28 Nov 2013


MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika toleo lililopita la gazeti hili, iliyobeba kichwa cha habari ‘Nani kinara wa CCM urais 2015?’
Lakini kabla sijaingia kiundani, nadhani ni vema nikarejea nilichoandika katika makala iliyopita kuhusu kukua kwa uwezekano wa CCM kubaki madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Wiki iliyopita ilishuhudia chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, kikiingia katika mtafaruku mkubwa ambao licha ya kutishia uhai wake unazidi ‘kupapalia’ mazingira mwafaka ya ushindi kwa CCM.
Awali, CHADEMA ilitangaza kuwavua madaraka viongozi wake waandamizi watatu, Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na kuwapa siku 14 kujieleza kwa nini wasivuliwe uanachama baada ya kupatikana kwa nyaraka inayodaiwa kulenga kukihujumu chama hicho.
Jumapili iliyopita, Zitto na Kitila waliitisha mkutano na waandishi wa habari ambao kimsingi haikusaidia japo kupunguza moto unaozidi ‘kuunguza nyumba ya CHADEMA.’ Kwa kifupi, wanasiasa hao wawili walipinga vikali shutuma zilizoelekezwa kwao na kuhalalisha kile kilichotafsiriwa na uongozi wa chama hicho kama hujuma, huku wao wakibainisha kama matumizi ya demokrasia kwa minajili ya kuiboresha CHADEMA.
Pasi haja ya kuingia kwa undani katika sokomoko hilo, ni wazi kwamba uamuzi wa kuwavua madaraka viongozi hao na msimamo uliotolewa na ‘wahanga’ hao unaendeleza mapambano ya madaraka ndani ya CHADEMA. Kubaki au kuondoka kwa akina Zitto hakuwezi kukirejesha chama hicho katika mahala kilipokuwa. Kibaya zaidi, japo hakuna tathmini yoyote iliyokwishafanywa kuhusu athari za mgogoro huo, ni wazi Watanzania wengi wameanza kupoteza matumaini kwa chama hicho kilichotarajiwa sio tu kutoa upinzani mkubwa kwa CCM bali pia hata kuweza kuingia Ikulu mwaka 2015.
Nihitimishe suala hili la CHADEMA kwa kutanabaisha kuwa japo inafahamika kuwa lolote linawezekana katika siasa, ukweli kwamba tumebakiwa na takriban mwaka na ushee tu kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, sambamba na ukweli kuwa hakuna dalili ya mgogoro huo wa CHADEMA kumalizika hivi karibuni, itakuwa vigumu mno kwa chama hicho kujipanga upya na vyema, kuweza kutoa ushindani wa maana katika Uchaguzi Mkuu ujao. Nitaijadili kwa kirefu hatma ya CHADEMA katika makala zijazo.
Tukiendelea na mada ya urais kwa tiketi ya CCM, niliahidi kuwa wiki hii nitajadili ‘odds’ (uwezekano wa kufanikiwa au la) zinazowakabili wanasiasa wawili ambao tathmini yangu inawaona kama ndio vinara katika mbio za kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete kupitia CCM, yaani Edward Lowassa na Bernard Membe.
Pengine hadi siku chache zilizopita, kikwazo kikubwa kwa wote wawili kingeweza kuwa uwezekano wa CCM kubwagwa na CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu ujao. Lakini kwa kuzingatia mwenendo ulivyo katika chama hicho kikuu cha upinzani, yayumkinika kuhitimisha kuwa kikwazo hicho ni kama kimekufa kifo cha asili.
Kwa upande wa Lowassa, doa kubwa linaloonekana kuendelea ‘kuchafua’ jina na wasifu wake ni tuhuma za ufisadi wa Richmond. Bila kujali kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu uwaziri mkuu kufuatia kashfa hiyo ni ‘kutolewa kafara’ au ‘alivuna alichopanda,’ tafsiri ya haraka kwa wananchi wengi wa kawaida inabaki kuwa ‘ni vigumu kumtenganisha mwanasiasa huyo na moja ya matatizo makubwa kabisa yanayoikabili nchi yetu, yaani ufisadi.’
Ukweli kwamba Tanzania yetu sio tu ni moja ya nchi masikini sana bali pia inazidi kuwa masikini huku ufisadi ukizidi kushamiri, umesababisha kujengeka kwa hisia (pengine zisizopendeza) kuwa kila mwenye uwezo wa kifedha ni fisadi. Hisia hizo hazimsaidii Lowassa ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa mstari wa mbele katika harambee za kuchangisha mamilioni ya fedha hususan kwenye taasisi za dini. Badala ya ukarimu wake kumjenga kama kiongozi anayejali, kuna wanaotafsiri jitihada zake hizo kama ‘rushwa’ ya kutaka urais mwaka 2015.
Kadhalika, kuna hisia hasi kuwa hata hizo fedha anazotoa kusaidia miradi mbalimbali ‘ni chafu’ kwa maana ya hisia kuwa huenda ni zile zilizotokana na tuhuma za ufisadi. Kibaya zaidi, kutofahamika chanzo cha kinachotajwa kama utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo kunaimarisha hisia hizo za ufisadi.
Vile vile, na hili linawagusa wote-Lowassa na Membe- ukweli kwamba wanasiasa hao wanatajwa kama sehemu muhimu ya ‘mtandao’ uliomwingiza madarakani Rais Kikwete mwaka 2005, unaleta hisia za ‘mvinyo mpya kwenye chupa ya zamani’ (kwa wasiofahamu, thamani ya mvinyo inaelemea sana kwenye ‘ukale’ wake na si upya wake)
Sasa, kama tukiafikiana kuwa mtizamo wa Watanzania wengi ni kuwa utawala wa Kikwete (ambao uliingizwa madarakani na ‘mtandao’ uliowashirikisha Lowassa na Membe) umetawaliwa zaidi na tuhuma za ufisadi huku hali ya maisha ya Mtanzania ikizidi kuwa ngumu, kwa nini basi watu hao wapewe fursa ya kuboronga mambo zaidi?
Faraja kubwa kwa Lowassa (na hata Membe kwa ‘uhusika wake katika mtandao) kuhusu tuhuma za ufisadi ni ukweli mchungu kuwa Watanzania ni wepesi kusahau ‘mabaya.’ Wanasiasa wetu wengi wanafahamu kuhusu udhaifu huo ambao kwa kiasi kikubwa umewasaidia wengi kuendelea kuwapo madarakani licha ya ‘madudu’ yao.
Iwapo ‘kete ya fedha’ niliyobainisha katika makala iliyopita kuwa inamsaidia sana Lowassa itaendelea kutumika, basi kuna uwezekano mkubwa wa mwendelezo wa ‘who cares?’ (nani anajali?) ambapo mahitaji ya muda mfupi kama vile sukari, khanga, mchele na mengine kama hayo yatafunika mahitaji ya muda mrefu kama vile kuondokana na umasikini sambamba, kupambana na ufisadi, na hatma ya taifa letu kwa ujumla.
Kwa upande wa Membe, kikwazo kikubwa kwake ni kutokuwa maarufu ndani na nje ya CCM. Na ukubwa wa kikwazo hicho unatokana na ukweli kwamba ‘mpinzani’ wake, yaani Lowassa, ni mwanasiasa maarufu kuliko wote ndani ya CCM hivi sasa (bila kujali umaarufu huo ni stahili au la). ‘Wajuzi wa mambo’ wanaeleza kuwa inahisiwa Lowassa anaungwa mkono na zaidi ya asilimia 75 ya viongozi wa chama wenye uwezo wa kufanya uamuzi, huku wengi wao wakiwa watu waliofanyiwa fadhila zilizosababisha wawepo madarakani hivi sasa.
Tegemeo pekee kwa Membe dhidi ya Lowassa ni lile nililogusia katika makala iliyopita; nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika kumpata mgombea urais ajaye (ndani ya CCM). Kama kuna kitu chochote kinachoweza kumzuia Lowassa kuingia Ikulu, na pengine kumsaidia Membe kupata fursa hiyo, ni pale Idara hiyo itakapoamua ‘kumbeba mwenzao’ (Membe ni shushushu mstaafu). Na hilo si gumu kama inavyoweza kudhaniwa. Moja ya maeneo ambayo mashushushu wetu wanayomudu sana ni hujuma (sabotage) na uzandiki (subversion).
Ni hivi, kwa vile tayari kuna hisia za ‘uchafu’ kuhusu Lowassa (yaani tuhuma za ufisadi) basi haitokuwa vigumu kwa mashushushu kuzikuza na kuziendeleza katika namna ya kile kinachofahamika kama character assassination. Lakini kwa vile Lowassa bado yupo katika ‘himaya’ ya Idara ya Usalama wa Taifa (kama waziri mkuu wa zamani, anapatiwa huduma za ulinzi na Idara hiyo) ni rahisi kwa mashushushu kuibua mengi (ya kweli au hata ya kutunga) dhidi yake, iwapo wataona haja ya kufanya hivyo.
Kwa hiyo, kwa kifupi, kufanikiwa kwa Membe kutategemea kukwama kwa Lowassa. Na pengine katika hatua hii, ni vema nikitanabaisha waziwazi kuwa mwana-CCM anayeongoza katika kinyang’anyiro hicho ni Lowassa akifuatiwa kwa karibu kiasi na Membe.
Nihitimishe makala hii kwa kueleza kuwa mada hii ni endelevu, kwa maana ya kuwa nitaendelea na uchambuzi na mjadala huu kadri tunavyoelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Hata hivyo, ninapenda kurejea tena mtizamo wangu kuwa CCM kurejea tena madarakani mwaka 2015 ni janga kwa Watanzania. Chama hicho tawala sio tu kimeishiwa na kila mbinu ya kuongoza nchi lakini pia hakipo kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Na kama uchambuzi huu ulivyoonyesha kuwa uwezekano mkubwa wa aidha Lowassa au Membe kuwa mgombea kwa tiketi ya chama hicho ni kwa aidha fedha au ‘sanaa za giza’, yeyote kati yao atakapopata urais hatokuwa tofauti na utawala uliopo madarakani hivi sasa ambao nao ulitumia mbinu ya ‘mtandao.’
Kwa bahati mbaya au makusudi, watu tuliodhani wangeweza kutusaidia kuiondoa CCM madarakani, yaani CHADEMA, wanaonekana kuwa ‘bize’ kupigana ngwala kugombea madaraka ndani ya chama chao. Sasa kama zoezi dogo tu la kupata uongozi wa chama linasababisha ‘watiane vidole machoni’ kwenye uongozi wa nchi itakuwaje? Ni ukweli mchungu lakini usioepukika na hivyo ni vema kujiandaa kisaikolojia kuendelea kuwa chini ya utawala wa CCM (ninatamani kuwa na suluhisho mbadala lakini sijalipata hadi muda huu)

Soma zaidi kuhusu:

- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015-ii#sthash.RAQui2j5.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube