15 Jul 2009


na Charles Mullinda

IMEBAINIKA kuwa, Ofisi ya Bunge imetumia vibaya mamilioni ya shilingi yaliyotolewa na serikali kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2007/2008.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wabunge wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika mahojiano yao na Tanzania Daima Jumatano yaliyofanyika wiki iliyopita mjini Dodoma kwa wakati tofauti.

Wakizungumza kwa sharti la majina yao kutoandikwa gazetini, kwa kile walichoeleza kuwa ni kuogopa kuandamwa na baadhi ya wabunge wenzao, walisema ushahidi wa maelezo yao umo katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CGA) ya mwaka wa fedha wa 2007/2008.

Mmoja wa wabunge hao alieleza kuwa licha ya ripoti ya CGA kubainisha matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha katika Ofisi ya Bunge, Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, alizuia kujadiliwa kwa ripoti hiyo baada ya kushauriana na baadhi ya vigogo wa Ofisi ya Bunge, jambo ambalo linazuia kuchukuliwa hatua zozote za kisheria au kurekebisha hali hiyo hadi sasa.

Alisema Ofisi ya Bunge imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kuhakikisha ripoti hiyo haijadiliwi na PAC, kwa hofu kwamba inaweza kusababisha baadhi ya watendaji kuwajibishwa na baadhi ya wanasiasa kuchafuka majina yao.

Cheyo, Mwenyekiti wa PAC na Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), alipoulizwa na gazeti hili kuhusu madai hayo, alisema ni kweli ripoti ya CAG kuhusu matumizi ya fedha za serikali katika Ofisi ya Bunge si nzuri, kwa sababu inaonyesha upungufu mkubwa wa urejeshaji masufuru pamoja na matumuzi mengine mabaya ya fedha za ofisi hiyo.

Hata hivyo, alikana kuikalia ripoti hiyo kwa namna yoyote na kueleza kuwa, aliamua kuiweka pembeni baada ya kushauriana na kukubaliana na wajumbe wote wa kamati hiyo kuwa hawawezi kuijadili, kwa sababu walishindwa kumhoji Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ambaye wakati kamati hiyo akikutana kujadili ripoti mbalimbali za CGA kuhusu hesabu za taasisi za serikali, alikuwa hajaapishwa na rais kushika wadhifa huo.

“Ni kweli ripoti ya CAG kuhusu matumuzi ya fedha katika Ofisi ya Bunge si nzuri, inaonyesha upungufu mkubwa katika urejeshaji wa masurufu, na ripoti zote ambazo zinaonyesha hivyo kihasibu huwa ni mbaya. Sasa kwa Spika hii si nzuri, inamtia doa, anaweza asiaminike tena iwapo itawekwa wazi, kwa sababu ataonekana hafanani na kauli zake.

“Siyasemi haya kwa sababu nina kisasi na Spika, bali ni kwa sababu umeniuliza. Unajua Spika amenijeruhi hivi karibuni, sasa sitaki nionekana kama ninalipa kisasi. Lakini ukweli unabaki pale pale kwa sababu umeandikwa vitabuni kuwa kuna kasoro katika Ofisi ya Bunge ambayo inasimamiwa na Spika,” alisema Cheyo.

Spika Sitta alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Cheyo, alisema hahusiki kwa namna yoyote na uchukuaji wa masurufu, hivyo hapaswi kunyooshewa kidole iwapo imebainika kuwapo kwa kasoro zozote za matumuzi mabaya ya fedha za serikali katika ofisi yake.

Spika alisema taratibu ziko wazi kuwa wanaochukua masufuru kwa ajili yake ni wasaidizi wake wanaohusika kumuandalia safari zake zote, ndani na nje ya nchi.

“Mimi sihusiki kuchukua masurufu, wanaohusika ni wasaidizi wangu, sasa kama kuna kasoro, wao ndio wanajua. Nina ofisi yangu binafsi kama viongozi wengine wakuu wa kitaifa, sitembei na fedha mfukoni, wasaidizi wangu wa ofisi hiyo ndio wanaoniandalia safari na ziara zangu zote. Wao ndio wanaonilipia kila kitu, walinzi, maradhi, kila kitu, ndio wanaochukua fedha za masurufu kwa niaba yangu,” alisema Spika Sitta.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa alitumia fedha nyingi za Ofisi ya Bunge kugharamia vikao na tafrija zilizokuwa zikifanyikia nyumbani kwake wakati mkewe, Margaret Sitta, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, akiwania nafasi ya kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alisema madai hayo inabidi yafafanuliwe.

“Ninachokijua mimi kuhusu hili, ni kweli kulikuwa na vitu vya aina hiyo wakati huo, lakini ninachokumbuka ni kwamba gharama nyingi za mikusanyiko hiyo nilikuwa ninatumia fedha zangu za mfukoni, nilikuwa nalipa mwenyewe. Lakini hili ili nilielewe vizuri, inabidi lifafanuliwe,” alisema.

Naye Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah alipoulizwa kuhusu hali hiyo, alisema hawezi kuzungumza jambo hilo, kwa sababu alipoingia katika wadhifa huo alikuta hali hiyo imeshatokea.

Alibainisha kuwa ni kweli hakuhojiwa na Kamati ya PAC kwa sababu alikuwa hajaapishwa na rais, lakini kwa sasa kamati hiyo inaweza kuendelea na kazi zake kama kawaida, bila kupata kipingamizi kutoka kwa mtu yeyote.

“Mimi nilipoingia katika ofisi hii, hali hiyo niliikuta, hivyo siwezi kusema kitu, kwa sababu sikuwapo, siwezi kuizungumzia. Ninachoweza kukitolea maelezo ni kile ambacho kimefanyika wakati wa kipindi changu.

“Lakini suala la ripoti hiyo kukaliwa halipo, PAC ikitaka kukaa kuijadili hata kesho ni sawa tu, hakuna tatizo, waje wakae, wao wana ratiba zao za vikao, kuna ripoti nyingi tu hazijajadiliwa, hizi hazijakaliwa, naomba kwa sababu linahusu Ofisi ya Spika, isichukuliwe kuwa linazimwa,” alisema Dk. Kashililah.

Ripoti ya CAG, ambayo Tanzania Daima Jumatano imeiona, katika ukurasa wake wa 43, fungu la 42, inaitaja Ofisi ya Bunge katika orodha ya taasisi za serikali zilizopewa hati zenye shaka, kwa kukiuka taratibu za kihasibu.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa Ofisi ya Bunge ilifanya malipo ya matibabu nje ya nchi ya zaidi ya sh milioni 101 bila kuidhinishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, uhamisho wa fedha wa zaidi ya sh milioni 63 kutoka kifungu kimoja kwenda kingine bila kibali na malipo yenye thamani ya sh milioni 7.8 yalifanyika bila kibali.

Upungufu mwingine uliotajwa katika ripoti hiyo ni malipo yenye nyaraka pungufu ya sh milioni 526, malipo yasiyo halali ya sh milioni 102.5, malipo yenye shaka ya sh milioni 63.9, mishahara isiyolipwa na ambayo haikurejeshwa Hazina sh milioni 17.1, sh milioni 3.4 za mishahara ya watumishi walioachishwa kazi inayoendelea kulipwa kwenye akaunti zao benki na usuluhisho wa tofauti ya sh milioni 1.1 kati ya bakaa ya benki na bakaa inayoonyeshwa katika daftari la mapato na matumizi haukufanyika.

Marekebisho yasiyostahili yaliyojumuishwa kwenye hundi ambazo hazijawasilishwa benki ni sh milioni tano, masurufu maalumu ya sh milioni 50.2


KINACHOKWAMISHA VITA DHIDI YA UFISADI NI HUU MTINDO WA KUENDESHA MAMBO KISHKAJI.UKITAFAKARI KAULI YA CHEYO KUHOFIA KUHUSISHA HABARI ZA UFISADI HUO NA HATUA YA SPIKA KUMTOA NJE YA BUNGE HIVI KARIBUNI UTAGUNDUA KUWA BADALA YA MBUNGE HUYO KUSHUGHULIKIA SUALA HILO KAMA MWENYEKITI WA KAMATI HUSIKA,YEYE ANAJIONA KAMA JOHN MOMOSE CHEYO ALIYETOLEWA NJE NA SAMUEL SITTA,BADALA YA OFISI YA BUNGE ILIYO CHINI YA SPIKA NA WATENDAJI KADHAA.

NA UNAFIKI MWINGINE NI WA HAO WABUNGE WALIONUKULIWA KATIKA HABARI HII AMBAYO HAWATAKI KUTAJWA MAJINA KISA WANAOGOPA KUANDAMWA NA WABUNGE WENZAO.KWANI WALIINGIZWA BUNGENI NA HAO WABUNGE WENZAO WANAOWAOGOPA AU WANANCHI HUKO MAJIMBONI?

WIZI MTUPU!


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube