21 Sept 2014

Scotland
Kura ya kuamua hatma ya Uskochi kama ibaki kuwa sehemu ya United Kingdom au iwe nchi huru imekwisha, wak asilimia 55 ya wapigakura kusema HAPANA na 45 kusema NDIYO.Kwa matokeo hayo, muungano unaounda UK, wenye umri wa miaka 307 umesalimika.

Wakati nitaielezea kwa undani zaidi kura hiyo ya uhuru wa Uskochi katika makala yangu ya Jumatano ijayo ndani ya jarida la RAI MWEMA,katika post hii nitazungumzia kinachoanza kuonekana kama 'Uskochi kuingizwa mkenge' kufatia kuanza kuparaganyika kwa baadhi ya ahadi za msingi zilizopelekea ushindi wa kundi lililotaka Uskochi iendelee kuwa sehemu ya Muunganowa UK.

Mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kama waliofanikisha kuunusuru Muunganowa UK ni Waziri Mkuu wa zamani, Gordon Brown, ambaye kama Waziri Mkuu wa sasa, David Cameron, kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Ed Milliband, Naibu Waziri Mkuu na kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, Nick Clegg, na kiongozi wa 'kampeni ya Better Together' ya kuunga mkono muungano ambaye pia alikuwa 'Waziri wa Fedha' wa serikali ya Labour, Alistair Darling, kwa pamoja waliwaahidi wapigakura ya uhuru wa Uskochi kuwa wakikataa uhuru 'watazawadiwa' kwa nchi hiyo kupatiwa mamlaka zaidi ya kiutawala na kimaamuzi.

Mamlaka hizo zinafahamika kama 'Devo Max.'Kimsingi Devo Max, kifupisho cha Maximum Devolution,  inamaanisha Bunge la Uskochi kuwa na nguvu katika kila kitu ispokuwa ulinzi na mambo ya nje. Hata hivyo licha ya ahadi kuwa Uskochi itapatiwa mamlaka zaidi, uwezekano wa kupatia Devo Max kwa maana halisi ya nguvu zote kabisa zinazohitajiwa ni kama haupo.

Kwa sasa, na hadi wakati inapigwa kura ya uhuru au la, Uskochi imepewa mamlaka ya kujiamulia mambo yake yenyewe katika sekta za elimu, afya, huduma za jamii, makazi, utalii, mazingira, uvuvi, misitu, kilimo, sheria na usalama wa raia, na baadhi ya maeneo katika sekta ya usafiri. Kwa upande mwingine, serikali kuu ya Uingereza (Westminster) ina mamlaka katika sekta ya ulinzi, hifadhi ya jamii (social security), mafao kwa jamii (benefits)- kwa hapa Uingereza, watu wasio na kazi wanalipwa fedha ya kujikimu na kodi ya nyumba na serikali,gesi na mafuta, nishati ya nyuklia, uhamiaji, ajira, mawasiliano ya radio na runinga, biashara na viwanda sera za nje, masuala ya walaji (cunsumer affairs) na Katiba. 

Sasa kilichoahidiwa na Cameron na wenzake kushawishi Waskochi wakatae uhuru kuhusiana na Devo Max hakipo bayana sana. Miongoni ya yaliyomo kwenye ajenda ni Uskochi kuwa na mamlaka zaidi ya ukusanyaji kodi na mafao ya makazi kwa wasio na ajira. Suala la gesi na mafuta na kodi za mashirika (corporation tax) hayapo kabisa katika makubaliano hayo ambayo kimsingi bado hayajafikiwa.

Lakini hata kabla shamrashamra za kusherehekea kusalimika kwa Muungano wa UK hazijaisha, kizaazaa kimeibuka katika jinsi ya kutekeleza ahadi hiyo ya kutoa mamlaka zaidi kwa Uskochi. Kwa upande mmoja, ahadi hiyo iumevutia madai ya mamlaka zaidi kutoka Wales na Northern Ireland kama nchi ambazo pamoja na Uskochi na England zinaunda muunganowa UK. Kwa upande mwingine, baadhi ya 'mikoa' yenye wakazi wengi, kama vile Manchester, Yorkshire, Cornwall, nk nayo imeanza kudai kupatiwa mamlaka zaidi ya kiutawala.

Ttatizo kubwa zaidi lipo katika kupata mwafaka kati ya chama tawala Conservatives na wapinzani wao wa Labour. Ili Uskochi iweze kupatiwa mamlaka iliyoahidiwa, Bunge la Muungano huko Westminster litalazimika kufanya mabadiliko ya katiba. Hilo tu ni tatizo pia, kwani kwa mujibu wa taratibu za hapa UK, mabadiliko ya katiba ya nchi hii ni zoezi linalohitaji muda mrefu. Lakini muda haupo upande wa Serikali Kuu kwa vile kuna matarajio makubwa kutoka kwa Waskochi waliokataa uhuru.

Hata urasimu wa mabadiliko ya Katiba ukiwekwa kando, bado kuna tatizo linalowakabili Cameron na Conservatives wenzie na Milliband na Labour yake. Kwa Cameron, ile kuahidi tu kuwa ataipatia Uskochi mamlaka zaidi, wabunge wengi tu katika chama hicho nao wameanza kudai mamlaka zaidi kwa majimbo yao. Kwa Milliband, tatizo ni kubwa zaidi. Kwa sasa, chama cha Labour kina wabunge 49 kutoka Uskochi katika Bunge Kuu la Muungano, ambao pia wanapiga kura katika maamuzi yanayoihusu England pekee. Hii imerejesha kinachoitwa 'swali la Lothian ya Magharibi' (the West Lothian Question), yaani kuhoji kwanini wabunge kutoka Uskochi katika Bunge la Muungano waruhusiwe kupigia kura masuala yanayoihusu England pekee ilhali wabunge kutoka England hawana fursa hiyo. Hii inalingana na 'kilio' cha baadhi ya wanasiasa wa Tanzania Bara wanaodhani si sawia kwa wabunge kutoka Zanzibar katika Bunge la Muungano kuhusika katika maamuzi ya masuala yanayohusu Bara pekee ilhali hakuna mbunge wa Bara mwenye mamlaka kama hiyo katika Bunge la Zanzibar. Kama ilivyo huko nyumbani, hakuna mbunge wa England katika Bunge la Uskochi, kama ambavyo hakuna mbunge kutoka Bara katika Bunge la Zanzibar.

Wakati chama cha Labour kitaanza Mkutano wake Mkuu hapo kesho na ajenda kuu ya Milliband ilipangwa kuwa kuzungumzia taasisi muhimu ya huduma za afya (National Health Service-NHS) sasa anaweza kulazimika kuzungumzia uwezekano wa chama hicho kupunguziwa nguvu katika Bunge Kuu la Uingereza iwapo mpango wa kuwanyima malaka ya kimaamuzi wabunge kutoka Uskochi katika Bunge la Muungano utatekelezwa.

Na siku hiyohiyo ambapo Labour wanaanza mkutano wao mkuu, Cameron anatarajiwa kutoa hotuba kuhusu kinachoiwa 'kura za Waengland kwa sheria za England' (English votes for English laws), kwa maana ya kura zinazopigwa katika Bunge Kuu katika masuala yanayohusu England zipigwe na wabunge wa England pekee, na wale wa kutoka Uskochi wasiruhusiwe kupiga kura hizo.

Tayari Cameron ameanza kumlaumu Milliband kwa upinzani wake dhidi ya mpango huo, akidai kuwa kiongozi huyo wa Labour anaisaliti England. Kwa upande wake, Labour inamshutumu Cameron na chama chake kwa kile inachokiona kama jitihada za kupinguzia Labour nguvu katika Bunge la Muungano.

Mhanga wa 'mgogoro' huo ni Uskochi kwani pasi kufikiwa mwafaka kati ya vyama hivyo viwili, uwezekano wa Uskochi kutekelezewa ahadi ya kuongezewa mamlaka ya kiutawala sio tu utachukua muda mrefu bali pia unaweza kukwama kabisa.

Na Waziri Mkuu wa Uskochi, Alex Salmond, aliyetangaza kuachia ngazi mwezi Novemba tayari ameingilia kati suala hilo na kuwakumbusha Cameron na Milliband kwamba tofauti zao zitapelekea waliopiga kura ya kukataa uhuru wa Uskochi kujiona kama 'wameingizwa mkenge' kwa kupewa ahadi za hadaa.

Kwa mtizamo wangu ninadhani mwamuzi ni muda (time will tell) lakini kama nilivyosapoti kambi iliyotaka uhuru wa Uskochi, imani yangu kutoka kwa Cameron, Milliband na wanasiasa wengine wa Westminster ni ndogo. Na hoja hii ilijitokeza wakati wa kampeni za kampeni za uhuru ambao kuna waliohoji, kama tupo 'Better Together' hivi sasa, kwanini basi mambo hayaendi sawia-kwa maana ya wanasiasa wa Westminster kuahidi mengi lakini kutekeleza machache. Kadhalika, kwa kukataa uhuru wa Uskochi kwa ahadi kutoka kwa wanasiasa, Waskochi wanaweza kuwa wamerudi kulekule kwa kurejea hatma yao mikononi mwa wanasiasa, tofauti na suala zima la kura ya uhuru lilivyoendeshwa  kwa kiasi kikubwa na wananchi wenyewe kwa mustakabali wao

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube