Showing posts with label WILBROAD SLAA. Show all posts
Showing posts with label WILBROAD SLAA. Show all posts

27 Aug 2010

Sheria ni msumeno: Rais Kikwete akisaini kwa mbwembe Sheria ya Gharama za Uchaguzi,ambayo Chadema wanamtuhumu kuikiuka na hivyo wanamwekea pingamizi.
Geofrey Nyang'oro na Lilian Mazula

SHERIA ni msumeno na sasa imgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete atalazimika kufanya kazi ya ziada isimdhuru baada ya Chadema kumwekea pingamizi rais huyo wa serikali ya awamu ya nne.Kikwete alisaini Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa mbwembwe mapema mwaka huu akitaka itumike mwaka huu, lakini Chadema imeitumia sheria hiyo kumwekea pingamizi, ikidai kuwa mgombea huyo wa CCM ameikiuka.

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Kikwete amekiuka sheria hiyo kwa kwa kutangaza ongezeko la mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma akiwa kwenye mikutano ya kampeni.

"Wanasheria wetu wanashughulikia suala hilo kwa kusaidiana na naibu katibu mkuu, John Mnyika kukamilisha pingamizi hilo na kesho (leo) asubuhi tutawasilisha pingamizi letu kwa msajili wa vyama vya siasa,"alisema Dk Slaa ambaye pia ni mgombea urais kwa tiketi ya Chadema.

Dk Slaa alidai kuwa Kikwete alikiuka kipengele cha 6, sehemu ya 21 (1) cha sheria hiyo inayotoa tafsiri ya mambo yanayokatazwa wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea na kampeni za uchaguzi.

Alisema Kikwete amekiuka kifungu hicho kwa kutangaza ongezeko la mishahara ya wafanyakazi akiwa katika majukwaa ya kampeni, jambo ambalo linaweza kutafsiriwa na sheria hiyo kuwa ni rushwa ya uchaguzi.

Alieleza kuwa Kikwete amekiuka sheria hiyo kwa kuwa yeye kama mgombea, hana mamlaka ya kuongeza mshahara wa wafanyakazi katika kipindi hiki cha kampeni.
Dokta Slaa

"Kwa kutungwa kwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi na kusainiwa Julai 17 mwaka huu pamoja na marekebisho yake, tulitegemea kungesaidia kuleta mabadiliko," alisema Dk Slaa ambaye kitaaluma amebobea kwenye sheria.

"Kitendo cha Kikwete kukiuka sheria hiyo kimenishtua sana.

Watanzania tungependa kupewa ufafanuzi; fedha hizo za (mishahara) zimetoka wapi na kwa mamlaka ya nani kwa kuwa wenye mamlaka ya kuidhinisha matumzi ya fedha za umma ni Bunge," alisema Dk Slaa.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa katiba, Bunge ndilo lenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha ikiwa ni pamoja na ongezeko la mishara kwa wafanyakazi wa umma.

"Kitendo cha serikali kuamuru ongezeko hilo nje ya vikao vya bunge, ni ukiukwaji wa sheria za nchi na ndio mwanya uliosababisha kutoweka kwa fedha za Akaunti ya Madeni ya nje(EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT)," alisema Dk Slaa.

"Sehemu ya tano ya sheria hiyo sura ya 21.-(1) inaweka bayana vitendo vinavyokatazwa wakati wa uteuzi wakati wa kampeni za uchaguzi na inasomeka:

"(a)Kila mtu ambaye kabla au wakati wa kipindi cha kampeni, moja kwa moja au kwa namna nyingine yoyote, kupitia kwa mtu mwingine yeyote au kwa niaba yake, anatoa, anakopesha au anakubali kutoa au kukopesha, au anatoa, anaahidi au kumpatia au anajaribu kumpatia fedha yoyote au kitu chochote chenye thamani,

mpiga kura au kwa ajili ya mtu yeyote kwa niaba ya mpiga kura yeyote au kwa ajili ya mtu mwingine yeyote kwa nia ya kumshawishi kupiga kura, au kuacha kupiga kura au kumrubuni mtu yeyote kutendo hicho kwa niaba ya mpiga kura huyo kupiga kura au kuacha kupiga kura katika kura za maoni au uchaguzi wowote;

"Kikwete alisema yeye mwenyewe hahitaji kura za wafanyakazi, na akasisitiza katika hotuba yake iliyoitoa kwa wazee wa Dar es Salaam kuwa serikali haina uwezo wa kulipa mishahara hiyo na kama wanafanya hivyo kwa kushinikiza kigezo cha kura, yeye hazitaki; leo mishahara imeongezeka, fedha hizo zimetoka wapi?Tunataka utueleze matumizi hayo ya fedha za umma kinyume na utaratibu."

Kwa mujibu wa Dk Slaa mgombea urais anapaswa kulinda katiba na sheria zilizopo, ili kulifanya taifa liendelee kuwa katika hali ya amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Dk Slaa alisema kuwa kitendo cha rais kutumia nafasi hiyo kutangaza mishahara kwenye kampeni ni kujipa upendeleo kwa kushawishi watu kumpigia kura kwa kutumia nafasi aliyonayo.

Dk Slaa pia alitumia fursa hiyo kukemea kitendo cha kufanya maamuzi kwa kukiuka sheria zilizopo akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Dk Slaa pia alienda mbali zaidi na kuituhumu CCM kwamba imekiuka taratibu za uchaguzi kwa kutengeneza mabango yake ya mgombea nchini Canada.

"CCM wametumia Sh1.5 bilioni kutengeneza mabango nje ya nchi kwa kutumia fedha za serikali pia ankara ya malipo "invoice" inaonyesha imeandikwa 'VAT INVOICE' kitu ambacho hakieleweki," alisema Dk Slaa.
Alisema kuwa ni muhimu CCM kutoa ufafanuzi juu ya hilo kwa kuwa ushahidi upo na unaonyesha kuwa kuna mchezo mchafu umeanza kufanywa.

CHANZO: Mwananchi

26 Aug 2010

Rostam Aziz
Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005,mfanyabiashara controversial Rostam Aziz alitumia raslimali zake nyingi kuhakikisha mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM,Jakaya Kikwete,anashinda kwa gharama yoyote ile.Na kutokana na utajiri mkubwa alionao pamoja na mbinu zake mbalimbali,mchango wake ulimsaidia sana Kikwete kuingia Ikulu,na sasa ni Rais wetu anayeomba tena ridhaa ya kutuongoza kwa miaka mitano ijayo.

Kati ya mwaka 2005 (baada ya Kikwete kuingia Ikulu) na sasa,Rostam ameibuka kuwa kiumbe mwenye nguvu za kutisha sio tu ndani ya CCM bali kwenye siasa za Tanzania kwa ujumla.Lakini kubwa zaidi katika kipindi hicho ni kwa mfanyabiashara huyo kuhusishwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi na Kikwete na serikali yake kushindwa kuwaridhisha Watanzania kwamba "hamkumbatii swahiba wake huyo".Haihitaji kurejea namna Rostam alivyohusishwa na ufisadi wa EPA (Kagoda) na ujambazi wa Richmond.
Jakaya Kikwete

Mwaka 2010,yaani mwaka huu,Rostam anaelekea kurejea tena ulingoni japo si kwa wazi sana.Ushahidi wa kimazingira unaonyesha kuhusika kwa mfanyabiashara huyo katika kampeni za Kikwete.Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Rostam vimekuwa vikiendesha kampeni ya chuki dhidi ya mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,Dokta Wilbroad Slaa,mwanasiasa anayeonekana kuwa  tishio kwa mfanyabiashara huyo na vitendo vyake dhidi ya maslahi ya taifa.
Magazeti yanayomilikiwa na Rostam

Na kama hilo la vyombo vya habari vya Rostam kumuandama Dkt Slaa halitoi mwangaza wa kutosha basi taarifa kwamba mwandishi mwandamizi wa kampuni ya Habari Corporation (inayomilikiwa na Rostam),Muhingo Rweyemamu,anatajwa kuwa mratibu wa kampeni za Kikwete.Itakumbukwa kuwa mwaka 2005,waliokuwa waandishi waandamizi wa Habari Corporation,Salva Rweyemamu na Dokta Gideon Shoo walitumika sana kwenye kampeni hizo.Baada ya kuingia Ikulu,Kikwete "alimzawadia" Salva ukurugenzi wa habari wa Ikulu,nafasi anayoshikilia hadi sasa.
Muhingo Rweyemamu

Kama alivyo Salva,Muhingo anasifika kwa uwezo wake wa hali ya juu wa kujenga hoja.Kwa bahati mbaya au makusudi,uwezo huo pia unatumika ipasavyo kutengeneza fitna.Wengi watakumbuka namna Dokta Salim Ahmed Salim,mmoja wa wana-CCM waliokuwa wanawania kuchuana na Kikwete,alivyoundiwa zengwe kubwa na kumhusisha na kundi la Hizbu la huko Zanzibar.Inaelekea kuwa mbinu hizohizo zimeanza kutumika dhidi ya Dokta Slaa,na kuna kila sababu ya kuamini kuwa kuna mengi yatakayoibuliwa dhidi yake.
Salva Rweyemamu  (kushoto) na Gideon Shoo

Yayumkinika kuamini kuwa waandishi wa habari wanaotumiwa kumchafua Dokta Slaa na Chadema kwa ujumla wanafanya hivyo kwa minajili ya "kupeleka mkono kinywani".Kubwa zaidi ni sapoti ya Rostam kwa Kikwete.Wakati mwaka 2005 alijibidiisha ili kufanikisha maslahi yake binafsi ya kibiashara (na amenufaika kweli-kwa kuangalia ishu za Kagoda na Richmond/Dowans) safari hii Rostam anahaha kumzuia Dokta Slaa kwa vile anafahamu fika kwamba laiti mwanasiasa huyo wa Chadema anayesifika kwa msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi akiingia Ikulu,zama za mafisadi kutumia jeuri yao ya fedha "kuendesha serikali kwa remote control" itakuwa imefikia kikomo.

Kwahiyo,Dokta Slaa na Chadema kwa ujumla wanapaswa kuelewa kuwa safari hii Rostam ana "special mission" ya kuhakikisha "survival (kusalimika) yake.Atatumia kila raslimali aliyonayo kuhakikisha Dokta Slaa haingii Ikulu.Anafanya hivyo akifahamu wazi kuwa rais yeyote mwenye kujali maslahi ya nchi yake "atamkalia kooni" mfanyabisahara huyo na washirika wake.

Hata hivyo,kwa vile si fedha za Rostam au wanahabari wake zitakazopiga kura kwenye uchaguzi mkuu,bali mimi na wewe pamoja na kila Mtanzania aliyechoshwa kuona nchi yetu ikigeuzwa "shamba la bibi",ni muhimu kwa wapiga kura kusema HAPANA.Tusitoe fursa kwa watu wenye maslahi binafsi kuipeleka nchi yetu kwenye maangamizi.Na ni muhimu zaidi kutambua kuwa baadhi ya watu hao wana utata wa kutosha tu kuhusu asili ya mahali walipozaliwa.Hiyo inamaanisha kuwa "wakishaiingiza Tanzania kwenye mtaro",watakuwa na sehemu ya kukimbilia.

KILA MTANZANIA MWENYE KUITAKIA MEMA NCHI YETU ANAPASWA KUPAMBANA NA WAHUNI WA KISIASA WANAOTAKA KUTUWEKEA MADARAKANI VIONGOZI WANAOWAMUDU NA HIVYO KUENDELEA KUTUFISADI KAMA ILIVYOKUWA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITANO ILIYOPITA.


INAWEZEKANA,TIMIZA WAJIBU WAKO

22 Aug 2010

Blogu hii ya KULIKONI UGHAIBUNI inafungua ukurasa mpya na kuweka historia ya kipekee katika fani ya habari nchini Tanzania kwa kutangaza hadharani kuwa inam-endorse mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema,Dokta Wilbroad Slaa.

Kuna sababu lukuki za kufanya hivyo lakini hapa nitaziorodhesha chache.Kwanza,blogu hii inataka kuachana na unafiki unaojidhihirisha katika baadhi ya vyombo vya habari vyetu ambapo wahusika wanadai hawafungamani na upande wowote lakini matendo yao yanawasuta kwa kupendelea chama tawala huku wakivibinya kwa nguvu baadhi ya vyama vya upinzani.Hapa simsimangi mtu bali nadhani ni vema kuweka msimamo wazi ili kama chombo cha habari ni wakala wa CCM na JK basi ni vema wasomaji wakafahamishwa bayana.

Pili,blogu hii inaamini kuwa kila Mtanzania mwenye uchungu wa dhati kwa nchi yetu anapaswa kumsapoti Dkt Slaa.Katika utumishi wake kwa umma,mgombea huyo wa Chadema ametuthibitishia kuwa ni mtetezi halisi wa haki za wanyonge na ustawi wa taifa letu.Ni nani asiyefahamu namna Dkt Slaa alivyohatarisha maisha yake kwa “kuwavua nguo mafisadi hadharani” alipotangaza ile “list of shame”?Walitishia kumpeleka mahakamani lakini hakuna mmoja wao aliyediriki kufanya hivyo,na sanasana baadhi yao wakaishia kuburuzwa mahakamani na serikali katika “kujikosha”.Blogu hii inaamini kuwa Dokta Slaa ni mkombozi na suluhisho mwafaka la matatizo lukuki yanayotukabili.

Tatu,binafsi naamini kuwa mgombea wa CCM,Jakaya Mrisho Kikwete,ameshindwa kabisa kutimiza matarajio ya Watanzania licha ya ahadi lukuki alizozitoa wakati wa kampeni zake mwaka 2005 na anazoendelea kuzitoa hadi leo.Ungetegemea kuwa mwezi huu wa toba Kikwete angemwogopa Mola wake na kutubu kwa Watanzania kwamba kuna maeneo mengi tu ambapo yeye na chama chake wamewaangusha Watanzania.Lakini kama ilivyo jeuri ya wanasiasa wengi wa Kiafrika,JK ameendeleza wimbo wa “mafanikio ya Awamu ya Nne”.Yani hata kushamiri kwa ufisadi na “uchakachuaji” wa kura za maoni ndani ya CCM ni mafanikio!

Sababu ya nne inashabihiana na hiyo ya tatu.Naamini kuwa afya ya mgombea wa CCM,Jakaya Kikwete,inapaswa kuwekwa kwenye darubini na wapiga kura wanapofanya maamuzi ya kumchagua rais wa awamu ya tano.JK ameshaanguka hadharani mara tatu na kila mara tunapewa excuse moja baada ya nyingine.Mwaka 2005 tuliambiwa “swaumu na uchovu wa kampeni”.Alipoanguka Mwanza tuliambiwa uchovu wa safari (kana kwamba safari hizo ni zile za Wamachinga wanaotembea juani kwa mguu!).Na jana kaanguka tena jukwaani halafu tunaambiwa sababu ni swaumu.Kwani Makamba hajafunga?Au Rais Karume naye “kobe”?Kuna tatizo zaidi ya swaumu au uchovu lakini kwa vile viongozi wetu wamezowea sifa na sio kasoro basi kuweka hadharani kinachomsibu kiongozi huyo inaonekana ni sawa na uhaini.Blogu hii imaanimi kuwa ili Tanzania ijikwamue katika lindi la umasikini wa kutupwa,sambamba na kukabiliana na janga la ufisadi,tunahitaji kiongozi mwenye afya timilifu,kimwili na kiakili.Hatujui JK ameshaanguka matra ngapi asipokuwa hadharani lakini haihitaji hata cheti cha short course ya utabibu kumaizi kuwa JK ana matatizo ya kiafya yanayofichwa,aidha kutokana na uoga wa wanaopaswa kuujulisha umma kuhusu hilo au maagizo yake mwenyewe kuwa “yuko fiti”.All in all,uzito wa matatizo yanayoikabili Tanzania unahitaji mtu aliye fiti kweli,na sio kwa anavyodhani yeye au anavyotaka umma uamini hivyo ilhali ni kinyume na hali halisi.

Kama nilivyoandika mwanzoni,kuna sababu nyingi zilizopelekea blogu hii kuamua kum-endorse Dkt Slaa lakini chache zilizotajwa hapo juu zinawakilisha hizo nyingine.Nawakaribisha ndugu zangu wa Chadema kuitumia blogu hii kufikisha habari kwa Watanzania pasipo hofu ya kuwa habari hizo zitachujwa,kuminywa au “kuchakachuliwa”.

Natambua bayana kuwa baadhi ya wasomaji wa blogu hii sio wafuasi wa Dkt Slaa au Chadema lakini napenda kuwakikishia kuwa endorsement hii haimaanishi kashfa,matusi,dharau au mambo yasiyofaa dhidi ya wagombea wa vyama vingine.Kuweka wazi msimamo wangu haimaanishi chuki dhidi ya vyama hivyo na wagombea wake bali ni imani yangu kuhusu nani anayeweza kuipatia Tanzania “uhuru wa pili” (mapambano dhidi ya Watanzania wenzetu wanaotafuna raslimali zetu zaidi ya alivyofanya mkoloni).

Mwisho,nawahamasisha bloga wenzangu na vyombo vingine vya habari kwa ujumla kuweka bayana misimamo yao ili kuepuka lawama zinazoweza kujitokeza pale habari za vyama flani zinaponyimwa fursa katika vyombo hivyo.Endorsement ya mgombea au chama ni jambo la kawaida katika nchi za Magharibi lakini hii ni mara ya kwanza kwa chombo cha habari cha Kitanzania kufanya hivyo,na kwa hakika najivunia kuweka historia hiyo.

6 Aug 2010

Usikose kutembelea blogu ya Dokta Wilbroad Slaa, mgombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).Blogu hiyo inayoitwa Friends of Slaa- Marafiki wa Slaa  inapatikana katika anuani ya mtandao http://www.friendsofslaa.blogspot.com

21 Jul 2010

Kuna habari kuwa huenda Katibu Mkuu wa Chadema,Dkt Wilbrod Slaa,atakuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.Kwa mujibu wa gazeti la Daily News,Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana jana jijini Dar imemuomba Dkt Slaa kugombea nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa habari hizo,Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,Zitto Kabwe,alinukuliwa akisema "Kamati Kuu (ya Chadema) imemuomba Dkt Slaa kuwa mgombea wa chama (katika nafasi ya urais)".Hata hivyo,Zitto alieleza kuwa uamuzi wa Kamati hiyo Kuu sio wa mwisho kwani itabidi mgombea urais wa chama hicho athibitishwe na Mkutano Mkuu wa chama hicho ambao umepangwa kufanyika Agosti 10.Kadhalika,Zitto hakuweza kueleza kama Dkt Slaa,ambaye gazeti hilo halikufanikiwa kumpata kuthibitisha habari hizo, amekubali ombi hilo au la.

Hata hivyo,vyanzo vya gazeti hilo katika kikao hicho (kilichokuwa kinaendelea wakati gazeti hilo linaenda mtamboni) vinaeleza kuwa Dkt Slaa,ambaye licha ya Ukatibu Mkuu wa Chadema ni Mbunge wa Karatu kwa tiketi ya chama hicho, amekubali ombi hilo.Habari hiyo ya Dkt Slaa kukubali ombi la kugombea urais kwa tiketi ya Chadema imeandikwa pia kwenye mtandao maarufu kwa habari na mijadala makini,Jamii Forums.

Dokta Slaa amejikusanyia umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi.Japo ni mapema kubashiri nafasi yake katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu,ni dhahiri kuwa iwapo atasimama kama mgombea wa Chadema anaweza kutoa upinzani mkubwa kwa mgombea wa CCM,Rais (wa sasa) Jakaya Kikwete hususan katika namna chama hicho tawala kilinavyoonekana kama kichaka na hifadhi ya ufisadi na mafisadi.


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.