Showing posts with label UBADHIRIFU. Show all posts
Showing posts with label UBADHIRIFU. Show all posts

15 Jan 2013


Haya ndio matokeo ya kumkabidhi mtu mbabaishaji kuongoza nchi.Naam,namzungumzia Rais Jakaya Kikwete.Wengi wanaomfahamu vizuri wanatambua kwanini nchi yetu inazidi kupoteza mwelekeo.Majambazi waliojivika joho la uongozi wanazidi kufilisi nchi yetu, Na sasa kila Mtanzania amebebeshwa deni la takriban shilingi laki tano kila mmoja kutokana na zigo zito la misumari la deni la ndani la taifa la shilingi 22,000,000,000,000 (TRILIONI 22). Na hilo ni deni la NDANI TU.

Wakati tunakabiliwa na mzigo huo wa deni hilo kubwa,serikali ya Kikwete imelipa takriban SHILINGI MILIONI 100 kugharamia makazi ya Naibu Waziri wa Uchukuzi Dkt CHARLES TIZEBA (Ni muhimu kujikumbusha Waziri KAMILI wa Uchukuzi ni yule anayetajwa kama kuwa mfano wa viongozi safi wachache ndani ya CCM, Dkt Harrison Mwakyembe).

Uchunguzi wa gazeti la Kiingereza la Guardian umefukua uhuni huo unaotokea katika Hoteli ya Kitalii ya New Africa jijini Dar,ambapo gharama za makazi ya Dkt Tizeba zimeendelea kuchajiwa hata pale anapokuwa nje ya jiji la Dar.

Gharama za malazi katika hoteli hiyo zinaangukia katika makundi matatu: vyumba vya kawaida dola 160 kwa usiku mmoja; vyumba vya klabu dola 180 kwa usiku mmoja; na vyumba maalumu (suites) dola 300 kwa usiku mmoja.Dkt Tizeba anaishi kwenye chumba maalumu (suite) lakini hoteli hiyo imekubali kupunguza gharama hadi dola 250 kwa usiku mmoja.

Hadi kufikia Jumamosi iliyopita (Januari 12, 2013) Naibu Waziri huyo angekuwa ameishi hotelini hapo kwa sangalau siku 247,na hivyo kufanya gharama za malazi yake hotelini hapo kufikia dola 61,750 (sawa na SHILINGI MILIONI 98.8)

Hata hivyo jumla hiyo ni ya malazi na kifungua kinywa tu ( bed and breakfast), ikimaanisha kuwa gharama za jumla zinaweza kuwa kubwa zaidi ikijumlishwa na zile za mlo,ambapo mlo mmoja (buffet) unagaharimu angalau shilinhi 21,000.

Kadhalika,kwa vile Naibu Waziri huyo ana familia,gharama hizo zinaweza kuwa kubwa zaidi.Hivi karibuni Naibu Waziri Tizeba alitembelewa na wanawe wawili walioishi hotelini hapo kwa zaidi ya wiki kwa gharama ya dola 100 kwa kila usiku.

Alipotafutwa na gazeti hilo,Dkt Tizeba ambaye ni Mbunge wa jimbo la Buchosa kupitia CCM, alishauri suala hilolielekezwe kwa mamlaka zinazohusika na makazi ya mawaziri na viongozi wengine wa umma.

"Siwezi kujipangia makazi mie mwenyewe...kuna mamlaka zenye jukumu hilo,kwahiyo tafadhali ongea nao na upate tamko rasmi.Hata hivyo,vyanzo vya gazeti hilo vimeeleza kuwa gharama za makazi ya Naibu Waziri huyo hotelini hapo zinabebwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Hta hivyo,Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Paniel Lyimo alikataa kuzungumzia suala hilo,hususan haja ya kupunguza gharama kwa kumpatia Dkt Tizeba makazi ya kudumu badala ya kuishi hotelini na hivyo kuongeza gharama.

