2 Aug 2013
20 Jul 2010
3 Mar 2010
Meela alisema serikali inahitaji sera na mikakati iliyojengwa na matokeo ya tafiti kama hizo kufanya gharama za maisha ziwe nafuu kwa kila mtu.
Utafiti huo ulihusisha sampuli nasibu za idadi ya watu 2,000 waliopatikana katika mikoa yote 21 ya Tanzania Bara, na visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema matokeo ya sampuli hizo yalipangwa katika jedwali na kufanyiwa upembuzi uliozingatia makadirio ya idadi ya watu milioni 40 nchi nzima ili kupata takwimu zilizokaririwa katika ripoti hiyo.
Utafiti huo umebainisha kuwa rushwa na umaskini ni matatizo yanayowaathiri zaidi wanaume kuliko wanawake.
CHANZO: Tanzania Daima
20 Jun 2009
Na Mwandishi Wetu
IKIWA imesalia takriban miezi 18 kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwakani, sasa ni dhahiri kuwa Rais Jakaya Kikwete ana kibarua kigumu cha kukamilisha ahadi lukuki alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Mazingira hayo pia yanawaweka njiapanda wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kutetea tena nafasi zao.
Baadhi ya wabunge tayari wameliona hilo na miongoni wamelisema bungeni wakiwashutumu mawaziri ambao wamekuwa wakilimbikiza miradi ya maendeleo kwa upendeleo kwenye maeneo yao bila kuzingatia vipaumbele vya taifa, hata baadhi yao walifikia hatua ya kutishia kukwamisha bajeti iliyopitishwa Alhamisi iliyopita.
Kauli kali zaidi ilitoka kwa Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii aliyeomba dua kwa Mungu awalaami mawaziri hao.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, ahadi kadhaa alizozitoa Rais Kikwete bado hazijatekelezwa na kwa kipindi kilichosalia ni vigumu kufanya hivyo.
Miongoni mwa ahadi alizotoa Rais Kikwete na hazijaonekana matunda yake dhahiri ni zile zilizoandamana na kaulimbiu yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya na mpango wa ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’.
Kigogo mmoja ndani ya CCM amelieleza gazeti hili kwamba ahadi hiyo ya maisha bora ndiyo ilimpatia Kikwete kura za kishindo na isipotengenezewa mkakati maalumu inaweza kuwa ndio kitanzi chake na wabunge wengi wa CCM.
Alisema ahadi hiyo imesababisha baadhi ya vigogo wa chama na serikali kubadili kauli, na kusema kwamba maisha bora hayatawafuata wananchi kama hawafanyi kazi kwa bidii.
Kwa mujibu wa watu mbalimbali waliozungumza na Mwananchi Jumapili, na hata kauli za wabunge wanapochangia bungeni, Watanzania walio wengi bado wana hali duni ya kimaisha, jambo ambalo litakuwa gumu kulieleza kwa wapigakura hapo mwakani.
Kutokana na ahadi hiyo serikali ilitoa Sh30 bilioni ambazo zilipewa jina la mabilioni ya Kikwete, lakini hazikufika kwa maskini walio wengi kutokana na masharti yake kuwa magumu, na kuangukia kwenye mikono ya wasio wajasiriamali wadogo, hivyo kukwamisha mpango huo wa rais.
Ahadi nyingine zinazoelekea kushindikana ni ya mwafaka wa kisiasa wa Zanzibar ambao Rais Kikwete aliuweka kwenye kipaumbele, lakini hadi sasa hakuna mafanikio yoyote na tayari Chama cha Wananchi (CUF), kimetangaza kujitoa katika mazungumzo.
Ahadi nyingine ni ujenzi wa madaraja ya Kilombero mkoani Morogoro na Kigamboni, jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa ahadi kubwa alizotoa Kikwete na hadi sasa hakuna dalili zinazoweza kuashiria kuwa ipo nia ya utekelezaji.
Hata hivyo, Waziri wa Miundombinu, Dk Shukuru Kawambwa alipoulizwa alisema kwamba daraja la Kilombero limetengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2009/10.
Kuhusu daraja la Kigamboni, alirudia kauli za muda mrefu kuwa hilo limo kwenye mkakati wa kuanza kujengwa wakati wowote chini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali.
Ahadi nyingine ambazo hazijatekelezwa, zimeelezwa kuwa ni kilio cha mahakama nchini juu ya suala la masilahi ya watumishi na vifaa vya kazi.
Hivi karibuni, Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan alisikika akilalamika kuwa kiwango cha mafungu yanayoahidiwa kutengwa kwa mahakama hufika kwao kikiwa pungufu.
Suala jingine limeelezwa kuwa ni uboreshaji wa mashirika ya umma ambayo bado yako mikononi mwa serikali, lakini kila kukicha yamekuwa na matatizo na kuzua malalamiko mengi.
Kwa upande wa barabara ambazo ziliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na ambazo bado ni Tabora-Nzega, Bunda-Ukerewe na Marangu-Mkuu Rombo-Tarakea-Kamwanga.
Aliahidi pia kulifanya jimbo la Rorya mkoani Mara kuwa wilaya, lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua.
Mambo mengine ilikuwa ni kupambana na rushwa, lakini pamoja na hali hiyo kuonekana kuzaa matunda kwa mambo mengi yaliyokuwa yamejificha kuchimbuliwa na kuwekwa hadharani, malalamiko yanayoibuka ni baadhi ya watuhumiwa kutofikishwa mahakamani.
Rais Kikwete pia aliahidi kuondoa kero nyingi za Muungano lakini licha ya kuunda kamati ya kuzijadili na kuzishughulikia chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, zipo dalili za baadhi ya wananchi kutoridhika.
Tatizo kubwa linalojitokeza ni baadhi ya Wazanzibari, wakiwamo viongozi wa SMZ kutoa kauli zinazoonyesha dalili za waziwazi kwamba wanadhulumiwa ndani ya Muungano.
Pamoja na hali hiyo, Rais Kikwete atajivunia kwa kutekeleza ahadi yake ya kulifanya Bunge kuwa huru kwani limeonyesha dhahiri kuwa na meno kwa kufichua udhaifu wa baadhi ya vigogo serikali bila kuwa na woga.
Ameonyesha mafanikio pia katika ahadi yake ya kuendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu.
Hata hivyo, katika kipengele hicho kuna manung’uniko kadhaa kama vile baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kuendelea na nyadhifa zao wakati taratibu za utumishi wa umma ziko wazi kwamba wangepaswa kusimamishwa au kupewa likizo ama kuhamishiwa sehemu nyingine, ili uchunguzi huru ufanyike.
Mafanikio mengine ni kutekeleza ahadi ya kuongeza nafasi za elimu ya juu baada ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Ahadi nyingine ambayo Rais Kikwete ameonekana wazi kuivalia njuga ni kuboresha kilimo; na tayari mikakati kadhaa ikiwepo ya pembejeo za kilimo imewekwa, ingawa kuna malalamiko ya pembejeo kutofika kwa wakulima na wakulima wa karafuu na kahawa kutokuwa huru kutafuta masoko yao nje ya nchi.
Nguvu kubwa ya serikali yake kuielekeza kwenye kilimo imechagizwa na mtikisiko wa uchumi duniani ambao umetishia uchumi wa nchi nyingi hasa maskini ambazo zinategemea chakula kutoka nje.
Licha ya mafanikio hayo, serikali ya Kikwete inakabiliwa na changamoto kadhaa hasa za wananchi kutoridhika na mambo mbalimbali yanayotendwa na serikali yake.
Lingine ni wananchi kuona kuwa bado serikali ina matumizi makubwa ya fedha na wakati huo huo inawabidi kufunga mkanda ili kuihudumia huku wakikabiliwa na mazingira magumu ya kipato.
Malalamiko mengine ni baadhi ya watendaji serikalini kuendelea kutumia magari ya kifahari na kutenga Sh19 bilioni kwa ajili ya chai maofisini.
22 Mar 2009
15 Oct 2008
Wanakijiji Ichonde wakimbia makazi
BAADHI ya wanakijiji cha Ichonde wilayani Kilombero, Morogoro, wamedaiwa kukimbia makazi yao kutokana na mateso ya viongozi wa kijiji hicho .Kwa nyakati tofauti wanakijiji hao walizungumza na Tanzania Daima, wakilalamikia mateso na fedheha wanazofanyiwa na viongozi wao wanapolazimishwa kuchangia elimu.
Haji Kawogo, mkazi wa Ichonde, alisema uongozi wa kijiji hutumia mgambo wa vijiji vingine kuwakamata nyakati za usiku, kuwafunga kamba na kuwaweka kwenye moja ya madarasa ya shule ya msingi kijijini hapo.
Alisema, wanakijiji hao hulazimishwa kuchangia elimu huku viongozi hao wakishindwa kuitisha mikutano ya kijiji na kuwasomea mapato na matumizi kama inavyotakiwa.
“Viongozi wetu wanatudhalilisha hasa sisi wanaume maana usiku umelala na familia yako wanakuvamia tena kwa kuwatumia mgambo wa vijiji vingine.
“…Wanatutoa nje ya nyumba zetu usiku, wanatufunga kamba na kutulazimisha kulala sehemu moja ndani ya darasa la shule ya msingi Ichonde,” alisema Kawogo.
Naye Asha Hassan, alisema kukosekana kwa maendeleo ya Kijiji cha Ichonde, kunasababishwa na uongozi mbovu uliopo hivyo aliiomba halmashauri ya wilaya kuingilia kati, ili kunusuru ubabe wa viongozi hao.
“Kijiji cha Ichonde, tunakosa maendeleo kwa sababu ya viongozi wetu, hawatushirikishi katika bajeti ya kijiji wanachojua ni kukusanya michango, lakini hawatuelezi kiasi kilichopatikana wala matumizi yake,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji hicho Deogratias Makinda, akana tuhuma hizo na kueleza kwamba hana taarifa za kukamatwa, kufungwa kamba wala kulazwa katika shule ya msingi.
“Mimi sina dola ya kuwakamata wanakijiji, sina taarifa za wao kuteswa ndiyo kwanza nasikia hapa,” alisema mwenyekiti huyo.
Aidha, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ichonde, Salum Sadala, alikiri kwamba wapo wanakijiji wanaokamatwa na kupelekwa katika shule hiyo kwa lengo la kuhamasisha uchangiaji wa maendeleo ya kijiji.
13 Oct 2008
2008-10-13 10:24:10
Na Thobias Mwanakatwe, Kyela
Rais Jakaya Kikwete amesema kushuka kwa uchumi wa dunia hivi sasa ni lazima kutaathiri uchumi wa taifa, na hivyo hakuna sababu kwa wananchi kulaumu kwamba serikali inawatesa kutokana na hali ngumu ya maisha.
Akiwahutubia wananchi wa mji wa Kyela juzi, alisema hivi sasa uchumi wa dunia umekumbwa na msukosuko mkubwa kuliko yote katika historia toka mwaka 1930 ambapo hali hiyo haijawahi kujitokeza.
Alisema pamoja na kuwepo kwa msukosuko huo wa uchumi wa dunia, hata hivyo serikali bado haijaanza kujipanga kukabiliana na hali hiyo lakini baada ya miezi michache ijayo athari zitaanza kujitokeza.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema serikali inaendelea kutafakari ni jinsi gani itaikabili hali hiyo ili kusijitokeze athari zaidi katika uchumi.
Alisema hivi sasa kutokana na msukosuko wa uchumi, serikali ya Marekani imetenga Dola 700 bilioni kujaribu kuokoa mabenki yanayofilisika, mkakati ambao pia unafanywa na Uingereza,Ujerumani, Japan pamoja na nchi nyingine.
``Wenzetu wanao uwezo mkubwa wa kiuchumi sijui yakitufika sisi itakuwaje, tunaendelea kutafakari ili na sisi yatakapotukuta tufanye nini lakini siyo kazi rahisi,`` alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo hakuna sababu kwa wananchi kulalamika kuwa serikali inatutesa kwa sababu kushuka kwa uchumi wa dunia athari zake zinazikumba nchi maskini ikiwemo Tanzania.
CHANZO: Nipashe