27 Aug 2010

Sheria ni msumeno: Rais Kikwete akisaini kwa mbwembe Sheria ya Gharama za Uchaguzi,ambayo Chadema wanamtuhumu kuikiuka na hivyo wanamwekea pingamizi.
Geofrey Nyang'oro na Lilian Mazula

SHERIA ni msumeno na sasa imgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete atalazimika kufanya kazi ya ziada isimdhuru baada ya Chadema kumwekea pingamizi rais huyo wa serikali ya awamu ya nne.Kikwete alisaini Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa mbwembwe mapema mwaka huu akitaka itumike mwaka huu, lakini Chadema imeitumia sheria hiyo kumwekea pingamizi, ikidai kuwa mgombea huyo wa CCM ameikiuka.

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Kikwete amekiuka sheria hiyo kwa kwa kutangaza ongezeko la mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma akiwa kwenye mikutano ya kampeni.

"Wanasheria wetu wanashughulikia suala hilo kwa kusaidiana na naibu katibu mkuu, John Mnyika kukamilisha pingamizi hilo na kesho (leo) asubuhi tutawasilisha pingamizi letu kwa msajili wa vyama vya siasa,"alisema Dk Slaa ambaye pia ni mgombea urais kwa tiketi ya Chadema.

Dk Slaa alidai kuwa Kikwete alikiuka kipengele cha 6, sehemu ya 21 (1) cha sheria hiyo inayotoa tafsiri ya mambo yanayokatazwa wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea na kampeni za uchaguzi.

Alisema Kikwete amekiuka kifungu hicho kwa kutangaza ongezeko la mishahara ya wafanyakazi akiwa katika majukwaa ya kampeni, jambo ambalo linaweza kutafsiriwa na sheria hiyo kuwa ni rushwa ya uchaguzi.

Alieleza kuwa Kikwete amekiuka sheria hiyo kwa kuwa yeye kama mgombea, hana mamlaka ya kuongeza mshahara wa wafanyakazi katika kipindi hiki cha kampeni.
Dokta Slaa

"Kwa kutungwa kwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi na kusainiwa Julai 17 mwaka huu pamoja na marekebisho yake, tulitegemea kungesaidia kuleta mabadiliko," alisema Dk Slaa ambaye kitaaluma amebobea kwenye sheria.

"Kitendo cha Kikwete kukiuka sheria hiyo kimenishtua sana.

Watanzania tungependa kupewa ufafanuzi; fedha hizo za (mishahara) zimetoka wapi na kwa mamlaka ya nani kwa kuwa wenye mamlaka ya kuidhinisha matumzi ya fedha za umma ni Bunge," alisema Dk Slaa.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa katiba, Bunge ndilo lenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha ikiwa ni pamoja na ongezeko la mishara kwa wafanyakazi wa umma.

"Kitendo cha serikali kuamuru ongezeko hilo nje ya vikao vya bunge, ni ukiukwaji wa sheria za nchi na ndio mwanya uliosababisha kutoweka kwa fedha za Akaunti ya Madeni ya nje(EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT)," alisema Dk Slaa.

"Sehemu ya tano ya sheria hiyo sura ya 21.-(1) inaweka bayana vitendo vinavyokatazwa wakati wa uteuzi wakati wa kampeni za uchaguzi na inasomeka:

"(a)Kila mtu ambaye kabla au wakati wa kipindi cha kampeni, moja kwa moja au kwa namna nyingine yoyote, kupitia kwa mtu mwingine yeyote au kwa niaba yake, anatoa, anakopesha au anakubali kutoa au kukopesha, au anatoa, anaahidi au kumpatia au anajaribu kumpatia fedha yoyote au kitu chochote chenye thamani,

mpiga kura au kwa ajili ya mtu yeyote kwa niaba ya mpiga kura yeyote au kwa ajili ya mtu mwingine yeyote kwa nia ya kumshawishi kupiga kura, au kuacha kupiga kura au kumrubuni mtu yeyote kutendo hicho kwa niaba ya mpiga kura huyo kupiga kura au kuacha kupiga kura katika kura za maoni au uchaguzi wowote;

"Kikwete alisema yeye mwenyewe hahitaji kura za wafanyakazi, na akasisitiza katika hotuba yake iliyoitoa kwa wazee wa Dar es Salaam kuwa serikali haina uwezo wa kulipa mishahara hiyo na kama wanafanya hivyo kwa kushinikiza kigezo cha kura, yeye hazitaki; leo mishahara imeongezeka, fedha hizo zimetoka wapi?Tunataka utueleze matumizi hayo ya fedha za umma kinyume na utaratibu."

Kwa mujibu wa Dk Slaa mgombea urais anapaswa kulinda katiba na sheria zilizopo, ili kulifanya taifa liendelee kuwa katika hali ya amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Dk Slaa alisema kuwa kitendo cha rais kutumia nafasi hiyo kutangaza mishahara kwenye kampeni ni kujipa upendeleo kwa kushawishi watu kumpigia kura kwa kutumia nafasi aliyonayo.

Dk Slaa pia alitumia fursa hiyo kukemea kitendo cha kufanya maamuzi kwa kukiuka sheria zilizopo akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Dk Slaa pia alienda mbali zaidi na kuituhumu CCM kwamba imekiuka taratibu za uchaguzi kwa kutengeneza mabango yake ya mgombea nchini Canada.

"CCM wametumia Sh1.5 bilioni kutengeneza mabango nje ya nchi kwa kutumia fedha za serikali pia ankara ya malipo "invoice" inaonyesha imeandikwa 'VAT INVOICE' kitu ambacho hakieleweki," alisema Dk Slaa.
Alisema kuwa ni muhimu CCM kutoa ufafanuzi juu ya hilo kwa kuwa ushahidi upo na unaonyesha kuwa kuna mchezo mchafu umeanza kufanywa.

CHANZO: Mwananchi

1 comment:

  1. Kama nilivyohisi imekuwa kweli. Magazeti ya mwananchi hayapatikani kwenye mtandao. Ninaomba isje ikawa ni ujuma toka kwa watu wanaojipendekeza kwa watu wachache na kudharau/kusigina ethics za kazi zao. UBINAFSI NI TATIZO KUBWA SANA KWA WATZ. mtu ajali maslai ya taifa kwa kitu kidogo tu atakachohongwa

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.