Katibu huyo Mkuu alimtaka mwandishi kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), akidai maongezi kwenye simu hayakuwa sawia.Lakini masaa mawili baadaye,mwandishi alipokea ujumbe kutoka kwa mtu aliyedai kuwa ni Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo akisema:

"Kuhusu taarifa ulizokuwa ukisaka kutoka kwa Lyimo,Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, ningependa kukufahamisha kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi ameshapangiwa nyumba kitambo sasa."

Hata hivyo kuna taarifa kuwa Dkt Tizeba amekataa kuhamia kwenye nyumba hiyo,ambayo awali ilikuwa ikitumiwa na mtangulizi wake, Athuman Mfutakamba. kwa madai kuwa "haiendani na hadhi yake."

Lakini alipotakliwa kutoa msimamo wake, Dkt Tizeba 'aliponda' tuhuma hizo akidai zinasambazwa na maadui zake.ambao walikuwa wakipambana na harakati za Wizara yake kuweka mambo sawa (kupambana na ufisadi).

Gazeti hilo limepata taarifa kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, naye aliishi hotelini hapo kwa angalau miezi miwili baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

HII NDIO SERIKALI YA RAIS KIKWETE AMBAYO IAN DENI LA NDANI LA SHILINGI TRILIONI 22 NA DENI LA NJE (HADI KUFIKIA AGOSTI MWAKA JANA) LA DOLA BILIONI 10.35 (SHILINGI 16,050,000,000,000),YAANI ZAIDI YA SHILINGI TRILIONI 16.KWAHIYO KIMSINGI JUMLA YA DENI LA NDANI NA LA NJE NI TAKRIBAN SHILINGI TRILIONI 40 (40,000,000,000,000) AMBALO LINAMFANYA KILA MTANZANIA KUDAIWA TAKRIBAN SHILINGI MILIONI MOJA KILA MMOJA (NI WASTANI WA SHS 888,888,.89 )

LAKINI LICHA YA UZITO WA DENI HILO BADO SERIKALI YA KIKWETE HAIJALI KUMLIPIA NAIBU WAZIRI TAKRIBAN SHILINGI MILIONI 100 KWA MAKAZI YA HOTELINI (MNAZIKUMBUKA ZILE NYUMBA ZA MAWAZIRI PALE VICTORIA JIRANI NA KAMBI YA USALAMA WA TAIFA NA HOSPITALI YA KAIRUKI?)

SIJUI HALI YA NCHI YETU ITAKUWAJE HAPO 2015 KIKWETE ATAKAPOONDOKA MADARAKANI.ILA MOJA LILILO WAZI NI KUWA DENI HILI LA MATRILIONI YA SHILINGI LITAKUWA LIMEZALIANA KWA KASI PENGINE ZAIDI YA KASI YA KUZALIANA KWA MAFISADI HUKO NYUMBANI.



5 May 2009


Ikulu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Makamu wa Rais, Polisi, Msajili wa Vyama vya Siasa na Sekretarieti ya Maadili ni kati ya ofisi ambazo, mahesabu yake yalionekana kuwa na mapungufu na kutofuata kanuni za fedha au kufanya malipo yenye nyaraka pungufu.
Mapungufu hayo yamo kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Serikali (CAG) kwa mwaka 2007/08 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita.

Kutokana na mapungufu hayo, ripoti ya CAG inaonyesha kwamba ofisi hizo, licha ya kupewa hati ya ukaguzi inayoridhisha, kila hati imeambatana na mambo ya msisitizo yenye kuzitaka ofisi hizo zisirudie makosa hayo.

Ripoti hiyo inafafanua: ``Kimsingi, aya inayohusu `Mambo ya Msisitizo` ni tahadhari kwa Afisa Masuuli na taarifa muhimu kwa watumiaji wa taarifa za fedha. Vivyo hivyo, kama udhaifu huo haujarekebishwa, unaweza kusababisha hati isiyoridhisha (kutolewa) kwa kaguzi zijazo.``

Ofisi nyingine zilizopewa hati yenye mambo ya msisitizo ni Magereza, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) (Ngome), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Kimataifa, Ofisi ya Rais na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko na Wizara ya Ardhi na Makazi.

Zingine ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Fedha na Uchumi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Tume ya Mipango, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya, Tume ya Utumishi wa Umma na Tume ya Kudhibiti Ukimwi.

Vilevile zipo sekreterieti za mikoa kadhaa kama vile Arusha, Mara, Iringa, Kigoma, Pwani, Kilimanjaro, Mbeya, Singida, Morogoro, Shinyanga, Kagera, Dar es Salaam na Rukwa ambazo zilipata hati inayoridhisha yenye msisitizo.

Kuhusu Ikulu, kwa mfano, ripoti ya CAG inaonyesha katika mwaka wa fedha 2007/08 hakukuwa na mpango wa mwaka wa manunuzi, kinyume na kifungu cha 45 (a) hadi (e) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Pia mahesabu ya Ikuku yalikuwa na mambo yasiyosuluhishwa katika taarifa za benki, yanayofikia Sh. 2,710,000.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanya malipo yenye nyaraka pungufu yanayofikia Sh. milioni 21.8 na malipo yaliyolipwa mara mbili yenye thamani ya sh. milioni 45.

Idara ya Mhasibu Mkuu imeelezwa kufanya malipo yanayofikia sh. milioni 570 kwa M/s Fifth Africa Population bila nyaraka ambatanifu, huku mishahara yenye thamani ya Sh. milioni 8.6 ikilipwa kwa watu walioondoka kwenye utumishi wa umma.

Kwa upande wa ofisi ya Makamu wa Rais, malipo ya madeni ya Sh milioni 89.2 yalifanyika kwenye bajeti ya mwaka huu bila idhini huku stakabadhi za kukiri malipo ya Sh. Milioni 8.9 zikishindwa kuwasilishwa ili kukaguliwa. Pia ofisi inalaumiwa na CAG kwa kufanya manunuzi ya Sh milioni 20.8 kutoka kwa M/s Colour Print (T) Ltd bila kufanya ushindani wa zabuni.

Kuhusu jeshi la polisi, ipo milolongo kadhaa ya makosa ya kihasibu, lakini moja wapo ni malipo ya Sh. milioni 74.1 kufanywa bila nyaraka sahihi na masurufu yasiyorejeshwa kufikia sh. milioni 131.

Ofisi zilizopewa hati yenye shaka ni pamoja na ya Bunge, Wizara za Kilimo, Chakula na Ushirika, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mambo ya Ndani, Jinsia na Maendeleo ya Watoto, Nishati na Madini, Maliasili na Utalii, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Miundombinu.

Sekretareti za mikoa zilizopewa hati yenye shaka ni Dodoma, Lindi, Mtwara, Mwanza, Ruvuma, Tabora na Tanga. Pia kwenye kundi hilo imo Mahakama ya Ardhi.

Ufafanuzi wa ofisi ya CAG unaonyesha kwamba hati zenye shaka hutolewa pale kunapokuwa na udhaifu wenye uzito na unaoathiri taarifa za fedha lakini hausababishi taarifa hizo kukosa maana kabisa.

Taarifa inasema Bunge lilipewa hati yenye shaka kutokana na mlolongo wa makosa ya kanuni za fedha ikiwa ni pamoja na kulipa matibabu ya Sh. Milioni 102 nje ya nchi bila kuidhinishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Ofisi zilizopewa hati isiyoridhisha, kwa mujibu wa ufafanuzi, udhaifu unaojitokeza unapotosha kabisa tarifa za hesabu ni pamoja na Wizara ya Kazi, Idara ya Uhamiaji na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Wizara hiyo katika ripoti hiyo inaonyesha kulikuwa na upotevu wa Sh. milioni 90.9 na taarifa za masurufu yasiyorejeshwa ilikuwa inatofutiana.

CHANZO: Nipashe



Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.