24 Jan 2011



Kwa hakika inachosha kila unapoingia mtandanoni na kukutana na episode mpya ya sakata la Dowans.Tangu mwanzo ilishabainika Rais Jakaya Kikwete yuko upande gani katika ishu ya ujambazi wa waziwazi (daylight robberies) ulioshamiri kwenye sekta ya nishati.Lakini si vibaya kujikumbusha tumetoka wapi na uhusika wa Kikwete katika ufisadi unaokaribia kuadhimishwa kitaifa kwa tuzo kubwa ya mabilioni ya shilingi kwa kampuni ya kijambazi ya Dowans.


Muda si mrefu baada ya Kikwete kuingia madarakani,aliendeleza mlolongo wa porojo zake za kuwaletea Watanzania maisha bora kwa kulipatia ufumbuzi tatizo sugu la nishati ya umeme.Na hapo tunaweka kando uhusika wa Kikwete katika mkataba mwingine wa kitapeli unaoiwezesha kampuni ya IPTL kulipwa mamilioni ya shilingi hata wasipoipatia Tanesco mchango wa umeme katika gridi zake.

Huku baadhi ya Watanzania wakiendelea kuamini kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu,aliwaahidi kuwa tatizo la umeme litakuwa historia pindi itapowasili mitambo ya umeme kutoka nchini Marekani.Na hatimaye mitambo hiyo ikawasili kwa mbwembwe ikiwa imekodiwa dege kubwa la mizigo.Picha zikapigwa,wahusika katika radio,runinga, magazeti na blogu wakaripoti.

Lakini kama wasemavyo waswahili kuwa za mwizi arobaini,mitambo hiyo ikabaki kuwa mitambo tu.Kumbe sio tu ilikuwa bomu bali hata kampuni iliyopewa dili na Kikwete-RICHMOND HIYO- nayo ilikuwa bomu.Actually,ilikuwa ni kampuni yenye ofisi kwenye brifukesi.

Kikwete akaufyata kana kwamba si yeye aliyeutangazia umma kuwa mitambo feki ya richmond ingekuja kumaliza tatizo la upatikanaji wa nishati ya umeme.Lakini kwa vile Kikwete hakuwa peke yake kwenye dili hilo,swahiba wake wa karibu,na Waziri wake Mkuu kwa wakati huo,Edward Lowassa,akaamua kulivalia njuga suala hilo na kuanzisha jitiahada za makusudi kuzuwia mjadala wowote kuhusu utapeli huo.Katika harakati hizo,blogu hii ilikumbwa na zahma pale mwandishi wa habari wa Lowassa,Said Nguba alodiriki kuandika comments kali hapa bloguni akinishambulia Truly Yours baada ya mie kumkemea Lowassa kuhusu jitihada zake za kuzuwia mjadala wa Richmond Bungeni. 

Kadhalika,msimamo wangu na wa blogu hii kuhusu suala hilo ilipelekea kupewa karipio kali kutoka kwa aliyekuwa mwajiri wangu wakati huo huku bosi aliyenipigia simu kuwasilisha karipio hilo akihoji nimekuja Uingereza kusoma au kuandika habari za uchochezi.Kichwa maji huyu alijifanya haelewi kuwa mie nilikuwa najinyima muda wangu wa masomo ili kufanya kile mwajiri wangu alipaswa kukifanya in first place,na laiti angefanya basi leo hii tusingekuwa tunajadili malipo kwa mrithi wa Richmond,yaani kampuni ya kiharamia ya Dowans.Kwa sababu za kimaadili,siwezi kumtaja mwajiri huyo. 

Ofkoz,Nguba na bosi huyo walikuwa wanatekeleza tu wajibu wao uliokuwa unawawezesha kupeleka mikono yao kinywani.Hata hivyo,kile kile nilichokiasa kwenye makala iliwasukuma wazushi hao kunikaripia,kilitokea miaka miwili baadaye: Lowassa alilazimika kujiuzulu baada ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dr Harrison Mwakyembe kuchunguza sakata hilo la Richmond kukamilisha kazi yake.

Kufupisha habari,baadaye Richmond ikarithishwa kwa jambazi mwingine Dowans.Na muda wote huo Kikwete akaendelea kuuchuna kana kwamba kinachotokea hakihusiani na maamuzi yake finyu.Baadaye mjadala wa Richmond ukarejeshwa tena bungeni lakini kwa vile wahusika walishajipanga vyema kuukabili,na kwa vile CCM ilishajitambulisha kuwa ni kichaka cha mafisadi,mjadala huo ukamalizwa kishkaji.Hakuna aliyewajibishwa,na Watanzania kama kawaida yao wakaendelea na maisha yao kana kwamba hakuna fedha zilizoibiwa.

Kelele za hapa na pale zilikuwepo,lakini kimsingi zilikuwa kama kelele za kutimiza wajibu tu (talking for sake of hearing own voice).Ni katika kipindi hicho pia kukazuka mjadala nini kifanyike kuhusu mitambo feki ya Dowans.Baadhi ya wenzetu,kwa mfano Mbunge Zitto Kabwe,walishauri mitambo hiyo itaifishwe.Wengine wakasisitiza kuwa kutaifisha pekee hakutoshi pasipo kuwawajibisha waliotuingiza mkenge katika suala hilo.Wakati wote huo Kikwete aliendelea kujifanya bubu na kiziwi kuhusu ishu hiyo.

Lakini kabla kidonda hakijapona,zikasikika habari kuwa Mahakama moja ya Kimataifa imeipa ushindi Dowans na serikali kuamuriwa ilipe mabilioni kama fidia.Kichekesho,or rather matusi,ni ukweli kwamba habari kuwa serikali imeshtakiwa na Dowans zilifanywa siri.Na kama kuongeza uzito wa matusi,viumbe waliopaswa kuwa watetezi wa umma kupinga malipo kwa majambazi wa Dowans-hapa namaanisha Waziri wa Nishati William Ngeleja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Werema- wakaibuka kuwa watetezi wa Dowans.Uchizi,kulewa madaraka,sintofahamu au sheer ufisadi!!!???Yani mshtakiwa anakuwa bize kuhalalisha hukumu dhidi yake?Kwanini basi nguvu wanayotumia mafisadi hawa baada ya hukumu kutolewa haikutumika kuhakikisha wanashinda kesi husika (assuming kulikuwa na kesi kweli,maana kuna tetesi kuwa mahakama yenyewe ilikuwa katika mfumo wa mlo wa jioni hapo Movenpick).

Back to Rais wetu Kikwete.Ameendelea kuuchuna hadi majuzi.Awali,alipotuhumiwa kuwa ndio mmiliki wa Dowans,mpambe wake Salva Rweyemamu akakurupuka na kauli chafu kabisa dhidi ya mwakilishi wa umma,Dkt Willibrod Slaa,aliyeamua to call a spade a spade kwa kubainisha kwamba Kikwete ndiye Dowans.Siku chache baadaye Kikwete akamjibu Dkt Slaa kwa vitendo: akaagiza askari wake (through IGP Said Mwema) wapige hadi kuua wananchi wasio na hatia huko Arusha.

Lakini,again za mwizi arobaini.Juzi tumefahamishwa bayana kuwa kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokaa chini ya uenyekiti wa Kikwete kimeridhia malipo kwa Dowans.Huhitaji japo short course ya uchambuzi wa siasa kutambua kuwa laiti Kikwete angekuwa upande wa wananchi na hivyo kupinga malipo kwa kampuni hiyo ya kifisadi,Kamati Kuu isingethubutu kuridhia malipo hayo.Kwa hiyo at last Kikwete ameweza kuibua sura yake aliyoficha mchangani kwa ukimya wa kuzungumzia suala la Dowans,na ametujulisha bayana kuwa kamwe hawezi kukata mkono unaomlisha.Hawezi kuamuru Dowans isilipwe ilhali yeye ni mhusika mkuu katika ujio wa Richmond iliyorithiwa na Dowans.


Nihitimishe kwa kutoa wito kwa Kikwete na washirika wake wa Dowans kuwa sasa tumechoshwa na drama hii.Wameshaamua kujilipa,wajilipe.Hakuna haja ya kuendeleza mchezo huu mchafu wa kuigiza.In fact,hakukuwa na haja kwa CCM kutoa tamko la kuridhia malipo hayo kwani walishaamua mapema kuwa watailipa Dowans.Kwanini wasiilipe wakati inawadai fadhila?Actually,kwanini wasijilipe wakati wao ndio wamiliki wa kampuni hiyo?Wanasaini mikataba fyongo kwa makusudi ili baadaye waivunjue kisha wajishtaki mahakamani na kudai fidia,na hatimaye wajilipe.Yaleyale ya kununua bima ya moto kisha mnunuzi wa bima hiyo anachoma moto alichokiwekea bima,na kuishia kulipwa mara 1000 ya gharama halisi bima husika.

Sio kama nimechoka kupiga kelele dhidi ya ufisadi bali katika ishu hii ya Dowans naona kama kelele zetu zinamaliza sauti bure.Kwenda Mahakama Kuu kuzuwia malipo kwa Dowans ni wazo zuri,only if we forget nani anayewateua majaji tunaowapelekea kesi hiyo.Mnadhani kasi ya Kikwete kuteaua majaji ni coincidence tu?Anaweza kuwa dhaifu katika kuitumikia Tanzania ipasavyo lakini yuko makini sana katika kuhakikisha maslahi yake binafsi na ya washkaji zake hayaathiriwi kwa namna yoyote ile.

1 comment:

  1. Lakini ni kweli litakuwa ni historia ambayo watu hawataisahau ya kuibiwa na viongozi wa ngazi za juu, na pia kwa Tanesco kufanikiwa kuongeza gharama za kulipia huduma ya giza na kutokutoa umeme. Ni historia duniani kabisa, kupandisha gharama za kuwauzia watu giza.
    Viongozi wetu hueleza ukweli wao kwa kificho.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.