25 Oct 2010Siku moja nilikuwa na mazungumzo na babu mmoja wa Kiskotish.Kwa vile ilikuwa ni safari ya masaa kadhaa kwenye treni kutoka mji mkuu wa Uingereza,London kuelekea mji wa kaskazini mashariki mwa Scotland,Aberdeen,tulipata wasaa wa kuongea mengi.Babu huyo ameshawahi kukaa Tanzania,na anajua maneno mawili matatu ya Kiswahili.Swali moja aliloniuliza,na ambalo limeendelea kuumiza kichwa changu hadi leo ni kwanini Tanzania ni masikini licha ya utajiri mwingi ilionao na watu wakarimu,wapenda amani na wenye kiu ya maendeleo.Sio siri,nilijiumauma kutoa jibu la kueleweka.

Uzuri kuhusu hawa wenzetu ni kwamba hawajui kumwonea mtu aibu.Babu huyo alinieleza waziwazi kuwa nimeshindwa kumpa jibu la kuridhisha sio kwa vile sifahamu kwanini Tanzania ni masikini bali nimeona aibu tu ya kutoa jibu sahihi.Na huo ni ukweli.Nilijua nikimwambia kwamba tatizo kubwa kwa maendeleo ya Tanzania ni uongozi,angeweza kuniuliza "kwani viongozi hao ni wakoloni au Watanzania wenzenu?"

Katika maongezi yetu babu huyo alinipa fundisho moja muhimu ambalo nadhani sote tunapaswa kulitilia maanani.Alinieleza kuwa zamani hizo wakati Uingereza inajengwa,Waingereza hawakuwa wanafikiria kuhusu mahitaji yao tu bali pia mahitaji ya vizazi vijavyo.Alifafanua kuwa kadri anavyoelewa,Waingereza wengi wanajibidiisha sio tu kwa ajili ya leo bali hata miaka 200 ijayo.Akanipa mfano wa namna walivyojenga treni za chini ya ardhi,hospitali zao kuubwa kama kijiji kizima,vyuo vilivyotapakaa sehemu kubwa za miji na maendeleo mengineyo.

Akatanabaisha kuwa wengi wa walioshiriki katika ujenzi huo wa Uingereza ya leo kwa sasa ni marehemu.Na akanikumbusha kuwa japo wakati wanajituma kujenga nchi yao walikuwa wanafahamun kuwa watafaidi matunda ya jitihada zao kwa muda mfupi tu kabla Mungu hajawachukua lakini hiyo haikuwakatisha tamaa kwa vile walifahamu kuwa vizazi vijavyo vingetaraji waliowatangulia wangetumia nafasi zilizokuwepo muda huo kuwaandalia mazingira mazuri ya kuishi.

Nifupishe stori.Jumapili ijayo tuna Uchaguzi Mkuu ambao binafsi nauona kama tukio muhimu kabisa kwa historia ya nchi yetu.Takriban miaka 50 baada ya uhuru kuna wenzetu wengi tu ambao wanaishi katika mazingira mabovu kuliko kabla ya ujio wa mkoloni.Lakini pia,kuna wachache ambao angalau wanamudu mahitaji ya msingi ya kila siku.Ni kundi hili ambalo ningependa kuelekeza rai yangu kwao.

Hebu tutafakari stori za huyo babu niliyekutana nae kwenye treni.Laiti kizazi chao kingeridhika na hali waliyokuwa nayo wakati huo basi huenda Uingereza ya leo isingekuwa imepiga hatua kama ilivyo sasa.Laiti wangekuwa wabinafsi wa kufikiria maslahi yao tu wasingejihangaisha na mipango ya maendeleo ambayo matunda yake yangeonekana baada ya vifo vyao.Lakini kwa vile waliweka mbele maslahi ya jamii badala ya maslahi binafsi,hawakusita kujenga msingi wa jamii ya Uingereza kwa wakati huo na karne kadhaa baadaye.

Tunaweza kuendelea kuwalaumu wakoloni kwa kukwaza maendeleo yetu.Lakini wakoloni walishaondoka takriban miaka 50 iliyopita.Sasa badala ya kupiga hatua,kuna nyakati tunajikuta tunarudi nyuma zaidi ya wakati wakoloni wanaondoka.

Na japo siwatetei wakoloni,lakini angalau wao walikuwa na excuse.Hawakuwa Watanzania wenzetu.Hawakuwa na uchungu na nchi yetu wala vizazi vijavyo.Vipi kuhusu viongozi wetu wa sasa?Hivi sio hawa waliosomeshwa bure buleshi lakini leo wanakataa katakata kuwa elimu ya bure haiwezekani?Kama iliwezekana wakati huo ambapo hatukuwa na maendeleo ya kutosha,kwanini ishindikane wakati huu ambapo tumeweza kugundua vyanzo mbalimbali vya mapato?

Tukiridhika na mishahara inayotuwezesha kwenda Twanga Pepeta kial wikiendi,au vikao vya bia kila jioni kisha tukasahau kuwa kuna wenzetu (na wengi wao ni ndugu zetu kabisa) huko vijijini hawana uhakika wa kifungua kinywa,wamesahau ladha ya chumvi kwenye mlo kwa vile chumvi imegeuka anasa japo iko kibwena huko Uvinza,sukari imegeuka muujiza hata huko Kilombero ambako wana kiwanda cha sukari na miwa inayozalisha sukari inaozeana mashambani.Kuna wenzetu ambao wali nyama au ugali nyama ni milo inayowezekana kwenye sherehe,misiba au wanapobahatika mara moja kwa mwaka kupelekwa hotelini licha ya maelfu kwa maelfu ya ng'ombe,mbuzi,kondoo na wanyama pori lukuki,sambamba na mchele,mahindi,mihogo,mtama,nk.

Sasa hali hii itaendelea hadi lini?Tunaweza kupuuza shida za wenzetu hawa ambao ni wengi kuliko sie lakini ni dhahiri kuwa ndani kabisa ya nafsi zetu tunateseka tunapokumbuka kuwa punje za wali tunazosafisha kwa minajili ya kuzitupa zinahitajika kwa udi na uvumba katika nyumba moja au nyingine.Hivi kama hawa "wazungu" na ubinafsi wao (hawa familia ni baba,mama na watoto.Habari za shangazi,binamu,mjomba,babu,bibi ni kama kachumbari kwenye mlo: inapendeza lakini sio muhimu). waliweza kuvikumbuka vizazi vijavyo na hivyo kujenga nchi zao hadi kufikia zilipo leo,wakni sie ambao familia ni zaidi ya mume,mke na watoto?

Kuna wenzetu wanaokumbatia mafisadi kwa vile tu wanahofia kuwa mafisadi hao wakiondoka basi nao hawatakuwa na namna ya kumudu maisha yao.Hiyo si kweli kwani hata nyakati za mkoloni kuna waliokuwa wanatumikia wakoloni na kuwakandamiza waafrika wenzao,lakini watu hao waliendelea kuwa hai,huru na kumudu maisha yao...tena kwa njia halali pasipo hofu ya kuonekana wasaliti.

Kura utakayopiga Jumapili ijayo ni zaidi ya kura yako binafsi.Ni kura kwa ajili ya memba wote wa ukoo wako (ambao katika mazingira ya kawaida kuna wengi tu wenye kuhangaika na maisha ya kila siku),rafiki zako wa zamani ambao baada ya kukosa nafasi ya kuendelea na masomo wakajaribu bahati zao kwenye kilimo lakini jitihada zao zinakwazwa na vyama vya ushirika vinavyojua kukopa zaidi kuliko kuuza mazao.Ni pamoja na wale ambao waliamua kufany kazi za wito kama ualimu au uuguzi lakini sasa wanajiuliza kama "wanafanya kazi ya Kanisa" kwani licha ya mshahara kuwa kijungujiko lakini pia hauna uhakika wa kufika katika muda stahili.Kuna wale jamaa zako walioamua kujiari lakini wanaandamwa na polisi na kubambikiwa kesi za bangi,uzururaji,nk kila wanaposhindwa kutoa rushwa kwa askari au mgambo.

Wafikirie hawa wakati unapiga kura.Weka kando mafanikio yako binafsi.

Na kwa wale wanaoteseka kwa vile watawala wamekuwa bize zaidi na kuongeza idadi ya magari yao ya kifahari,kuongeza idadi ya mahekalu yao,kuongeza idadi ya nyumba ndogo zao,na matumizi mengine ya anasa kama hayo,huu ndio wakati wenu wa kulipa kisasi.Kama mlibebwa kwa malori kwenda kwenye mkutano wa Kikwete au mgombea mwingine wa CCM,well,hakuwaomba bali walijipendekeza wenyewe.Hivi hamsangai ukarimu huu wa ghafla umetoka wapi?Hamjiulizi kuwa wakati mnahangaika kupeleka wagonjwa na akina mama wajawazito hospitalini kwa vile hakuna magari ya vimulimuli wao walikuwa wantembelea magari ya thamani huku wakiwatimulia vumbi,lakini ghafla leo wanawabeba kwenye malori mkawasikilize.MSIDANGANYIKE.Mkishawapa kura,hamtawaona tena mpaka mwaka 2015.

Japo nimesema kuwa uchaguzi huu una umuhimu wa kipekee,lakini ni muhimu kukumbuka kuwa tulikuwa na chaguzi kama hizi huko nyuma,na wa karibu zaidi ni wa mwaka 2005.Hivi hamkupata matumaini Kikwete alipoahidi maisha bora kwa kila mmoja wenu.Je mmeshayaona maisha hayo bora?Kama bado,kwanini mnataka kumwamwini tena safari hii japo amekaa madarakani miaka mitano na ameshindwa kutimiza ahadi aliyoweka mwenyewe bila kushikiwa mtutu wa bunduki (hakulazimishwa)?

Na yule mbunge aliyeahidi miujiza lakini akaishia kuongeza kitambi chake na idadi ya watoto kupitia hawara zake,kwanini umpe tena kura?Unataka aendelee kukusanifu?Maana ulifanya makosa mwaka 2005 ukiamini kuwa ahadi zake zilionyesha anakujali.Lakini miaka hii mitano iliyopita inatosha kukuthibitishia kuwa huyo ni tapeli wa kisiasa,na hakuna tapeli anayeaminika.Lakini sio yeye tu bali hata chama chake.

Hesabu umri wako.Halafu jiulize lini ulianza kuisikia CCM.Kumbuka magapi wameahidi katika miaka yote hiyo uliyokuwa unawafahamu.Linganisha maendeleo yako na hao wenye CCM halisi.Kwanini bado unaendelea kukiamini chama hiki?Kama waliahidi 1995 hawakufanya,lakini wakarejea tena kuahidi mwaka 2000,na hawakufanya.Na bila aibu wakarejea tena mwaka 2005,na safari hii wakiahidi kuwa wanajua matatizo yako na ya familia yako.Wakaahidi pia kuwa maisha yako yatakuwa bora kwa vile hilo linawezekana.Na wakaonyesha namna watakavyowezesha maisha bora kwa kila Mtanzania.Je wametimiza?

Lakini pengine wameshindwa kutimiza kwa sababu za kibinadamu.Sasa kwanini badala ya kukuomba msamaha na kueleza kwanini wameshindwa kukuletea maisha bora,wanakufanya mjinga kwa kukuahidi yaleyale waliyoahidi mwaka 2005 na kutoyatekeleza?Kumbuka: ukiwachagua tena hutokuwa na sababu ya kuwalaumu kwani wameshakuthibitishia kwa miaka kadhaa kuwa hawawezi kukusaidia lakini ukaendelea kuwaamini.Sasa,japo inakera kuona unaendela kuwaamini matapeli hawa,ni muhimu kukumbushana pale tunapokosea.Kufanya kosa si kosa bali kurejea kosa.Na umesharejea makosa hayo mara kadhaa.Sasa umefika wakati wa kusema IMETOSHA.

Nimalizie kwa kukumbusha kuwa katika uchaguzi huu tumebahatika kumpata Nyerere wa pili.Huyu ni Dokta Wilbroad Slaa.Kama ambavyo Nyerere alijitoa mhanga kuhakikisha mkoloni anaondoka,Dokta Slaa amethibitisha kuwa ni mzalendo mwadilifu ambaye ameamua kupambana na mafisadi hadi watokomee.Kama aliweza kuwakalia kooni mafisadi alipokuwa mbunge tu,jiulize atakayofanya atapokabidhiwa urais.Wakati akiwa mbunge silaha yake pekee ilikuwa ni maneno,lakini tukimkabidhi dola atakuwa na nyenzo mbalimbali za kuipeleka nchi yetu inapostahili kwenda.

Usihadaishwe na wasiwasi kuhusu wizi wa kura.Kuiba wataiba lakini ili waweze kuiba za kutosha kuwabakiza mafisadi madarakani itategemea zaidi idadi ya kura tutakazompa Dokta Slaa.Ni rahisi kuiba kura chache lakini ni vigumu kuiba maelfu au mamilioni ya kura.Wingi wa kura kwa Dokta Slaa utakuwa silaha muhimu ya kuwatia aibu mafisadi katika kujaribu kuchakachua kura au matokeo ya uchaguzi huo.

INAWEZEKANA.TIMIZA WAJIBU WAKO

4 comments:

 1. Mkuu ni heri ya mkoloni mzungu kuliko ukoloni wa mwafrika kwa mwafrika au mtanzania kwa mtanzania. Nchi ya Finland haijawahi kutawala nchi yeyote bali wao walipata kutawaliwa na Warusi na Waswidi.
  But today Finland is the most prosperous country in the whole world. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba historia ya kutawali isiwe ni kigezo na visingizio vya umasikini wetu. Umasikini wetu chimbuko lake ni Uongozi mbovu.

  ReplyDelete
 2. Sisi siyo maskini. Tumefanywa maskini na viongozi wenye umaskini wa uongozi na mawazo mgando. Wengi wao tunawaita mafisadi kwa heshima tu. Ukweli wao ni mafisi si mafisadi tu. Ni zaidi ya hapo. Wana roho mbaya akili mbaya tabia mbaya nia mbaya mawazo mabaya na kila kitu kibaya tu. Kuirejesha CCM madarakani ni dhambi ambayo hata shetani hawezi kuisamehe. Nawasikitikia wale misukule ya CCM yaani wanaojiita wapenzi na mashabiki. Hawa ndiyo chanzo cha maafa kuliko hata CCM yenyewe maana bila wao CCM si chochote si lolote.
  Askari wetu nao wanaotumiwa kama nepi inabidi mwaka huu wakengeuke na kujikomboa kwa kughahamu kutumia na CCM kama kawaida kuiba kura.

  ReplyDelete
 3. Mpendwa wangu Evarist Chahali na wana chadema wote popote mlipo.nawakumbusha tu kuwa imebaki siku moja au masaa kadhaa hivyo nyote mnaombwa kupiga kura kesho...mimi nitampigia JK na wabunge wake...wewe je

  ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.