5 May 2009


Ikulu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Makamu wa Rais, Polisi, Msajili wa Vyama vya Siasa na Sekretarieti ya Maadili ni kati ya ofisi ambazo, mahesabu yake yalionekana kuwa na mapungufu na kutofuata kanuni za fedha au kufanya malipo yenye nyaraka pungufu.
Mapungufu hayo yamo kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Serikali (CAG) kwa mwaka 2007/08 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita.

Kutokana na mapungufu hayo, ripoti ya CAG inaonyesha kwamba ofisi hizo, licha ya kupewa hati ya ukaguzi inayoridhisha, kila hati imeambatana na mambo ya msisitizo yenye kuzitaka ofisi hizo zisirudie makosa hayo.

Ripoti hiyo inafafanua: ``Kimsingi, aya inayohusu `Mambo ya Msisitizo` ni tahadhari kwa Afisa Masuuli na taarifa muhimu kwa watumiaji wa taarifa za fedha. Vivyo hivyo, kama udhaifu huo haujarekebishwa, unaweza kusababisha hati isiyoridhisha (kutolewa) kwa kaguzi zijazo.``

Ofisi nyingine zilizopewa hati yenye mambo ya msisitizo ni Magereza, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) (Ngome), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Kimataifa, Ofisi ya Rais na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko na Wizara ya Ardhi na Makazi.

Zingine ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Fedha na Uchumi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Tume ya Mipango, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya, Tume ya Utumishi wa Umma na Tume ya Kudhibiti Ukimwi.

Vilevile zipo sekreterieti za mikoa kadhaa kama vile Arusha, Mara, Iringa, Kigoma, Pwani, Kilimanjaro, Mbeya, Singida, Morogoro, Shinyanga, Kagera, Dar es Salaam na Rukwa ambazo zilipata hati inayoridhisha yenye msisitizo.

Kuhusu Ikulu, kwa mfano, ripoti ya CAG inaonyesha katika mwaka wa fedha 2007/08 hakukuwa na mpango wa mwaka wa manunuzi, kinyume na kifungu cha 45 (a) hadi (e) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Pia mahesabu ya Ikuku yalikuwa na mambo yasiyosuluhishwa katika taarifa za benki, yanayofikia Sh. 2,710,000.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanya malipo yenye nyaraka pungufu yanayofikia Sh. milioni 21.8 na malipo yaliyolipwa mara mbili yenye thamani ya sh. milioni 45.

Idara ya Mhasibu Mkuu imeelezwa kufanya malipo yanayofikia sh. milioni 570 kwa M/s Fifth Africa Population bila nyaraka ambatanifu, huku mishahara yenye thamani ya Sh. milioni 8.6 ikilipwa kwa watu walioondoka kwenye utumishi wa umma.

Kwa upande wa ofisi ya Makamu wa Rais, malipo ya madeni ya Sh milioni 89.2 yalifanyika kwenye bajeti ya mwaka huu bila idhini huku stakabadhi za kukiri malipo ya Sh. Milioni 8.9 zikishindwa kuwasilishwa ili kukaguliwa. Pia ofisi inalaumiwa na CAG kwa kufanya manunuzi ya Sh milioni 20.8 kutoka kwa M/s Colour Print (T) Ltd bila kufanya ushindani wa zabuni.

Kuhusu jeshi la polisi, ipo milolongo kadhaa ya makosa ya kihasibu, lakini moja wapo ni malipo ya Sh. milioni 74.1 kufanywa bila nyaraka sahihi na masurufu yasiyorejeshwa kufikia sh. milioni 131.

Ofisi zilizopewa hati yenye shaka ni pamoja na ya Bunge, Wizara za Kilimo, Chakula na Ushirika, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mambo ya Ndani, Jinsia na Maendeleo ya Watoto, Nishati na Madini, Maliasili na Utalii, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Miundombinu.

Sekretareti za mikoa zilizopewa hati yenye shaka ni Dodoma, Lindi, Mtwara, Mwanza, Ruvuma, Tabora na Tanga. Pia kwenye kundi hilo imo Mahakama ya Ardhi.

Ufafanuzi wa ofisi ya CAG unaonyesha kwamba hati zenye shaka hutolewa pale kunapokuwa na udhaifu wenye uzito na unaoathiri taarifa za fedha lakini hausababishi taarifa hizo kukosa maana kabisa.

Taarifa inasema Bunge lilipewa hati yenye shaka kutokana na mlolongo wa makosa ya kanuni za fedha ikiwa ni pamoja na kulipa matibabu ya Sh. Milioni 102 nje ya nchi bila kuidhinishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Ofisi zilizopewa hati isiyoridhisha, kwa mujibu wa ufafanuzi, udhaifu unaojitokeza unapotosha kabisa tarifa za hesabu ni pamoja na Wizara ya Kazi, Idara ya Uhamiaji na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Wizara hiyo katika ripoti hiyo inaonyesha kulikuwa na upotevu wa Sh. milioni 90.9 na taarifa za masurufu yasiyorejeshwa ilikuwa inatofutiana.

CHANZO: Nipashe



0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.