24 Jan 2011

Makao Makuu ya MI6 jijini London
Makao Makuu ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jijini London

Mashirika ya ushushushu ya Uingereza,MI5 na MI6,leo yalitarajiwa kuieleza Mahakama Kuu ya hapa kwamba siku zijazo  taarifa za kiusalama zitazokusanywa nje ya nchi hazitawekwa hadharani kortini hata kama zimepatikana kwa kuwatesa watuhumiwa (torture).

Mwaka jana,mahakama ya rufaa ilitupilia mbali kesi kwa kile ilichokiita jaribio la kudhoofisha kanuni ya msingi ya sheria: mshtakiwa lazima aone na kusikia ushahidi uliotumiwa kujenga kesi dhidi yake.

Sasa mashirika hayo ya usalama wa ndani (security) na ujasusi (intelligence) yanapambana na uamuzi huo.Baadhi ya vyombo vya habari vya hapa,magazeti ya The Guardian na The Times,na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC)-chombo cha umma hicho kama TBC1,Daily News na Habari Leo-pamoja na vikundi vya haki za binadamu vya Liberty na Justice,vilitarajiwa kutoa hoja mbele ya majaji waandamizi kabisa wa hapa kuwa kama hoja ya mashirika hayo ya kishushushu ikikubaliwa,itabomoa nafasi ya kesi kuwa ya haki na kumomonyoa  imani ya umma kwa maamuzi ya mahakama.Mawakili wa taasisi hizo za habari na haki za binadamu walitarajiwa kudai kuwa kanuni hizo ni muhimu hasa panapokuwa na madai ya maafisa wasiomudu majukumu yao ipasavyo (incompetent) au kutenda makosa.

Shauri hilo linatokana na madai ya raia (citizens) sita na mkazi (resident) mmoja wa Uingereza waliokuwa wakishikiliwa katika jela ya kuhifadhi watuhumiwa wa ugaidi ya Ghuba ya Guantanamo,kwa kile wanachodai ushirika wa siri kati ya MI5 na MI6 na mamlaka za Marekani.Watuhumiwa hao waliyataka mashirika hayo ya ushushushu kuonyesha ushahidi wa nyaraka kuhusu ufahamu wa  mashirika hayo katika uamuzi wa siri wa Marekani kuwapeleka jela hiyo,na ushiriki wa MI5 na MI6 katika suala hilo.

Japo watuhumiwa hao wameshafikia makubaliano ya fidia inayokisiwa kuwa mamilioni ya pauni za Kiingereza  (baada ya kuachiwa kutoka Guantanamo),mashirika hayo ya kishushushu yanataka kuanzisha kanuni mpya kwamba hakuna taarifa ya kiusalama itakayowekwa hadharani kwenye kesi yoyote ile ya madai au ya jinai.Tayari MI5 na MI6 wameshaonyesha wasiwasi wao katika mgogoro wa kitambo sasa kati yao na majaji wa mahakama kuu juu ya shinikizo kwa mashirika hayo kuonyesha ushahidi wa kuhusika kwao katika mateso aliyopewa (mmoja wa watuhumiwa hao) Binyam Mohamed,mkazi wa Uingereza aliyeshikiliwa kwa siri katika jela nchini Pakistan na Morocco kabla ya kupelekwa Guantanamo.Majaji waruka pingamizi la aliyekuwa 'Waziri wa Mambo ya Nje' (Foreign Secretary) wa hapa ,David Miliband,na kuweka hadharani muhtasari wa taarifa za (Shirika la Ujasusi la Marekani) CIA kwa MI5 na MI6.

Kama mashirika hayo ya usalama na ujasusi yakishinda madai yao,taarifa yoyote ya kiusalama na/au kijasusi inayohusu kesi ya madai au jinai itaonyeshwa kwa majaji na waendesha mashtaka pekee na sio washtakiwa au hata mawakili wao.Badala yake,taarifa hizo zitaonyeshwa kwa "mawakili maalumu" waliohakikiwa kiusalama (vetted).

Mwaka huu, Serikali ya Uingereza inatarajiwa kuchapisha muswada kupendekeza kipengele cha sheria kinacholitaka Bunge kuzuwia ushahidi wa uliopatikana kwa njia za ushushushu kuwekwa hadharani kortini,hatua ambayo inapingwa na majaji.  

Habari hii nimeitafsiri (kadri nilivyoweza) kutoka toleo la jana la gazeti la The Guardian la hapa Uingereza.Lengo la kutafsiri na kuiweka habari hiyo hapa bloguni ni kutoka changamoto kwa vyombo vyetu vya habari-hususan vya umma-kusimamia haki za jamii.Wengi wetu tumekuwa tukihudhunishwa na namna TBC,Daily News na Habari Leo,taasisi za habari zinazoendeshwa kwa fedha za walipakodi (pasipo kujali itikadi zao za kisiasa) wanavyoendesha shughuli zao kana kwamba ni vyombo vya habari vya CCM.Ikumbukwe kuwa vyombo vya habari ni mhimili  wa nne wa utawala wa nchi (pamoja na Bunge,Mahakama na Serikali),na hivyo kuwa na wajibu wa kutopendelea au kuegemea upande wowote dhidi ya maslahi ya umma.
    

1 comment:

  1. Hiyo ndio kazi ya vyombo vya habari katika demokrasia zilizokomaa. Kwetu hapa Bongo, hilo haliwezekani hadi Katiba mpya isukwe na wananchi wenyewe. Mabadiliko ya kiutamaduni katika utendaji wa watawala (kuwajibika) hayawezi kuja bila Katiba mpya iliyotengenezwa kwa kushirikisha umma. Ninawashangaa wanazuoni wanaodai kuwa hakuna haja ya kulilia katiba mpya kabla ya kuwepo kwa maadili ya kitaifa!! Maadili ya kitaifa hayadondoki kama mvua au snow, bali yanajengwa na uwepo na usimamiaji mzuri wa sheria zinazotokana na katiba nzuri.
    wakatabahu.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube