10 Dec 2011
Kikwete, Lowassa hapatoshi

Saed Kubenea's picture
Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 November 2011
Printer-friendly versionSend to friend
HATIMAYE Edward Lowassa ametoka hadharani na kuonyesha kuwa anataka kupimana ubavu na Rais Jakaya Kikwete.
Ameeleza hadharani kuwa Rais Kikwete anahusika kwenye mkataba tata wa Richmond/Dowans; lakini pia, kuwa hafuati taratibu katika kuongoza chama chake.
Lowassa ambaye alikuwa nguzo muhimu katika mbio za urais wa Kikwete mwaka 2005, ameonekana kumgeuka waziwazi swahiba wake huyo kwa kuanika kile wachunguzi wanaita “udhaifu katika uongozi.”
Ndani ya kipindi cha siku nne, Lowassa ametoa kauli tatu nzito zinazoonyesha dhahiri ameamua kufanya mapambano na Kikwete.
Akiwa ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lowassa alinukuliwa akieleza hatua kwa hatua namna kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (RDC), ilivyopewa zabuni ya kufua umeme wa dharura nchini.
Lowassa alijiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2008 kufuatia kashfa ya mkataba wa Richmond, kampuni iliyopewa kwa upendeleo zabuni ya kuzalisha umeme wakati haina fedha, haina uzoefu wala fedha za kufanyia kazi hiyo.
Alikiambia kikao cha NEC mjini Dodoma, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo wewe Rais Kikwete hukulifahamu au hukunituma” kuhusu Richmond/Dowans.
Alisema, “…Mwenyekiti, natukanwa kwa ufisadi wa Richmond wakati wewe unafahamu yalichosababisha kashfa ya Richmond ni makosa ya watendaji walio chini yangu? Sasa kosa langu ni lipi? Ni kule kukubali kuwajibika kwa ajili ya serikali yangu na chama chetu? Kwa nini nihukumiwe kwa kosa hilo?”
Huku akimtolea macho Kikwete alisema, “Unakumbuka vema jinsi nilivyotaka kuvunja mkataba ule. Nilikupigia simu ukiwa nje ya nchi, lakini ukasema umepata ushauri wa kamati ya makatibu wakuu, ushauri ambao ulisababisha mkataba usivunjwe?”
Lowassa alisema Kikwete anafahamu kila kitu kwa kuwa ni yeye aliyeridhia Rostam Aziz kutafuta mbia baada ya Richmond kushindwa kuleta umeme.
“Uliponitaka ushauri wa mtu wa kutusaidia ili kuondokana na aibu ya Richmond kushindwa kutimiza mkataba wake, nilipokutajia jina la Rostam, haraka ulikubali na kusema, naona hilo ni sawa,” alieleza Lowassa kwa njia ya kumsuta Kikwete.
Hatua ya Lowassa kumuingiza Kikwete kwenye tope la Richmond/Dowans imezima moja kwa moja kauli yake iliyodai, “Siwajui wala siwafahamu wamiliki wa makampuni ya Dowans Tanzania Ltd na Dowans Holdings SA.”
Akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, tarehe 5 Februari 2011, mjini Dodoma, Kikwete alikana kufahamu wamiliki wa kampuni hiyo na kwamba hajawahi kuwaona wamiliki wake.
Alisema, “Nataka kuuhakikishia umma kwamba, sihusiki na kampuni hii. Siifahamu na wala sijawahi kuwaona wamiliki wake…Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.”
Kauli ya Kikwete ya kutoitambua Dowans wala wamiliki wake, ilikuwa ni mwendelezo wa kauli kama hizo zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wasaidizi wake, zikilenga kumuondoa kwenye kashfa hiyo iliyomlazimu kuvunja baraza lake la mawaziri.
Akizungumzia kwa undani jinsi Richmond ilivyoingia na jinsi yeye na Kikwete walivyokuwa kitu kimoja kuhakikisha mkataba unasainiwa na kutekelezwa, Lowassa alisema, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo Rais Kikwete hukulifahamu.”
Akizungumzia kwa undani suala hilo kwa mara ya kwanza tangu ajiuzulu wadhifa wa waziri mkuu, Februari 2008, Lowassa alisema, “Mwenyekiti kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama, hivi hatukujua kama kuna kamati hizo za maadili?”
Lowassa alikuwa akichangia pendekezo la Kamati Kuu (CC) ya CCM lililotaka kurejeshwa kwa suala la “kujivua gamba” kwenye vikao vya chini vya chama hicho baada ya watuhumiwa, isipokuwa Rostam Aziz, kukataa kuachia uongozi katika chama.
Kikwete alikiambia kikao cha NEC kuwa, uamuzi wa kutaka jambo hilo lirejeshwe kwenye vikao vya chini, umetokana na “taratibu kukosewa.”
Hata hivyo, kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama hicho aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu, uamuzi wa Kikwete kulirejesha suala la kujivua gamba kwenye vikao vya chini ulitokana na hofu ya NEC kujaa wajumbe wengi kutoka kwa kundi la Lowassa.
“Unajua mle NEC, Kikwete hana chake. Mle ndani kuna kundi kubwa la Lowassa, ndiyo maana jamaa ameogopa suala hilo la kuvuana magamba lijadiliwe,” ameeleza kiongozi huyo ambaye ni waziri katika serikali ya Rais Kikwete.
Kanuni za CCM zinaeleza kabla ya tuhuma kufikishwa NEC, sharti wale wanaotuhumiwa wapewe haki na fursa ya kujitetea mbele ya vikao vya kamati ya usalama na maadili.
Akifunga mjadala huo kwa angalizo mwanana, Kikwete aliagiza suala hilo lipelekwe kamati ya maadili ambako alitaka kuwasilishwa ushahidi wa vielelezo na siyo hujuma dhidi ya watuhumiwa.
Wakati Lowassa akishusha tuhuma kwa Kikwete, kiongozi huyo wa nchi alionekana kama amepigwa ngazi. Hakukana hata tuhuma moja miongoni mwa yaliyoelezwa na swahiba wake huyo wa zamani.
Kikwete na Lowassa, wamejitambulisha mara kadhaa kuwa ni marafiki, huku mmoja akisisitiza, “Hatukutana barabarani.”
Haijafahamika mahusiano yao yamefikia wapi kwa sasa baada ya Lowassa kumhusisha mwenzake katika kashfa ya Richmond katika kile wachunguzi wanasema amechukua tabia ya “tufe sote au tukose wote.”
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kauli ya Lowassa ambayo ilitolewa mbele ya viongozi wake wakuu, akiwamo rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ililenga kuonyesha udhaifu wa Kikwete ndani ya CCM kwa kuasisi falsafa ya kujivua gamba na kuikimbiza moja kwa moja kwenye CC na NEC, kinyume cha taratibu na kanuni za chama chake.
Kama hiyo haitoshi, juzi Jumapili akiwa mkoani Singida alikokwenda kusimamia harambaee ya kuchangia fedha za ujenzi wa kanisa, Lowassa alinukuliwa akisema, “Kwa vyovyote vile, nitaibuka mshindi dhidi ya vita vya kuvuana magamba.”
Akitiwa moyo na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kati, Ushirika wa Amani, mjini Singida, Eliufoo Sima aliyesema, “suluhu ya mapambano ni kukabiliana nayo,” mwanasiasa huyo alisema, amekuwa akihusishwa na tuhuma ambazo hazina ukweli.
Askofu Sima alisema mapambano katika maisha hayatakwisha na “suluhisho siyo kuyaogopa, isipokuwa kuyatafutia majawabu kwa upole, hekima na utulivu.”
Vita vya magamba viliasisiwa na Kikwete 5 Februari 2011, kabla ya kudakwa na baadhi ya watendaji wa Sekretarieti ya CC ambao kwa miezi saba sasa, wamekuwa wakituhumu Lowassa na wenzake wawili - Rostam Aziz na Andrew Chenge – kuwa mafisadi wanaokidhalilisha chama mbele ya jamii.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa kutoka ndani ya CC zinasema kushindwa kwa Rais Kikwete kutekeleza mkakati wake wa kumfukuza Lowassa ndani ya chama chake, kulitokana na upinzani mkali uliotokea kwenye mkutano wa CC.
“Ni kweli kabisa, ndani ya CC, Lowassa alipata uungwaji mkono mkubwa, kiasi ambacho mwenyekiti alilazimika kulipeleka suala hilo NEC. Alipofika NEC na kuona moto umekuwa mkubwa, ndipo alipoamua kuliondoa na kutaka lifanyiwe kazi kwenye vyombo vya chini,” kimeeleza chanzo kimoja cha gazeti hili.
Amesema wajumnbe wa Zanzibar, wakiongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho visiwani, Amani Abeid Karume, muda wote wa mkutano walisimama imara kuhakikisha Lowassa hafukuzwi kwenye chama.
“Kuna wakati watu kutoka Bara walikuwa wanakaribia kushinda. Lakini baadaye Zanzibar wakapata nguvu pale Karume aliposimama na kusema, shutuma zote hizo hazijafuata taratibu,” ameeleza.CHANZO: Mwanahalisi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.