SERIKALI imetia saini mkataba wa uwekezaji wa pamoja kati yake na kampuni ya Marekani kwa ajili ya kuanza mradi wa usafiri wa treni ya kisasa itakayoanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam.


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesisitiza ni lazima kufanya haraka kwani mwekezaji, Kampuni ya Ms Shimoja ya Marekani, iko tayari hata sasa kuleta treni hizo aina ya Diesel Multiple Unit (DMU) ambazo ni za kisasa, itakayopita kila baada ya nusu saa.



Usafiri huo wa treni kwenye njia ya umbali wa kilometa 13 kutoka uwanja wa ndege hadi katikati ya jiji, unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu au mapema mwakani ukilenga kubeba abiria kati ya 800 na 1,000.



Katika hafla ya kutia saini kati ya mwekezaji huyo na Shirika la Reli Tanzania (TRL) jana jijini Dar es Salaam, Waziri Mwakyembe aliwaambia watendaji kwamba ikiwa watafanya haraka, baada ya wiki mbili watasaini makubaliano ya mwisho na kuanza urekebishaji na ujenzi wa vituo sita vya kupandia treni kwa kadi.



Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya Ms Shimoja, Dk Robert Shumake na Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu walitia saini jana katika hafla iliyoshuhudiwa na Waziri Mwakyembe na Katibu Mkuu wake, Dk Shaaban Mwinjaka.



Waziri Mwakyembe alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kusafisha njia ya kupata wawekezaji, akiwemo mfanyabiashara huyo mkubwa ambaye ametajwa kuwa na imani kuwekeza katika mradi huo utakaogharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 35.



Kwa mujibu wa waziri, waliamua kuanza mradi huo baada ya kuhamasisha mashirika makubwa ya ndege kufanya safari katika kiwanja hicho cha ndege. Hata hivyo, alisema wasafiri wanapata kero ya usafiri kufika katikati ya jiji jambo wanalotegemea mradi kuondoa kero hiyo.



“Mabehewa hayo yataunganishwa kulingana na idadi ya abiria waliopo na muda, huku mwekezaji akiwekeza bila masharti kama walivyo wengine; kama vile kutaka dhamana ya serikali,” alisema Mwakyembe.



Hata hivyo alisisitiza, “lakini ni lazima watendaji waache ukiritimba kwa kufanya utaratibu haraka ili kazi zianze.”



Alisema katika utaratibu wa PPP, uwekezaji na idara nyingine lazima wafanye haraka. Aidha alitaka watendaji TRL kumsihi mfanyabiashara huyo kuleta treni nyingine mbili za Ubungo mpaka Stesheni na kwingineko.



Treni hiyo itasaidia kupunguza adha kwa abiria wanaosafiri kwa ndege, ambapo katika kituo cha Karakata, itajengwa njia ndogo ya treni mpaka barabarani. Pia litajengwa daraja kwa ajili ya wasafiri kuvuka na mizigo yao.



Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kisamfu alisema watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha usafiri huo unaanza mapema iwezekanvyo kutoka katikati ya jiji hadi Pugu kupitia maeneo ya Karakata, kwenye Uwanja wa Ndege kwa kutumia Reli ya Kati.



Mwekezaji Dk Shumake ambaye ni Balozi wa Heshima Tanzania nchini Marekani, alisema wako tayari kuanza mradi huo hata leo kama utaratibu utakamilika.
Alisisitiza kwamba uwekezaji huo utaondoa tatizo la foleni barabarani kutoka uwanja huo wa kimataifa wa ndege hadi katikati ya jiji.

CHANZO: Habari Leo