5 Dec 2009


TOFAUTI na alivyojigamba kwamba ni mlipaji mzuri wa madeni anayodaiwa na serikali, Mbunge wa Igunga, Rostam Azizi anadaiwa Sh. 2,576,583,013 tokea mwaka 1993, MwanaHALISI limegundua.

Alikopeshwa Sh. 2 bilioni (2,025,739,660) mwaka 1993 na 1997 na Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa (CIS) uliokuwa ukifadhiliwa na serikali ya Japan na kusimamiwa na Wizara ya Fedha na Uchumi.

Alitumia makampuni ya Africa Tanneries Ltd, Tanzania Leather Industries Ltd na Africa Trade Development.

Fedha nyingine alizokopeshwa ni Sh. 1,516,024,125. Hizi alikopeshwa na serikali ili kuagiza mchele kupitia mpango wa Counterpart Fund. Alitumia Kampuni ya African Trade Development.

Imethibitika kwamba Rostam ameshindwa au hataki kulipa deni hilo lililodumu kwa miaka 16 sasa.

Akizungumza na vyombo vya habari 3 Mei 2009, siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski jijini Dar es Salaam, Rostam alitamba kuwa ni mlipaji mzuri wa madeni yake kwa serikali.

Alikuwa akijibu tuhuma mbalimbali za ufisadi anaodaiwa kufanya kwa kutumia makampuni yake mbalimbali. Gazeti hili lina kumbukumbu za jinsi alichukua fedha hizo, zilizokusudiwa kuboresha biashara nchini.

Uchunguzi umebaini kuwa mwaka 1993 alichukua Sh. 280 milioni kupitia Kampuni ya African Tanneries Limited. Mwaka 1997 alitumia Kampuni ya Tanzania Leather Industries Limited kuchukua Sh. 725,943,120.

Mwaka huohuo Rostam alitumia Kampuni yake nyingine ya African Trade Development kubeba Sh. 1,019,796,540 kutoka mfuko huo.

Mwishoni mwa mwaka jana, baada ya ‘mshike mshike nguo kuchanika,’ Rostam alilipa Sh. 500 milioni akikusudia kupunguza deni la “mchele.”

Lakini kutokana na kuwepo deni jingine la zaidi ya Sh. 1bilioni katika mfuko wa CIS, mamlaka husika zikaamua kutumia kiasi hicho kupunguza madeni hayo.

Kwa sasa anadaiwa na mfuko huo Sh. 1.060,558,888. Deni hilo likijumlishwa na deni alilokopa kuagiza mchele, Rostam anadaiwa jumla ya Sh. 2,576,583,013. Katika mazungumzo yake na serikali kwa nyakati tofauti, alikiri na kuahidi kulipa ingawa hadi sasa ameendelea kukaidi kulipa.

MwanaHALISI limebaini kuwa tayari mmoja wa wanasheria jijini Dar es Salaam, anayeshughulikia suala la kukusanya madeni hayo anaandaa taarifa ya kisheria itakayokabidhiwa kwa wadeni sugu wakati wowote kuanzia sasa.

Jukumu jingine analotekeleza mtaalamu huyo wa sheria ni kumshauri Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, kufanya mpango wa kutumia mamlaka ya Kamishna Mkuu wa TRA ili kutekeleza azma ya kufilisi mali za Rostam na vigogo wenzake wanaodaiwa.

Pamoja na Rostam, wadeni sugu wengine ambao walizungumza na serikali, wakakiri kudaiwa na wakaahidi kulipa madeni kwa kadri walivyoomba lakini badala ya kulipa wakaingia ‘mitini’ ni pamoja na Mbunge wa Temeke, Abass Mtemvu (CCM).

Mbunge huyo mwaka 1998 alitumia Kampuni ya A.M. General Agency kukopa Yen 20,000,000 sawa na Sh. 280 milioni. Ingawa alikiri kudaiwa na kuahidi kulipa deni, hadi sasa hajalipa hata shilingi moja.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Utumishi na Mbunge wa Mlangege, Zanzibar, Fatma Said Ali (CCM), mwaka 1998 alitumia Kampuni ya Tanzania Save Way Co. Ltd., kukopa Yen 20,000,000 lakini akakopeshwa Yen 10,000,000 sawa na Sh.140 milioni. Aliwahi kupunguza Sh. 23,400,000 tu.

Aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wakati wa serikali ya awamu ya pili na ya tatu, ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Henry Shekiffu, mwaka 2000.

Alitumia kampuni ya Shemshi & Sons Limited kukopa Sh. 399,560,000. Amewahi kupunguza Sh. 65,340,051. Hadi sasa anadaiwa Sh. 279,653,794.

Nicodemas Banduka, mwaka 2000 alitumia kampuni ya Kadolo Investment kukopa Yen 105,210045 sawa na Sh. 147,294,630. Aliwahi kulipa Sh. 22,500,000. Hadi sasa anadaiwa Sh.124,794,630.

Mwingine ambaye arobaini zake zimekaribia ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka, aliyetumia kampuni ya Petmon Investment, mwaka 2000. Alikopa Sh. 140 milioni, aliwahi kupunguza Sh. 24,712,200. Hadi sasa anadaiwa Sh. 115.287,800.

Ufuatiliaji unabainisha kuwa idadi kubwa ya makampuni yaliyotumiwa na vigogo hao yalianzishwa kwa lengo la kuchota fedha hizo. Mengi kati ya hayo hayapo tena.

Vigogo wengine waliobainika kukopeshwa na CIS lakini taarifa hazielezi kama mali wanazomiliki pia zitafilisiwa, ni aliyekuwa mbunge wa Sengerema, Dk. William Shija ambaye sasa ni Katibu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola.

Alikopa Sh. 140 milioni kwa kutumia kampuni ya Pyramid Investments Limited, mwaka 2000. Amewahi kupunguza Sh. 22,650,000.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira, naye jina lake limo kwenye orodha ya wanaodaiwa ingawa taarifa muhimu, mathalani alikopa kiasi gani, lini na amelipa au bado hazionyeshwi katika kumbukumbu hizo.

Ingawa serikali inaelezwa kuwa kwenye hatua za kukamilisha mipango ya kufilisi mali za wadeni wake hao na wengine, bado inasuasua.

Mkataba wa kufanikisha mikopo hiyo unaruhusu serikali kupitia kwa Kamishna Mkuu wa TRA kufilisi mali za asiyetekeleza mkataba katika kipengele cha kulipa, tena bila kulazimika kwenda mahakamani. Haijafahamika kwa nini TRA haijachukua hatua hiyo.

Dhana inajengeka kwamba huenda “kigugumizi” hicho katika kukusanya madeni ya walipa kodi wa Tanzania, kinatokana na wadaiwa wengi kuwa vigogo ambao miongoni mwao bado wapo kwenye nyadhifa za juu serikalini.

CIS ilianzishwa kwa nia njema ya kukuza sekta ya biashara nchini, kwa kuwasaidia wafanyabiashara kufanya biashara za kimataifa. Kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka nchi tofauti, zilizofadhili mpango huo.

Mpango huo ulikuwa ukitekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Uchumi. Hata hivyo taarifa zinaonyesha kuwa jumla ya Sh. 44 bilioni zilichotwa na wizara nane katika mazingira ambayo hadi sasa serikali haijafafanua.

CHANZO: Mwanahalisi

INAUDHI,INAUMA NA KUSONONESHA LAKINI IT LOOKS AS IF NCHI HAINA WENYEWE KWANI WALIOIBIWA WAKO KIMYA KANA KWAMBA WAMERIDHIKA.JE TUMEKUBALI UFISADI KUWA SEHEMU YA MAISHA YETU YA KILA SIKU?

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.