23 Oct 2010



Makala yangu katika jarida la Raia Mwema toleo la wiki iliyopita ililenga kuchokoza mjadala kuhusu "mashushushu".Nilijaribu kutengeneza mazingira ya kumwezesha msomaji kuhitimisha iwapo madai ya mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,Dokta Wilbroad Slaa,kuwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imesambaza Maafisa Usalam wa Taifa nchi nzima ili wamsaidie Kikwete kurejea Ikulu (wachakachue kura).Katika toleo la wiki hii la jarida hilo,jamaa mmoja anayejiita Almas Kajia ametoa majibu kwa niaba ya Idara yab Usalama wa Taifa.Nasema "anayejiita" kwa vile ameshindwa japo kuweka barua pepe yake au namba ya simu just in case ningehitaji kumjibu one to one.

Anyway,naomba nichapishe makala yake nzima,japo unaweza pia kuisoma katika jarida la Raia Mwema.

Kazi ya mashushushu ni usalama si kuhujumu uchaguzi
Almasi Kajia
Oktoba 20, 2010
RAIA Mwema namba 155 la Oktoba 13-19, 2010 liliandika makala iliyokuwa ikiuliza kama mashushu hutumiwa kuhujumu uchaguzi.
Makala hiyo iliyochapishwa katika safu hii ya Raia Mwema Ughaibuni ya Evarist Chahali anayeishi Uskochi, ilikuwa na kichwa kidogo cha habari “Dk. Slaa aibua madai fikirishi”.
Mashushu ambao mwandishi anaulizia kama wanaweza kutumiwa kuhujumu uchaguzi ni maafisa Usalama wa Taifa wa Tanzania na uchaguzi anaozungumzia ni Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010.
Katika makala yake, mwandishi ameanza kwa kujisifu kwamba ana ufahamu wa kutosha juu ya Usalama wa Taifa au intelijensia, ameisomea fani ya Usalama wa Kimataifa na kwamba anaijua vizuri Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania.
Pamoja na sifa, tambo na majigambo yote haya, mwandishi anasema anachojaribu kuandika hakisemeki au hakizungumziki na anasema kwa kutekeleza kile anachotaka kukifanya lazima tujiulize maswali magumu na pengine ya kuogofya.
Napenda niseme kwamba kuanzia mwanzo kabisa katika kupitia makala yote ya mwandishi huyu hakuna chochote alichoandika ambacho hakizungumziki na hakuna swali lolote gumu wala la kuogofya ambalo amelidhihirisha katika makala yake.
Nilichogundua katika makala yake ni kuwa kama huo si mtindo wake wa kuwavutia wasomaji napenda kuamini kwamba yeye ni mshika bango wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ameendeleza tu yale yanayofanywa na chama hicho yasiyofurahisha kila mtu, ni mambo yanayorandana na afanyayo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mgombea urais kupitia chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Hata hivyo, ameeleza mambo ya msingi sana katika kuthibitisha kwamba amejifunza fani ya usalama wa kimataifa kwa kusema kwamba uimara wa taifa lolote duniani unategemea uimara wa idara yake ya usalama wa taifa na kulegalega kwa mambo katika nchi yoyote duniani kunaashiria upungufu wa idara hiyo.
Lakini katika hali ambayo sikutarajia, mwandishi anakiri kwamba kwa miaka mingi sasa, Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania ni miongoni mwa idara bora duniani. Hilo pengine lilitokana na maelezo yake kwamba anaifahamu vya kutosha Idara hiyo.
Wapo waandishi wengine ambao wamekuwa wakiandika habari kama hizo, lakini wakiwa na mitazamo inayotofautiana. Jambo ambalo linanishangaza au pengine linanitia shaka katika makala yake ni kama Idara anayoisifu hivyo imekwishakupoteza sifa hizo na kama ni hivyo je, hiyo ndiyo sababu ya yeye kuanza kuwa na shaka kama Idara hiyo sasa inaweza kutumika kuhujumu matokeo ya uchaguzi?
Amesema idara ya usalama wa taifa duniani kote hufanya kazi kwa siri kubwa kabisa na usiri huo ni sehemu ya utekelezaji wa kazi zake. Anasema usiri ni muhimu kabisa na wa lazima katika ukusanyaji wa taarifa nyeti.
Jambo ambalo wasomaji walitakiwa walijue kutoka kwa mwandishi ni ikiwa usiri wa Idara ya Usalama wa Taifa ndio utakaotumika kuhujumu matokeo ya uchaguzi na kama hilo ndio lengo ni kwa nini Idara hiyo ifanye hivyo, kwa kutumiwa na CCM au kwa utashi wake yenyewe?
Mwandishi amezitaja nchi za Uingereza na Marekani kama mifano kwamba mara chache wakuu wa vyombo vya intelijensia huitwa kutoa ufafanuzi kwa mambo yanayohusu usalama wa Taifa wa nchi hizo.
Kwamba aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Central Intelligence Agency (CIA) ya Marekani, George Tennet aliitwa kueleza juu ya ushahidi kwamba Iraki ilikuwa na mipango ya kutengeneza silaha za maangamizi.
Anasema katika nchi hizo mbali na kuondoa katika orodha baadhi ya mambo ambayo ni siri, mabunge yao yana kamati zinazoshughulikia masuala ya usalama na zinawaita viongozi wa idara hizo kutoa ufafanuzi katika masuala yanayohusu intelijensia pale inapokuwa lazima kufanya hivyo.
Suala hili halifanyiki kwa siri anayoizungumzia mwandishi na kama nia yake ingekuwa ni kulifahamu hilo angemuuliza Dk. Slaa ambaye amekuwa mbunge kwa miaka 15 na anafahamu kwamba ipo Kamati ya Bunge ambayo inafanya kazi kama zile zinazofanywa na mabunge ya Uingereza na Marekani.
Amerejea swali lake kama Idara ya Usalama wa Taifa inaweza kutumiwa na CCM kuhujumu uchaguzi na akaunganisha masuala mengine mawili kwamba; hakuna ofisa usalama atakayefurahi na tuhuma za Slaa zikibainika kama ni uongo na Watanzania watakuwa na hofu kama itabainika kwamba tuhuma hizo ni za kweli.
Swali kwamba Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa wapi wakati ukitokea ujambazi wa EPA na je, Idara hiyo ilikuwa ikifanya nini wakati mikataba ya kifisadi ikitokea. Mwandishi anajihami mapema kwa kusema kwamba maswali haya yatazua uhasama kati yake na idara hiyo.
Labda niseme tu kwamba si maofisa wa Idara ya Usalama tu watakaochukia bali Watanzania hawatafurahi kuona tuhuma hizi za Dk. Slaa ambazo ni za uongo zinazidi kuendelezwa na watu wenye hadhi za kisomi kama mwandishi mwenyewe kwa ahadi ambazo nina hakika hazitatimia.
Wananchi wa kawaida ambao wamekwishakuelewa kwamba Chadema ina tabia ya kuzua mambo na ambao wanaamini kwamba nchi hii ina ulinzi wa kutosha, hawawezi kuingiwa na hofu kwa kutegemea tu propaganda za askari wetu kutoka Uskochi.
Ninachotarajia mimi ni kwamba Idara ya Usalama wa Taifa haitamjibu mwandishi. Nililo na uhakika nalo ni kwamba itanyamaza bila kusema chochote kwa kuwa mwandishi mwenyewe amesema kuwa Idara hiyo inafanya kazi zake kwa siri kubwa kabisa.
Ninahisi kwamba mara zote Idara hii inaacha wajinga wajielimishe wenyewe. Swali kwamba Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa wapi wakati ufisadi wa EPA ukitokea sio la msingi bali jambo la muhimu ambalo Mtanzania wa kawaida anaweza kusema ni kwamba suala la EPA limeshughulikiwa sana na Serikali na baadhi ya wahusika wamefikishwa mahakamani.
Naamini kwamba ufisadi si sera ya Serikali wala ya Chama tawala-CCM- na ni vyema ikubalike kwamba, kwa sasa pengine tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ufisadi ni suala la mtizamo na hulka ya mtu kuliko kuonekana kama mtindo wa maisha wa baadhi ya Watanzania.
Serikali ya Tanzania inazingatia utawala wa sheria na tungejali sana suala la mtu kumiliki vitu kama gari, nyumba nzuri, vitu ambavyo wengine hawana, mtu huyu akaonekana kuwa fisadi, Watanzania wengi wangeishia jela.
