30 Jul 2009


Kizitto Noya, Dodoma


SASA ni wazi kwamba sakata la Richmond limeingia katika hatua nyingine baada ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ofisi Rais kutangaza kwamba, Rais Jakaya Kikwete hahusiki kwa namna yoyote na kashfa hiyo ambayo inaendelea kulitikisa taifa kwa muda sasa.

Hatua ya Rais Kikwete kutotaka kuhusishwa na kashfa hiyo ya Richmond kunazidi kuibua maswali mengi kutoka kwa wananchi kwamba, ni nini hatima ya mjadala huo ambao unazidi kupamba moto kila kukicha nje na ndani ya Bunge.

Wakati Rais Kikwete akijivua kutoka katika sakata hilo, Kamati ya Nishati na Madini imetoa maazimio ya kupinga jinsi serikali inavyotekeleza maazimio ya Bunge kuhusu ripoti ya Richmond. Jana jioni Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilitoa taarifa ikimuepusha rais na kashfa hiyo.

"Tumepata kusema huko nyuma, na tunapenda kusisitiza kwa mara nyingine kuwa, Rais hana mkono katika Richmond na hata Ripoti ya Bunge iliyotolewa kufuatia uchunguzi katika suala hilo la Richmond, haikumhusisha Rais Kikwete," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa ya Ikulu, imetolewa huku Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba akidai kwamba, Rais Kikwete anahusika na Richmond kwa kuwa maamuzi yalifanyika chini ya serikali anayoiongoza.

Habari kutoka Dodoma zinadai kuwa kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wa maazimio ya Bunge kutaka maafisa wa serikali waliohusika kwa njia moja au nyingine na mchakato wa kampuni hiyo kupewa zabuni Tanesco, wachukuliwe hatua.

Kundi mojawapo la wabunge limeeleza kutoridhishwa na ripoti ya serikali iliyotolewa bungeni hivi karibuni kuwasafisha. Kundi hilo limepanga kumchukulia hatua kubwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ndiye kiongozi mkuu wa serikali bungeni, kutokana na kuwanusuru maafisa waliotuhumiwa kuhusika na kashfa hiyo.

Wakati kamati hiyo ikitoa msimamo huo, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikutana jana usiku katika Ukumbi wa Pius Msekwa kutafakari sakata hilo.

Ingawa tangazo la Mwenyekiti wa Bunge, Job Ndugai jana mchana halikueleza agenda za kikao hicho, vyanzo huru vya habari vililidokeza gazeti hili kuwa wabunge hao wangejadili ripoti ya Richmond na kuweka mkakati wa kuinusuru serikali.

Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini ambaye hakutaka kutajwa gazetini akihofia kuvunja Kanuni za Bunge kwa kutoa siri za vikao, alisema kamati haikuridhishwa na ripoti ya serikali hasa katika suala la kuwasafisha Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.

"Kamati haikubaliani na ripoti hiyo hasa pale iliposema Dk Hoseah na Mwanyika hawana hatia. Tumekuwa na vikao kwa siku mbili jana (juzi), leo (jana) na bado tunaendelea kesho (leo),”alisema.

Alisema mapendekezo ya kamati ya Bunge kuhusu Richmond yalijitosheleza kimaamuzi na serikali ilitakiwa kuyatekeleza tu na sio kuendesha uchunguzi mwingine.

"Uchunguzi ulishafanywa na Bunge, serikali ilitakiwa kutekeleza tu. Ilikuaje ifanye tena uchunguzi kwa muda zaidi ya ule uliopangwa na Bunge badala ya kufanya utekelezaji?" alihoji.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Shelukindo na Makamu wake, Dk Harrison Mwakyembe hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na simu zao za mikononi kutopatikana kabisa.

Mjumbe wa kamati iliyoundwa na Bunge kuchunguza suala la Richmond, Habib Mnyaa alikiri kuwa na taarifa ya kamati ya kisekta kukutana na kujadili ripoti hiyo, lakini akaeleza kuwa kikao hicho kilichokaa juzi na jana, kinamalizika leo.

"Kikao kimekuwapo, lakini hakijafikia maamuzi hayo unayosema," alisema Mnyaa akirejea hoja ya mwandishi wa habari aliyetaka kuthibitisha taarifa kwamba, kikao hicho kimejenga hoja ya kutokuwa na imani na serikali katika suala la Richmond.

Hata hivyo, habari nyingine zinadai kuwa kamati hiyo leo inatarajia kumweka kiti moto Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ili awaeleze ni kwanini serikali imeshindwa kutekeleza mapendekezo ya Bunge.

Hata hivyo, mjumbe mwingine, Lucas Selelii alilieleza gazeti hili kuwa vikao vyote vilivyojadili Richmond, vimemaliza kazi na kuwasilisha hoja zake kwa spika wa Bunge Samuel Sitta ambaye leo atatoa mwongozo bungeni.

"Mjadala wa Richmond umemalizika na mambo yote kesho (leo) yako hadharani. Kamati ya kisekta imekaa na kuandaa taarifa ambayo amekabidhiwa spika wa Bunge leo (jana). Kikubwa jamii ijue kwamba, kamati iko makini, haimwonei wala kumpendelea mtu," alisema Selelii.

Alipotakiwa kuthibitisha kama amepokea hoja za kamati hiyo kuhusu Richmond na kwamba ataruhusu mjadala wake bungeni leo, Spika Sita alisema: "Haijanifikia bado".

Alifafanua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini anatarajia kuwasilisha hoja za Kiwira na Richmond kesho, siku ambayo pia wenyeviti wa kamati za Miundombinu, Ardhi, Maliasili na Mazingira watawasilisha hoja zao.

Alibanwa zaidi aeleze kama endapo angeipata jana jioni angekuwa tayari kuiwasilisha leo kama ilivyoelezwa, alijibu:

"Hata kama nitaipata sasa, siwezi kuitable kesho (leo) kwani nahitaji muda kuisoma na kuielewa".

Awali mbung wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema suala la Richmond limeanza kuligawa taifa na njia pekee ya kuirudishia jamii imani na serikali, ni Rais kwa mamlaka ya kuwa mkuu wa nchi kuunda jopo la majaji kupitia upya hoja zote na kutoa maamuzi.

"Suala hili limeonekana kuigonganisha mihimili mikuu miwili ya dola, Bunge na Serikali, dawa yake sasa ili liishe, ni Rais kama mkuu wa nchi nasisitiza, mkuu wa nchi sio serikali kuunda tume ya majaji wapitie Maazimio ya Bunge, utekelezaji wa serikali na watoe maamuzi," alisema.

Alisema: "Inavyoonekana kila upande unavutia kwake, wakati Bunge likitaka serikali itekeleze mapendekezo yake ndani ya miezi mitatu, serikali imetumia karibu mwaka na nusu na bado inakuja na majibu ya kubabaisha.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube