21 Aug 2014

Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe
‘UKAWA waapa kutorudi bungeni’;
‘Katiba mpya kupatikana bila UKAWA;
Safu hii haitoshi kuorodhesha vichwa vya habari vinavyotawala vyombo mbalimbali vya habari kuhusu sakata linaloendelea kuhusu Katiba mpya.
Ukifuatilia mijadala mbalimbali ya Watanzania kuhusu suala hilo, hasa katika mitandao ya kijamii, utaona masikitiko waliyonayo, hasa kwa vile mchakato mzima wa kupata Katiba mpya umeshagharimu mabilioni ya shilingi.
Lakini pengine Watanzania wengi ni watu wa kuishi kwa matumaini kuliko kuishi kwa kuzingatia hali halisi. Hakuna ubaya kuwa na matumaini lakini ni vema kuwa na matumaini yanayoendana na hali halisi.
Nisingependa kurejea jinsi Bunge Maalumu la Katiba lilivyoanza kwa ‘kwikwi’ lakini tunachoweza kukumbushana ni pamoja na sura za wateuliwa wa Rais kama wawakilishi wa makundi mbalimbali ya jamii.
Wengi wa wateuliwa walikuwa watu wenye ‘ukaribu na chama tawala, CCM,’ na hilo tu lilitosha kuonyesha kuwa hatma ya upatikanaji wa Katiba mpya ingekuwa na mushkeli.
Lakini kosa jingine lilikuwa ‘kuwahamisha’ wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa wajumbe ‘wa moja kwa moja’ wa Bunge Maalumu la Katiba. Nadhani hakuna Mtanzania asiyefahamu mapungufu mengi yanayolikabili Bunge letu la Muungano, na uamuzi wa ‘kuwahamisha’ wabunge wa Bunge hilo katika Bunge la Katiba ulikuwa sawa na kuhamishwa matatizo mapya.
Kwa mtizamo wangu, Bunge letu la Muungano ni miongoni mwa taasisi zisizowatendea wananchi kwa kiwango kikubwa.
Japo kila kikao cha Bunge hilo kinapoanza utakutana na vichwa mbalimbali vya habari magazetini, kama vile ‘Bunge kuwaka moto,’ ukweli mchungu ni kuwa moto pekee unaowaka ni wa kutafuna fedha za walipakodi.
Kwa kiasi kikubwa Bunge letu limegeuka uwanja wa matusi, mipasho, uhuni, na kila jambo linalokera. Badala ya kutekeleza majukumu yake muhimu kama kutunga sheria, taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kuvunja sheria.
Kadhalika, Bunge letu limepoteza kabisa umuhimu wa mgawanyo wa madaraka katika ya serikali (kwa maana ya executive), Bunge na Mahakama, kwa sababu limekuwa kama muhuri wa kupitisha matakwa ya serikali.
Kwa kutumia wingi wa wabunge wa CCM, Bunge hilo likipitisha takriban kila hoja inayoletwa na serikali ya chama hicho. Pengine hiyo si dhambi bali tatizo ni ukweli kwamba kubwa lililowapeleka wabunge hao wa CCM bungeni ni kuwawakilisha wananchi pasi na kujali itikadi za vyama vyao. Katika mazingira ya kawaida tu, maslahi ya nchi (kwa maana ya wapigakura) yanapaswa kupewa kipaumbele zaidi ya maslahi ya kiitikadi.
Na tatizo hilo la wingi wa wabunge wa CCM katika Bunge la Muungano kutumika vibaya ni miongoni mwa vikwazo vya ufanisi katika Bunge Maalumu la Katiba. Badala ya kuangalia Katiba mpya kama suala lenye umuhimu mkubwa kwa Taifa, wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotokana na ubunge wa chama hicho, wakishirikiana na wajumbe wa kuteuliwa na Rais ‘ wenye mahusiano’ na CCM, wameligeuza suala la kichama.
Sasa sijui matumaini waliyonayo Watanzania wengi kwa Bunge hilo yanatoka wapi.
Tukija kwenye sakata la Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA kususia Bunge la Katiba, binafsi ninaona tupo njia panda: wakirejea bungeni tutaendelea kushuhudia matusi, vijembe, na upuuzi mwingine na pengine tukirudi kulekule kulikosababisha UKAWA kususa.
Wakiendelea kususa kinachoendelea huko Dodoma kitakuwa ni kupoteza tu fedha za walipakodi, na hata wakifanikiwa kupata idadi ya kura zinazohitajika kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba mpya, basi litakuwa ni suala la kulazimisha na linaloondoa uhalali wa zoezi hilo zima.
Hata tukiafikiana kwa minajili tu ya makala hii kwamba UKAWA wanaweza kurejea katika Bunge la Katiba, ni vigumu mno kudhani kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, ataacha upendeleo wake kwa wana-CCM wenzie.
Kadhalika, ni vigumu zaidi kutarajia kwamba UKAWA wakikubali kurejea katika Bunge hilo, ghafla kutopatikana mwafaka wa kuacha matusi na vijembe na badala yake kuweka kipaumbele kwa mustakabali wa Katiba mpya na Taifa kwa ujumla.
Sana sana tutachoshuhudia ni hotuba ndefu za ‘wajumbe wa CCM’ kuwasema wenzao wa UKAWA, kutonesha majeraha ambayo hata hayajaanza kukauka, na hatimaye uwezekano mkubwa ni kwa wana-UKAWA kususa tena.
Na huko ‘mtaani’ kumeanza tetesi kwamba hata tishio la ugonjwa hatari wa ebola limeanza kutumika kwa minajili ya kufanya ‘usanii’ katika mchakato wa kupata Katiba mpya.
Tetesi nyingine ni taarifa zilizojitokeza mwishoni wa wiki iliyopita kuhusu ‘ugaidi wa CHADEMA,’ zilizotolewa na mwanachama wa zamani wa chama hicho cha upinzani, Habib Mchange.
Inasikitisha sana kuona fursa hii adimu ya kutengeneza mustakabali mwema wa Taifa inafanyiwa uhuni. Kuna wenzetu wasiotaka kabisa kuiangalia Tanzania yetu zaidi ya muda tulionao. Baadhi ya wenzetu hawa wana watoto na wajukuu lakini ubinafsi wao unawatia upofu wa kutengeneza mazingira mema kwa vizazi vijavyo.
Kwa mara ya kwanza nimejikuta nikiunga mkono ushauri uliotolewa na mwanasiasa ambaye kwa muda mrefu nimekuwa nikimwona kama kikwazo cha kupatikana ‘mwafaka wa kitaifa’ katika jambo lolote lile.
Hapa ninamzungumzia Mwigulu Nchemba, ambaye hivi karibuni alitoa wito wa kuangalia uwezekano wa kusitisha Bunge Maalumu la Katiba hadi utapopatikana mwafaka na UKAWA.
Lakini ‘sauti za busara’ za watu kama Mwigulu haziwezi kusikika wala kufanyiwa kazi, kama ilivyojitokeza kwa kiongozi mwingine wa CCM, Nape Nnauye, kupinga vikali wazo hilo la kuahirisha Bunge la Katiba, hoja yake kuu ikielemea kwenye mtizamo fyongo kuwa CCM ndio Tanzania.
Nimalizie kwa ‘kubahatisha’ kuomba busara itumike ili kumaliza sintofahamu inayoendelea kuhusu Katiba mpya.
Ni vema tukakubali kujifunza katika makosa yaliyotufikisha hapa, na pia kukubali kuwa ‘tumeliwa’ kwa maana ya gharama tulizokwishaingia kutafuta Katiba mpya, na kisha tuahirishe mchakato huo hadi mazingira yatakaporuhusu kujadili suala hilo nyeti.
Ubabe wa kulazimisha Katiba mpya waweza kuipeleka Tanzania yetu kubaya zaidi ya tulipo hivi sasa.
Ndiyo, twaambiwa na Mwanasheria Mkuu Jaji Werema kuwa Rais Jakaya Kikwete hana mamlaka ya kuvunja Bunge Maalumu la Katiba.
Lakini kwa hakika yawezekana Bunge lenyewe la Katiba kufikia mwafaka kuwa halina uhalali wa kuendelea na vikao vyake, au hata vikiendelea litaishia ‘kuzaa’ matokeo ya kulazimisha.
Ni bora tuchelewe kupata Katiba mpya lakini tutapoipata iwe kwa maslahi na hatma ya Taifa kuliko kutumia ubabe kulazimisha suala hili ambalo ni wazi limeshindikana.
Penye nia pana njia. Mungu Ibariki Tanzania

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube