20 Sept 2014


Kwanza ninaomba kukiri bayana kuwa nimehuzunishwa na matokeo ya kura ya maoni kuhusu uhuru wa Uskochi. Hiyo inatokana na ukweli kwamba sio tu nilikuwa naunga mkono kambi ya 'Yes' iliyokuwa inataka uhuru wa taifa hili bali pia nilipiga kura ya 'Ndiyo.'

Lakini kwa vile uamuzi wa iwapo Uskochi iwe nchi huru au iendelee kubaki sehemu ya United Kingdom ulipaswa kuamuliwa kwa wingi wa kura-hata ingekuwa moja tu- sina budi kuafiki matokeo na kukubaliana na ukweli. Ukweli kwamba asilimia 55 ya wapiga kura wametaka Uskochi iendelee kuwa sehemu ya UK huku waliotaka uhuru wakiwa asilimia 45 inamaanisha wengi wa Waskochi wanataka iwe hivyo. Na ukweli unabaki kuwa ukweli hata kama ni mchungu.

Hata hivyo, wakati ninatambua umuhimu wa sie kama Watanzania kujifunza kuhusu kura hiyo ya uhuru wa Uskochi, binafsi ninaona kuna unafiki mkubwa katika suala hili zima la 'tujifunze kutoka Uskochi.' Naomba nieleweke. Ni vema tujifunze kutoka kwa hawa wenzetu kuhusu hatma ya Muungano wetu lakini ninadhani ni unafiki kuamua kuchagua jema moja na kupuuzi mema mengine lukuki ya kujifunza kutoka kwa hawa wenzetu.

Eneo la kwanza la unafiki huo ni katika suala la uraia pacha. Moja ya hoja kuu iliyouwa wazo la uraia pacha kwa Watanzania walio nje ya nchi hiyo ni dhana fyongo kwamba uraia pacha ni tishio kwa usalama wa Tanzania. Si wanasema 'tujifunze kutoka Uskochi'? Sasa kwa taarifa tu ni kwamba katika kupiga kura hiyo ya uhuru wa Uskochi, baadhi ya wakazi wa taifa hili ambao japo si wazaliwa wala raia wa hapa waliruhusiwa kupiga kura. Kila mkazi wa Uskochi ambaye anatoka nchi za Jumuiya ya Madola aliruhusiwa kupiga kura. Na mie- hata kama ningekuwa sina sababu nyingine zilizoniruhusu kupiga kura- ningeweza kupiga kura kwa kigezo cha kuzaliwa Tanzania ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola.


Ni muhimu sana kutambua kuwa haki ya kupiga kura ni moja ya haki muhimu mno kwa mwananchi kwa sababu inachangia upatikanaji wa uongozi wa mahala husika, sambamba na ushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa taifa husika, kama ilivyo kwa suala la kura ya uhuru wa Uskochi.

Je Waskochi ni wendawazimu kuruhusu hata watu wasio na urai wa nchi hii kupiga kura? Hapana. Wenzetu wanathamini na kutambua mchango wa kila mwenye uhusiano na nchi hii, iwe wa kuzaliwa, asili au makazi. 

Na je kwa Waskochi kuruhusu  wakazi wa nchi hii ambao sio wazaliwa wa hapa, au wasio na uraia wa hapa, kupiga kura imehatarisha usalama wake? 

Naomba ieleweke kuwa haki ya kupiga kura haimfanyi mhusika kupewa uraia wa hapa bali ni moja ya vitambulisho muhimu sana. Kwa mfano, daftari la wapiga kura ni moja ya nyenzo muhimu katika uchunguzi unaofanywa na taasisi za fedha (credit check) kabla ya kutoa mkopo au hata kufungua akaunti ya benki. Kimsingi, kuwemo kwenye daftari hilo kunampatia mkazi wa hapa haki flani ambazo japo si sawa na uraia zinamsaidia katika maeneo mbalimbali.

Oh yes, tujifunze kutoka taifa tajiri la Uskochi linalowaenzi wageni wasio raia wa taifa hili ilhali masikini sie tunawahofia Watanzania wenzetu ambao kwa sababu moja au nyingine wamelazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine. Hapo kuna neno sahihi zaidi ya unafiki?

Twende katika maeneo mengine. Moja ya kumbukumbu muhimu kwenye runinga wakati matokeo ya kura hiyo yanatangazwa ni kuonekana kwa mkimbizi wa kisiasa kutoka Papua New Guinea, Benny Wanda, (pichani) akielezea anachojifunza kutoka kwa zoezi hilo la kidemokrasia 
Benny Wenda from West Papua, Indonesia

Wanda alikuja Uskochi kama mgeni wa kikundi kinachoitwa Radical Independence kujifunza jinsi kura ya maoni kuhusu uhuru inavyoandaliwa na kufanyika. Katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha BBC, kiongozi huyo alieleza jinsi alivyoguswa mno na jinsi uhuru ulivyokuwa ukitafutwa kwa uhuru mkubwa, akitolea mfano kutokuwepo kwa wanajeshi au polisi au vifaru mitaani tofauti na hali ilivyo nchi kwake wakati wa harakati za kudai uhuru kutoka Indonesia. Naam, tunasema tujiefunze kutoka Uskochi, lakini kimatendo ni kama picha hii hapa chini inavyoonyesha, na hapa sio katika harakati za wananchi kudai uhuru bali kutumia tu haki yao ya kikatiba kupinga uhuni unaofanywa dhidi ya upatikanaji wa Katiba mpya huko Dodoma 




Hebu tuache unafiki. Hivi kama hiyo haki 'kidogo' tu ya kuandamana kwa amani kwa minajili ya kutetea upatikanaji wa Katiba yenye maslahi kwa Watanzania wote, sambamba na kuokoa mabilioni ya fedha yanayotafunwa kwa Bunge 'feki' la Katiba huko Dodoma linazua haya, je tunaweza kukaribia japo kiduchu walipofika Waskochi kupiga kura kwa amani na utulivu kuhusu hatma ya nchi yao?

Na hata tukiweka kando hilo la matumizi makubwa ya nguvu za dola kunyamazisha sauti za wananchi, sambamba na kulazimisha matakwa ya watawala, bado kuna unafiki mwngi ne mwingi tu kama unavyotanabaishwa na picha zifuatazo


Picha hiyo juu inapigia mstari hoja yangu kuhusu unafiki. Naam, gazeti la serikali Daily News latoa rai kuwa tujifunze kutoka Uskochi, lakini picha iliyopo katika ukurasa huo inakinzana kabisa na hali ilivyo hapa Uskochi. Picha hiyo ni ya Rais Jakaya Kikwete akihutubia nchini Marekani ambapo amekwenda TENA kwa ziara ya WIKI MBI. Ni majuzi tu alikuwepo huko kwa siku kibao, lakini katika kuendeleza spirit ya 'safari ni safari' ameenda tena nchi humo.Ni hivi, ni nadra mno kusikia Waziri Mkuu wa Uskochi Alex Salmond akizurura huku na kule, au Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron akiwa kiguu na jia hapa na pale, au hata Malkia Elizabeti kuwa msafiri wa kila kukicha. Na hawa ni viongozi wa taifa hili tajiri kabisa lakini sio wazururaji kama Rais wetu.

Ndio rais lazima asafiri lakini sio kila baada ya wiki kadhaa, tena kurejea sehemu zilezile alizokwishatembelea. Hivi tangu 2014 hii ianze Kikwete ameshakwenda Marekani mara ngapi? Ndio, tujifunze kutoka Uskochi kuhusu kura ya uhuru wao lakini pia tujifunze kuhusu umuhimu wa viongozi kama Kikwete kutambua kuwa Tanzania yetu ni maskini isiyoweza kubeba gharama zisizo za lazima za Rais wake kusafiri kila anapojiskia.

Natambua ukweli kuwa kutokana na umasikini wetu, kuna haja ya viongozi wetu kwenda nje kusaka misaada. Lakini ni nani asiyejua kuwa asilimia kubwa ya misaada hiyo inaishia kwenye akaunti za mafisadi? Kadhalika, busara kidogo tu inaweza kutufundisha kwamba safari hizo za mara kwa mara za Kikwete zinatafuna sehemu ya fedha zinazosakwa kama misaada kwa nchi yetu.


Katika gazeti hili hapo juu tunakutana tena na wito wa kujifunza kutoka kwa kura ya uhuru wa Uskochi, lakini chini yake kuna habari kwamba deni la taifa limepaa hadi kufikia shilingi TRILIONI 42, kwa tarakimu ni shilingi  42,000,000,000,000 Na wakati hali yetu ikiwa mbaya kiasi hicho, bado twashuhudia serikali yetu ikifanya matumizi ya kitajiri kwa mfano kuruhusu uhuni unaoendelea huko Dodoma kwa jina la Bunge la Katiba, huku Kikwete akiendlea na safari zake za uuvumbuzi wa dunia.


Na picha ya hapo juu inathibiths unafiki wa kauli ya 'tujifunze kutoka Uskochi.' Kwa kifupi, zoezi zima la hadi kufikia kupigwa kura ya maoni liliambatana na uwazi na haki kwa kiwango cha juu kabisa. Japo ajenda ya uhuru ilikuwa katika manifesto ya chama tawala hapa Uskochi cha SNP, suala la uhuru lilibaki kuwa mikononi mwa Waskochi wote. Sasa kama mnavyoona hapo kwenye picha, kichwa kikuu cha habari kinahusu mwanasiasa wa upinzani Lema kupigwa marufuku na wafuasi wake kuandamana. Hivi haiwezekani wakaruhusiwa kuandamana huku wakisindikizwa na polisi? Na uzoefu umeonyesha kuwa mara nyingi polisi wakiridhia, maandamano hufanyika na kumalizika kwa amani. Mara nyingi pia, uamuzi wa polisi kulazimisha wananchi wasiandamane hupelekea vurugu na maafa yasiyo ya lazima


Pichani juu ni maandamano ya wanauonga mkono Uskochi kubaki sehemu ya UK, yaliyofanyika jana jioni hapa Glasgow, na polisi walikuwepo kwa minajili ya kuhakikisha hakuna uvunjifu wa amani lakini sio kuyazuwia maandamano hayo.

Nimalizie makala hii ndefu kidogo kwa kutilia mkazo kuwa tuna mengi ya kujifunza kutoka Uskochi na sio suala hilo la kura ya maoni pekee. Wanasiasa wa Uskochi na pengine Uingereza kwa ujumla wametoa darasa zuri kwa wababaishaji wetu huko nyumbani ambao licha ya kuwalipa mamilioni ya shilingi kwa mwezi kama mishahara na posho lakini tunachoishia kushuhudia ni matusi, vijembe, malumbano na upuuzi mwingine kwenye vikao vya Bunge la kawaida na hili la Katiba.

Ndiyo, umoja ni nguvu, na kura ya maoni ya uhuru wa Uskochi kumalizika kwa nchi hiyo kubaki sehemu ya United Kingdom kunatukumbusha sie wana-Muungano wa Tanganyika na Zanzibar juu ya umuhimu wa mshikamano lakini ni muhimu kutambua kuwa mazingira waliyopitia Waskochi kufikia hapa yameletwa heshima na utambuzi wa haki za kibinadamu, kidemokrasia sambamba na kuangalia mustakabali wa nchi hii sio kwa leo na kesho tu bali pia miaka mingi ijayo.





0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.