8 Oct 2014

Kuna msemo kuwa historia huandikwa na wenye uthubutu. Kadhalika, kuna msemo mwingine kwamba ile kushiriki tu katika shindano ni sehemu ya ushindi. 

Kwa siku kadhaa sasa, kundi la wanaharakati mtandaoni wakitumia mtandao wa kijamii wa Twitter wamekuwa wakiuliza maswali mbalimbali kuhusu mradi wa treni za kisasa jijini Dar ambao Wizara husika imeshasaini mkataba wa awali na kampuni moja ya Kimarekani.

Naomba kukiri kuwa najiskia fahari kuwa miongoni mwa wanaharakati hao ambao wameendelea kuuliza maswali kadhaa yanayotokana na utata unaozunguka mradi huo na mwekezaji husika. Ukifuatilia makala zangu zilizopita utaelewa vizuri nini kilichopelekea harakati hizi.

Pengine ni watu wachache walioshuhudia historia mpya ikiandikwa katika suala la uwekezaji nchi Tanzania, ambapo kwa mara ya kwanza kabisa, mwekezaji mtarajiwa amelazimika 'kuibuka' na kujaribu kujibu maswali kadhaa yanayoelekezwa kwake kuhusu mpango wake wa uwekezaji huko nyumbani. 
Hili si jambo dogo hata chembe kwani laiti moto huo uliaonzishwa na wanaharakati hao ukiweza kusambaa kwa wananchi wengi zaidi, basi kwa hakika tutakuwa tumeingia katika zama mpya ya 'uongozi wa wananchi wenyewe' au wananchi kama viongozi' kwa maana ya nguvu za umma/umoja wao kutumika kufuatilia masuala mbalimbali yanayowahusu, badala ya kusubiri taasisi za serikali au wanasiasa washughulikie.
Historia imeonyesha jinsi gani kero mbalimbali za wananchi zikiyeyuka huko Dodoma licha ya vichwa vya habari magazetini kudai 'Bunge kuwaka muhutu kuhusu ufisadi wa X au Y.' Kimsingi moto pekee huko Bungeni huishia kuwa vijembe na matusi kama sio kuteketea kwa fedha za walipakodi.
Nimeandika hapo juu kuhusu msemo 'ile kushiriki tu ni sehemu ya ushindi.' Japo ni mapema mno kubashiri matokeo ya jithada za wanaharakati hao, ukweli kwamba wameweza kumwibua mwekezaji kutoa ufafanuzi, ni kama ushindi flani wa kihistoria. Lakini ni muhimu kutambua kuwa ninaposema 'ushindi' simaanishi kuwa haya ni mashindano. Hapana. Hizi ni jithada za kutumia uwezo, akili na vipaji kuihudumia jamii ipasavyo. Ukiangalia wasifu wa wanaharakati hao ni watu wanaotoka katika kada mbalimbali kimaisha. Na tofauti na harakati za wanasiasa ambazo mara nyingi husukumwa na matarajio ya kupata kura au kujijenga kisiasa, jitihada za wanaharakati hawa ni kusaka haki kwa niaba ya wananchi wenzao. Ni kile Waingereza wanakiita 'sauti ya wasio na sauti (voice of the voiceless).
Japo hadi wakati ninaandika makala hii hakujapatikana 'majibu ya maana' kutoka kwa mwekezaji huyo, nina matarajio makubwa kwamba harakati hizi zitazaa matunda ya aina flani. Na hata kama matokeo yatakuwa tofauti, basi kwa hakika kinachofanyika sasa kinaweza kuuhamasisha umma kutambua kwamba kwa vile wao ndio wahanga wakubwa wa amsuala mbalimbali yanayofanywa na viongozi kwa niaba yao (na wakati mwingine pasi ridhaa yao), kamwe wasitarajie watu haohao 'wanaochanganya madawa' wajitokeza kutatua matatizo yanapojitokeza. 

Endelea kutembelea blogu hii kufuatilia maendeleo ya harakati hizo kuhusu utata unaokabili mradi huo wa treni za kisasa jijini Dar.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.