Amezungumza mengi ikiwa ni pamoja na ikiwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye shughuli zake si za siri anaonyesha wazi kuipendelea CCM kwa kuingilia majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hali ikoje katika Idara ya Usalama wa Taifa.
Nilijaribu kuhoji pale mwanzo kama mwandishi alikuwa anahisi nini juu ya usiri aliousifia sana, usiri wa Idara ya Usalama wa Taifa, kama usiri huo ndio utatumika kuhujumu matokeo ya uchaguzi.
Kinachojidhihirisha hapa ni kwamba mwandishi anataka Watanzania waamini kwamba Idara ya Usalama wa Taifa kwa kutumia kigezo cha usiri, inaingilia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama alivyofanya Msajili wa Vyama vya siasa kwa nia ya kuhujumu matokeo ya uchaguzi (kama kweli alifanya hivyo).
Inaonekana anaamini kwamba usiri huu ndiyo utakaotumika kukipatia ushindi CCM kwa kuihujumu Chadema.
Lakini kila mtu anajua kwamba kazi ya Idara hiyo kama chombo cha usalama ni kuhakikisha Usalama wa Taifa ambao ni pamoja na uchaguzi kuendeshwa kwa amani, si kuuhujumu.
Inavyoonekana, mwandishi mara zote anaiangalia Idara ya Usalama wa Taifa kama chombo chenye uamuzi wa mwisho kwa kila kitu na anasema kwamba Idara hiyo inamfahamu mmiliki wa Kagoda, ama kwa njia zisizo rasmi au njia rasmi.
Hivi kama kweli kazi za Idara hiyo ni za siri ni vipi itathubutu kutekeleza au hata kama imetekeleza, ieleze wazi kwamba imefanya hivi na hivi kwa watuhumiwa wa aina yoyote, achilia mbali wa Kagoda.
Binafsi nina shaka juu ya uelewa wake wa usalama wa kimataifa na ufahamu wake juu ya Idara hii ambayo anadai ni moja ya idara bora duniani na inayotenda kazi zake kwa usiri.
Ni utaalamu gani anaozungumzia mwandishi unaoweza kutumika kushinikiza Serikali kwa njia zilizo rasmi na zisizo rasmi. Nimejaribu kudadisi kwa wajuzi wa masuala ya Usalama wa Taifa, nikaambiwa kwamba kazi ya idara hiyo duniani kote ni kutoa ushauri na si kushinikiza kama mwandishi anavyotaka tuamini.
Nilitaka kujua kama ameifahamu Idara hiyo vipi kwa kuhadithiwa au pengine alishawahi kuwa mtumishi kwenye chombo hicho nyeti? Kwa yote mawili nilipata jibu moja kwamba hata kama alihadithiwa au alifanya kwenye Idara hiyo, kulingana na kanuni za usiri ambao ameukiri yeye mwenyewe, hawezi kusimama hadharani na kusema kwamba amekuwa mtumishi wa chombo hicho.
Anasema pia kwamba idara ya usalama wa taifa kote duniani ni kama nusu jeshi (paramilitary) na viongozi wake wanaogopwa kupindukia na uamuzi wao hauhojiwi.
Katika udadisi wangu, niliambiwa mambo mawili kwamba kuogopwa kupindukia kunatokana na usiri wa idara zenyewe na nikaamini kwamba usichokijua ni sawa na usiku wa giza.
Kwamba wanaoiogopa idara ni wasioifahamu na anachotaka kusema mwandishi ni kwamba wasomaji waendelee kuiogopa Idara yao ya Usalama wa Taifa.
Nafikiri hilo si la lazima kwa sababu wananchi wana haki ya kukifahamu chombo ambacho kwanza kinahakikisha kuwa Taifa ni salama na kinatumia kodi za wananchi katika utendaji wake wa kazi wa kila siku. Hakuna sababu ya kukiogopa, ni chombo chao na ambacho kimewekwa kisheria.
Mwandishi ametaka pia wasomaji wake wapime madai fikirishi ya Dk. Slaa ambayo yametolewa kama tuhuma ikiwa hadithi au ni kitu kinachowezekana. Ukiyavulia nguo maji sharti uyakoge na kwa hilo mwandishi haamini kwamba anachosema Dk. Slaa ni hadithi tu, anaamini kwamba ni ukweli ingawa hoja yake imejengwa katika nadharia tu.

