Showing posts with label Ebola. Show all posts
Showing posts with label Ebola. Show all posts

30 Dec 2014



Nesi mmoja aliyekwenda Sierra Leone kusaidia harakati za kukabiliana na janga la ugonjwa wa Ebola, amerudi Uingereza akiwa ameambukizwa ugonjwa huo, na hivi sasa amelazwa kwenye kituo cha maradhi ya kuambukiza cha Browlee katika Hospitali Kuu ya Gartnavel, hapa Glasgow.

Nesi huyo anatarajiwa kuhamishiwa London kwenye hospitali maalum ya Royal Free Hospital.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Uskochi, Nicola Sturgeon, amewahakikishia wakazi wa Glasgow na Uskochi kwa ujumla kuwa uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo kutokana na maambukizi ya nesi huyo ni 'sawa na sifuri.'

Hata hivyo, bado kuna maswali ilikuwaje nesi huyo aliyepimwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow, London, kabla ya kuunganisha ndege na kuja Glasgow, hakugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo hatari usio na kinga wala tiba.

Profesa Jonathan Ball, mtaalam wa 'molecular virology' katika Chuo Kikuu cha Nottingham, ameeleza kuwa kesi hiyo inaashiria ugumu wa mkakati wa kupima wasafiri kutoka nchi zilzoathirika na Ebola wanapoingia Uingereza.

Chini ni baadhi ya picha zinazohusiana na habari hii ambayo waweza kuisoma kwa kirefu HAPA

A female health worker who returned from Sierra Leone last night is being treated for Ebola at Glasgow's Gartnavel Hospital (pictured), the Scottish Government confirmed
Hospitali ya Gartnavel

Safari ya nesi aliyeambukizwa Ebola, kutoka Sieera Leone hadi Glasgow.



The health worker was admitted to hospital early yesterday morning after feeling unwell and was placed in isolation 

The ebola patient is being treated at the specialist Brownlee Unit for Infectious Diseases at Gartnavel Hospital
Kituo cha maradhi ya kuambukiza cha Brownlee

15 Oct 2014

Oktoba 20 mwaka huu itakuwa siku muhimu kwa Nigeria kwani siku hiyo taifa hilo litaadhimisha siku 42 tangu mtu wa mwisho kuthibitishwa kuwa na maambukizi ya Ebola. Idadi hiyo ya siku ni mara maradufu ya muda ambao Ebola yaweza kujitokeza hadharani (incubation period). Kwa maana hiyo, siku hiyo, Nigeria itakuwa na haki ya kujitangaza kuwa ipo huru dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Hata hivyo, jana, Nigeria iliadhimisha tukio jingine ambalo pengine isingependa kulikumbuka: miezi sita kamili tangu kikundi cha kigaidi cha Kiislamu cha Boko kilipowateka wanafunzi wa kike 276 na kupelekea kelele takriban kila kona ya dunia kwa kampeni ya #BringBackOurGirls (Warejesheni Mabinti zetu).

Hata hivyo, licha ya kampeni hiyo, mabinti 219 bado wanaendelea kuwa mateka wa magaidi hao tangu walipotekwa katika eneo la Chibok. Licha ya tukio hilo la kinyama kuvuta hisia na sapoti ya watu wengi duniani, magaidi hao wanaendelea kufanya unyama wao uliopelekea maelfu ya mauaji, hususan katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Maadhimisho hayo mawili yanazua swali linalokanganya: imewezekanaje kwa Nigeria kumudu kuidhibiti Ebola lakini imeshindwa kuidhibiti Boko Haram? Kwanini taifa hilo limeweza kulishughulikia tatizo moja kwa ufanisi mkubwa ilhali ikilishughulikia jingine kwa udhaifu mkubwa?

"Ebola inamgusa kila mtu."

Moja ya sababu ni jiographia ya kisiasa (political geography) ya Nigeria.ambayo tangu nchi hiyo kupata uhuru wake imekabiliwa na machafuko. Taifa hilo lenye watu milioni 170 ambao wamegawanyika katika makabila lukuki, limeshindwa kwa kiasi kikubwa kujenga umoja,mshikamano na maelewano kati ya wengi wa Wakristo wanaojiweza kwa upande wa kusini mwa nchi hiyo na wengi wa Waislamu wanaokabiliwa na ufukara upande wa kaskazini mwa nchi hiyo.

Boko Haram ambayo maana yake ni ni 'elimu ya kimagharibi ni dhambi,' inautumia mwanya huo.Kundi hilo linafanya zaidi shughuli zake katika majimbo matatu ya kaskazini mashariki, yote yakiwa chini ya uongozi wa chama cha upinzani cha All People's Party (APP), na ambako imani kwa Rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan, ni haba.

"Watu wengi kaskazini mwa Nigeria wanaichukia Boko Haram," anaeleza Rudy Atallah wa taasisi ya The Atlantic Council na mtaalam wa masuala ya nchi hiyo. "Lakini kwa vile idadi kubwa ya watu wa kaskazini mwa nchi hiyo wanaona kama wametelekezwa na wenzao wa kusini kwa muda mrefu, wengi wanaiona Boko Haram kama chombo kinachoweza kuambana na serikali," anatanabaisha mtaalam huyo.

Katika hali tofauti, Patrick Swayer, Mwamerika mwenye asili ya Liberia alipogundulika kuwa na Ebola alipowasili Lagos, alijikuta katika jiji lililosheheni miundominu ya kisasa ya huduma za afya na makao makuu ya taasisi nyingi za kimataifa, Na tofauti na mapambano dhidi ya Boko Haram, mapambano dhidi ya Ebola yanavuka mipaka ya ukabila, siasa na dini.

"Ebola inamgusa kila mtu," anasema Atallah. "Haina madhehebu wala kundi maalum."

'Kasheshe' nyingine nchini humo yatarajiwa Februari mwakani wakati taifa hilo litakapofanya uchaguzi wa Rais. Baada ya mhula mmoja madarakani, Rais Jonathan anaruhusiwa kugombea tena. Ushindi kwa chama chake cha People's Democratic Party, ambacho kimeitawala Nigeria kwa miaka 14, na ambacho kina sapoti kubwa kusini mwa nchi hiyo, waweza kuchochea mgawanyiko zaidi nchini humo, sambamba na ugumu wa kuwaokoa mateka waliosalia mikononi mwa Boko Haram.

CHANZO: Makala hii imetafsiriwa kutoka hifadhi yangu ya habari muhimu, ninazokutana nazo mtandaoni na kuzihifadhi katika app ya Instapaper. App nyingine ninayoitumia kwa hifadhi ya habari ninazozitumia kama reference ni Pocket. Kadhalika, app nyingine muhimu ninayoitumia kuhifadhi vitu mbalimbali ninavyokutana navyo mtandaoni au hata mtaani ni Evernote





Chris Brown is sharing his thoughts about Ebola. (Getty Images)
Dunia yetu imesheheni watu wanaoitwa 'conspiracy theorists,' Sina uhakika wa tasiri ya kiswahili ya neno hilo, lakini nadhani neno la karibu ni 'wazushi.' Hata hivyo, tofauti ya wazushi tuliowazowea ambao mara nyingi huzusha jambo kwa minajili ya kuzusha tu, kwa conspiracy theorist uzushi wao huambatana na 'ushahidi wa kimazingira,' japo si ajabu ushahidi huo nao kuelemea zaidi kwenye uzushi kuliko facts.

Sasa msanii maarufu wa Marekani, Chris Brown, nae ameingia katika kundi la conspiracy theorists baada ya kudai kuwa ugonjwa hatari wa Ebla ni moja ya mbinu za kudhibiti idadi ya watu duniani.

