10 Oct 2014

Kwanza soma taarifa ifuatayo kutoka Ikulu kisha tuijadili pamoja
Kweli Tanzania yetu haina uhaba wa mazingaombwe. Lakini hilo dogo, kubwa ni 'akili' za baadhi ya wasaidizi wa Rais. Binafsi nimekuwa mpinzani sana wa hoja kuwa 'tatizo si JKI bali wasaidizi/ watendaji wake,' kigezo changu kikubwa kikiwa 'kwani walimshikia mtutu wa bunduki awateue na kisha kumtahadharisha kuwa akiwatimua pindi watapoboronga watamdhuru'?

Lakini ukiangalia mlolongo wa 'makanusho' yanayotolewa na wasaidizi wa Rais, unaweza kukubaliana na wanaosema kuwa 'wasaidizi/ watendaji wa JK wanamwangusha' (japo siafiki wanaotaka kutumia sababu hiyo kama excuse ya kumsafisha JK mwenyewe.)


Hebu tuichambue kauli hiyo ya Ikulu hatua kwa hatua. Kwanza, Ikulu haikuwahi kukanusha lundo la picha (kama hiyo inayoambatana na kichwa cha habari hii) zilizowekwa mtandaoni zikimwonyesha Rais Kikwete akipokea zawadi ya saa, huku maelezo yakibainisha waziwazi kuwa 'Rais Jakaya Kikwete akipokea zawadi ya saa..." Najua kwanini hawakuhangaika na taarifa hizo za awali: hazikuhusiana na 'utata' unaomkabili mwekezaji aliyetoa zawadi hiyo.
Lakini baada ya gazeti la Raia Mwema kueleza bayana kuwa mwekezaji wa mradi wa treni ya kisasa Dar ndiye huyo alompa zawadi ya saa Rais Kikwete, na kutanabaisha maswali kadhaa yanayouzunguka mradi husika na wasifu wa mwekezaji huyo, Ikulu ikakurupuka na kanusho hili. WALIKUWA WAPI MUDA WOTE HUO?

Mwandishi wa taarifa hiyo ameonyesha ni mtovu wa nidhamu wa kutokana na matumizi ya maneno yasiyopaswa kutoka ofisi iliyopo sehemu 'tukufu' kama Ikulu. Matumizi ya maneno kama "ni habari ya uzushi na UPUUZI..." na  "...kumhusisha Rais na zawadi ya KIPUUZI kama saa..."Huwezi kuita upuuzi habari inayohoji suala la msingi, ambapo logically, mfanyabiashara anaonekana akitoa zawadi kwa Rais (iwe saa au suti), kisha siku chache baadaye mfanyabiashara huyo anatangaza 'mradi wa utata'...Kwanini wananchi (waandishi wa gazeti hilo ni sehemu ya wananchi hao) wasihoji suala hilo ambalo mwandishi wa Ikulu anaona ni la kipuuzi?

Na kwa kinachoweza kuelezwa kama uhuni na si ubabaishaji, taarifa hiyo ya Ikulu imekwepa kabisa kuzungumzia maswali lukuki yanayoiandama kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara huyo, wasifu wa mfanyabiashara mwenyewe, sambamba na 'sintofahamu' lukuki kuhusu uwekezaji huo.

Kimsingi, habari Ikulu 'imejishtukia' tu inapodai "Ni habari ya uzushi na upuuzi. Ni habari inayolenga kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwamba amepokea zawadi kutoka kwa mtu ambaye anajaribu kupewa kandarasi ya kujenga ya usafiri wa treni jijini DSM na ambaye pia anahusishwa kwenye shughuli nyingine za kibiashara zenye utata huko kwao Marekani."

Kwa wapambe hao wa Rais ni upuuzi na kumdhalilisha Rais kupokea zawadi kutoka kwa mtu ambaye WANAKIRI BAYANA kuwa anahusishwa na shughuli nyingine za kibiashara ZENYE UTATA huko Marekani. 

Kwanini taarifa hiyo isingewekeza nguvu katika 'kumsafisha' Rais kwa 'kujihusisha' na mtu huyo wanayekiri kuwa na shughuli zenye utata, badala ya kung'ang'ania hoja moja tu 'ya kipuuzi' kuhusu 'zawadi ya kipuuzi' ya saa?

Kilicho bayana ni kasumba iliyoota mizizi kwenye utawala wa Kikwete wa kudhani Watanzania wanaishi karne ya 18, hawana access na internet kufuatilia masuala mbalimbali yanayoihusu nchi yao, na hata wakifuatilia na kupatwa na hofu basi wakae kimya!

Suala la msingi si Rais kupewa zawadi, iwe ni Rolex au 'souvenir watch' nyingine, bali ni utata unaozunguka kampuni inayotaka kuwekeza katika mradi wa treni za kisasa, na inayomilikiwa na mtu ambaye anazungukwa na habari zenye utata, na ambaye alimzawadia Rais saa (iwe halisi au souvenir' tu) siku chache kabla ya kutangazwa taarifa za uwekezaji huo. Surely huu sio upuuzi bali ni kuihoji serikali yetu ambayo ina historia 'nzuri tu' ya kuingia mikataba ya 'ajabu ajabu' kama ule wa kitapeli wa Richmond.

Nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha wasaidizi wa Rais Kikwete kwamba Watanzania wana haki ya msingi kuuliza maswali kuhusu masuala yanayohusu taifa lao. Kadhalika, wanahabari wana haki ya kuhoji utata unapojitokeza katika mahusiano ya serikali au viongozi wake (hususan Rais) na watu au taasisi mbalimbali.

By the way, ajira ya mwandishi wa taarifa hiyo inategemea kumtetea bosi wake, na hakuna cha ajabu katika kujitokeza kwake kwa ukali kukanusha taarifa hiyo. Lakini kama wana ujasiri, basi wajibu maswali haya tuliyomuuliza mwekezaji huyo badala ya kung'ang'ania 'hoja ya kipuuzi ya "SIO ROLEX" au kutuhadaa kuwa "saa aliyopewa Rais Kikwete ni mali ya Watanzania" (mbona hawakutangaza kuwa Rais amekabidhiwa saa ambayo ni mali ya Watanzania hadi walipoona habari hiyo kwenye gazeti la Raia Mwema?)

Rais Kikwete amekuwa ajitianabaisha kama muumini wa dhana ya 'open goverment' inayopigia mstari haja ya wananchi kufahamu utendaji kazi wa serikali yao. Lakini wakati huohuo, wasaidizi wake huwa wakali kweli pindi wananchi wanapotaka kufuata dhana hiyo na kuhoji 'maswali magumu' kama hayo yanayouzunguka mradi wa treni za kisasa Dar.

Ni muhimu kwa watendaji wa serikali yetu kutambua kwamba Rais wanayemtumikia ni mwajiriwa wa Watanzania, na kila mwajiriwa anatambua haki ya mwajiri wake kuhoji masuala mbalimbali yanayomtatiza. Tanzania ni yetu sote na si ya kikundi kidogo cha miungu-watu wasiotaka kuuliza 'kulikoni?' hata katika masuala yanayohitaji 'akili ndogo' tu ya ku-Google kuhusu mtu au taasisi flani (kama ilivyo kwa ishu ya 'M/S Shumoja a.k.a Shumake Rails.'


1 comment:

  1. Picha husika ni kielelezo juu ya zawadi hiyo,binafsi sitojikita ktk kuangalia zawadi iliyotolewa,cha msingi tungetaraji kauli yoyote au taarifa yoyote juu ya anayedaiwa kuwa mwekezaji kwa kuangalia ni aina gani ya mwekezaji ambayo serikali inaingia ubia na tuhuma alizonazo mwekezaji huyo ambaye taarifa zake zinaaonekana kuwa na utata.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.