ya kuhojiwa, 25 kutoka kila kijiji/mtaa," alisema.

"Na kati ya watu 50 waliohojiwa katika kila wilaya, 25 walitakiwa wawe wanawake na wengine 25 wawe wanaume na uchaguzi wote wa wahojiwa ulifanyika kwa kutumia njia ya sampuli nasibu."

Alisema ukiacha masuala mengine ya utendaji wa mawaziri, waliohojiwa walitakiwa kutoa tathimini yao kuhusu utendaji kazi wa Rais Kikwete katika kipindi cha takriban miaka mitatu ya utawala wake kwa kutoa maoni yao kama wanaridhika sana, wanaridhika kiasi au hawaridhiki.

Dk. Killian alisema kati ya wote waliohojiwa, asilimia 39.5 walisema wanaridhishwa sana na utendaji wa Rais Kikwete, asilimia 39.0 walisema wanaridhika kiasi na asilimia 19.3 walisema hawaridhiki na utendaji kazi wa mkuu huyo wa nchi.

Alisema hata hivyo kwa ujumla, matokeo ya utafiti wa Novemba mwaka jana yanaashiria kwamba, utendaji kazi wa Rais Kikwete bado unaonekana kuridhisha idadi kubwa ya watu pale ambapo makundi mawili ya wahojiwa yanapojumlishwa pamoja yaani wale wanaosema wanaridhika sana asilimia 39.5 na wale wanaosema wanaridhika kiasi asilimia 39 ikiwa inafanya idadi hiyo ya wahojiwa wote kufikia asilimia 78.5.

Dk Killian alisema sababu za kuridhika au kutoridhika na utendaji kazi wa serikali ya Rais Kikwete ni kutoridhishwa na ahadi yake ya kuboresha hali ya maisha. Asilimia 31.0 ya waliohojiwa walisema ameshindwa kuboresha hali ya maisha, wakati asilimia 24 walisema hajatimiza ahadi na asilimia 12.2 walisema hafuatilii utekelezaji wa ahadi zake.

"Sababu nyingine zilizotolewa na wahojiwa ni kuchagua viongozi wasiofaa asilimia 10.8, ameshindwa kupambana na rushwa asilimia 8.0, lakini pamoja na kwamba utafiti huu ulifanywa kipindi ambacho "vigogo" walikuwa wanapelekwa mahakamani kuhusiana na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na wengine kutuhumiwa na wizi wa fedha za akaunti ya madeni ya nje (EPA), ni asilimia 6 tu ndiyo waliotaja moja kwa moja suala hili kama sababu ya kutoridhishwa au kuridhishwa kiasi na utendaji kazi wa rais," alisema.

Alisema sababu za wananchi kutoridhika na utendaji wa serikali iliyo madarakani ni kutofuatilia utekelezaji asilimia 30.7, serikali kujihusisha na rushwa asilimia 29 na inapitisha mikataba mibovu asilimia 10.0.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa bunge ndio linaongoza kwa kutoridhisha wananchi baada ya asilimia kubwa ya waliohojiwa kueleza kuwa hawaridhishwi na taasisi hiyo ya kutunga sheria.

Bunge limeonekana kutoridhisha wengi tofauti na taasisi za serikali kama polisi, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini, serikali za mitaa na kadhalika.

Dk. Killian alisema bunge linaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya kiwango cha kutoridhika ambacho ni asilimia 77.4, ikifuatiwa na serikali za mitaa asilimia 75.6 wakati baraza la mawaziri linashika nafasi ya tatu kwa asilimia 63.

Kwa upande wa utendaji kazi wa Rais Amani Abeid Karume wa Zanzibar, utafiti unaonyesha kuwa asilimia 44 tu ya wote waliohojiwa wanaridhika sana, wakati asilimia 24 wanaridhika kiasi na asilimia 26 walisema hawaridhiki.

Alisema kiwango cha utendaji wa Rais Karume kimeonekana kupanda kwa asilimia 9 ukilinganisha na utafiti wa Oktoba 2007 wakati asilimia 35.5 tu ilimkubali baada ya kuporomoka kutoka asilimia 47.8 aliyopata kipindi cha hadi Oktoba 2006 na baadaye kupanda kutoka asilimia 35.5 Oktoba 2007.

CHANZO: Mwananchi



Nyota ya Kikwete Bado Yang'ara
na mwandishi Wetu


Watanzania walio wengi, zaidi ya asilimia 80, bado wana imani na Rais Jakaya Kikwete, kuliko miaka minne iliyopita alipochaguliwa kuwa Rais. Pia asilimia kubwa ya Watanzania inaridhishwa na utendaji kazi wa Rais na Serikali yake.

Kura ya maoni iliyoendeshwa na taasisi ya uchunguzi inayojitegemea ya REDET kuhusu utendaji wa Serikali ya Kikwete katika miaka mitatu iliyopita ya uongozi wake, inaonyesha kuwa asilimia 83.7 ya Watanzania wana imani naye.

Kundi hilo la Watanzania wanaothibitisha kuwa na imani na Rais Kikwete likigawanywa katika makundi ya ulinganisho wa imani, asilimia 50 inasema ina imani sana kwa kiongozi huyo, asilimia 33.7 inasema ina imani kiasi cha kutosha kwake.

Asilimia hiyo ni kubwa kuliko ile ya ushindi wa urais mwaka 2005, alipochaguliwa kwa kishindo ambapo alichaguliwa kwa asilimia 82. Hakuna mwanataaluma yeyote wa REDET ambaye alikubali kuzungumza na gazeti hili kuhusu kura hiyo ya maoni licha ya kupatikana kwa nakala ya matokeo ya utafiti huo.

Lakini habari zinasema matokeo kamili ya kura hiyo yanatarajiwa kutangazwa rasmi wiki ijayo na uongozi wa REDET. Kubwa zaidi katika ripoti hiyo, ni ukweli kuwa asilimia ya Watanzania wenye kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Kikwete bado iko juu.

Utafiti huo wa kisayansi na wa kina uliofanyika katika sehemu mbalimbali za nchi mijini na vijijini unaonyesha kuwa asilimia 78 ya Watanzania wanaridhishwa na utendaji kazi wake. Matokeo ya kura hizo yamethibisha kwa mara nyingine, ukweli ambao umebakia bila kubadilika kuhusu imani ya wananchi kwa Rais Kikwete na utendaji wake tangu alipoingia madarakani.

Kura zote za maoni ambazo zimefanyika tangu wakati huo, zimekuwa zikionyesha kuwa kiwango cha imani ya wananchi wake na kwa utendaji kazi wake kimebakia kwenye eneo la asilimia 80. Kura hizo pia zinaonyesha kuwa imani ya wananchi kwa wasaidizi wake wakuu ni ya juu.

Zinaonyesha pia kuwa asilimia 82.7 wana imani na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein akiwa nyuma ya Rais kwa asilimia moja, wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda anavutia asilimia 84. Utafiti huo pia unathibitisha kuwa wananchi kiasi cha asilimia 70 wana imani na Baraza la Mawaziri, wakati asilimia 66 wana imani na wakuu wa mikoa. Imani ya wananchi inashuka kidogo kwa Bunge ambalo lina asilimia 65.

Katika namna ambayo pia itakipa nguvu na kuifurahisha CCM, asilimia ya Watanzania ambao wanasema wanaridhishwa na utendaji kazi wa chama hicho ni 72.8 wakati asilimia 75.6 wanasema wana imani na chama hicho. Matokeo hayo yatakifurahisha chama hicho kwa sababu asilimia hiyo kubwa ya kukubaliwa na Watanzania imebakia ya kiwango hicho hicho kwa karibu miaka 17 tangu kuanzishwa kwa vyama vya upinzani nchini.

Mwaka 1992 wakati CCM na serikali zilipoongoza mageuzi ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi, ilikuwa baada ya uchunguzi uliothibitisha kuwa ni asilimia 20 tu ya Watanzania waliokuwa wanataka mfumo wa vyama vingi. Kwa namna moja au nyingine, asilimia hiyo imebakia na kujithibitisha mara nyingi kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitia uchaguzi mkuu ambao umefanyika tangu wakati huo na hasa uliopita uliomwingiza Rais Kikwete madarakani mwaka 2005. Kwa upande wa vyama vya upinzani, asilimia ya Watanzania ambayo inasema haina imani na vyama hivyo inabakia juu kwa asilimia zaidi ya 31.



CHANZO: HabariLeo



































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.