8 Aug 2014

Rais Kikwete safarini
NIMEAMKA asubuhi nikakutana na habari kwenye blogu mbalimbali inayohusu kanusho kutoka Benki yetu Kuu (BoT) kuhusu Benki ya FBME.
Kwa mujibu wa BoT “habari zilizosambazwa kwenye mitandao kuwa kesho Jumatatu FMBE itafungwa na shughuli zote kuwekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu si za kweli...na benki hiyo haipo chini ya usiamizi wa BoT na itaendelea kutoa huduma kama kawaida.”
Takriban wiki moja baadaye, ninakutana na habari kama hiyo, lakini kichekesho cha kukera ni kwamba sasa benki hiyo ya FBME hatimaye imewekwa chini ya usimamizi wa BoT.
Nabaki ninajiuliza, siku kama tano zilizopita BoT ilikanusha vikali ‘tetesi’ kuwa FBME itawekwa chini ya usimamizi wake, leo kinatokea kilekile kilichokanushwa na taasisi hiyo nyeti!
Ninaamini kuwa kanusho la awali kutoka BoT lilisababishwa na ubabaishaji. Japo mimi si mtaalamu wa masuala ya benki au fedha, ninachoelewa ni kwamba benki hiyo ya kigeni ilishatuhumiwa na taasisi za usalama za Marekani kwamba inahusika na uhalifu wa kifedha.
Sasa bila haja ya kuwa mtaalamu wa uendeshaji au usimamizi wa benki, yayumkinika kuhitimisha kuwa BoT ilipaswa kuanza uchunguzi mara moja kuhusiana na taarifa hizo, badala ya kukunausha na kutoa matumaini hewa.
Nikadhani kwamba huenda ubabaishaji huo ungefanya wahusika  BoT ‘kukaliwa kooni.’ Lakini hadi wakati ninaandika makala hii hakuna lolote lililotokea.
Awali kulisikika tetesi kuwa uongozi wa BoT unatarajiwa kujiuzulu lakini tetesi hizo zilipotea kwa kasi kama zilivyoanza.
Nilishaeleza katika makala zangu kadhaa huko nyuma kuwa nimejijengea utaratibu wa kuanza kila siku yangu kwa kupitia habari za huko nyumbani kupitia mtandao. Lakini kutokana na kukerwa na kioja hicho cha BoT na Benki ya FBME, nikajiuliza “kwanini nihangaike kufuatilia habari za Tanzania ilhali kuna wawakilishi wetu hapa Glasgow katika Michuano ya Jumuiya ya Madola?”
Nikaamua ‘nijipe likizo kidogo’ na kuelekeza nguvu zangu za kusaka habari zinazohusu nchi yangu, hapa nilipo. Lakini kama wenzangu mlivyoona kwenye runinga zenu na ilivyoripotiwa kwenye vyombo vingine vya habari, wawakilishi wetu hao wameendelea kudumisha historia ya kuwa ‘watalii.’
Lakini cha kukera zaidi ni kauli ya Naibu Waziri mwenye dhamana ya michezo, Juma Nkamia, kwamba wawakilishi wetu hao hapa Glasgow asilaumiwe kwa matokeo mabaya.
Huyu mtu sijui anaishi sayari gani! Katika utetezi wake kwa wawakilishi wetu hao walioboronga vibaya, Naibu Waziri Nkamia alidai kuwa matokeo mabaya yalitokana na ushindani. Sasa haihitaji japo busara kidogo kutambua kuwa tulipoleta timu yetu hapa Galsgow hatukuja kutalii bali kushindana. Hao waliomudu kufanya vizuri hawakuwa wanatumia roboti bali ni wanadamu kama wawakilishi wetu. Nao pia walifahamu fika kuwa kuna ushindani, wakajiandaa vya kutosha. Sasa sie ‘tunaokumbuka shuka wakati kumeshakucha’ tunakuwaje kituko cha kutambua kuwa michuano hiyo ingekuwa na ushindani baada ya kuboronga?
Kweli, hatuwezi kujilinganisha na ‘nchi’ kama England walioibuka kidedea kwa idadi ya medali, lakini mbona majirani zetu wa Kenya wameweza kufanya vizuri mara kadhaa zaidi yetu?
Wakati sisi tunasikia akina Nkamia wakitoa visingizo vya kitoto, wenzetu Kenya watakuwa wakipongeza wanamichezo wao waliokuja Glasgow kuiwakilisha nchi yao kwa dhati. Ni nyakati kama hizi mtu waweza kujiskia vibaya kuwa Mtanzania.
Na wala tusitaraji ya kuwa matokeo yetu mabaya katika michuano hiyo iliyomalizika hapa mwishoni mwa wiki iliyopita yatawaamsha akina Nkamia na viongozi wengine wa michezo. Kikubwa cha kutarajia kutoka kwao ni kilio cha kila siku cha maandalizi mabovu na ahadi za kizushi kuwa watafanya maandalizi bora zaidi huko mbele.
Kwa vile hata habari za nchi yangu kutoka hapa Glasgow ni kama hizo ninazokutana nazo kila asubuhi kutoka huko nyumbani, ninaamua kuendelea kufuatilia yanayojiri huko.
Nakutana na habari ya Rais Jakaya Kikwete kukumbuka utaratibu wake wa kuhutubia taifa kila mwisho wa mwezi. Yaelekea hakuna anayefahamu kwanini alikuwa kimya kitambo sasa.
Lakini kwa waliodhani kuwa ukimya wa Rais Kikwete katika hotuba zake za kila mwisho wa mwezi ungemalizwa na matumaini mapya katika hotuba yake ya majuzi, ninahisi walibaki na mfadhaiko.
Kubwa katika hotuba hiyo lilikuwa sakata la Katiba mpya, ambapo Rais wetu alijivua lawama kuhusu sintofahamu inayoendelea na kuwatupia lawama nyingi wana-kikundi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi- UKAWA.
Kwa kifupi, hotuba ya Rais Kikwete haikuwa na jitihada zozote za kuleta suluhu au kuongeza jitihada za kupata Katiba mpya. Historia na uzoefu vyaonyesha kuwa lawama si tu  hazijengi bali si ufumbuzi wa matatizo.
Najipa matumaini kwamba labda kutakuwa na habari njema kutoka Msumbiji ambako timu yetu ya taifa ilikuwa ikitafuta nafasi ya kushiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika.
Kocha wetu Mart Nooij aliahidi ushindi, nami japo kwa hali ya wasiwasi, niliamini anachoahidi. Matokeo yake, tukachapwa bao 2-1.
Nadhani hadi hapa msomaji mpendwa utatambua ugumu wa kukutana na ‘habari nzuri’ kuhusu nchi yetu. Lakini tufanyeje? Kujinyima habari hakufanyi habari ‘mbaya’ zipotee. Na ndio maana sikuweza ‘kuzikwepa’ kelele za mtandaoni dhidi ya Wizara ya Afya kuhusiana na janga la ugonjwa hatari wa ebola.
Wananchi kadhaa walikuwa wanauliza kama serikali yetu ina taarifa yoyote kuhusu ugonjwa huo na imejipanga vipi kukabiliana nao.
Hatimaye Wizara husika ikatoa taarifa kuwa ‘imejipanga vizuri’ kukabiliana na tishio la ebola. Nilitamani niamini tamko hilo la Wizara lakini nikabaki ninajiuliza, ‘hivi hospitali ya Muhimbili ambayo inaelezwa kuwa katika hali mbaya kabisa si ipo chini ya Wizara hiyohiyo inayotaka kutuaminisha kuwa ipo vema kukabiliana na ebola?’
Sitaki kuonekana mtu wa ‘kuombea mabaya’ tu lakini kwa ninachoweza kuwashauri Watanzania wenzangu ni kuzidisha sala/ dua ili janga hilo la ebola lisiingie huko nyumbani badala ya kuamini ‘kauli za kirasimu’ kutoka Wizara husika na serikali.
Ninamaliza wiki yangu kwa kukutana na picha na habari inayomwonyesha Rais Jakaya Kikwete akiwa nchini Marekani kuhudhuria ‘mkutano mmoja muhimu.’ Najiuliza, ‘hivi si majuzi tu Rais wetu alikuwa Marekani?
Najaribu kuhesabu idadi ya safari alizokwishafanya nchini humo, nabaki na bumbuwazi. Naomba nieleweke vizuri, si kwamba Rais wetu asisafiri nje ya nchi lakini nadhani kila Mtanzania anafahamu kuwa Rais Kikwete anasafiri mno. Na kwa hakika safari hizi ni mzigo kwa taifa letu linalokabiliwa na matatizo lukuki ya kiuchumi.
Watetezi wa safari hizo wamekuwa wakijitahdi kutuaminisha kuwa zina manufaa makubwa kwa taifa. Ni rahisi kuyaeleza manufaa kwa kutumia takwimu na ‘kusahau’ kuwa takwimu hizo ni watu.
Hivi kweli laiti safari za ‘kila kukicha’ za Rais wetu huko nje zingekuwa na mafanikio tunayoelezwa bado tungekuwa tunasuasua kiuchumi kulinganisha na majirani zetu kama Rwanda ambao ni nadra kuskia Rais wao yupo safarini nje ya nchi?
Na kabla sijamaliza kujiuliza kuhusu safari za Rais Kikwete nje ya nchi nikutana na lundo la habari za kusikitisha kuhusu ajali zilizopoteza maisha kadhaa ya Watanzania.
Lakini kwa bahati mbaya (au pengine), ajali sasa zinaanza kuonekana ni jambo la kawaida, kama ilivyo kwa mgao wa umeme au matukio ya ufisadi.
Imefika mahala hata vyombo vya habari vinaripoti matukio ya ajali kwa ‘uzito mdogo’ labda kwa kutambua kuwa ‘hakuna anayeguswa’ na habari hizo. Ni jambo la kawaida sasa.
Nihitimishe kwa kufafanua kuwa makala hii imelenga kuamsha tafakuri kuhusu yanayojiri huko nyumbani kama yanavyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari.
Kwa tunaofuatilia takriban kila kinachojiri nchini Tanzania tunajikuta katika wakati mgumu kukutana na habari ya ‘kuleta tabasamu’ au matumaini. Sijui tunaelekea wapi lakini nadhani ni vema wakati huu tunajiandaa na Uchaguzi Mkuu hapo mwakani tukakuna vichwa na kujiuliza kuhusu hatma ya Taifa letu.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.