15 Oct 2014

Oktoba 20 mwaka huu itakuwa siku muhimu kwa Nigeria kwani siku hiyo taifa hilo litaadhimisha siku 42 tangu mtu wa mwisho kuthibitishwa kuwa na maambukizi ya Ebola. Idadi hiyo ya siku ni mara maradufu ya muda ambao Ebola yaweza kujitokeza hadharani (incubation period). Kwa maana hiyo, siku hiyo, Nigeria itakuwa na haki ya kujitangaza kuwa ipo huru dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Hata hivyo, jana, Nigeria iliadhimisha tukio jingine ambalo pengine isingependa kulikumbuka: miezi sita kamili tangu kikundi cha kigaidi cha Kiislamu cha Boko kilipowateka wanafunzi wa kike 276 na kupelekea kelele takriban kila kona ya dunia kwa kampeni ya #BringBackOurGirls (Warejesheni Mabinti zetu).

Hata hivyo, licha ya kampeni hiyo, mabinti 219 bado wanaendelea kuwa mateka wa magaidi hao tangu walipotekwa katika eneo la Chibok. Licha ya tukio hilo la kinyama kuvuta hisia na sapoti ya watu wengi duniani, magaidi hao wanaendelea kufanya unyama wao uliopelekea maelfu ya mauaji, hususan katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Maadhimisho hayo mawili yanazua swali linalokanganya: imewezekanaje kwa Nigeria kumudu kuidhibiti Ebola lakini imeshindwa kuidhibiti Boko Haram? Kwanini taifa hilo limeweza kulishughulikia tatizo moja kwa ufanisi mkubwa ilhali ikilishughulikia jingine kwa udhaifu mkubwa?

"Ebola inamgusa kila mtu."

Moja ya sababu ni jiographia ya kisiasa (political geography) ya Nigeria.ambayo tangu nchi hiyo kupata uhuru wake imekabiliwa na machafuko. Taifa hilo lenye watu milioni 170 ambao wamegawanyika katika makabila lukuki, limeshindwa kwa kiasi kikubwa kujenga umoja,mshikamano na maelewano kati ya wengi wa Wakristo wanaojiweza kwa upande wa kusini mwa nchi hiyo na wengi wa Waislamu wanaokabiliwa na ufukara upande wa kaskazini mwa nchi hiyo.

Boko Haram ambayo maana yake ni ni 'elimu ya kimagharibi ni dhambi,' inautumia mwanya huo.Kundi hilo linafanya zaidi shughuli zake katika majimbo matatu ya kaskazini mashariki, yote yakiwa chini ya uongozi wa chama cha upinzani cha All People's Party (APP), na ambako imani kwa Rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan, ni haba.

"Watu wengi kaskazini mwa Nigeria wanaichukia Boko Haram," anaeleza Rudy Atallah wa taasisi ya The Atlantic Council na mtaalam wa masuala ya nchi hiyo. "Lakini kwa vile idadi kubwa ya watu wa kaskazini mwa nchi hiyo wanaona kama wametelekezwa na wenzao wa kusini kwa muda mrefu, wengi wanaiona Boko Haram kama chombo kinachoweza kuambana na serikali," anatanabaisha mtaalam huyo.

Katika hali tofauti, Patrick Swayer, Mwamerika mwenye asili ya Liberia alipogundulika kuwa na Ebola alipowasili Lagos, alijikuta katika jiji lililosheheni miundominu ya kisasa ya huduma za afya na makao makuu ya taasisi nyingi za kimataifa, Na tofauti na mapambano dhidi ya Boko Haram, mapambano dhidi ya Ebola yanavuka mipaka ya ukabila, siasa na dini.

"Ebola inamgusa kila mtu," anasema Atallah. "Haina madhehebu wala kundi maalum."

'Kasheshe' nyingine nchini humo yatarajiwa Februari mwakani wakati taifa hilo litakapofanya uchaguzi wa Rais. Baada ya mhula mmoja madarakani, Rais Jonathan anaruhusiwa kugombea tena. Ushindi kwa chama chake cha People's Democratic Party, ambacho kimeitawala Nigeria kwa miaka 14, na ambacho kina sapoti kubwa kusini mwa nchi hiyo, waweza kuchochea mgawanyiko zaidi nchini humo, sambamba na ugumu wa kuwaokoa mateka waliosalia mikononi mwa Boko Haram.

CHANZO: Makala hii imetafsiriwa kutoka hifadhi yangu ya habari muhimu, ninazokutana nazo mtandaoni na kuzihifadhi katika app ya Instapaper. App nyingine ninayoitumia kwa hifadhi ya habari ninazozitumia kama reference ni Pocket. Kadhalika, app nyingine muhimu ninayoitumia kuhifadhi vitu mbalimbali ninavyokutana navyo mtandaoni au hata mtaani ni Evernote





0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.