Msanii huyo ali-post mtizamo wake huo kwenye ukurasa wake wa Twitter, ambapo ana 'wafuasi' (followers) milioni 13.7. Hata hivyo, baadhi yao walipingana nae waziwazi

"Wajua mjadala kuhusu ugonjwa wa Ebola ulichokuwa unahitaji? Upuuzi zaidi. Hapa anaingia Chris Brown..." aliandika mmoja wa wafuasi wake.

"Chris Brwon anadai Ebola ni moja ya mbinu za kudhibiti idadi ya watu. Ajaribu ugonjwa." alitwiti mwingine  huo  akimaanisha msanii huyo ni miongoni mwa watu wanaohitaji kudhibitiwa.

"Chris Brown anadai kuwa Ebola ni njia ya kudhibiti widadi ya watu. Kwa hakika hiyo si kweli, na laiti ingekuwa kweli basi tungempa ugonjwa huo yeye kwanza," aliandika mwingine.

Brown ambaye hivi karibuni alitumikia kifungo cha siku 108 jela kwa kukiuka taratibu za uangalizi wa kimahakama (probation) kufuatia kosa la kumpiga mpenzi wake wa zamani, msanii Rihanna, baadaye alionekana kutafakari upya kauli yake, na kutanabaisha kuwa 'anafunga mdomo wake,' japo si kwa maneno ya kistaarabu.

Lakini muda mfupi baadae 'alipandisha mzuka' na kuwashambulia waliopingana na mtizamo wake huo, na kutwiti maneno makali: "naandika ninachotaka. Kama hutaki nyonya %$*£$ yangu (tusi)

Hata hivyo, licha ya baadhi ya watu kupingana na conspiracy theory hiyo ya msanii huyo, watu kadhaa katika mtandao huo wa Twitter walionekana kuafikiana nae kwa tweet hiyo kupata takriban  'Retweets' 30,000 na 'Favourites' 22,000.

Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola umeshasababisha vifo zaidi ya 4000 huku Afrika ya Magharibi ikiwa ni eneo lililoathirika vibaya zaidi japo tayari kuna wagonjwa wachache waliokumbwa na maradhi hayo huko Hispania na Marekani.

CHANZO: Imetafsiriwa kutoka mtandaoni



7 Oct 2014

10_06_DrSenga-cropped
Dokta Senga Omeonga (pichani), daktari bingwa wa upasuaji nchini Liberia, anadhani anajua jinsi gani aliambukizwa ugonjwa hatari wa Ebola.

Julai 15 mwaka huu, bosi wa daktari huyo aliingia ofisini kwake katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph, jijini Monrovia, akiwa na mashaka makubwa. Bosi huyo, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, alimwambia Dokta Omeonga, amepeana mkono na mtu ambaye baadaye aligundulika kuwa na ugonjwa wa Ebola, na sasa hajiskii vizuri. Mkurugenzi huyo alisema alikuwa akitapika, anasikia kuumwa na kichwa, na alikuwa na homa kali. Lakini siku mbili baadaye, baada ya vipimo vya maabara kuonyesha hajaathirika, na hofu ya Ebola kuondoka, Dokta Omeonga na wenzie walianza kumhudumia bosi wao kama mgonjwa wa kawaida wa malaria au homa ya matumbo.

"Tulivaa glovu wakati tunamhudumia, lakini si katika hali ya tahadhari sana," alisema Dokta huyo.

Wiki moja baadaye, afya ya Mkurugenzi ilizidi kuwa mbaya, na akachukuliwa vipimo vingine. Safari hii majibu yakaonyesha anaugua Ebola, ikiwa ni tukio la kwanza la vipimo vya awali kuonyesha mgonjwa hana maambukizi kabla ya vipimo vya pili kuonyesha ana maambukizi. Neno la kitabibu kwa hali hiyo ni 'false negative.'

Ghafla, kila aliyemhudumia Mkurugenzi huyo akawa katika hofu kubwa. na mwenye uwezekano wa kuwa ameambukizwa Ebola. Hospitali hiyo ikawekewa karantini, na Mkurugenzi akafariki Agosti 2, siku ambayo Dokta Omeonga alianza kutojiskia vizuri kiafya. Kati ya watumishi 20 waliomhudumia Mkurugenzi huyo, 15 walikutwa na Ebola, ikiwa ni pamoja na Dokta Omeonga. Tisa kati yao wameshafariki, ila yeye na wenzie watano wamesalimika.

Daktari huyo aliongea kwa simu na jarida la Newsweek la Marekani kutoka nyumbani kwake nchini Liberia, ambapo wiki tano baada ya kubainika kuwa hana virusi vya ugonjwa huo, bado anajikongoja kurejesha nguvu mwilini.

Hivi mtu anajiskiaje anapokuwa na Ebola?

Ni vigumu kueleza. Mie ni mtu mwenye afya njema. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuugua kiwango hicho. Hali ilikuwa mbaya sana sana. Unajiskia dhaifu kupita kiasi na uchovu mwingi. Unatapika na unajiskia homa na kichwa kuuma. Sio kama malaria. Ukiwa na malaria waweza japo kutembea, na unaweza kumeza dawa zako. Ebola ni tofauti kabisa. Ni kama mwili wako haupo nawe tena. Unajiskia huwezi kujihudumia mwenyewe, lazima awepo mtu wa kukuhudumia muda wote.

Ilikuwaje kwako na wenzio pale hospitali yenu ilipowekewa karantini?

Sote tulikuwa na dalili zinazofanana. Kila siku, mmoja baada ya mwingine alikuwa akilalamika kuhusu hali ilivyokuwa inazidi kuwa mbaya. Wakati mwingine tulikuwa tukicheka pamoja na kila kitu kuonekana kama kipo sawia.Lakini pale hali ilipoanza kubadilika, hakuna aliyweza japo kuamka kutoka kitandani.

Walikuwa wakichukua wagonjwa wale tu ambao walikuwa na hali mbaya kupindukia na kuwapelekea kwenye eneo la matibabu ya Ebola. Mie nilikuwa miongoni mwa waliokuwa na nafuu kidogo, kwahiyo ilibidi nisubiri kitambo. Eneo hilo la matibabu lilikuwa ni moja tu kwa jiji zima la Monrovia. Vitanda 40 tu. Ilibidi nisubiri wiki nzima kabla ya kupatia kitanda. Japo walikuwa wakitoa kipaumbele kwa watumishi wa sekta ya afya, bado ilichukua wiki nzima kupata kitanda.

Ulikuwa mmoja wa watumishi watatu wa hospitali yako kupatia dawa ya majaribio ZMapp. Ulijiskiaje ulipoanza kutumia vidonge hivyo?

Nilipewa ZMapp wiki moja baada ya kulazwa katika eneo la matibau ya Ebola. Nilikuwa nikijiskia ahueni kidogo, kuhara kulikuwa kumesimama. Nilikuwa sitapiki tena, na nilikuwa nikijilazimisha kula japo kidogo. Sikuwa na hali mbaya sana wakati naanza kutumia vidonge hivyo. Ninachoweza kusema ni kwamba labda vidonge hivyo vilisaidia kasi ya uponyaji wangu lakini huenda ningeweza kupona bila hata kuvitumia.


Ulijiskiaje kutumia dawa mbayo ilikuwa katika majaribio?

Nilikuwa na hofu kiasi. Lakini pia sikujali sana kwa sababu nilikuwa sina njia nyingine.Hiyo ilikuwa nafasi yangu ya kupata uponyaji. Kama ingenisaidia, ningeiridhia.

Wewe na wenzako mliyamudu vipi matibabu ya vidonge hivyo?

Kwa bahati mbaya, daktari aliyepaswa kupewa vidonge hivyo alifariki siku vilipowasili. Kwahiyo walimpatia mwingine aliyekuwa amepoteza fahamu. Shukrani kwa Mungu kwani hali yake ilikuwa mahututi na uwezekano wa kusalimika ulikuwa mdogo.Lakini baada ya kumeza vidonge hivyo hali yake iliboreka na kila mtu alishangaa. Siku iliyofuata alirejewa na fahamu. Siku chache baadaye aliweza kutembea. Daktari mwingine aliyepatiwa vidonge hivyo alifariki. Kwahiyo kati yetu watatu, mmoja alifariki na sie wawili tulisalimika.

Je dawa hizo zilikuwa na matokeo yasiyokusudiwa (side effects)?


Nilipatwa na matatizo katika dozi ya mwisho ya ZMapp lakini nadhani ilitokana na kasoro za kitabibu, kwa sababu hawakunipatia dawa ya kuzwia aleji niliyostahili kupewa. Nilipatwa na hali mbaya, nikawa najiskia baridi kali, shida katika kupumua vizuri, na maumivu makali ya kichwa. Hali ilikuwa mbaya sana. Kwahiyo ilibidi wasitishe matibabu na kunipatia dawa aina ya cortisone. Baada ya hapo nikawa dhaifu sana. Sikumudu japo kutoka kitandani. Baadaye nikaanza kujisikia nafuu.Nilikaa katika eneo la matibabu ya Ebola kwa wiki mbili unusu.

Wajiskiaje sasa?


Nimekuwa nyumbani kwa mwezi na wiki moja sasa. Kuna maendeleo ya kuridhisha kila siku. Nguvu zangu zanirejea. Lakini hatua ya kuwa katika afya ya kawaida inakuja taratibu sana. Bado naskia maumivu ya viungo, na udhaifu mwilini bado upo. Ni vigumu kusema lini nitakuwa nimepona kabisa- labda pengine mwezi mzima kutoka sasa. Hakuna anyefahamu hali inakuwaje baada ya kupona Ebola kwa sababu virusi vya ugonjwa huo vinateketeza kila kitu mwilini.

Je una familia?

Familia yangu haipo hapa nami, vinginevyo wote wangekuwa wameambukizwa. Wapo nchini Kanada.

Utafanya nini baada ya kupona kabisa?


Nitarejea kazini. Nitawahudumia wagonjwa kama kawaida. Kwa sasa nina kinga dhidi ya aina ya maambukizi (strain) ya Ebola niliyoambukizwa. Hiyo ni moja ya aina hatari kabisa za maambukizi ya Ebola, kwahiyo kama una kinga dhidi yake basi yawezekana kuwa na kinga dhidi ya aina nyinginezo pia.

Nitatumia zana za kujikinga. Hiyo ni lazima kwani kuna hatari ya kuwaambukiza wagonjwa wengine baada ya kuwabeba wagonjwa.  Hospitali yangu imefungwa kwa takriban miezi miwili sasa. Wizara ya Afya imenyunyizia dawa hospitali hiyo, na tuna mpango wa kuifungua tena baada ya miezi miwili.

Unadhani kwanini watumishi wengi wa sekta ya afya wameambukizwa Ebola?


Hatuna zana za kutosha za kujikinga na maambukizi. Hiyo ni changamoto kubwa na tatizo kubwa. Ndio maana hospitali nyingi zimefungwa. Hakuna zana za kutosha kwa kila mtumishi wa sekta ya afya. Wanaweza kukupatia glovu lakini wasikupe magauni rasmi ya kuhudumia wagonjwa wa Ebola. Au wanaweza wasikupe kinga ya uso (mask). Lakini sasa kutokana na misaada ya kimataifa, hali inazidi kuwa bora., na kama hatuna zana za kujikinga na maambukizi hatuwahudumii walioambukizwa. Lakini kwa kutowatibu, wagonjwa wanarudi majumbani na kuambukiza jamii zao. Hilo ni tatizo kubwa.

CHANZO: Imetafsiriwa kutoka jarida la NEWSWEEK





Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.