26 Apr 2015

Embedded image permalink
Moja ya taarifa zilizozagaa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ni kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi.Lakini shilingi au sarafu nyingine inashukaje thamani yake? Haya ni maswali ambayo ninaamini watu wengi wasio wachumi watakuwa wanajiuliza muda huu.

Nami pia ninajiuliza maswali hayo kama yalivyo kwenye kichwa cha habari.Ninajiuliza kwa sababu mie si mchumi, na jaribio langu pekee la kuingia fani ya uchumi lilikuwa wakati napata elimu ya sekondaria ambapo nilisoma Book Keeping hadi kidato cha nne na Commerce hadi kidato cha pili.

Naujua uchumi 'kijuu-juu' tu, na sana ni katika mahusiano yake na siasa au jamii, lakini kwa vile mie ni dhaifu sana wa hisabati, uchumi unaohusisha tarakimu ni 'no-go area.'

Kwahiyo, samahani msomaji mpendwa kama maswali hayo kwenye kichwa cha habari yalikupa hisia kwamba labda nitayajibu. Hapana. Ni maswali ninayotaka yapatiwe majibu na serikali au/na wataalamu wa masuala ya uchumi.

Kwa sie tunaoishi nje ya Tanzania, dalili kuu ya kushuka kwa thamani ya shilingi yetu ni pale tunapotuma fedha nyumbani kusaidia ndugu na jamaa zetu. Huo ndio muda unatulazimisha kufahamu viwango vya kubadilishia fedha. Kwahiyo kama ninataka kutuma shilingi laki kadhaa za Kitanzania, inanilazimu kufahamu ninatakiwa kutuma paundi za Kiingereza ngapi.Sasa kwa vile zoezi hili la kutuma misaada nyumbani ni la mara kwa mara, inakuwa rahisi kutambua kama 'shilingi ipo imara au imeyumba,' kwa maana kwamba unalinganisha, kwa mfano, "kutuma shilingi laki nne mwezi uliopita ilinigharimu takriban paundi mia na sitini, lakini safari hii imenigharimu paundi laki na arobaini."

Je Mtanzania wa kawaida anafahamu vipi kuhusu kuporomoka kwa thamani ya shilingi wakati hana sarafu ya kigeni ya kufanya mlinganisho? Na sio tu kufahamu kama thamani ya shilingi imepanda au imeshuka, lakini pia anapaswa kujua kama ina athari zozote kwake.

Kidogo ninachoelewa ni kwamba kuporomoka kwa shilingi kunaweza kuwa na 'faida' flani. Wanadai thamani ya sarafu ikishuka, bei ya bidhaa za nchi husika katika masoko ya kimataifa inashuka pia.Kushuka huko kwaweza kuwasukuma wanunuzi katika masoko hayo 'kuchangamkia tenda,' na hiyo inaweza kupelekea nchi kuuza mazao yake kwa wingi, na wakati huohuo hiyo inaweza kuhamasisha wakulima wa mazao au wauza bidhaa za export kuongoze uzalishaji. Sina uhakika sana kuhusu hilo kwa vile kama nilivyotanabaisha hapo juu, mie ni mbumbumbu wa uchumi.Sina A wala B ninalojua katika eneo hili.

Nimalizie makala hii kwa kutoa changamoto kwa serikali sio tu kuwafahamisha wananchi kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi yetu bali pia kueleza sababu za kushuka huko na athari au faida zake kwa Mtanzania. Kadhalika, ninatoa changamoto kwa wataalamu wetu wa uchumi kuisaidia jamii kwa kutupa somo kuhusu suala hili.Na nitumie fursa hii kumkaribisha mtaalam yeyote kunitumia makala kuhusu suala hjilo nami nitaichapisha hapa bloguni au kuituma kwa jarida la RAIA MWEMA ninaloandikia makala kila wiki.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube