28 Oct 2012


KABLA ya kuingia kwa undani katika makala hii ambayo ni mwendelezo wa makala iliyochapishwa katika toleo la wiki iliyopita, naomba niwasimulie wasomaji mkasa ambao unaweza kuwa “funga kazi” katika utitiri wa vimbwanga vya watawala wetu.
Wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliwatia aibu Watanzania akiwa Afrika Kusini alipodai kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaundwa kwa Muungano kati ya kisiwa cha Bahari ya Hindi cha Pemba na Zimbabwe. Ukidhani ninamsingizia, basi angalia video hii kupitia kiunganishi hiki; http://goo.gl/uW6H2
Na licha ya kufanya madudu hayo, Mulugo ‘alilikoroga’ zaidi alipodai kuwa Muungano huo wa ‘Zimbabwe na Pemba’
ulitokea mwaka, (namnukuu) “one nineteen sixty-four.” Mwaka huo hauleti maana yoyote, iwe kwa Kiingereza au kwa Kiswahili, kwani 1-19-64 inaweza tu kuleta maana kwa mfumo wa tarehe wa Marekani (yaani tarehe 19 mwezi wa kwanza mwaka 64).
Ninaomba nitamke bayana kuwa Naibu Waziri Mulugo ni mzembe wa hali ya juu. Yawezekana aliandaliwa hotuba hiyo, lakini haihitaji busara japo kidogo kuwa huwezi kukurupuka kutoa hotuba kabla hujaipitia. Sijui Rais Jakaya Kikwete alijisikiaje baada ya kuona video hiyo yenye hotuba ya Mulugo, lakini kwa kosa hilo la ajabu kabisa, Naibu Waziri Mulugo sio tu anapaswa kutuomba radhi Watanzania kwa kupotosha historia ya taifa letu bali pia ingefaa aondolewe katika wadhifa wake unaoshughulikia elimu (elimu gani hiyo ambayo wakati Tanzania ‘haijamalizana’ na Malawi kuhusu mpaka kwenye Ziwa Nyasa, yeye ‘anaihamasisha Zimbabwe ‘idai Pemba ni sehemu ya nchi hiyo?’)
Nisiongelee sana suala hilo bali ninawaachiwa Watanzania wenzangu kuhitimisha wenyewe kuhusu madudu haya ‘ya karne.’
Kama nilivyoahidi katika toleo lililopita, wiki hii ninaendelea na mjadala kuhusu vurugu za kidini ambazo kwa siku za karibuni zinaonekana kushika kasi.
Katika makala iliyopita, nilijaribu kuonyesha sababu zilizojenga msingi wa manung’uniko ya Waislamu katika masuala ya elimu na ajira. Mwishoni mwa makala hiyo niliuliza maswali yafuatayo (ninajinukuu)
“Je; kilichotokea Mbagala ni hasira tu za baadhi ya Waislamu waliochukizwa na kitendo cha ‘mtoto wa Kikristo’ kukojolea Kuran Tukufu?
Je; udini ni tatizo kubwa katika Tanzania yetu ingawa halizingumzwi vya kutosha? Binafsi, ninaamini jibu la swali hilo, ni ndiyo. Kama ni ndiyo, kwa nini tunalikwepa tatizo hili?
Je; yawezekana udini ni turufu muhimu kwa baadhi ya wanasiasa mufilisi?”
Kwa swali la kwanza, nilishabainisha kwenye makala hiyo kuwa kwa mtizamo wangu, vurugu hizo za Mbagala zilisababishwa na zaidi ya hasira za baadhi ya Waislamu waliokasirishwa na kitendo cha mtoto kuikojolea Kuran Tukufu.
Yayumkinika kusema kuwa hasira za baadhi (na pengine ni wengi) ya Waislamu huko nyumbani (Tanzania) ni dhidi ya kile kinachotajwa kama ‘Mfumo Kristo.’ Kwa kifupi, wanaoamini hivyo wanauona mfumo huo unawapendelea Wakristo sambamba na kuwabagua Waislamu, hususan katika sekta za elimu na ajira, ambazo kimsingi zinahusiana kwa karibu.
Japo, kama nilivyobainisha katika makala yangu iliyopita kuwa Ukristo kwa kushirikiana na ukoloni ulichangia kutengeneza hali ya kutokuwa na usawa katika elimu na ajira, haimaanishi moja kwa moja kuwa Wakristo wanawabagua Waislamu. Naomba nieleweke hapa: kuna tofauti kati ya mfumo na watu wanaonufaika au kuathiriwa na mfumo huo.
Ninasema hivyo kwa sababu, wakati hoja ya kuwa Wakristo wanawabagua Waislamu ingeweza kuwa na mashiko wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa, ambao wote ni Wakristo, ni vigumu kwa hoja hiyo kuwa na uzito kwenye Awamu ya Pili na hii ya sasa (ya Nne) za marais Waislamu Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, kwa mtizamo wangu, viongozi hao wote wanne, hawawezi kukwepa lawama kuwa kwa kiasi kikubwa hawajafanikiwa sio tu kuyatupia macho kwa makini malalamiko ya Waislamu bali pia wamekuwa wakikwepa kuyashughulikia kwa uzito unaostahili.
Angalau kwa upande wa Baba wa Taifa tunaweza kukubaliana kuwa sio tu kwamba alishakiri kuwa kukosekana kwa usawa katika elimu na ajira kwa Waislamu ni tatizo, lakini pia alikwenda mbali zaidi na kujaribu kuukarabati mfumo wa elimu ili uweze kutoa fursa kwa Watanzania wote bila kujali imani zao.
Ni muhimu kukumbuka kuwa licha ya ukweli kuwa Mwalimu alikuwa Mkristo na mshika dini, mafanikio yake katika harakati za kupigania uhuru yalichangiwa zaidi na Waislamu.
Lawama ‘kubwa’ inayoweza kuelekezwa kwa Mwalimu ni jinsi serikali yake ilivyoshughulikia suala ‘nyeti’ la uundwaji Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na kupigwa marufuku Jumuiya ya Ustawi wa Waislamu wa Afrika Mashariki (East African Muslim Welfare Society- EAMWS).
Kwa kifupi, tangu kuundwa kwake, kwa kiasi kikubwa BAKWATA imeshindwa kujitenganisha na serikali, na pia imeshindwa kufuta hisia kuwa ‘ni chombo kinachotumiwa na serikali kuwagawanya na kuwakandamiza Waislamu.’
Japo EAMWS ilikuwa taasisi ya kidini lakini ilionekana kama ‘mkombozi wa Waislamu’ hususan kwenye sekta ya elimu, na yayumkinika kusema kuwa laiti kuundwa kwa BAKWATA kungeibua taasisi yenye ufanisi kama EAMWS, basi pengine pengo lililopo kwenye maeneo ya elimu na ajira kati ya Waislamu na Wakristo lingekuwa limepungua kwa kiasi kikubwa.
Ufinyu wa nafasi unaninyima fursa ya kuingia kwa undani kujadili hoja za kuifungia EAMWS na hatimaye kuanzisha BAKWATA, lakini ukweli kwamba serikali hiyo hiyo iliyoipiga marufuku EAMWS ilishiriki kikamilifu katika uundwaji wa BAKWATA umechangia kudumu kwa hisia kuwa ‘BAKWATA iliundwa kama chombo cha serikali dhidi ya Waislamu.’
Na katika utafiti wangu, matokeo ya awali yanaonyesha Waislamu wengi hawaridhishwi na mwenendo wa BAKWATA katika kutetea maslahi yao. Kimsingi, moja ya jambo lilionekana ‘kuwaunganisha’ wahojiwa wangu wa Kiislamu (ambao nilieleza katika makala iliyopita kuwa niliwagawanya katika makundi mawili ya ‘walio na msimamo mkali’ na ‘wa kawaida’- kwa minajili ya kiutafiti- ni suala hilo la BAKWATA.
Sasa katika mazingira haya ambacho chombo pekee kikuu kinachotarajiwa kuwaunganisha Waislamu kinaonekana kuwa kinawakandamiza, na-kuwanukuu baadhi ya wahojiwa- ni sehemu ya ‘Mfumo Kristo’ ni wazi kuwa baadhi (na pengine wengi) ya Waislamu wanajiona kama ‘mateka wa mfumo,’ kwa maana ya hisia za kubaguliwa na Wakristo na kubaguliwa na chombo kinachopaswa kutetea maslahi yao (BAKWATA).
Kwa mtizamo wangu, kuwa ‘mateka wa mfumo usiokubalika’ kunasababisha kuuchukia, na kama tujuavyo, chuki huzaa hasira. Hasira hizo zinasubiri mazingira ‘mwafaka’ ili zichomoze hadharani. Na tukio kama la Mbagala lilitoa ‘fursa mwafaka’ kwa hasira hizo.
Na ‘hasira’ hizo zinatoa jibu la swali la pili kuhusu udini. Kwamba Waislamu wanawachukia Wakristo, sitaki kuamini hivyo. Kwamba Waislamu (baadhi au wengi) wanachukizwa na mfumo wanauona kuwa unawabagua na kuwapendelea Wakristo, binafsi jibu langu ni ndio.
Na kwa vile ni vigumu kutofautisha ‘Mfumo Kristo’ na Wakristo kama waumini wa dini, ni muhimu kutambua kuwa kwa namna fulani-kubwa au ndogo- kuna uhasama wa kisaikolojia au kihisia kati ya madhehebu haya mawili. Kinachosaidia ‘kuficha’ uhasama huo ni misingi iliyojengwa huko nyuma ambayo ilisisitiza zaidi Utanzania wetu kuliko Uislamu au Ukristo wetu.
Kwa bahati mbaya-au makusudi-misingi hiyo inavunjwa kwa nguvu na wanasiasa waliokuja baada ya Mwalimu Nyerere. Kwa kifupi, wakati siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ilijenga misingi ya kutuunganisha Watanzania tuwe kitu kimoja, ‘ubabaishaji’ uliofuatwa-kwa mfano kinachoitwa Azimio la Zanzibar- umechangia sana kukuza ombwe lililotokana na ‘kifo cha Ujamaa,’ na wakati huo huo kutoa fursa kwa wenye ‘hasira’ zao kuziweka hadharani.
Kama nilivyowahi kuandika katika makala moja huko nyuma kuhusu unafiki wetu kuhusu suala la ushoga (hoja kubwa ikiwa ni imani zetu za kidini na mila na desturi zetu), kuna unafiki unaoendelea katika sio tu kuzungumzia suala la udini kwa uwazi zaidi bali pia hakuna utashi wa kisiasa (na hata kijamii) kukabili tatizo hili.
Ni nani asiyejua kuwa wakati wa utawala wa Mwinyi kulikuwa na baadhi ya Wakristo waliokuwa wakinung’unika chini chini kuwa teuzi za Mwinyi zilikuwa zinapendelea Waislamu? Ni nani pia asiyejua kuwa alipokuja Mkapa lawama kama hizo ziliendelea kuwapo chini chini kuwa Mkapa alikuwa akiwapendelea Wakristo? Na ni nani atakayejifanya hajui kuwa utawala wa Rais Kikwete umekuwa ukilaumiwa chini chini kuwa unawapendelea Waislamu?
Ninafahamu kuna watakaosema hizi ni hisia zangu tu. Hawa ndio ninaowaita wanafiki. Na unafiki huu ndio miongoni mwa vikwazo vikubwa vya kujadili tatizo la udini, na vurugu zinazohusishwa na tatizo hilo, kwa hofu ya kuitwa mdini. Niseme hivi, bora niitwe mdini kwa kujitoa mhanga kuanzisha mjadala wa suala hili kuliko ‘nionekane mwema’ ilhali tunalipeleka taifa letu mahali kusikofaa.
Nitajitahidi kuhitimisha mfululizo wa makala hizi kuhusu vurugu za kidini kwenye toleo lijalo, au pengine makala mbili zijazo. Hata hivyo, nihitimishe makala hii kwa jibu fupi kwa swali la tatu kuhusu udini unavyotumiwa na wanasiasa mufilisi kwa minajili yao binafsi.
Ninaamini sote tunakumbuka jinsi kampeni za uchaguzi mkuu uliopita zilivyogubikwa na tuhuma za udini. Na hapa nisiume maneno: chama tawala CCM kilifanya kila jitihada kuufanya ‘upadri’ wa mgombea wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kuwa turufu muhimu ya kumnyima kura za Waislamu. Hili nitalijadili kwa kirefu katika makala ijayo, lakini kwa namna fulani, CCM haiwezi kukwepa lawama kuwa ni miongoni mwa vyanzo vya vurugu za kidini tunazoshuhudia hivi sasa.
Chama cha siasa kinapoamua kwa makusudi kuwagawa wapiga kura kwa misingi ya imani zao za kidini, kinaandaa ‘viungo’ kwa ajili ya vurugu za kidini. Na ikumbukwe kuwa ni CCM hii hii iliyowahadaa Waislamu kuhusu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi (huku ikitambua kuwa haina dhamira ya dhati ya utekelezaji wa ahadi hiyo) na hadi sasa inaendelea kucheza danadana katika suala hilo.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa tuna kila kitu cha kupoteza (everything to lose) kwa kutengana kwa misingi ya kidini na hatuna cha kupoteza (nothing to lose) tukiendelea kuwa wamoja, kama majeruhi wa ufisadi, umasikini, magonjwa na dhahma nyingine zinazotukabili ambazo hazijali imani zetu za kidini. Ili Tanzania yetu ifike mahala tunapotamani ifike, au inapostahili kuwa, ni lazima tuwe kitu kimoja. Tukumbuke, UMOJA NI NGUVU NA UTENGANO NI UDHAIFU
Makala hii itaendelea toleo lijalo


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.