6 Feb 2015

WIKI iliyopita, kwa mara nyingine tena, Watanzania walishuhudia jinsi Jeshi la Polisi lilivyo mahiri katika ukiukaji wa haki za binadamu baada ya kuwapiga na kuwajeruhi wanachama wa CUF pamoja na Mwenyekiti wao, Prof Ibrahim Lipumba kwa ‘kosa la kuandamana kinyume na maagizo ya jeshi hilo.’
Kwa hakika nilitokwa na machozi nilipoangalia video ya tukio hilo ambayo imesambaa mtandaoni. Vipande vya video hiyo ambavyo vilinitia uchungu zaidi ni pale binti mdogo tu alipopigwa vibaya na polisi kadhaa wa kiume, na pale waandamanaji hao waliposhushwa kwenye magari ya polisi na kurushwa kichura kuingia kwenye kituo cha polisi. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Lakini pamoja na tukio hilo kusikitisha mno, binafsi sioni kama ni la kushangaza kwani sote twakumbuka ruhusa iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa polisi kuwa “(wananchi) wapigwe tu.”
Ukiangalia video hiyo kwa makini (waweza kuiona hapa http://goo.gl/zbmnTG
(link is external)
) utabaini ukweli mmoja wa kutisha. Angalia dakika ya 03:14 hadi dakika ya 03:19, baadhi ya waandamanaji wanasema "TUUENI..."

Angalia pia kuanzia dakika ya 3.21 ambapo polisi wanaanza kurusha risasi (sina hakika kama ni risasi za moto au bandia) lakini kitu cha kukiangalia kwa makini ni ukweli kwamba ukiacha watu wachache wanaoonekana kutishwa na milio hiyo ya risasi, idadi kubwa tu ya watu inaonekana kutotishika. Hali hiyo inaendelea hata baada ya 'king'oling'oli' cha polisi kinapooanza kulia na hatimaye polisi kutembeza kipigo cha kinyama.
Licha ya kuumia mno kuona Polisi wakitumia nguvu kubwa katika tukio ambalo lingeweza kabisa kumalizwa kwa amani pasipo haja ya kurusha risasi japo moja au kuwapiga na hatimaye kuwakamata waandamanaji akiwemo Mwenyekiti wa CUF Prof Lipumba, kilichonipa hofu ni jinsi taratibu wananchi wanavyoanza kuota 'usugu' dhidi ya unyanyasaji wa polisi.
Inapofika mahala wananchi wanaashiria bayana kuwa wapo radhi kuuawa, na kuwaambia polisi waziwazi kuwa TUUENI, basi kwa haki tumeshafika mahala pabaya. Na kama nilivyobainisha hapo juu, na kama inavyoonekana kwenye video hiyo, imefika mahala wananchi wameanza kuzowea sauti za risasi sambamba na mabomu ya machozi.

Hii ina maana gani? Wakati tayari wananchi wameshaonyesha kuzowea unyanyasaji na unyama wa polisi wetu na kuwa tayari kwa lolote lile, yayumkinika kubashiri kuwa kuna siku sio tu wananchi wataweka kando uoga na kuendeleza 'usugu' huo nilioueleza hapo juu bali pia wanaweza kujibu mashambulizi.
Uchambuzi mwepesi ni kwamba wakati polisi hawana njia nyingine zaidi ya hizi wanazotumia kila siku: kutumia nguvu kuvunja maandamano ya amani, wananchi wanapata nguvu mpya kwa kuondoa uoga na kuwaacha polisi wafanye watakalo. Upo uwezekano wa wananchi hao kutoishia hapo tu bali badala ya kuwaachia polisi wawaonee, WANAWEZA KUJIBU MASHAMBULIZI. Na kwa mwenendo ulivyo, hatuko mbali na hali hiyo.
Ni vigumu kubashiri ni lini polisi wetu watathamini haki za binadamu na uhai wa wananchi wasio na hatia. Ni vigumu zaidi kutarajia mabadiliko kutoka kwa mwana-CCM yoyote yule atakayemrithi Kikwete baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Na ndio maana hatujaskia yeyote kati ya waliotangaza nia ya kuwania Urais kupitia CCM akilaani unyama huo wa polisi. Kwanini walaani ilhali wao wana kinga ya kudumu dhidi ya uonevu na unyama wa polisi wetu? Japo Rais kutoka chama cha upinzani anaweza kutugeuka, lakini katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu angalau yeye naye atakuwa ameshaonja unyama wa polisi wetu na ni rahisi kwake kuchukua hatua kuliko hao wasioguswa na polisi.
Mmoja wa wana-CCM waliotangaza nia ya kugombea urais, January Makamba, amekuja na kauli-mbiu ya ‘Tanzania mpya.’ Nadhani moja ya maeneo yanayopaswa kuwa mapya katika Tanzania hiyo mpya ni utendaji kazi wa jeshi letu la polisi. Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa upya katika maeneo mbalimbali yanayoihusu nchi yetu, tatizo kubwa ninaloliona ni udhati katika utekelezaji wa dhamira hiyo. Lakini pia kuna suala la lini hiyo Tanzania mpya ianze kama sio sasa? Nadhani jibu rahisi ni kwamba uhuni unaofanywa na jeshi letu la polisi sio suala la bahati mbaya. Ni mkakati madhubuti unaoinufaisha CCM dhidi ya wapinzani wake.
Kwanini iwe ruhusa kwa CCM kuandamana muda wowote wanaotaka lakini wapinzani wakiomba kufanya maandamano wanakataliwa?
Sasa pamoja na dhamira nzuri ya January ya kutuletea Tanzania mpya, ni wazi CCM haiwezi kuruhusu tuwe na ‘jeshi la polisi jipya’ litakaloendana na ‘Tanzania mpya’ kwa vile hali hiyo itatoa mazingira bora ya kushamiri kwa demokrasia huko nyumbani, na hili litaiathiri CCM.
Tukirejea kwenye tukio hilo la kinyama dhidi ya wana-CUF wasio na hatia, mazingira yote yanaonyesha sio tu kuwa hakukuwa na haja kwa polisi kutumia mabavu bali pia lingeweza kumalizwa kwa amani.

Lakini kwa polisi waliozowea kufanya ubabe, kulimaliza suala hilo kwa amani kungewafanya wajiskie kama ‘wameshindwa kazi.’ Au huenda walihofia ‘kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa kukiuka agizo la Waziri Mkuu Pinda kuhusu kupiga raia.’
Ukweli mchungu ni kwamba jeshi la polisi litaendelea na unyama wake kwani hakuna dalili yoyote ya serikali kuchukua hatua za kukomesha tabia hiyo. Na kwa vile tunaelekea msimu wa uchaguzi ambapo miongoni mwa shughuli za kawaida kisiasa katika chaguzi ni pamoja na maandamano na mikutano, kuna uwezekano mkubwa wa kushuhudia wanachama wa vyama vya upinzani na/au viongozi wao wakinyanyaswa na polisi wetu.
Nihitimishe makala hii kwa kurejea tahadhari niliyoitoa hapo juu.

Ipo siku wananchi wanaonyanyaswa na polisi wetu wataamua ‘liwalo na liwe’ na watajibu mashambulizi. Japo ninaomba Mungu atuepushe tusifikie hatua hiyo, ukweli mchungu ni kwamba twaelekea huko. Imefika mahala wananchi wanawaambia polisi waziwazi “tuueni” na wanasikia milio ya risasi lakini hawakimbii.
Yayumkinika kuhisi kuwa kitakachofuata si wananchi kuwapa polisi uhuru wa kuwapiga na kuwajeruhi bali kupambana nao kwa nguvu zote. Ni sihitaji kukumbusha kuwa polisi wetu ni sehemu ndogo tu kulinganisha na umma wa wasio-polisi.

TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube