Showing posts with label CAG. Show all posts
Showing posts with label CAG. Show all posts

14 Apr 2019

[Uchambuzi wa ACT Wazalendo Kuhusu Maeneo Kumi (10) Muhimu Kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18].

- Ikulu Yatumika Kuficha Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege

- Bilioni 800 Hazikutolewa kwa Ukaguzi
- Trilioni 4.8 Zimetumika Bila Kupita Mfuko Mkuu wa Hazina
- Mikopo ya Ndani Yashindwa Kulipa Madeni Kikamilifu
- 40% ya Bajeti yategemea Mikopo na Misaada Kutoka NjeNdugu WanahabariA: Utangulizi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad ametoa taarifa yake ya Ukaguzi wa Mapato na Matumizi ya Fedha za Umma kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Licha ya changamoto mbalimbali zilizotokea kabla ya CAG kukamilisha wajibu wake huu wa kikatiba, taarifa hiyo sasa iko wazi kwa umma, baada ya kuwa imekabidhiwa rasmi bungeni. Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini na kama Chama cha Upinzani Bungeni. Tunafurahi kupata fursa ya kuwa nanyi hapa ili kuzungumza na umma, kupitia nyinyi, juu ya maeneo Kumi (10) muhimu kwenye ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha wa 2017/18.B: Maeneo Kumi (10) Muhimu Katika Ripoti ya CAG1. Bajeti ya Serikali Sio Halisia, Mapato Yasiyokusanywa ni Tarakimu MbiliKwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17, ambayo ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano, mipango ya Serikali ilikuwa ni kukusanya shilingi 29.5 trilioni, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya 2016/17, kati ya fedha hizo, Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni. Na hivyo, kutokufikia lengo la makusanyo kwa 14.33%. Kwenye uchambuzi wetu wa mwaka jana tulieleza kuwa bajeti za Serikali si halisia.Kwenye ripoti hii ya mwaka 2017/18, kwa mara nyengine, CAG amelithibitishia Taifa kuwa Serikali ya awamu ya tano inatunga Bajeti ambayo sio halisia. Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/18 jumla ya shilingi 31.7 trilioni zilitarajiwa kukusanywa na zilipitishwa kutumika na Bunge. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hii ya CAG, Serikali iliweza kukusanya kutoka vyanzo vyake vyote shilingi 27.7 trilioni tu, na kutumia shilingi 26.9 trilioni. Hivyo ikikosa makusanyo kwa 12.66% na ikikosa matumizi kwa 15.2%.Kwa miaka mitatu ya mwisho ya Serikali ya awamu ya nne, wastani wa lengo lisilofikiwa na Serikali katika ukusanyaji wa mapato ya Bajeti ni tarakimu moja, 6.3% tu, ambapo kwa mwaka 2013/14 lengo halikufikiwa kwa 9%, kwa mwaka 2014/15 nako lengo halikufikiwa kwa 4%, na kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 lengo halikufikiwa kwa 6% tu.Hii inadhihirisha Kwa mara nyengine tena kuwa Serikali ya Awamu ya Tano hutangaza viwango vikubwa vya Bajeti ili kufurahisha umma ilhali uhalisia ni kuwa Bajeti ni ndogo zaidi. Kwa miaka 2 mfululizo CAG ametuonyesha kuwa Serikali inashindwa kufikia makadirio ya Bajeti Kwa zaidi ya shilingi Trilioni 4 kutoka Bajeti inayopitishwa na Bunge.2. 40% ya Bajeti Inategemea Misaada na MikopoRipoti ya CAG imetuonyesha kuwa ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya tano uwezo wetu wa kujitegemea kibajeti umezidi kuzorota. Kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 nchi yetu ilijitegemea Kibajeti kwa 65% kwa mapato ya ndani ya nchi, na 35% iliyobaki ndiyo iliyotokana na mikopo pamoja na misaada ya Wahisani. Hali Hiyo ni tofauti kwa mwaka wa Fedha wa 2017/18, tumedidimia zaidi.CAG ameonyesha katika uchambuzi wake kuwa, nanukuu “Uchambuzi unaonyesha kwamba bila Mikopo na misaada kutoka kwa wahisani wa maendeleo, makusanyo ya ndani ya nchi yetu yangeweza kugharamia matumizi yote ya Serikali kwa asilimia 60 tu” (Chanzo: Ripoti ya Ukaguzi-Serikali Kuu-2017/18: Ukurasa wa 89).Hii inaonyesha kuwa Bajeti yetu ya Tanzania ni tegemezi kwa 40% tofauti na tunavyoelezwa na Serikali kila wakati kuwa nchi yetu inaondoa utegemezi kwenye bajeti. Kwa mwaka 2016/17 utegemezi wetu uliongezeka kwa 27%, na kwa mwaka 2017/18 utegemezi wetu umeongozeka kwa 22%.CAG ameonyesha kuwa Serikali ilikusanya shilingi 27.7 trilioni tu (makusanyo yote, ikiwemo misaada na mikopo kutoka ndani na nje) kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Makusanyo ya ndani yakiwa ni shilingi 16.7 trilioni, sawa na 60% ya makusanyo yote, na kwamba matumizi ya kawaida yaliyofanyika mwaka huo ni shilingi 15.3 trilioni, ambayo ni sawa na asilimia 55% ya makusanyo yote lakini ni 93% ya mapato ya ndani. Utegemezi huu utaathiri sana nchi yetu kwani gharama za kulipia mikopo (riba) zitakuwa kubwa kuliko hata uwezo wetu wa kuongeza mapato ya ndani.3. Shilingi 800 Bilioni Hazikutolewa kwa UkaguziKatika Uchambuzi wetu wa mwaka jana tulionyesha kuwa 6% ya fedha zilizokuwa zimekusanywa na Serikali hazijulikani zilipokwenda. Hizi zilikuwa ni shilingi 1.5 trilioni ambazo mjadala wake ulichukua mwaka mzima. Hoja yetu hiyo ilipelekea kufanyika kwa uhakiki maalumu na CAG, na ambapo bado Serikali ilishindwa kuonyesha zilipokwenda fedha hizo, zaidi ya kudai kuwa ilihamishia Ikulu matumizi ya shilingi 976 bilioni kati ya hizo 1.5 trilioni bila kumpa CAG uthibitisho wa uhamishaji huo wala kuonyesha fedha hizo zimefumikaje huko Ikulu.Katika ukaguzi wa CAG wa Bajeti ya mwaka 2017/18, ambayo ni Bajeti ya Pili ya Serikali ya awamu ya 5, ameonyesha kuwa katika Bajeti ya shilingi 31.7 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya shilingi 27.7 trilioni tu kutoka kwenye vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo. Serikali ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi 4 trilioni kama ilivyokuwa mwaka uliopita ingawa sasa ni sawa na 13% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Hata hivyo CAG anaonyesha kuwa shilingi 26.9 trilioni tu ndio zilitolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali na kwenda kutumika, hivyo shilingi 800 bilioni kati ya shilingi 27.7 trilioni zilizokusanywa kutokujulikana ziliko na hazikutolewa kwa ukaguzi.4. Shilingi 4.8 Trilioni Zimetumika Bila Kupita Kwenye Mfuko MkuuKatika Ukurasa wa 91 wa ripoti yake yam waka wa fedha wa 2017/18, CAG anasema, nanukuu “Ikilinganishwa taarifa ya kutoa fedha (exchequer issue report) na taarifa ya Fedha zilizopokelewa na kuripotiwa katika taarifa za fedha za Mafungu husika pamoja na barua za kukiri mapokezi ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, imebaini utofauti wa taarifa zilizoripotiwa…”. CAG ameeleza kuwa tofauti hiyo imesababishwa na kutokuwepo kwa mifumo thabiti ya usuluhishi kati ya fedha zilizotolewa na hazina na fedha zilizotolewa na wahisani wa maendeleo moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo katika Wizara. Ni muhimu sana kusisitiza hapa kuwa kwa mujibu wa CAG kuna fedha shilingi trilioni 4.8 ambazo makusanyo yake hayakuingizwa mfuko mkuu wa Serikali (tazama uk 91 wa Taarifa, tanbihi namba 15).Suala la udhaifu wa Mifumo Katika Hazina pia limeelezwa kwa kina Katika Taarifa ya CAG ya Uhakiki wa Tofauti ya shilingi 1.5 Trilioni Katika mwaka wa Fedha 2016/17. Bado udhaifu huu unaendelea na madhara yake Katika usimamizi wa Fedha za Umma ni makubwa sana.5. Bilioni 678 za Mamlaka Nyengine Ziliporwa na Mlipaji Mkuu wa SerikaliKwenye ripoti ya CAG ya 2017/18 imeonyeshwa kuwa bado Serikali inatumia fedha ambazo sio zake (ring fenced) kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya mwaka 2016/17. Kwa mwaka 2017/18 CAG amebaini jumla ya shilingi 678 bilioni zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa niaba ya taasisi nyengine hazikuhamishwa kwenda kwenye taasisi husika, na badala yake zilihamishiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambapo huko hazikuonekana kwenye ukaguzi kama sheria inavyotaka. Fedha zilizoporwa na Hazina ni pamoja na shilingi 169 bilioni za Shirika la Reli, shilingi 168 bilioni za Wadau wa Korosho nchini na shilingi bilioni 16 za Wakala wa Umeme Vijijini (REA). CAG kwa mara nyengine tena amependekeza sheria iheshimiwa kuhusu matumizi ya fedha hizi za Taasisi mbalimbali. Kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17 kiasi cha shilingi 2.2 trilioni za mamlaka mbalimbali nchini hazikurejeshwa kwenye mamlaka husika mara baada ya fedha hizo kukusanywa na TRA. Tabia hii ya kupora Fedha za Mamlaka nyengine licha ya Kwamba Fedha hizo zimewekwa kisheria na kikatiba inaua misingi ya matumizi bora ya Fedha za Umma.Kwa Upande wa TRA Bado kuna changamoto kubwa ambazo zinahitaji kutatuliwa. Makusanyo yetu ya kodi Bado ni kidogo sana (tax yield) tukiwa wa mwisho Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, uwiano wa makusanyo ukiwa ni 12% tu ya Pato la Taifa. Hii inatokana tax base kuwa ndogo na mifumo sio rafiki kwa walipa kodi. Inawezekana TRA huchukua Fedha za Taasisi kupeleka Hazina ili kuonyesha makusanyo zaidi ilhali hali sio hiyo. Serikali inapaswa kukaa na sekta Binafsi kujadili kwa unyoofu (honestly) njia bora ya kupanua wigo wa Kodi ili nchi iweze kujitegemea. Katika uchambuzi wetu tumeacha mambo Mengi ikiwemo upotevu mkubwa wa mizigo ya transit ambao CAG ameuonyesha.6. Kushuka kwa Thamani ya Shilingi Kunakuza Zaidi Deni la TaifaRipoti ya CAG ya 2017/18 imetuonyesha kuwa Deni la Taifa (Deni la Serikali) limefikia shilingi 50 trilioni mpaka Juni 30, 2018 likiwa na ongezeka la shiingi 4.85 trilioni, sawa na 10% kutoka shilingi 46 trilioni za Juni 30, 2017, deni hili likikua kwa shilingi 9.8 trilioni kwa muda wa miaka miwili tu kutoka Juni 30, 2016 mpaka Juni 30, 2018. CAG ameeleza kwamba kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni kumechangia kuongezeka kwa Deni kwa 20% kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 (ongezeko kubwa zaidi ukilinganisha na 9% za mwaka wa fedha wa 2016/17). Hii inatokana na Deni letu la Nje kuwa kwenye Fedha za Kigeni na hivyo kuathirika sana kutokana na thamani ya shilingi kutetereka. Baada ya makosa ya kimaamuzi kwenye suala la Zao la Korosho, ni dhahiri kuwa Deni letu la Nje litaongezeka zaidi baada ya shilingi ya Tanzania kutetereka zaidi kwa kukosa Mapato ya Fedha za Kigeni. MAARIFA makubwa yanahitajika kuhami nchi kutokana na janga la Deni la Taifa.7. Mikopo ya Ndani Yashindwa Kulipa Madeni Kikamilifu Lakini pia CAG ameeleza kuwa sababu Kuu zaidi ya kukua kwa deni la Taifa ni kwa kuwa tunaendelea kukopa zaidi. Kwa miaka mitatu iliyopita kukopa zaidi kulichangia ukuaji wa deni letu kwa 70%, ambapo kwa mwaka 2016/17 ilikuwa juu zaidi na kufikia 88%.Zaidi CAG ameonyesha pia kuwa tulikopa mikopo ya ndani ya shilingi 5.7 trilioni kwa mwaka 2017/18 ambayo pamoja na kuwa na athari mbaya kwenye mikopo ya sekta binafsi nchini (maana inapunguza fursa ya wafanyabiashara wetu kukopeshwa na taasisi za ndani za fedha), lakini pia mikopo hiyo imeshindwa kulipa riba za mwaka za shilingi 6.1 trilioni. Na hivyo ilibidi Serikali kutafuta shilingi 448 bilioni kutoka kwenye vyanzo vingine ili kuweza kulipa riba hizo. Ripoti ya CAG imeeleza, nanukuu “Deni la Ndani halikuchangia kwenye miradi ya Maendeleo”. Hivyo tulikopa ndani ya nchi si kwaajili ya kufanya shughuli za maendeleo, bali kulipa deni la nyuma, na bado hata hiyo mikopo haikutosheleza ulipaji wa hayo madeni ya nyuma. Hali hii si afya kwa taifa letu.Mfano kwa mwaka 2017/18 Kiwango cha kuhudumia Deni la nchi ni 108% ya fedha zilizopatikana kutoka kwenye mikopo ya ndani, na CAG ameonya kuwa jambo hilo lina athari kubwa. Ukurasa wa 141 wa Ripoti ya Ukaguzi wa Serikali Kuu CAG ameeleza, nanukuu “kuna uwezekano wa kuwa na madhara kwa uchumi (hali ya kuhudumia deni kwa 108%) isipotafutiwa ufumbuzi”. CAG pia ameonyesha kuwa kasi ya kukua kwa mikopo ya nje ni 38%, hali ambayo inaongeza gharama za kuhudumia madeni. Na jambo baya zaidi ni kuwa tunakopa zaidi mikopo ya kibiashara. CAG ameshauri watunga sera kuwa na busara wakati wa kuchagua miradi ya kupewa fedha za mikopo ya kibiashara, akishauri maamuzi yazingatie uzalishaji wa miradi husika. Vinginevyo Bajeti ya Taifa itakwenda kuhudumia deni tu.Kwenye eneo hilo la Deni la Taifa pia ripoti ya CAG imeonyesha kuwa kuna upotoshwaji mkubwa wa mapokezi ya mikopo kutokana na mapungufu ya udhibiti wa ndani. Pia CAG ameonyesha kuwa mifumo wa kutunza madeni ni kianalojia (ya kizamani), jambo ambalo linaathiri kumbukumbu za madeni. 8. Serikali Imeanza Kushindwa Kulipa Madeni (Defaulting)Ripoti ya CAG imeonyesha kuwa Serikali imeshaanza kushindwa kulipa baadhi ya madeni yake (Defaulting). Tayari kuna fedha kiasi cha shilingi 212.7 bilioni Serikali imeshindwa kuzilipa kwa Benki Kuu nchini (BOT), zikiwa shilingi 199.79 bilioni ni riba ya nakisi ya Serikali, na shilingi 12.9 bilioni ni sehemu ya Serikali ya gharama za kudhibiti ukwasi kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2017/18.Serikali ilisaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na BOT, ambao unaitaka kulipa kila robo mwaka sehemu yake ya gharama ya kudhibiti ukwasi pindi hati ya madai inapotolewa. Ucheleweshwaji huu wa malipo utaongeza uwepo wa mali za BOT zisizo na tija, na ni dalili ya Serikali kushindwa majukumu yake kifedha.9. Ikulu Yatumika Kuficha Ukaguzi wa Manunuzi ya NdegeHatujafanikiwa kuona Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege ikiwemo Ununuzi wa Ndege za Shirika la Ndege Nchini, ATCL ambao kwa sehemu umefanyika mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18.Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka jana (ripoti ya mwaka wa fedha wa 2016/17) tuliwaeleza kuwa katika ripoti ile licha ya kuwa ni taarifa bora sana kwa maudhui na uchambuzi, kuna mambo muhimu kadhaa ambayo CAG aliyaacha. Na tukamtaka kwenye ripoti yake ya mwaka 2017/18 ayafanyie kazi, mojawapo ni ukaguzi wa Ununuzi wa Ndege Sita (6) zinazoendeshwa na Kampuni ya Ndege nchini, ATCL.Mpaka sasa Serikali imeshatumia jumla ya Shilingi Trilioni1 kununua ndege sita (6) na katika makadirio ya Bajeti ya mwaka 2019/20 yanayoendelea sasa bungeni Serikali imeomba Bunge liidhinishe shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kulipia ndege mpya nyengine. Ufuatiliaji wetu umegundua kuwa Serikali imekuwa ikichukua Fedha za Umma kupitia Fungu 62 (Wizara ya Uchukuzi) na kufanya manunuzi ya ndege. Ndege hizo wanakabidhiwa Wakala wa Ndege za Serikali kama wamiliki na shirika la ATCL inakodishiwa ndege hizo kwa Mkataba maalumu (ambao haujawekwa wazi popote, hata kwa Bunge).Tulitarajia kuwa ripoti hii ya CAG ya mwaka 2017/18 kwenye ukaguzi wa fungu Namba 62 tungeweza kuona ukaguzi wa manunuzi ya ndege hizi. Lakini Serikali kwa lengo la kuficha taarifa imeamua kuhamishia kwenye Ofisi ya Rais (fungu 20) Wakala wa Ndege za Serikali kupitia tangazo la Serikali namba 252 la Juni 2018.Tumetafuta taarifa ya ukaguzi wa fedha hizo za umma zilizofanya manunuzi ya ndege bila mafanikio. Tunamwomba CAG;
- Afanye Ukaguzi Maalumu wa Fedha za Umma Shilingi Trilioni 1 zilizotumika kununua ndege.
- Afanye Ukaguzi wa usimamizi wa mkataba wa ukodishwaji wa ndege hizo kati ya Wakala wa ndege za Serikali na Shirika la Ndege la ATCL ili Watanzania wajue matumizi sahihi ya Fedha zao za Kodi.Jambo hili ni muhimu sana, kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa kila jambo lenye harufu ya wizi au matumizi yenye mashaka basi Serikali huliamishia jambo hilo ikulu (Kwa kuwa inajua ukaguzi wake hautawekwa wazi). Hata kwenye fedha shilingi 1.5 trilioni ambazo tulizianisha kuwa hazijulikani ziliko kutokana na uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17, baada ya kuibana Serikali na kumtaka CAG afanye uchunguzi maalum, mwishowe Serikali ilihamishia Ikulu matumizi ya Shilingi 976 bilioni kati ya hizo shilingi 1.5 trilioni ili isihojiwe.Mafungu mawili, Fungu 20 (Ofisi ya Rais Ikulu) na Fungu 30 (Sekretariati ya Baraza la Mawaziri) yanapaswa kumulikwa sana katika matumizi ya Fedha za Umma. Tumeona mwaka huu Serikali inaomba Bunge litenge shilingi Bilioni 302 kwa Fungu 30 kwa kile kinachoitwa ‘matumizi mbalimbali ya kitaifa’. Mwaka ujao, Mungu akituweka hai, tutafuatilia kwa kina kaguzi za mafungu Haya kwani inaonyesha ndimo inakuwa kichaka Cha kuficha Taarifa za namna Fedha za Umma zinatumika.10. Hoja za Ukaguzi za Shilingi Bilioni 225 hazina majibu kabisa
Kwa ujumla, na kwa Serikali Kuu peke yake, Hoja zote za Ukaguzi zilizoibuliwa na CAG kwenye Hesabu za Mwaka 2017/18 ukiachana na hoja kubwa nilizoeleza hapo juu, zina thamani ya shilingi 225 bilioni kati ya Fedha zote zilizokusanywa kwenye mwaka wa Fedha husika. Hii inaonyesha kuwa bado Serikali haijaweza kufanyia kazi Hoja za CAG kwa wakati na kwamba mifumo ya Serikali bado inavujisha Fedha za Umma.C: Mapendekezo ya ACT Wazalendo Baada ya kusoma taarifa hiyo ya CAG na kuyaanisha maeneo Kumi (10) muhimu, sisi ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafuatayo:1. ACT Wazalendo tunawasihi Wabunge wote bila kujali vyama vyao kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia Serikali. Wabunge wasipotekeleza wajibu wao huo basi nchi yetu itaangushwa na matumizi mabovu na ya kinyume na Sheria kama tulivyoaina kwenye Uchambuzi wetu.2. Serikali iwe inatunga Bajeti Halisia ambayo inatekelezeka, tofauti na inavyofanya kwa miaka minne mfululilo sasa, ambapo inataja namba kubwa ambayo Bajeti husika huwa haipatikani kwa ukamilifu wake na hivyo kuathiri sana miradi ya Maendeleo ambayo inakuwa imepangiwa mafungu ya Fedha. Ni bora kuwa na Bajeti ndogo ambayo inatekelezwa badala ya kuwa na Bajeti kubwa ambayo haitekelezwi ipasavyo.3. Serikali itazame upya utekelezaji wa Sera zake za kiuchumi kwani dalili zinadhihirisha kuwa Uchumi wetu unaanguka. Ikibidi Kuwe na Mjadala wa Kitaifa juu ya hali ya uchumi wa nchi yetu, mjadala huo usaidie kupata uhalisia wa hali mbaya ya uchumi wetu, mbinu za kuunasua, na mawazo ya kuinasua nchi kutoka kwenye utegemezi wa misaaada pamoja na mikopo inayoongeza ukuaji wa deni la Taifa.4. Serikali ionyeshe ilipo shilingi 800 bilioni isiyoonekana matumizi yake katika ripoti ya CAG yam waka wa fedha 2017/18.5. Serikali ileze ni kwa nini Fedha Jumla ya shilingi Trilioni 4.8 hazikupita kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ili utolewaji wake uweze kufuata masharti ya Katiba na Sheria za nchi. Fedha hizi za Wafadhili zinaonekana Katika Vitabu vya Bajeti Lakini CAG hazioni kuingia mfuko Mkuu na hivyo kutoka kwake kunaweza kuwa ni kinyume Cha Sheria. Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe inafanya usuluhishi sahihi wa taarifa za fedha zilizotolewa kwa Wizara mbalimbali na fedha zilizopokelewa moja kwa moja na wahisani wa maendeleo katika miradi. Hazina ifanyiwe usafi maalumu ili kuhakikisha ‘credibility’ ya Taarifa zake.6. Serikali izingatie Sheria na Katiba Kuhusu Fedha za Taasisi ambazo zimetengwa kisheria Lakini Hazina inazitumia bila kujali Sheria. Hazina ihakikishe inazirejesha kwa wenyewe Ada, Tozo na mapato hayo ambayo TRA ilikusanya kwa niaba ya Idara, Wakala na Taasisi nyengine.7. Wabunge, kama sehemu ya wenye wajibu wa kutunga sera tunayo nafasi ya kuisimamia Serikali kwenye suala la kushuka kwa thamani ya shilingi, kwanza kwa kuwawajibisha wote waliosababisha sintofahamu ya zao la korosho ambalo kama tungeuza basi kungepatikana unafuu kwenye deni la Taifa.8. Ili kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Taifa, haswa Deni la Nje, kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi yetu, tunapendekeza kuwa Serikali ifanye hedging ya Deni la Nje ili kuwa na uhakika wa thamani ya fedha itakayotumika muda wote kuhudumia Deni hilo. Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha kutegemea sana mikopo ya kibiashara kutoka Mabenki ya Nje na hivyo kuweka nchi kwenye hatari kubwa ya Mtego wa Madeni (Debt Trap). Hedging inaweza kusaidia kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Nje.9. Tunamsihi ndugu Rais atambue kuwa njia ya bora ya kupambana na rushwa na ufisadi ni kuwezesha mifumo kufanya kazi. Mtu mmoja hawezi kamwe kuwa dawa ya ufisadi ulioota mizizi nchini kwetu. Ripoti za CAG na madudu yaliyoibuliwa kila kona inaonyesha dhahiri kuwa silaha ya uhakika ni kujenga Taasisi imara za Uwajibikaji ili kudhibiti Fedha za Umma. Miaka 4 aliyepo madarakani imethibitisha kuwa nguvu ya Mtu mmoja haitoshi kukomesha ubadhirifu bali Mifumo Imara.Ni matarijio yetu kuwa Watanzania wataendelea kuisoma na kuichambua Taarifa ya CAG na kuwaomba Wabunge watimize wajibu wao wa kuisimamia Serikali ili kujibu hoja zote za Ukaguzi. Bila Bunge kutimiza wajibu wake ipasavyo mzunguko wa uwajibikaji unakuwa haufungi. Tumeona Katika Taarifa ya CAG kuwa Hoja hazijibiwi na hivyo hazifungwi na madhara yake ni kuwa kila mwaka hoja zinaongezeka tu.


Ahsanteni Sana.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT W
azalendo
Aprili 14, 2019
Dodoma

2 Apr 2013Kampuni ya Mohamed Enterprises yauziwa viwanja kinyemela
*Bandari watumbua zaidi ya bilioni 1.5, waendesha miradi hewa
*Mabosi wanachomeka watumishi hewa, wanavuta mishahara
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2011; imeendelea kufichua namna kundi la watumishi wa umma na wafanyabiashara wakubwa wanavyoitafuna Tanzania. Utouh aliwasilisha taarifa hiyo bungeni mwishoni mwa wiki. Fedha na mali za umma zenye thamani ya mabilioni ya shilingi, ama zinaibwa au zinachukuliwa kwa namna ambayo ni vigumu kuamini kama kweli viongozi wakuu wa kitaifa wana dhamira ya kutokomeza ufisadi uliovuka mipaka. 


Kuuzwa kwa viwanja, majengo ya Serikali 
CAG amebaini kuwa kiwanja kilichopo katika Kitalu Na. 10 katika Barabara ya Nyerere, kimeuzwa kwa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) kinyemela. Amesema wakati uuzaji kiwanja hicho ulipaswa uratibiwe na Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC - mrithi wa PSRC), kazi hiyo ilifanywa na watu wasiokuwa na mamlaka kisheria. 
Nyaraka za mawasiliano kati ya MeTL, Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina zinazohusiana na uuzaji kiwanja hicho, zinaonyesha kuwa Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina ndiyo waliojihusisha moja kwa moja katika uuzaji wa mali hiyo ya umma, kwa kutoa maelekezo kwenye menejimenti ya CHC. Bodi ya Wakurugenzi haikushirikishwa kabisa. 
Hatimaye kiwanja hicho kiliuzwa kwa MeTL kwa Sh bilioni 2.046 bila kufuatwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005. 
Katibu wa Waziri aamuru kampuni ilipwe Sh bilioni 2.34
Utata wa matumizi mabaya ya fedha za umma, umemkumba aliyekuwa Katibu wa Waziri mwenye dhamana ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji kuhusu kiwanja namba 192 kilichopo Barabara ya Nyerere. Alimwandikia barua Mwenyekiti wa PSRC ailipe kampuni ya DRTC Sh milioni 954.72. 
Hata hivyo, Meneja Mkuu wa DRTC akamwandikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC akitaka alipwe haraka kiasi cha Sh bilioni 2.349. Kwenye barua hiyo, Meneja wa DRTC alisisitiza kuwa malipo hayo ni maelekezo kutoka serikalini, licha ya ukweli kwamba yalikuwa ni makubwa kuliko madai halisi na akalipwa. 
Kuuzwa kwa jengo la kampuni ya umma ya TMSC
Jengo la kampuni ya Tanzania Motors Services (TMSC) lipo katika kitalu namba 24 katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Jengo hilo liliuzwa kwa kwa kampuni ya Saddiq Super Service Station (SSSS) kwa Sh bilioni 1.3. Kampuni hiyo ilitoa malipo ya awali ya asilimia 10, yaani Sh milioni 130. Baadaye Wizara ya Fedha ikaitaarifu CHC kuwa Serikali imeghairi kuliuza jengo hilo lililopo kitalu namba 24 kwa kampuni ya SSSS. Wizara ya Fedha ikaitaka CHC ikubaliane na SSSS kuwafidia, kwani tayari kampuni hiyo ilishatoa kianzio cha Sh milioni 130. 
Kuona hivyo, kampuni ya SSSS ikawasilisha madai ya kulipwa fidia ya Sh bilioni 3.894 kwa ajili ya kupoteza biashara yake na Sh milioni 500 kama fidia kwa usumbufu. Hatimaye ikaamuliwa kuwa SSSS ilipwe Sh milioni 964 ambamo ndani yake kulikuwa na Sh milioni 130 ilizotoa awali na gharama za usumbufu. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alikuwa Mwenyekiti wa kikao kilichoidhinisha malipo hayo. Akawasilisha katika Wizara ya Fedha ambayo yeye ni kiongozi, ili ilipe kiasi hicho cha fedha kwa maelekezo ya kikao alichokiongoza yeye mwenyewe. 
Kwa uamuzi huo, Wizara ya Fedha ikailipa moja kwa moja SSSS Sh milioni 964.2; ilhali kama ni malipo, basi yalipaswa kufanywa na CHC. Malipo hayo, kwa mujibu wa taarifa ya CAG, yanaibua maswali juu ya dhamira ya Wizara ya Fedha kulipa fedha hizo haraka haraka bila kuishirikisha Menejimenti wala Bodi ya Wakurugenzi ya CHC. 
Malipo ya kushangaza kwa kampuni ya Tantrack
Tantrack Agencies ilikuwa mpangaji katika jengo la TMSC lilipo kitalu namba 24, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Ilipanga kwa miaka miwili kuanzia Julai Mosi 1993. Kampuni hiyo inasema ilitumia Sh milioni 24 kukarabati jengo kwa wakati wote wa mkataba wake wa upangaji, licha ya ukweli kwamba jambo hilo halikuwamo kwenye mkataba iliyoingia na TMSC. Ikakataa kulipa ada ya pango ikisema fedha hizo zilizotumika kwenye ukarabati zitambuliwe kuwa ndiyo ada ya pango. 
Tantrack ikafungua kesi ya madai namba 257 ya mwaka 1995 katika Baraza la Nyumba Mkoa wa Dar es Salaam (DRHT) dhidi ya TMSC, kwa kigezo kwamba TMSC ilikuwa ikivunja makubaliano. Ilifanya hivyo baada ya TMSC kuiandikia barua ikiipa notisi ya miezi sita ihame kutokana na kutotekeleza makubaliano ya mkataba. 
Wakati hayo yakiendelea, jengo la TMSC likauzwa kwa njia ya mnada kwa African Terminal Limited (ATL) kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa Sh milioni 3. CHC ikapeleka vielelezo vyake mahakamani ikionyesha mkataba ulivyokuwa kati yake na Tantrack. Kabla rufaa haijasikilizwa, ATL ikaweka pingamizi. Sasa ni miaka 15 suala hilo likiwa halijaamuliwa. 
CAG anasema imebainika kuwa kuna uzembe na kutowajibika kwa pande zote mbili zinazopambana kwenye mgogoro huo. 
Utata Kitalu namba 33 kilichotwaliwa na Kampuni ya Maungu Seeds
PSRC iliingia makubaliano na kampuni ya Maungu Seeds, kwa ajili ya kununua kiwanda cha Mzizima Maize Mill kilichopo Kitalu namba 33, Barabara ya Saza katika Eneo la Viwanda Chang’ombe jijini Dar es Salaam. 
Makubaliano hayo yalitiwa saini Septemba 1, 2004; na gharama ya ununuzi ilikuwa Sh milioni 620. Malipo yalikuwa yafanywe kwa awamu tatu. Maungu ikaanza kulipa Sh milioni 200 na kutoa dhamana ya benki (TIB) ya Sh milioni 420. 
Ikakubaliwa kuwa PSRC ingeikabidhi kampuni ya Maungu kiwanda hicho ndani ya miezi mitatu baada ya kutiliana saini ya ununuzi, na kwamba Maungu ingekabidhiwa nyaraka zote baada ya kukamilisha malipo. Iliyokuwa PSRC ikashindwa kukabidhi kiwanda kwa mujibu wa makubaliano kwenye mkataba kutokana na kwamba, kiwanda kilikuwa rehani kwa kampuni ya CDC London ya Uingereza tangu mwaka 1959. 
Hatimaye, ilipofika Aprili 26, 2006 rehani ikawa imeondolewa, lakini tayari muda wa dhamana ya benki ulikuwa umekwisha. Kiasi cha Sh milioni 420 kikawa hakijalipwa. Mwaka 2010 kampuni ya Maungu ikafungua kesi ya madai na ikaamuriwa kuwa ipewe hati ya eneo yenye namba 6639. PSRC (CHC) ikaamuriwa iilipe Maungu Sh milioni 200 haraka. Fedha hizo ni zilezile ilizokuwa imetoa kama malipo ya awali na ikarejeshewa. 
Kimsingi, Maungu ikawa haijalipa chochote, lakini ikawa imepewa kiwanda cha Mzizima bure kabisa bila kulipa kiasi chochote kwa mali hiyo ya umma. 
Madeni ya Simu 2000 yafutwa kienyeji
CAG ameonyesha wasiwasi mkubwa kwa uamuzi wa CHC wa kufuta madeni mengi ya iliyokuwa kampuni ya Simu 2000. Kampuni hiyo iliundwa na kuongozwa na familia ya Mama Anna Mkapa, kwa ajili ya kuuza zilizokuwa mali za Shirika la Posta na Simu. Kuna habari kwamba familia hiyo ilijitwalia mali kadhaa zenye thamani ya mabilioni ya shilingi. Miongoni mwa majengo yaliyouzwa ni maghorofa yaliyopo Ilala. 
Ulaji Chuo cha Ubaharia (DMI)
Ukaguzi uliofanywa na CAG umebaini kuwa Sh milioni 83.96 zimelipwa kama takrima na fedha za kujikimu kwa viongozi bila kuidhinishwa na mamlaka za kisheria. Katika malipo hayo, maofisa wa Wizara ya Mawasiliano walilipwa Sh milioni 12; na Sh milioni 51.8 zililipwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la DMI kama posho ya madaraka (honorarium), mafuta na posho ya vikao. 
Sh milioni 2.6 zililipwa kwa maofisa wa akaunti wa DMI bila wao wenyewe kuhudhuria vikao; Sh. milioni 10.4 zililipwa kwa watumishi wa DMI kama posho ya kujikimu Juni, 2009 bila wenyewe kuhudhuria kile kilichoitwa kuwa ni kikao cha kikosi kazi cha kupitia mitaala ya DMI. 
Katika hatua nyingine, DMI ilipokea Sh milioni 385 kwa ajili ya kuwalipa wadeni wake, lakini ukaguzi umebaini kuwa ni 205.8 pekee zilizotumika. Wafanyakazi 12 wa DMI wamelipwa mishahara ya ngazi ya PGSS 5 na zaidi bila kuidhinishwa na Baraza DMI. Aidha, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala amekuwa akijilipa mshahara kwa kiwango cha PHTS ambacho hakikuidhinishwa. 
Kompyuta za msaada zaibwa, zanyofolewa vifaa
Ukaguzi umebaini kuwa Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, kilitoa msaada wa kompyuta 25 kwa DMI kwa ajili ya maktaba yake. DMI ilimlipa wakala wa utoaji vifaa hivyo bandarini Sh milioni tatu Desemba 7, 2007. Lakini hadi ukaguzi unafanywa, kompyuta hizo zilikuwa hazijawasilishwa kama ilivyotarajiwa. 
Baadaye imebainika kuwa kati ya kompyuta hizo, ni kompyuta 13 pekee zilizowasilishwa katika maktaba, na kwamba ni kompyuta nne pekee zinazoweza kukarabatiwa. Kompyuta kenda haziwezi kutengenezwa kutokana na kuibwa vifaa muhimu kama Ram, Processors, Hard disks, Power Supply na Mother Boards. 
Bohari ya Dawa (MSD) inaingiza vifaa feki
Pamoja na kuwapo upotevu wa mamilioni ya shilingi zinazotolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, CAG amebaini kuwa baadhi ya vifaa na dawa vinavyosambazwa na MSD havina ubora. Ametoa mfano wa mashine za kupima shinikizo la damu na vifaa vinavyotumika kubebea wagonjwa. 
Pia dawa kama kwinini imebainika kuwa inasambazwa nyingine ikiwa na ubora wa hali ya chini, kutokana na pengine kutohifadhiwa vizuri. Aidha, ukaguzi umebaini kuwa vitambaa vinavyotumika kunyonya damu wakati wa upasuaji huwa vipo chini ya kiwango. 
Ukaguzi umebaini kuwa Sh bilioni 3.95, dola milioni 9.4 na euro milioni 1.5 ambazo zimetumika bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya MSD na hivyo kukiuka Sheri ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni 41 ya Tangazo la Serikali namba 97. 
Aidha, imebainika kuwa MSD imefanya ununuzi kwa zabuni nane huku upitiaji wa zabuni hiyo ukifanywa na mtu mmoja, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Zabuni zilizofikwa na hali hiyo ni za Sh milioni 134.4, dola 10,000 na Euro milioni 1.5. 
Ulaji wa kutisha Bandari ya Dar es Salaam
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliingia mkataba na kampuni ya Singapore PTE Limited kwa ajili ya kuweka ‘Radio Data Terminals’ Februari 2010 wenye thamani ya dola 339,600. Punde tu baada ya TPA kupata radio hizo, mambo kadhaa yalianza kujitokeza. 
Kwanza, menejimenti ikabaini kuwa ‘Radio Data Terminals’ hizo  haziwezi kufanya kazi bila kile kinachoitwa kitaalamu kuwa ni ‘Access Points’ (virusha mawimbi). Hatua hiyo ikaifanya PTA iingie mkataba mwingine na Singapore PTE Limited Juni 21, 2010 kwa ajili ya kuweka virusha mawimbi 68 kwa gharama ya dola 399,000. Baada ya kununua vifaa hivyo, ikabainika tena kwamba haviwezi kufungwa juu minara ya iliyokuwapo. Kwa sababu hiyo, PTA ikaingia mkataba mwingine na CATS (T) Limited Septemba 17, 2010 kwa ajili ya kuweka minara mingine kwa gharama ya dola 133,000. 
CAG anasema katika ukaguzi wake kwamba pamoja na kufanya yote hayo, bado ‘Radio Data Terminals’ hazikuweza kufanya kazi kama ilivyokusudiwa, kwa vile ilipaswa iunganishwe kwenye mkongo (fibre optic) kwa gharama ya dola 553,800 za Marekani. Kazi hiyo ikafanywa na EMEC. 
Kwa kifupi, TPA ikajiingiza kwenye gharama za ziada za dola milioni 1.09 na bado kilichokusudiwa hakikuweza kupatikana kwa muda kutoka kwa mkandarasi aitwaye CATS. Hakuna gharama zozote ambazo TPA imeweza kuzidai kutokana na kucheleweshwa au kuingia gharama kubwa kiasi hicho. Hii inatiliwa shaka kuwa ndiyo ulaji wenyewe. 
Sh milioni 100 zaliwa bila jengo la bosi TPA
TPA iliingia mkataba na kampuni ya AF MULT-CON LIMITED kujenga makazi ya Meneja wa Bandari Tanga kwa gharama ya Sh milioni 500. Utangazaji zabuni umebainika kuwa ulifuata taratibu zote. Hata hivyo, CAG amebaini kuwa kuna uzembe katika kufuatilia taratibu za mkataba wa zabuni. CAG mwenyewe alizuru eneo lililokusudiwa kujengwa jengo hilo, na hakushuhudia malighafi wala shughuli yoyote ya kuhalalisha malipo ya Sh milioni 100 ambazo tayari mzabuni alishalipwa. 
Mkataba mwingine wa utata TPA
Wakati wa ukaguzi, CAG alibaini kuwa TPA iliingia mkataba na kampuni ya Chibeshi Construction kwa ajili ya kujenga uzio katika kitalu namba moja kwenye Bandari ya Mtwara. Mkataba huo ulikuwa na thamani ya Sh milioni 679.8. Ulitiwa saini Aprili 14, 2009 na ujenzi ulipaswa ukamilike kwa wiki 26 kutoka siku ya kutiwa saini mkataba. 
Kabla ya mkandarasi kuanza ujenzi, TPA ikaamua kuvunja mkataba huo kwa maelezo kwamba hapakuwapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Uamuzi huo ukaifanya TPA iingie hasara ya Sh milioni 92.6 kama adhabu au faini. Ikamlipa mkandarasi. Fedha zikachukuliwa na mkandarasi bila kufanya kazi yoyote. 
Mkataba mwingine wa utata waingiza hasara TPA
Katika ukaguzi, CAG amebaini kuwa PTA iliingia mkataba na kampuni ya WiA kwa ajili ya kuweka mawasiliano ya intaneti katika Makao Makuu ya TPA, na bandari nyingine zilizo chini ya Mamlaka hiyo. Mkataba huo ulikuwa wa miezi mitatu kuanzia Julai 2010. Hata hivyo, mradi huo haukukamilika baada ya muda uliopangwa kumalizika. TPA ikaamua kumwongeza mkandarasi muda hadi Februari 28, 2011 na mkandarasi bado alishindwa. TPA ilipaswa kumtoza mkandarasi kiasi cha dola 95,000 kwa kushindwa kutekeleza mkataba kwa muda, lakini haikufanya hivyo. 
Hazina yalipa mamilioni ya mishahara hewa
Wakati wa ukaguzi, CAG amebaini kuwa Hazina imeendelea kutumia mamilioni ya shilingi kuwalipa wafanyakazi hewa katika taasisi mbalimbali. Katika ukaguzi huo, imebainika kuwa Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE) kumekuwa na majina 42 ya watu wanaolipwa mishahara licha ya ukweli kwamba si watumishi wa chuo hicho. Imebainika kuwa kuanzia Oktoba 2009 hadi Juni, 2010 MUCE ilipokea Sh milioni 612 na kuwalipa watumishi hewa. 
Katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Hazina imeendelea kuwalipa mishahara watu ambao si watumishi chuoni hapo. Baadhi ya waliostaafu na MNMA kupeleka majina yao Hazina, wanaendelea kulipwa. Hali hiyo imesababisha Sh milioni 134.74 zitumike kuwalipa watu ambao si watumishi katika chuo hicho. Fedha hizo hazikurejeshwa Hazina. 
Katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, orodha ya majina kutoka Hazina inaonyesha kuwa hata wale ambao si watumishi tena wa chuo hicho, majina yao yapo kwenye orodha ya wanaostahili kulipwa mishahara. Kuanzi Oktoba 2010, Machi 2011, Mei 2011 na Juni 2011 Sh milioni 194.4 zimetumika kuwalipa watu ambao si watumishi katika chuo hicho. 
Imebainika pia kwamba baadhi ya watumishi waliojiuzulu au kuacha kazi katika Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), majina yao yameendelea kuwa kwenye orodha ya Hazina ya watumishi wanaopaswa kulipwa. Sh milioni 181 zilikuwa zimetumika kuwalipa hadi wakati ambao CAG alikuwa akiandaa ripoti hii. 
Katika Chuo cha Elimu Dar es Salaam nako mambo ni kama hayo. Watu 56 ambao hawapo kwenye utumishi wameweza kulipwa Sh milioni 778.7 licha ya ukweli kwamba hawapo chuoni hapo. Hakuna rekodi inayoonyesha kuwa fedha hizo zilirejeshwa Hazina. 
Fedha za Mifuko ya Jamii hatarini
Ukaguzi umebaini kuwa upo udhaifu mkubwa na hatari ya kupotea kwa mabilioni ya shilingi zilizowekezwa na Mifuko ya Jamii katika miradi mbalimbali nchini. 
Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetumia Sh bilioni 234.054 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Kati ya fedha hizo, ni Sh bilioni 35.218 pekee ambazo zilisainiwa katika ujenzi wakati wa awamu ya kwanza. Fedha zilizotolewa katika ujenzi wa awamu ya pili, hazikusainiwa. Majengo ya awamu ya kwanza yamekamilika, lakini Serikali haijaanza kurejesha fedha inazodaiwa na NSSF zenye riba ya Sh bilioni 14.157. 
Wabunge waondolewe kwenye Bodi
Kwa mara nyingine, CAG amependekeza wabunge wasiwemo kwenye Bodi za Mashirika ya Umma na bodi nyingine. Anasema mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba kuwamo kwao kwenye bodi husababisha mgongano wa masilahi. 
Anasema ni Tanzania pekee ambayo wabunge ni wajumbe katika bodi za mashirika ya aina hiyo. Utaratibu kama huo haupatikani mahali kwingineko duniani wala katika vyombo ambavyo Tanzania ni mwanachama. 
Uteuzi wa wajumbe wa Bodi
CAG anatoa mapendekezo kwamba maofisa watendaji wakuu wa kampuni/mashirika ni vizuri wakateuliwa na Bodi za Wakurugenzi badala ya utaratibu wa sasa, ambako ni Rais anayewateua. Anapendekeza Rais aachiwe madaraka ya kuteua mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi. 
Mapendekezo hayo, kwa mujibu wa CAG, yanalenga kuifanya Bodi ya Wakurugenzi iweze kuisimamia vema menejimenti na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa. 

Serikali ibane ununuzi mashangingi
CAG anapendekeza kuwa ili fedha nyingi zielekezwe kwenye maendeleo, Serikali haina budi kuweka utaratibu madhubuti wa kudhibiti matumizi hasa kwenye ununuzi wa magari ya kifahari, gharama za semina na kupunguza idadi ya wanaosafiri kwenye misafara ya viongozi ndani na nje ya nchi.


5 May 2009


Ikulu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Makamu wa Rais, Polisi, Msajili wa Vyama vya Siasa na Sekretarieti ya Maadili ni kati ya ofisi ambazo, mahesabu yake yalionekana kuwa na mapungufu na kutofuata kanuni za fedha au kufanya malipo yenye nyaraka pungufu.
Mapungufu hayo yamo kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Serikali (CAG) kwa mwaka 2007/08 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita.

Kutokana na mapungufu hayo, ripoti ya CAG inaonyesha kwamba ofisi hizo, licha ya kupewa hati ya ukaguzi inayoridhisha, kila hati imeambatana na mambo ya msisitizo yenye kuzitaka ofisi hizo zisirudie makosa hayo.

Ripoti hiyo inafafanua: ``Kimsingi, aya inayohusu `Mambo ya Msisitizo` ni tahadhari kwa Afisa Masuuli na taarifa muhimu kwa watumiaji wa taarifa za fedha. Vivyo hivyo, kama udhaifu huo haujarekebishwa, unaweza kusababisha hati isiyoridhisha (kutolewa) kwa kaguzi zijazo.``

Ofisi nyingine zilizopewa hati yenye mambo ya msisitizo ni Magereza, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) (Ngome), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Kimataifa, Ofisi ya Rais na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko na Wizara ya Ardhi na Makazi.

Zingine ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Fedha na Uchumi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Tume ya Mipango, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya, Tume ya Utumishi wa Umma na Tume ya Kudhibiti Ukimwi.

Vilevile zipo sekreterieti za mikoa kadhaa kama vile Arusha, Mara, Iringa, Kigoma, Pwani, Kilimanjaro, Mbeya, Singida, Morogoro, Shinyanga, Kagera, Dar es Salaam na Rukwa ambazo zilipata hati inayoridhisha yenye msisitizo.

Kuhusu Ikulu, kwa mfano, ripoti ya CAG inaonyesha katika mwaka wa fedha 2007/08 hakukuwa na mpango wa mwaka wa manunuzi, kinyume na kifungu cha 45 (a) hadi (e) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Pia mahesabu ya Ikuku yalikuwa na mambo yasiyosuluhishwa katika taarifa za benki, yanayofikia Sh. 2,710,000.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanya malipo yenye nyaraka pungufu yanayofikia Sh. milioni 21.8 na malipo yaliyolipwa mara mbili yenye thamani ya sh. milioni 45.

Idara ya Mhasibu Mkuu imeelezwa kufanya malipo yanayofikia sh. milioni 570 kwa M/s Fifth Africa Population bila nyaraka ambatanifu, huku mishahara yenye thamani ya Sh. milioni 8.6 ikilipwa kwa watu walioondoka kwenye utumishi wa umma.

Kwa upande wa ofisi ya Makamu wa Rais, malipo ya madeni ya Sh milioni 89.2 yalifanyika kwenye bajeti ya mwaka huu bila idhini huku stakabadhi za kukiri malipo ya Sh. Milioni 8.9 zikishindwa kuwasilishwa ili kukaguliwa. Pia ofisi inalaumiwa na CAG kwa kufanya manunuzi ya Sh milioni 20.8 kutoka kwa M/s Colour Print (T) Ltd bila kufanya ushindani wa zabuni.

Kuhusu jeshi la polisi, ipo milolongo kadhaa ya makosa ya kihasibu, lakini moja wapo ni malipo ya Sh. milioni 74.1 kufanywa bila nyaraka sahihi na masurufu yasiyorejeshwa kufikia sh. milioni 131.

Ofisi zilizopewa hati yenye shaka ni pamoja na ya Bunge, Wizara za Kilimo, Chakula na Ushirika, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mambo ya Ndani, Jinsia na Maendeleo ya Watoto, Nishati na Madini, Maliasili na Utalii, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Miundombinu.

Sekretareti za mikoa zilizopewa hati yenye shaka ni Dodoma, Lindi, Mtwara, Mwanza, Ruvuma, Tabora na Tanga. Pia kwenye kundi hilo imo Mahakama ya Ardhi.

Ufafanuzi wa ofisi ya CAG unaonyesha kwamba hati zenye shaka hutolewa pale kunapokuwa na udhaifu wenye uzito na unaoathiri taarifa za fedha lakini hausababishi taarifa hizo kukosa maana kabisa.

Taarifa inasema Bunge lilipewa hati yenye shaka kutokana na mlolongo wa makosa ya kanuni za fedha ikiwa ni pamoja na kulipa matibabu ya Sh. Milioni 102 nje ya nchi bila kuidhinishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Ofisi zilizopewa hati isiyoridhisha, kwa mujibu wa ufafanuzi, udhaifu unaojitokeza unapotosha kabisa tarifa za hesabu ni pamoja na Wizara ya Kazi, Idara ya Uhamiaji na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Wizara hiyo katika ripoti hiyo inaonyesha kulikuwa na upotevu wa Sh. milioni 90.9 na taarifa za masurufu yasiyorejeshwa ilikuwa inatofutiana.

CHANZO: NipasheCategories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube