29 Dec 2010Waziri Mkulo afanya kufuru
•  Akodi ndege kwenda Dodoma, aagiza shangingi toka Dar

na Bakari Kimwanga

WAKATI serikali ikisisitiza kutaka kupunguza gharama za matumizi kwa kuacha kuendelea kununua magari ya kifahari 'mashangingi', baadhi ya matumizi ya mawaziri yanatisha na kuwa mzigo kwa serikali.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano kwa muda mrefu sasa, umebaini kuwa wapo mawaziri na watendaji wengine wa serikali, wanaofanya ziara mikoani na kusafiri kwa ndege za kukodi, lakini hulazimika kuyaagiza mashangingi yao aina ya G8 kutoka Dar es Salaam hadi katika mikoa wanayokwenda kufanya ziara hata kama yatatumika kwa siku moja.

Mmoja wa mawaziri hao ni Waziri wa Uchumi na Fedha, Mustafa Mkulo, ambaye wiki iliyopita alikodi ndege kwa fedha za serikali kwenda kuhudhuria mahafari ya Chuo cha Mipango mjini Dodoma, lakini bado aliliagiza gari lake la uwaziri limfuate kutoka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kulitumia katika mji huo wakati Wizara ya Fedha na Uchumi, ina ofisi na magari mjini Dodoma.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano, ulibaini kuwa Desemba 17, mwaka huu, Waziri Mkulo mwenye dhamana ya fedha nchini, alikodi ndege ya Shirika la Tanzania Air, yenye namba za usajili 5HTZC na kuwasili katika uwanja wa ndege wa mjini Dodoma, majira ya saa nane mchana.

Wakati Waziri Mkulo akipasua anga la Dodoma kwa ndege ya kukodi, siku hiyo hiyo, dereva wake alilazimika kujaza mafuta shangingi la waziri huyo na kuweka kibindoni posho yake kumfuata bosi wake mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa habari hizo, ndege hiyo ilikodishwa kwa dola za Kimarekani 5,000, sawa na sh milioni 7.5.

'Mimi niko hazina, hivi sasa serikali haina fedha, kuna madeni mengi, kuna walimu zaidi ya 500,000 waliomaliza vyuo vya elimu ya juu tangu Mei mwaka huu wanasubiri ajira kutokana na ukosefu wa fedha, lakini hazina inafanya matumizi mabaya kila siku. Huku ni kulifilisi taifa bila sababu,' alisema mtoa habari wetu ambaye jina lake limehifadhiwa.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kuhusina na kashfa hiyo, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, John Haule, alikiri kuwa Desemba 17, mwaka huu, wizara yake ilikodi ndege kwa ajili ya kumuwahisha Waziri Mkulo kuwahi mahafali ya Chuo cha Mipango ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Haule ambaye alikuwa na wakati mgumu kutoa ufafanuzi huo, alisema walilazimika kufanya hivyo kutokana na umuhimu wa kazi alizokuwa nazo Waziri Mkulo siku hiyo kabla ya kuondoka kwenda Dodoma na kusisitiza kuwa ukodishwaji wa ndege ni jambo la kawaida kwa watendaji wa wizara hiyo.

'Hili ni suala la kawaida kabisa katika utendaji wa wizara yetu; siku hiyo ilikuwa lazima waziri aende Dodoma katika mahafali na kuzindua bodi ya chuo cha mipango, sasa kwa hili tulishirikiana na chuo chenyewe kulipia gharama za ndege kwa waziri,' alisema Haule bila kufafanua chuo kililipia kiasi gani na wizara kiasi gani.

Alisema gharama za kukodisha ndege hiyo ilikuwa dola za Kimarekani 350,000, sawa na sh milioni 5.2 na kusisitiza kuwa kiasi hicho kimelipwa na wizara kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango.

Alipoulizwa sababu ya wizara kulituma shangingi la waziri huyo kutoka Dar es Salaam wakati Dodoma kuna magari ya wizara hiyo yenye hadhi ya waziri, Haule alisema walilazimika kufanya hivyo ili Waziri Mkulo aende na kurudi kuwahi majukumu mengine jijini Dar es Salaam.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Naibu Waziri wa wizara nyeti inayochangia sehemu kubwa ya pato la taifa (jina lake limehifadhiwa), ambayo iliwahi kuwa katika wakati mgumu kutokana na kugubikwa na hoja ya ufisadi, alikumbwa na kashfa ya aina hiyo ya matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Waziri huyo akiambatana na msaidizi wake, alifanya ziara mkoani Kilimanjaro kwa kutumia usafiri wa ndege ya kampuni ya Precision, lakini alilitanguliza gari lake la uwaziri kutoka jijini Dar es Salaam hadi mkoani humo siku mbili kabla ambapo alilitumia kwa takriban saa sita tu na jioni alirejea Dar es Salaam kwa ndege hiyo na kuliacha gari lake likirudi na dereva pekee.

Gari hilo lilifika mkoani humo siku moja kabla ya waziri huyo na msaidizi wake kufika na mara alipotua katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), majira ya saa 2.30 asubuhi, tayari dereva wa gari lake alikuwa akimsubiri na kumpeleka katika ofisi ya wizara hiyo mkoani humo kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi.

Ilipofika majira ya saa 12 jioni siku hiyo hiyo, Naibu Waziri huyo ambaye ni mmoja wa mawaziri vijana na mara yake ya kwanza kuwa waziri baada ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko madogo ya baraza lake, aliwasili tena KIA na msaidizi wake kwa ajili ya safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kwa ndege na kuliacha shangingi lake lililorudi siku iliyofuata.

Kwa hali hiyo, serikali ililazimika kulipa posho ya siku tatu kwa dereva huyo na gharama za mafuta yaliyotumika kuliwezesha gari hilo kusafiri kwenda na kurudi mkoani Kilimanjaro.

Malalamiko ya matukio kama hayo, yaliwahi kutolewa bungeni na Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee (CHADEMA) wakati akichangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba kigogo mmoja mkoani Kigoma, alialikwa kwenye semina iliyofanyika mjini Bagamoyo na kusafiri kwa ndege, lakini alilitanguliza shangingi lake wiki moja kabla ya yeye kuwasili.

Halima ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kawe (CHADEMA), alisema gari hilo lilitumika kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na mwisho wa semina, alilitumia kumfikisha katika uwanja huo wa ndege na gari hilo lilisafari kurudi Kigoma baada ya kigogo huyo kuondoka.

Mbunge huyo alilalamikia kuwa hali hiyo imekuwa ikitumiwa na viongozi wengi wa serikali na kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa makini kudhibiti matumizi ya aina hiyo kwa watendaji wake.

Mawaziri hao pia wamekuwa wakilalamikiwa kwa matumizi binafsi ya magari ya serikali kama vile kuyatumia kuwapeleka watoto wao shule katika safari nyingine binafsi ambazo hutumia mafuta ya serikali.

Wakati yakitumika kwa shughuli hizo binafsi, magari hayo hung'olewa namba za uwaziri na kubandikwa zingine, jambo ambalo linaelezwa na duru za kisiasa kama ni aina nyingine ya ufisadi.

Chanzo: Tanzania Daima

4 comments:

 1. Ustawi wa mmea wowote unategemea mizizi au mzizi mkuu...na hapa mzizi mkuu ni Jakaya Mrisho Kikwete kama alivyojipachika Ma-doctotirate degree na kujiita pia naye ni Dr Jakaya Kikwete. Yeye mwenyewe ni Mr kutenda Madudu na mafinyufinyu pia anatewa watu wanaofanana na yeye kutenda madudu....Tena nawajulisha wale wote waliokuwa wanapewa khanga na fulana kwenda kwenye mikutano ya kampeni ya CCM hiyo ndiyo gahrama yake...Na sasa mtalipa tena kwa kutmia damu zenu ninyi watazania wazembe wa kufikiria

  ReplyDelete
 2. TANZANIA! TANZANIA! KWANZA NAONA HATA TUBADILISHE JILA LA NCHI, NIKISOMA HABARI ZA TANZANIA NAONA KAMA NACHANGANYIKIWA!! UNASOMA HABARI KICHWA KINA PIGA KELELE?! YAANI HAWA MAFISADI WANATUUWA KWA KILA SABABU, HATA KAMA HAUPO NAO KARIBU, MZALENDO WA KWELI INAKUCHOMA SANA. HUU UJINGA, UPUNGUWANI NA VIFO VINAVYOWAKABILI WATANZANIA KWA SABABU YA MAFISADI!! MTANZANIA ANAKOSA DAWA ANAKUFA, WAZIRI WAKE ANAKODISHIWA NDEGE YA MILIONI 5!TUNAANZIA WAPI JAMA? HII NI PANGA KWA PANGA HII! HAMUONI WANATUPIGA MAPANGA HAWA WATU? YAANI TUNAHITAJI BIG CHANGE.

  ReplyDelete
 3. Tusipoung'oa mzizi mkuu "Kikwete" matawi yatarudi tena tu. Watanzania wanavuna walichopanda. Na hii miaka mitano itakua michungu sana maana anajua ndio miaka yake yamwisho na watu wake. Huyo raisi atakayekuja kama kweli anauchungu na Tanzania anakazi kubwa saana, na kama ni msanii kama JK atakuja kuambulia makombo. Ni hayo tu am so sick with this country!!

  ReplyDelete
 4. SICK TO THE LEVEL!

  ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube