4 Nov 2011


Vigogo watafuna marejesho ya EPA
Thursday, 03 November 2011 21:27
Leon Bahati na Furaha Maugo
KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imebaini ufisadi mwingine wa mabilioni ya fedha kwenye marejesho ya zile zilizochotwa awali kifisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).Fedha hizo zaidi ya Sh50 bilioni zilizorejeshwa na Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuwa zitatumika kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo nchini, zinadaiwa kuchotwa kwenye Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kwa amri iliyotoka kwa vigogo serikalini.

Mkurugenzi wa TIB, Peter Noni alikiri jana mbele ya POAC kuwa sehemu ya Sh20 bilioni zilizotolewa na Hazina kwenda kwenye benki hiyo kwa ajili ya dirisha la kilimo, Serikali iliamuru zitolewe kama mkopo kwa wafanyabiashara ambao iliwataja kwa majina.

"Mbaya zaidi, baadhi ya wafanyabiashara waliopewa mikopo hiyo wanaonekana kukwama kurejesha, huku wakitoa ahadi ambazo hawazitekelezi," Noni alisema.

Wabunge wengi wa POAC walionyesha kushangazwa na jinsi serikali ilivyoingilia kati TIB na kuchagua watu ambao wanapaswa kupatiwa mikopo.Huku miongoni mwa wabunge hao wakisema wana taarifa za vigogo walioingia mlango wa nyuma na kuchukua tena fedha hizo katika mazingira ya kifisadi, waliendelea kumbana Noni kwa maswali.

Ingawa baadhi ya wabunge walimtaka mkurugenzi huyo wa TIB awataje kwa majini vigogo hao, Makamu Mwenyekiti wa POAC, Deo Filikunjombe, alisita na kumtaka Noni asitaje majina hayo.

Miongoni mwa wabunge waliotaka majina ya vigogo hao yawekwe hadharani ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya aliyesema, “Nina habari kuwa baadhi ya vigogo walihusika katika kupata mikopo hiyo… Naomba uyataje majina yao.”

Filikunjombe, alisema hakuna haja ya kutaja majina ya vigogo hao ambao alisema miongoni yamo kwenye taarifa waliyopatiwa kuhusu utendaji mzima wa TIB.

Lakini Noni ambaye alikuwa anasaidiwa pia na wasaidizi wake kujibu baadhi ya maswali mazito yaliyoulizwa na wabunge, alisema hakuna tatizo kutaja baadhi ya kampuni zilizohusika kwenye mikopo hiyo ambayo sasa inawatoa jasho TIB.

Noni alitaja mbele ya kamati hiyo kuwa moja ya kampuni zilizochukua fedha hizo na sasa zinaonyesha wasiwasi katika kuzirejesha ni Simon Group Ltd.Nyingine ni kampuni tano za kuuza maua nje ya nchi zenye makao yake makuu mjini Arusha, zikiwepo Tengeru Flowers na Mount Meru Flowers.

Kuhusu Kampuni ya Simon Group, ambayo ilielezwa kuwa ilikopeshwa Sh5 bilioni Noni alisema; “Tumekutana nao mara kadhaa na kutoa ahadi lakini hawakuzitekeleza.”

Aliongoza kuwa kampuni za kuuza maua nje ya nchi zilieleza tatizo lililowafanya kushindwa kurejesha mikopo hiyo kulingana na makubaliano kwamba, ni hasara waliyoipata kutokana na mdororo wa kiuchumi duniani.

Alifahamisha kuwa kutokana na hali hiyo, Serikali iliwaonea huruma na kuwaongezea kipindi cha miaka miwili kulipa deni hilo, muda ambao pia umeonekana kutotosha.

Ila akaahidi kwamba TIB itaanza mchakato wa kuwabana wadeni hao kwa kunadi mali ambazo ziliwekwa rehani wakati wa kuchukua mikopo hiyo.

“Uandaaji na usafirishaji wa maua walisema unahitaji gharama kubwa… Walilazimika kupitia Nairobi (Kenya)… Serikali iliona huruma ikawaongezea kipindi cha kulipa deni hilo,” alisema Noni huku wabunge wengi wakionyesha shauku ya kuendelea kumbana kwa maswali.

Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa ni kwa nini TIB ilikubali kutoa mkopo kwa biashara ambazo hazitabiriki? Noni aliweka wazi kwamba, benki hiyo haikuhusika katika mchakato wa kuchambua na kuridhia mikopo kutolewa kwa kampuni hizo.

Filikunjombe ambaye ni Mbunge wa Ludewa, alishangazwa na jinsi Serikali ilivyoingilia uhuru wa TIB na kuweka wazi kwamba si mara ya kwanza Serikali kuingilia mashirika ya umma kiutendaji na kwamba, historia inaonyesha kila ilipofanya hivyo iliziingiza taasisi hizo kwenye mzozo.

“Serikali iliwahi kuingilia kati na kushawishi Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) kuingia mikataba (ya kuzalisha umeme wa dharura) na Richmond na Dowans na kusababisha mzozo,” alitoa mfano Filikonjombe.

Hivyo, akaonya TIB kuhusu kupokea maagizo holela Serikalini kwa sababu mzigo wa matatizo yatakayotokea, itajiweka kando na kuiachia taasisi hiyo ya umma lawama na vibano kutoka kwa wananchi.

Mapendekezo ya Kamati
Ili kuikoa benki hiyo, Filikunjombe alitoa mapendekezo sita ambayo miongoni mwake ni kuitaka TIB ijitegemee na kufanya kazi zake kama shirika la umme lenye uwezo wa kufanya maamuzi yake ya kiutendaji bila kuingiliwa na wanasiasa serikalini.

“Mhakikishe hamuingiliwi na Wizara ya Fedha au Serikali katika suala la utoaji wa mikopo,” alishauri Filikonjombe.
Mapendekezo mengine ni muundo wa manunuzi katika taasisi yao uendane na sheria ya manunuzi, kuwa ni mikakati ya kushindana kibiashara na benki nyingine na kuhakikisha kuwa mtaji unakua.

Katika hatua nyingine, POAC ilishangazwa kuona kuwa kati ya zaidi ya Sh50 bilioni zilizokusanywa kwenye marejesho ya fedha zilizochotwa EPA, ni Sh20 bilioni pekee zilizoifikia TIB.
Wabunge hao walielezea kushangazwa na kitendo cha Menejimenti ya TIB kupokea fedha hizo tu na kushindwa kuishinikiza Serikali itoe fedha zaidi.

Noni alisema kuwa TIB haikuwa na mamlaka ya kuishinikiza Serikali ili iipatie fedha zote za marejesho ya EPA.
“Sisi tulichopewa ndiyo hicho. Hatukuwa na sababu ya kudai fedha zaidi,” alisema huku akizidi kuzua mtafaruku wa maswali kwa wabunge hao.

Wabunge wengi walionyesha kuamini kuwa fedha zote zilipelekwa TIB baada ya Serikali kuahidi kuwa fedha za marejesho hayo zitapelekwa kwenye shughuli za kilimo.

TIB ndiyo benki iliyoanzishwa na Serikali kwa malengo ya kuinua kilimo nchini ambacho kinategemewa na asilimia 80 ya Watanzania.Wananchi wengi wanaojishughulisha na kilimo nchini ndio wanaogubikwa na wimbi la umasikini kuliko sekta nyingine.

Hata hivyo, Serikali imeamua kuanzisha kampeni ya Kilimo Kwanza, yenye lengo la kufanya sekta hiyo kuwa yenye manufaa na inayoweza kuleta utajiri tofauti na mwonekano wa sasa wa kuwa ni ya kundi la wasio na taaluma.
Taarifa nyingine zilizopatikana jana baada ya kamati hiyo kumaliza kikao chake ni kwamba sehemu ya marejesho ya fedha za EPA, mbali na zile Sh20 bilioni zilizopelekwa TIB, zilitolewa kwa moja kwa moja kwa kampuni za pembejeo za kilimo.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walielezea kutokuwa na imani kama fedha hizo zilitumika kikamilifu kwa ajili ya pembejeo hizo za kilimo.

Mmoja wa wabunge kutoka CCM ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini alisema kuna uwezekano fedha hizo zimeliwa na wajanja.

“Hata ukiangalia suala la marejesho halikuwekwa wazi, maana Rais (Kikwete) mwenyewe alisema zimekusanywa Sh53 bilioni, mara wengine wakasema 60 bilioni na wengine 70 bilioni.Alisema kama ufisadi uliweza kupenya hadi fedha zilizotolewa kwenye taasisi makini ya benki (TIB) basi hakuna shaka hata zilizotolewa kimyakimya ziliingia kwenye mikono hiyo ya mafisadi.

Hata hivyo, gazeti la serikali liliwahi kumnukuu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mohamed Muya, akisema katika mgawanyo wa fedha za EPA, wizara hiyo ilipewa Sh40 bilioni ambapo Sh30 bilioni zilitumika kwa ruzuku ya pembejeo ya mbolea hali ambayo imesaidia katika uzalishaji. “Kutokana na ruzuku hizi, hata idadi ya wakulima wanaopata vocha za ruzuku hiyo imeongezeka kutoka wakulima 500,000 hadi wakulima milioni 1.5 mwaka huu na kupitia Kamati ya Maafa na ya Usalama wa Chakula, hali ya chakula mwaka huu ni nzuri kuliko mwaka jana,” alisema Muya. Alisema katika fedha hizo za EPA, Sh10 bilioni zilizobaki zilitumika katika maeneo matatu ya kilimo ambayo ni Mfuko wa Pembejeo ambao ulipewa Sh3 bilioni, Wakala wa Mbegu wa Taifa Sh1 bilioni na kutatua matatizo ya visumbufu kama vile nzige, kweleakwelea na viwavijeshi Sh6 bilioni.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube