7 Oct 2014

10_06_DrSenga-cropped
Dokta Senga Omeonga (pichani), daktari bingwa wa upasuaji nchini Liberia, anadhani anajua jinsi gani aliambukizwa ugonjwa hatari wa Ebola.

Julai 15 mwaka huu, bosi wa daktari huyo aliingia ofisini kwake katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph, jijini Monrovia, akiwa na mashaka makubwa. Bosi huyo, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, alimwambia Dokta Omeonga, amepeana mkono na mtu ambaye baadaye aligundulika kuwa na ugonjwa wa Ebola, na sasa hajiskii vizuri. Mkurugenzi huyo alisema alikuwa akitapika, anasikia kuumwa na kichwa, na alikuwa na homa kali. Lakini siku mbili baadaye, baada ya vipimo vya maabara kuonyesha hajaathirika, na hofu ya Ebola kuondoka, Dokta Omeonga na wenzie walianza kumhudumia bosi wao kama mgonjwa wa kawaida wa malaria au homa ya matumbo.

"Tulivaa glovu wakati tunamhudumia, lakini si katika hali ya tahadhari sana," alisema Dokta huyo.

Wiki moja baadaye, afya ya Mkurugenzi ilizidi kuwa mbaya, na akachukuliwa vipimo vingine. Safari hii majibu yakaonyesha anaugua Ebola, ikiwa ni tukio la kwanza la vipimo vya awali kuonyesha mgonjwa hana maambukizi kabla ya vipimo vya pili kuonyesha ana maambukizi. Neno la kitabibu kwa hali hiyo ni 'false negative.'

Ghafla, kila aliyemhudumia Mkurugenzi huyo akawa katika hofu kubwa. na mwenye uwezekano wa kuwa ameambukizwa Ebola. Hospitali hiyo ikawekewa karantini, na Mkurugenzi akafariki Agosti 2, siku ambayo Dokta Omeonga alianza kutojiskia vizuri kiafya. Kati ya watumishi 20 waliomhudumia Mkurugenzi huyo, 15 walikutwa na Ebola, ikiwa ni pamoja na Dokta Omeonga. Tisa kati yao wameshafariki, ila yeye na wenzie watano wamesalimika.

Daktari huyo aliongea kwa simu na jarida la Newsweek la Marekani kutoka nyumbani kwake nchini Liberia, ambapo wiki tano baada ya kubainika kuwa hana virusi vya ugonjwa huo, bado anajikongoja kurejesha nguvu mwilini.

Hivi mtu anajiskiaje anapokuwa na Ebola?

Ni vigumu kueleza. Mie ni mtu mwenye afya njema. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuugua kiwango hicho. Hali ilikuwa mbaya sana sana. Unajiskia dhaifu kupita kiasi na uchovu mwingi. Unatapika na unajiskia homa na kichwa kuuma. Sio kama malaria. Ukiwa na malaria waweza japo kutembea, na unaweza kumeza dawa zako. Ebola ni tofauti kabisa. Ni kama mwili wako haupo nawe tena. Unajiskia huwezi kujihudumia mwenyewe, lazima awepo mtu wa kukuhudumia muda wote.

Ilikuwaje kwako na wenzio pale hospitali yenu ilipowekewa karantini?

Sote tulikuwa na dalili zinazofanana. Kila siku, mmoja baada ya mwingine alikuwa akilalamika kuhusu hali ilivyokuwa inazidi kuwa mbaya. Wakati mwingine tulikuwa tukicheka pamoja na kila kitu kuonekana kama kipo sawia.Lakini pale hali ilipoanza kubadilika, hakuna aliyweza japo kuamka kutoka kitandani.

Walikuwa wakichukua wagonjwa wale tu ambao walikuwa na hali mbaya kupindukia na kuwapelekea kwenye eneo la matibabu ya Ebola. Mie nilikuwa miongoni mwa waliokuwa na nafuu kidogo, kwahiyo ilibidi nisubiri kitambo. Eneo hilo la matibabu lilikuwa ni moja tu kwa jiji zima la Monrovia. Vitanda 40 tu. Ilibidi nisubiri wiki nzima kabla ya kupatia kitanda. Japo walikuwa wakitoa kipaumbele kwa watumishi wa sekta ya afya, bado ilichukua wiki nzima kupata kitanda.

Ulikuwa mmoja wa watumishi watatu wa hospitali yako kupatia dawa ya majaribio ZMapp. Ulijiskiaje ulipoanza kutumia vidonge hivyo?

Nilipewa ZMapp wiki moja baada ya kulazwa katika eneo la matibau ya Ebola. Nilikuwa nikijiskia ahueni kidogo, kuhara kulikuwa kumesimama. Nilikuwa sitapiki tena, na nilikuwa nikijilazimisha kula japo kidogo. Sikuwa na hali mbaya sana wakati naanza kutumia vidonge hivyo. Ninachoweza kusema ni kwamba labda vidonge hivyo vilisaidia kasi ya uponyaji wangu lakini huenda ningeweza kupona bila hata kuvitumia.


Ulijiskiaje kutumia dawa mbayo ilikuwa katika majaribio?

Nilikuwa na hofu kiasi. Lakini pia sikujali sana kwa sababu nilikuwa sina njia nyingine.Hiyo ilikuwa nafasi yangu ya kupata uponyaji. Kama ingenisaidia, ningeiridhia.

Wewe na wenzako mliyamudu vipi matibabu ya vidonge hivyo?

Kwa bahati mbaya, daktari aliyepaswa kupewa vidonge hivyo alifariki siku vilipowasili. Kwahiyo walimpatia mwingine aliyekuwa amepoteza fahamu. Shukrani kwa Mungu kwani hali yake ilikuwa mahututi na uwezekano wa kusalimika ulikuwa mdogo.Lakini baada ya kumeza vidonge hivyo hali yake iliboreka na kila mtu alishangaa. Siku iliyofuata alirejewa na fahamu. Siku chache baadaye aliweza kutembea. Daktari mwingine aliyepatiwa vidonge hivyo alifariki. Kwahiyo kati yetu watatu, mmoja alifariki na sie wawili tulisalimika.

Je dawa hizo zilikuwa na matokeo yasiyokusudiwa (side effects)?


Nilipatwa na matatizo katika dozi ya mwisho ya ZMapp lakini nadhani ilitokana na kasoro za kitabibu, kwa sababu hawakunipatia dawa ya kuzwia aleji niliyostahili kupewa. Nilipatwa na hali mbaya, nikawa najiskia baridi kali, shida katika kupumua vizuri, na maumivu makali ya kichwa. Hali ilikuwa mbaya sana. Kwahiyo ilibidi wasitishe matibabu na kunipatia dawa aina ya cortisone. Baada ya hapo nikawa dhaifu sana. Sikumudu japo kutoka kitandani. Baadaye nikaanza kujisikia nafuu.Nilikaa katika eneo la matibabu ya Ebola kwa wiki mbili unusu.

Wajiskiaje sasa?


Nimekuwa nyumbani kwa mwezi na wiki moja sasa. Kuna maendeleo ya kuridhisha kila siku. Nguvu zangu zanirejea. Lakini hatua ya kuwa katika afya ya kawaida inakuja taratibu sana. Bado naskia maumivu ya viungo, na udhaifu mwilini bado upo. Ni vigumu kusema lini nitakuwa nimepona kabisa- labda pengine mwezi mzima kutoka sasa. Hakuna anyefahamu hali inakuwaje baada ya kupona Ebola kwa sababu virusi vya ugonjwa huo vinateketeza kila kitu mwilini.

Je una familia?

Familia yangu haipo hapa nami, vinginevyo wote wangekuwa wameambukizwa. Wapo nchini Kanada.

Utafanya nini baada ya kupona kabisa?


Nitarejea kazini. Nitawahudumia wagonjwa kama kawaida. Kwa sasa nina kinga dhidi ya aina ya maambukizi (strain) ya Ebola niliyoambukizwa. Hiyo ni moja ya aina hatari kabisa za maambukizi ya Ebola, kwahiyo kama una kinga dhidi yake basi yawezekana kuwa na kinga dhidi ya aina nyinginezo pia.

Nitatumia zana za kujikinga. Hiyo ni lazima kwani kuna hatari ya kuwaambukiza wagonjwa wengine baada ya kuwabeba wagonjwa.  Hospitali yangu imefungwa kwa takriban miezi miwili sasa. Wizara ya Afya imenyunyizia dawa hospitali hiyo, na tuna mpango wa kuifungua tena baada ya miezi miwili.

Unadhani kwanini watumishi wengi wa sekta ya afya wameambukizwa Ebola?


Hatuna zana za kutosha za kujikinga na maambukizi. Hiyo ni changamoto kubwa na tatizo kubwa. Ndio maana hospitali nyingi zimefungwa. Hakuna zana za kutosha kwa kila mtumishi wa sekta ya afya. Wanaweza kukupatia glovu lakini wasikupe magauni rasmi ya kuhudumia wagonjwa wa Ebola. Au wanaweza wasikupe kinga ya uso (mask). Lakini sasa kutokana na misaada ya kimataifa, hali inazidi kuwa bora., na kama hatuna zana za kujikinga na maambukizi hatuwahudumii walioambukizwa. Lakini kwa kutowatibu, wagonjwa wanarudi majumbani na kuambukiza jamii zao. Hilo ni tatizo kubwa.

CHANZO: Imetafsiriwa kutoka jarida la NEWSWEEK





0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.