Ukisoma kwa makini utagundua kuwa Bwana Almasi Kajia (tukiamini kuwa hilo ndilo jina lake halisi) ameelemea zaidi kwenye kujadili wasifu wangu kama mwandishi badala ya kujibu maswali muhimu niliyotoa katika makala ya mwanzo.Lakini kwa vile sipendi malumbano,naweza kufupisha kwa kuhitimisha kuwa makala yake imeshindwa kuthibitisha kuwa HAIWEZEKANI IDARA YA USALAMA WA TAIFA KUTUMIWA NA SERIKALI YA KIKWETE KUCHAKACHUA KURA.Yah,anaweza kusema madai ya Dokta Slaa ni nadharia kwa vile hata fedha za EPA zilipoibiwa tuliambiwa kuwa huo ni uzushi tu (na wahusika wakatishia kumfikisha Dokta Slaa mahakamani).

Haihitaji taaluma ya usalama japo wa mgambo kutambua kuwa fedha za EPA ziliibiwa wakati taasisi zenye jukumu la kuzuwia zikiwa kazini.Mkataba wa kitapeli wa Richmond ulisainiwa wakati wenye jukumu la kuuzuwia wanakenua meno tu.Same story kuhusu Kiwira,IPTL,Buzwagi,Meremeta,Tangold na skandali nyingine za ufisadi.

Wakati naandaa makala hiyo sikutegemea pongezi kutoka kwa wahusika.Nafahamu kuwa hawapendi kukosolewa sio kwa vile wako sahihi bali wanatambua kuwa aina yoyote ile ya ukosoaji inawafumbua macho kuonyesha udhaifu na mapungufu yao.Na hawataki hilo lijulikane kwa vile linaweza kupelekea Nguvu ya Umma kudai majibu kwa nguvu.

Mafisadi wangependa sana kuona kila Mtanzania akiwa mbumbumbu.Wanasali kwa bidii kusijitokeza wahaini wa kuhoji maswali magumu.Si mmesikia tishio kwa gazeti la Mwananchi kwa vile tu haliandiki kile watawala wamezowea kusikia?Wameleweshwa na sifa kiasi kwamba ukiwakosoa ni sawa na kuwatukana.

Finally,naomba kuthibitisha kuwa nilipoandika kuwa naifahamu taasisi hiyo vizuri nilikuwa na sababu zangu za msingi.Sihitaji kufafanua kwa vile hayo ni mambo binafsi.Lakini they and I know very well kuwa hilo la kuifahamu vyema halina ubishi.Mambo mengine hayawezi kuzungumzwa hadharani.

Nilichofarijika ni kile alichowahi kutamka Rais wa zamani wa Marekani,George W.Bush kwamba "ukisema au kufanya jambo flani,kisha watu waka-react basi ujue ulichoongea kimewagusa" maana laiti ingekuwa upumbavu au uzushi tu,Bwana Almasi asingepoteza  muda wake kunijibu.

AJIKUNAYE UJUE KAWASHWA

5 comments:

  1. "Naamini kwamba ufisadi si sera ya Serikali wala ya Chama tawala-CCM- na ni vyema ikubalike kwamba, kwa sasa pengine tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ufisadi ni suala la mtizamo na hulka ya mtu kuliko kuonekana kama mtindo wa maisha wa baadhi ya Watanzania.
    Serikali ya Tanzania inazingatia utawala wa sheria na tungejali sana suala la mtu kumiliki vitu kama gari, nyumba nzuri, vitu ambavyo wengine hawana, mtu huyu akaonekana kuwa fisadi, Watanzania wengi wangeishia jela."

    Ndugu Almasi acha kusikiliza propaganda za mafisadi (kama wewe sio mmojawapo). ‘ufisadi’ unaozungumzwa katika siasa makini (sio za mitaani) kisawe chake halisi katika Kiingereza ni “kleptocracy”. Kwa vile unatumia mtandao, jaribu ku-google uone ‘’kleptocracy” ilivyofasiliwa. EPA & co ni mifano hai isiyohitaji shahada ya uzamivu kuitambua. Hakuna sera ya chama cha upinzani inayochukia au kuzuia watu kumiliki mali na kuwa matajiri kama ni kwa njia halali. Sera za akina Dr. Slaa zinalaani UFISADI kama ambavyo utakuta umefasiliwa uki-google ‘kleptocracy’.

    mlalahoi

    ReplyDelete
  2. kwa kifupi ndugu zangu mnapaswa mfahamu kuwa vyombo vyoote vya dola yaani polisi, jeshi, magereza ikiwemo idara ya usalama vinatekeleza maslahi ya watawala kuhakikisha wanatawala kwa usalama bila bugudha wala usumbufu, ukilifamu hili nadhani utakuwa na majibu mazuri ya nini bwana chahali anataka kukumbusha , na ni jambo hili ambalo kila mtu anaogopa kulizungumza, wakuu na watumishi wa vyombo vya dola hula kiapo cha utii kwa amiri jeshi mkuu ambye pia ni Rais wa jamuhuri ya muungano na pia kwa nafasi yake ni mwenyekiti wa ccm, kazi kwenu!!!

    ReplyDelete
  3. Iwapo aliyejibu hiyo makala yako ni kweli mtu wa usalama wa Taifa!!!!!!!!, Na kama hayo yametokana na baraka za Taasisi hiyo basi tunasafari ndefu sana ya kuwa na taasisi inayotekeleza majukumu yake kwa ajili ya umma........!!!!!!!!

    ReplyDelete
  4. Almas awe wa kweli au feki hana alilchoongea zaidi ya jazba na kujikomba kwa kundi la mafisadi. Sijui kama ametumwa. Kwanini asijibu hoja badala yake aanze kebehi ambazo nazo hazijui?

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.